MZUKA WA GOFU: Tanzania na historia ya kibabe

GOFU ni miongoni mwa michezo mikongwe hapa nchini ukiachana na soka, riadha na ngumi ikielezwa kwamba ulianza kuchezwa mwaka 1950. Wakati mchezo huo unaanza kuchezwa ilikuwa ni miaka 10 kabla ya Uhuru wa Tanganyika (sasa Tanzania Bara) na kipindi hicho ulipendwa zaidi na Waingereza, historia ikiwa inaonyesha kwamba Watanzania walikuja kuanza kuucheza baadaye. “(Watanzania) wengi walikuja baadaye, walioanza kujifunza wengi walikuwa na ukaribu na Waingereza waliokuwa wakicheza wakati ule baadhi yao walifanya kazi kwa Waingereza na huo ndiyo ukawa mwanzo Watanzania wachache na watoto wao kuanza kujifunza kucheza gofu,” anaeleza Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TLGU), Gilman Kasiga. “Hiyo ilikuwa ni miaka ya nyuma kabisa, historia inasema ilipofika mwaka 1950, Tanzania ilifanya mashindano ya kwanza ya Afrika Mashariki na Kati na kuingia kwenye rekodi ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa mara ya kwanza.” Kwanini Tanga? Japokuwa chanzo cha mkoa huo kuteuliwa kuwa mwenyeji wa mashindano ya kwanza hakijawekwa wazi, lakini kuna tetesi kwamba nyakati hizo Tanga wakati huo wa ukoloni inatajwa kuwa lilikuwa ni jiji la viwanda. Ni miaka 73 sasa imepita tangu kufanyika mashindano ya kwanza ya gofu nchini, japo hivi sasa mkoa huo wa Tanga hauna rekodi bora zaidi kama ilivyo Dar es Salaam. Lakini kuna tetesi zinasema nyakati hizo mji huo ulikuwa wa viwanda na mwamko wa gofu ulikuwa juu zaidi, hivyo huenda ndiyo chanzo cha kamati kuuchagua kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ya kwanza. Matabaka yalitawala Kasiga anasema awali mchezo huo ilichezwa kwa matabaka tofauti na sasa ambapo kila mtu anaweza kuucheza. “Ukweli hauwezi kufichwa. Awali gofu ilionekana ni ya watu fulani wenye hadhi tofauti mabosi na vigogo, hiyo ndiyo ilikuwa kasumba ya mchezo huo wakati unaanza kuchezwa nchini,” anasema. “Hiyo ilisababishwa na asili yake, pia gharama za vifaa na mazingira ya mchezo wenyewe wakati ule. Ilikuwa ni ngumu kwa Watanzania wengi kuingia na kuanza kucheza. Wachache waliopata fursa hiyo ambao familia zao zilikuwa na ukaribu na Waingereza waliokuwa wakicheza ndiyo walipata fursa ya kujifunza.” Anasema kulingana na aina ya mchezo na mazingira ya namna ulivyoanza kuchezwa, fikra na mitazamo ya wengi ilionekana kuwa ni mchezo wa kitajiri. “Hivi sasa ni tofauti. Kila Mtanzania mwenye mapenzi na anayetamani kujifunza kucheza gofu ana fursa hiyo. Ili kufikia malengo hayo tumeanzisha programu za watoto kuandaa wachezaji ambao wataleta medali za kimataifa kwa kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa.” Uwanja wa kwanza Licha ya mashindano ya kwanza ya gofu kufanyika 1950, historia inaonyesha uwanja cha kwanza ulijengwa Tanzania 1919. “Wazungu ni watu wanaopenda michezo. Walianza kucheza kitambo japo haikuwa kwa ushindani hadi mwaka 1950 ndipo yalifanyika mashindano ya kwanza nchini. “Uwanja wa Gymkhana Dar es Salaam ulijengwa mwaka 1919, Moshi Golf (1922), Mufindi (1920) na Tanzania Open wa Tanga. Hivi ni viwanja vikongwe vya gofu nchini,” anasema. Gofu inachezwa huku Ukiachana na Dar es Salaam ambayo ina viwanja vya Gymkhana na Lugalo, Kasiga anasema maeneo mengine yenye viwanja hivyo ni Kilimanjaro yenye viwanja viwili sawa na ilivyo Arusha, huku Morogoro mjini, Kilombero Sugar, Geita na Zanzibar kukiwa na uwanja mmoja. “Viwanja vinavyotumika mpaka sasa viko 11. Vilikuwepo vingi baadhi vimebadilishwa matumizi, lakini bado kuna ujenzi unafanyika wa viwanja vingine, hivyo tunatarajia idadi kubwa zaidi,” anasema. “Malengo ni kuhakikisha gofu inachezwa na watu wengi na inakuwa ajira