Nkoma atajwa tena JKT

Mwanaspoti
Published: Jun 02, 2023 15:10:11 EAT   |  Sports

WAKATI Mabingwa wa Ligi ya Wanawake WPL msimu huu JKT Queens wakijiandaa na michuano ya kimataifa timu hiyo huenda ikamrudisha tena Sebastian Nkoma kama mbadala wa Ally Ally kutokana na kukosa leseni A ya Ukocha. Huenda Nkoma akarudi tena kuwatumikia wanajeshi hao kutokana na kuwa na Leseni A na aliwahi kuifundisha Simba Queens ambao walitwaa Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa kuifunga She Corporates ya Uganda bao 1-0. Katibu Mkuu wa timu hiyo, Dankan Beno amesema kuwa wako katika mchakato wa kumtafuta kocha huyo na kuongeza kuwa wameteua makocha watatu akiwemo Nkoma. Dankan amesema viongozi wa timu hiyo watakaa na kujadili kumchagua nani atakaeongoza kikosi hicho ambacho mwezi Agosti kitatakiwa kutwaa Ubingwa wa CECAFA ndipo washiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. "Siku mbili hizi viongozi wetu watakaa na kujadili kocha yupi anaweza kutufaa kwa sababu Kocha Ally hana leseni A lakini katika orodha ya makocha watatu Nkoma pia ni mmoja wapo na kama kamati ikipitisha basi ataongoza." alisema Dankan Kuhusiana na kushiriki michuano ya majeshi Katibu huyo amesema wachezaji hao walifanya mazoezi jana kwaajili ya maandalizi ya kwenda nchini Uholanzi mwezi huu. JKT Queens watashiriki mashindano hayo kama wawakilishi wa ngome ya Jeshi la kujenga Taifa Tanzania(JWTZ) yakiwa makundi matatu kutoka nchini tofauti. Kundi A likiongozwa na wenyeji Uholanzi, Nigeria, Uzbekistan na Ugiriki huku kundi B ikiwa na nchi ya Ufaransa, Tanzania, Korea Kusini na Canada. Na kundi la mwisho ambalo ni C linaongozwa na Cameroon, Korea Kaskazini, Ujerumani na Marekani.