Nguvu kiuchumi zimezibeba Simba, Yanga

Mwanaspoti
Published: Mar 22, 2023 18:45:46 EAT   |  Sports

MAKAMU wa Rais wa Yanga, Arafat Haji amesema kukua kwa nguvu za kiuchumi kwa klabu za Simba na Yanga imekuwa chachu kwa miamba hiyo ya soka la Tanzania kufanya vizuri kwenye michuano ya Kimataifa. Arafat amesema hayo kwenye mjadala wa Simba, Yanga kufuzu robo fainali ya michuano ya kimataifa nini maana yake kwa soka la Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki ambao umechukua nafasi kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ya Mwananchi. Kiongozi huyo ambaye alikuwa mmoja wa wachangiaji, alianza kwa kupongeza kufuatia uwepo wa mjadala huo ambao umewakutanisha pamoja wadau wa Simba na Yanga kisha kusema, "Nini kimeibeba Simba na Yanga, Wadau wamekuwa na mchango kwa maana ya kuingia kama wabia, tumeona Yanga wameenda kwa SportPesa na Simba kwa M-Bet huku wakiwemo wengine," "Hii ni faida ambayo naamini imechangia kwa timu hizi kufika mbali, mpira wa Afrika kuendesha ni ghamara kubwa sana, ili uendelee kuwa imara inahitaji kuwa sawa kiuchumi..." "Timu zetu zimeenda mbali kwa kuwa na mabenchi mapana kwa kuwa na kila mtu na eneo lake tofauti na zamani ambapo mtu mmoja alikuwa akifanya vitu vingi kwa wakati mmoja, zamani tulikuwa tukiona DR Congo ikifanya vizuri lakini kwa sasa imekuwa tofauti inamaana ya kuwa nguvu ya timu zetu kiuchumi zimekua," amesema makaumu huyo mwenyekiti wa Yanga. Aliendelea kufafanua kwa kusema; ,"Tumeona Simba wamemtoa Sakho (Pape) na kwenda timu ya taifa la Senegal, hata kwa Yanga kuna mchezaji kutoka Mali (Diarra), wachezaji mataifa makubwa kwa sasa wanahamasika kucheza hapa, hili inatakiwa kuleta changamoto kwa wachezaji wetu wazawa." Hata hivyo, Arafati kwenye uchangiaji wake hakusita kusema namna ambavyo hamasa ya Rais Samia Suluhu Hassan ilivyochochea kufanya vizuri kwa timu zetu huku akitoa wito kwa timu nyingine ambazo zitapata nafasi ya namna hiyo kufanya makubwa msimu ujao na isiishie kwa Simba na Yanga.