Nabi ashtukia mtego wa Waarabu

Mwanaspoti
Published: May 31, 2023 08:51:20 EAT   |  Sports

KOCHA mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema ameshtukia baadhi ya mambo na hivyo anatarajia kubadilisha mfumo wa timu yake kwenye mchezo wa fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Algier. Baada ya juzi Yanga kupoteza mchezo wa kwanza kwa kuchapwa 2-1, sasa mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara wameanza mikakati ya mechi ya marudiano itakayopiga Jumamosi ijayo, Juni 3, 2023, katika Uwanja wa Stade du 5 Juillet, huku wakipanga kuwavamia waarabu kishua zaidi. Wakati uongozi wa Yanga ukiendelea na mipango yao, kocha Nabi naye amestukia mtego wa Waarabu uwanjani na tayari ameutegua. Nabi alisema kupitia mechi ya juzi pale kwa Mkapa aligundua ni wapi USM Alger waliwazidi ujanja vijana wake na tayari ameanza kufanyia kazi ili kuhakikisha anashinda ugenini. "Yaliyotokea ni matokeo. Tulifanya baadhi ya makosa yaliyopelekea kupoteza mechi lakini bado tuna dakika 90 nyingine ugenini, na kuna mambo tumeshayagundua. USM Alger ni timu bora na yenye wachezaji wachangamfu, natambua ugumu wao hususani kwenye mechi ya ugenini lakini naamini tutajipanga upya na kwenda kutafuta matokeo mazuri kwao kwa kuwa tuna uwezo huo," alisema Nabi na kuongeza; "Kupitia mechi ya leo (juzi), nimeona wapi tulizidiwa na wapi tulikuwa bora, tutalifanyia kazi suala hilo katika siku chache tulizonazo na tutakuja na njia sahihi ya kuwakabili nyumbani kwao." Huenda Nabi katika mchezo wa marudiano akabadili mfumo na baadhi ya wachezaji katika kikosi chake alichokianzisha kwenye mchezo wa nyumbani. Yanga inahitaji ushindi wa kuanzia mabao 2-0 na kuendelea ugenini ili kutwaa taji hilo na kama itaweza kushinda 2-1 kama ilivyofungwa nyumbani basi mchezo huo utamaamuliwa kwa mikwaju ya penalti. Mashabiki wengi wa Yanga wanaimani timu yao inaweza kupindua meza ugenini wakikumbushia mechi ya mtoano kuwania kuingia Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo 'Wananchi' walikutana na Club Africain kutoka Tunisia na kutoa sare nyumbani kwa Mkapa lakini wakaenda kushinda ugenini 1-0, na kutinga makundi ya Shirikisho. Yanga inatarajiwa kuondoka nchini kati ya kesho Jumatano au Alhamisi kwa ndege maalumu iliyoandaliwa na serikali itakayoenda moja kwa moja hadi Algeria na timu ikifika huko imepanga kukaa kambi ya kishua zaidi kwa muda wote watakaokuwa huko kwa ajili ya mchezo huo. Msafara huo wa Yanga unatarajiwa kuwa na viongozi, wachezaji, benchi la ufundi, wanahabari, viongozi wa serikalini, wadau na mashabiki wa timu hiyo kutoka Tanzania. Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji kwenye moja ya mahojiano na Mwanaspoti alisema, uongozi unaifanya timu kuishi kishua ili wachezaji wajisikie vizuri na wenye bahati kuichezea Yanga hivyo hivyo wanaandaa makazi, malazi na mazingira bora zaidi katika kila nchini wanayokwenda kucheza ili kuwafanya wachezaji kutambua thamani na ukubwa wa Yanga kisha wakaipambanie uwanjani.