Kocha Monastir aipa nondo nne Yanga, amtaja Mayele

Mwanaspoti
Published: Mar 23, 2023 09:16:31 EAT   |  Sports

KOCHA wa US Monastir, Mserbia Darko Novic ameipa Yanga nafasi kubwa ya kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho na akawapa nondo kadhaa. Novic ambaye kwao aliipiga Yanga mabao 2-0, amesema ina mambo mazuri ambayo yanawabeba na wanapaswa kuyaongezea nguvu na kuyachukulia kama silaha muhimu na wasibezwe. Alisema ubora wa kwanza wa Yanga inayoongoza kundi lao ni uwepo wa kocha Nasreddine Nabi ambaye ameiweka katika eneo salama kimbinu kutofungika kirahisi na kwamba hata ikiwa nyuma unahitaji ubora kulinda bao lako. "Nilipocheza na Yanga tukashinda lakini muda wote hatukuwa na utulivu kuona kama tumemaliza mechi, nawaheshimu sana kwa kuwa wanaonyesha kuna kazi kubwa kocha wao amefanya, hata nilipokuwa nawafuatilia na kuangalia mechi zao sikuona kuna mchezo wamezidiwa umiliki wa mpira,"alisema Novic ambaye naye timu yake imefuzu hatua ya robo fainali licha ya kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Yanga. "Napenda wanavyocheza, wanakulazimisha wakati wote wanataka mpira uwe katika miliki yao, tulipocheza nao kisha kucheza na TP Mazembe ilitosha kuona kwamba watakuwa washindani wetu wakubwa katika kundi letu." Lakini alisema silaha nyingine kubwa ya Yanga ni washambuliaji wawili wakubwa katika eneo lao la mbele Kennedy Musonda na Fiston Mayele akisema jamaa wako vizuri. "Yule jezi namba tisa (Mayele) ni hatari anajua sana kufunga lakini pia ana kasi, kuna yule jezi namba ishirini na tano ndio tatizo zaidi, unapokuwa na washambuliaji wa namna ile wanawalazimisha mabeki kupoteza nidhamu yao kutokana na kasi yao kitu kibaya zaidi wanacheza kwa ushirikiano mkubwa. "Kwangu mimi nawaona watafika mbali kama watabahatika kupata bahati ya droo kwa kutokutana na timu ngumu najiandaa kuwaona watacheza hata nusu fainali,"alisema Kocha huyo ambaye timu yake ilikuwa tishio kwenye kundi. Mara ya mwisho Yanga kutinga robo fainali michuano inayoandaliwa na CAF, Clement Mzize ambaye ni straika wao chipukizi alikuwa hajazaliwa.Ilikuwa mwaka 1998. Kwa mujibu wa mchambuzi wa Mwanaspoti, Edo Kumwembe; "Kama ilivyo kwa Simba, Yanga wanahitajika kucheza kiume zaidi katika hatua inayofuata. Ukweli ni kwamba hauwezi kucheza fainali bila ya kucheza na timu ngumu katika hatua ya robo au nusu. Unaweza kukutana na timu dhaifu katika makundi lakini hauwezi kukutana na timu dhaifu katika robo fainali. Yanga wana wachezaji wa hadhi hiyo kwa sasa. Simba pia wana wachezaji wa hadhi hiyo. Jana asubuhi tumeona picha za mastaa Simba na Yanga wakiwa uwanja wa ndege kwa ajili ya kwenea kujiunga na timu zao za taifa. Kama wachezaji wanacheza katika timu za taifa za Congo, Zambia, Uganda, Senegal, Mali basi ni wazi kwamba wana hadhi ya kucheza robo fainali na kudaiwa ushindi. Wakati nikiamini kitu kizuri kwa Simba ni kuikwepa Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, binafsi naamini kitu kitu kwa Yanga ni kuikwepa timu ya Pyramids ya Misri. Ni kweli hawa hawapo katika hadhi ya Zamalek wala Al Ahly lakini bado wanabakia kuwa timu ngumu na inayocheza katika Ligi ngumu na yenye ushindani."