MZUKA WA GOFU: Marekani, Uholanzi na Hispania top 3 duniani

LICHA ya Waingereza kuwa waanzilishi wa gofu duniani, kibao kimegeuka sasa katika Top Ten ya dunia, nchi hiyo imeingiza nyota mmoja ikitolewa kwenye reli na Wamarekani wanaongozwa na kinara wa dunia, Scottie Scheffler. Scheffler mwenye wastani wa pointi 11.617 katika michezo 51 amekaa kileleni akiwa na pointi 592.46 na kupanda kwa nafasi moja, kutoka ya pili mwishoni mwa mwaka jana. Kinara huyo wa dunia, aliyevuna dola 21 milioni kwenye gofu, katika renki za mwishoni mwa 2022 alikuwa wa pili huku mwaka huu akimshusha Mholanzi Rory Mcllroy waliyebadilishana naye nafasi. Mcllroy ana wastani wa pointi 10.966 katika michezo 45 aliyocheza hadi sasa ambayo yote alivuna pointi 493.45 huku akiwa ameingiza kitita cha zaidi ya dola 13.9 milioni kwenye gofu. Katika mechi zake zote, Mcllroy amepoteza pointi -221.88 wakati Mhispania, Jon Rahm anahitimisha tatu bora ya dunia akiwa na wastani wa pointi 9.515 katika mechi 47. Staa huyo aliyevuna pointi 447.22 katika mechi hizo ana utajiri wa zaidi ya dola 16,5 milioni akiwa amepoteza pointi -224.24 katika mechi hizo. Viktor Hovland wa Norway ni wa nne akiwa na wastani wa pointi 7.788, staa huyo amevuna kitita cha zaidi ya dola 14.1 milioni kwenye gofu, katika mechi 52 alizocheza ambazo pia amepoteza pointi -170.33. Nafasi ya tano hadi saba ni ya Wamarekani Patrick Cantlay, XanderSchauffel na Max Homa, Cantlay ana wastani wa pointi 7.417 akiwa amevuna kitita cha zaidi ya dola 10.3 milioni. Amecheza mashindano 41 na kupoteza pointi -179.19. wakati Schauffele yeye ana wastani wa pointi 6.737 katika mashindano 46. Katika gofu, staa huyo amevuna kitita cha zaidi ya dola 8.4 milioni, akiwa amepoteza pointi -160.90 na Homa yeye ana wastani wa pointi 5.366 katika mashindano 48. Ana kitita cha zaidi ya Dola 10.5 milioni ambazo amevuna kwenye gofu akipoteza pointi -122.64 katika mashindano yote. Mwingereza kinara wa gofu ni Matt Fitzpatrick ambaye kwenye msimamo wa dunia ni wa nane akiwa na wastani wa pointi 5.172. Fitzpatrick amevuna zaidi ya kitita cha dola 8.1 milioni, amecheza mashindano 52 akiwa amepoteza pointi -147.84, wakati Brian Herman wa Marekani akikamata nafasi ya tisa akiwa na wastani wa pointi 5.106, Nyota huyo amevuna kitita cha zaidi ya dola 9.1 milioni, akiwa na rekodi ya kucheza mashindano 52 ambayo amepoteza pia pointi -77.84. Mmarekani mwingine, W Clark mwenye wastani wa pointi 4.956 katika mashindano 52 anahitimisha 10 bora ya dunia akiwa amevuna kitita cha zaidi ya dola 10.7 milioni licha ya kupoteza pointi -30.61. Aprili, 2019, aliyekuwa staa wa dunia, Eldrick ‘Tiger’ Woods alitamka kuwa ni wakati sahihi wa yeye kustaafu kucheza gofu, japo ameporomoka, bado ana rekodi ya kuwa mwanamichezo aliyelipwa pesa nyingi miaka ya nyuma. Woods aliyeanza kuwika kwenye gofu akiwa na miaka 20, na kuwa nyota wa dunia kwa miaka kadhaa kabla ya kuanza kuporomka na kupambana kwa miaka miwili hadi 2013 aliporudi kwenye ubora wake. Majanga yalianza kumkuta baada ya kufanyiwa upasuaji wa mkono, huku akipitia majanga kadha wa kadha ikiwamo kukosolewa kwa kutokuwa mwamifu kwenye ndoa yake na kukaa muda mrefu bila kushiriki mashindano makubwa. Mwaka 2011 aliangukia nafasi ya 58 duniani, mwaka 2014 majanga yaliendelea kumwandama na mwaka 2019 alionyesha nia ya kutaka kustafu ingawa mwaka 2021 alipata ajali mbaya ya gari huko Los Angels Marekani, ambayo imemuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu hadi sasa.