Mbeya City kama daraja kwa Yanga

Mwanaspoti
Published: May 30, 2023 16:09:57 EAT   |  Sports

MBEYA City huu ni msimu wa pili mfululizo mchezo wake dhidi ya Yanga hutumika kukabidhiwa ubingwa bingwa wa Ligi Kuu katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya. Msimu uliopita katika mchezo ulioisha kwa sare ya bao 1-1 kwa mabao ya Joseph Ssemujju dakika ya 50 kwa mkwaju wa penalti amabalo lilikuwa la kusawazisha baada ya Heritier Makambo kuitanguliza Yanga dakika ya 40. Yanga ilikabidhiwa ubingwa kwenye mchezo huo ikiwa imesalia na mchezo mmoja mkononi kumaliza msimu ambapo ilicheza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkapa na kushinda bao 1-0 lililofungwa na Denis Nkane dakika ya 81. Msimu huu tena imejirudia Yanga itacheza na Mbeya City Juni 6 Uwanja wa Sokoine ambapo mabingwa hao wakitarajia kukabidhiwa kombe lao huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya Tanzania Prisons. Katika mchezo wa kwanza msimu huu zilipokutana Novemba 26 mwaka jana Uwanja wa Mkapa Yanga ilishinda mabao 2-0 yote yakifungwa na Fiston Mayele dakika ya 24 na 79. Tangu Mbeya City ipande Ligi Kuu imeifunga Yanga mara moja mchezo uliopigwa Novemba 2, 2016 Uwanja wa Sokoine ukiwa mchezo wake wa kwanza Ligi Kuu ikiwa chini ya Kocha Juma Mwambusi ambapo ilimaliza nafasi ya nne kwa alama 34 sawa na Coastal Union. Mbeya City imekutana na Yanga kwenye ligi michezo 15 huku ikishinda mchezo mmoja, sare sita na kufungwa michezo nane huku kichapo kikubwa kikiwa cha mabao 5-0 ilichopokea Novemba 19,2017 wakati, Obrey Chirwa akipiga hat trick huku Emmanuel Martin akifunga mabao mawili. Mchezo unaofuata utakuwa wa aina yake sababu Mbeya City ikihitaji alama tatu ili kujinasua na eneo la kushuka daraja wakati Yanga ikisaka heshima ya kukabidhiwa kombe bila kufungwa. Katika michezo saba ya mwisho kukutana, Yanga imeshinda michezo miwili huku sare zikiwa tano na michezo yote Yanga ikishinda katika Uwanja wake wa nyumbani. Katika michezo 15 walizokutana Yanga imeshinda michezo miwili pekee Uwanja wa Sokoine, mchezo wa kwanza ulikuwa Mei 10, 2016 iliposhinda mabao 2-0 kisha Disemba 29, 2018 iliposhinda 2-1. Kocha wa Mbeya City, Abdalah Mubiru alisema wameendelea kujiandaa na mchezo huo ili kufanikiwa kupata ushindi ambao utawasaidia kupanda nafasi za juu kwenye msimamo.