Kipa Simba ampa tano Diarra

Mwanaspoti
Published: Jun 01, 2023 13:12:41 EAT   |  Sports

ACHANA na matokeo ya Yanga dhidi ya USM Alger kubwa ni kipa wa zamani wa Simba na timu ya Taifa, Taifa Stars, Kelvin Mhagama amesema makipa wa Tanzania wana vitu vingi vya kujifunza kutoka kwa nyanda wa Yanga Djigui Diarra. Diarra amekuwa kipa namba moja katika kikosi cha Yanga na ameiwezesha timu hiyo kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara pamoja na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho na la Azam Sports Federation( ASFC). Mhagama ambaye amewahi kuzidakia pia timu za Rayon na Polisi za Rwanda alisema, Diarra ana uwezo mkubwa langoni na magoli anayofungwa ni ya makosa ya kibinadamu. Alisema uwezo wake wa kucheza na miguu, kucheza ndani ya 18 na kuwapanga mabeki, makipa wa Bongo wanatakiwa kujifunza kutoka kwake. “Naamini Metacha Mnata na makipa waliopo pale Yanga watakuwa kila siku wanaendelea kujifunza lakini kubwa makipa wa Bongo nao wajifunze yule ni zaidi ya somo na kuna wakati nasema yupo Bongo kwa bahati mbaya,” alisema kipa huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar. Kuhusu mechi dhidi ya USM Alger, alisema bado haijaisha kwani katika soka kila kitu kinaweza kutokea kikubwa ni kujipanga na kucheza kwa kushambulia. “Wajipange, soka limebadilika unaweza kupata matokeo popote lakini ni lazima waongeze idadi ya washambuliaji, pia wacheze kwa tahadhari maana unaweza kukuta unamfukuza mwizi huku nyumbani umeacha mlango wazi,” alisema kipa huyo wa zamani ambaye amewahi kuifundisha CDA ya Dodoma.