kama ilivyo michezo mingine, hivyo ujenzi wa viwanja vingine unasaidia kuzifanya ndoto zetu ziwe rahisi kufikiwa.” Hata hivyo, Kasiga anasema baadhi ya viwanja vilibadilishwa matumizi akitoa mfano wa ule wa Mwanza kwamba eneo hilo kilijengwa Chuo cha Benki Kuu. “Mbeya pia ulibadilishwa matumizi kikajengwa chuo cha Veta, japo kulikuwa na kiwanja kingine bado tuko kwenye majadiliano, lakini kinatakiwa kubadilishwa matumizi wajenge hoteli.” Kasiga anasema pia kuna viwanja vinne viko kwenye mchakato wa kujengwa ukiwamo wa Serengeti unaojengwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), uwanja wa Jeshi Dodoma na mwingine unaotarajiwa kujengwa Manyara. “Pia Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kujenga uwanja wa gofu Chamwino, Dodoma, hivyo tunaendelea kujipambanua zaidi kwenye mchezo huu. Lengo ni kufika levo ya Olimpiki kwa timu ya taifa na kuwa na wachezaji wengi zaidi wa kulipwa,” anasema. Ni mchezo wa Matajiri? Kasiga anasema; “Ilimradi mtu anaweza akawa na nguvu ya kushika fimbo na kuucheza anakaribishwa ndio maana wanafunzi wanaweza wakatoka shule wanakwenda kujifunza kwenye programu ambayo ipo Lugalo (Dar) na ni bure kabisa.” “Kwenye mashindano mbalimbali tunayoyaandaa kuna watu wazima wengine wana miaka zaidi ya 80 bado wanacheza, tena unafanyika afya. Kulingana na mwendo unaotakiwa utembee kutoka shimo moja kwenda lingine unaweza ukatembea zaidi ya kilomita 10 na usichoke tofauti na kutembea mtaani ambako unaweza usizimalize.” Vigogo wa gofu Ukiachana na nyota wa kulipwa (mapro) ambao wanaiwakilisha nchi kwenye mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa ya gofu, na wale wa ridhaa, gofu inachezwa pia na wachezaji wenye nyadhifa mbalimbali wakiongozwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro; Nape Nauye (waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari), Jenerali mstaafu George Waitara na viongozi wengine wengi wakiwamo pia wasomi na watu wa kada mbalimbali. “Gofu inachezwa na watoto kuanzia miaka mitano hadi watu wazima wenye umri mkubwa. Mbali na kuwa ni mchezo, lakini pia ni sehemu ya mazoezi na afya,” anasema. Kasiga anamtaja Dk Ndumbaro kama mmoja wa mifano katika mchezo huo kabla ya kuwa waziri hadi sasa na ni mmoja wa waanzilishi wa mashindano ya Diplomatic. “Waziri Ndumbaro ni mwanzilishi wa mashindano yanayofanyika kila mwaka Songea ya Diplomatic yenye lengo la kusaidia kuwalipia ada watoto wanaotoka kwenye familia zisizo na uwezo kifedha. Pia Naibu waziri wake, Hamis Mwinjuma (Mwana FA) naye ni mdau mkubwa wa gofu.” Mkongwe wa gofu Kwa sasa Salim Mwanyenza ndiye mchezaji gofu mkongwe nchini akielezwa kwamba alianza kucheza kabla ya Uhuru wa Tanganyika wakati huo akiwa mkoani Tanga. “Nilianza kama kedi (mbeba vifaa vya gofu) kwa Waingereza. Nilikuwa shule ya msingi mwaka 1956, kwenye klabu ya Tanga Gymkhana Waingereza walikuwa wakicheza gofu. Nilijikuta tu naupenda. Wakati ule Waafrika wengi waliupenda, lakini ulikuwa ni mchezo wa Waingereza, hivyo wengi tuliingia kama makedi,” anasema Mwanyenza. Anasema kitendo cha wengine kucheza na kufurahi ndicho kiliwavutia Waafrika wengi kutaka kujifunza, japo shule za Kiafrika na za Waingereza hazikuwa pamoja, lakini mfumo ulikuwa wa Kiingereza. Mwanyenza anasema Uwanja wa Gymkhana Tanga ulikuwa karibu na nyumbani kwao, hivyo ilikuwa rahisi kutoka shuleni na kwenda uwanjani kuwabebea Waingereza vifaa wakati wakicheza na kuanza kujifunza. “Nilifanya hivyo hadi nikawa mchezaji. Hata baada ya shule nilipoanza kazi niliendelea kucheza. Mwaka 1970 nilihamia Dar es Salaam na kujiunga kuwa mwanachama wa klabu ya Gymkhana hadi leo hii bado nacheza gofu,” anasema.