KIJIWE CHA SALIM SAIDI SALIM: Vikapu vya magoli vya kutosha

Mwanaspoti
Published: Mar 24, 2023 12:32:54 EAT   |  Sports

KILA mchezo una rekodi zake, lakini baadhi ni kubwa na za aina yake. Mara nyingi kila napozitafakari rekodi za dunia za michezo zipo ambazo hunishangaza na kukataa kuziamini. Hatimaye baada ya kuhakikisha ni za kweli hujiliwaza kwa kujisemea mtu hatakiwi kufanyia mchezo mambo ya michezo. Baadhi ya rekodi unaposimuliwa habari zake unabaki kutabasamu na kujiuliza ilikuwaje hata ikatokea hivyo, jibu lake ni jepesi. Nayo huipati na unabaki kufurahi na kucheka na kama ukiwa umekaa peke yako pembeni anayekuangalia atajisemea nadhani yule jamaa waya mmoja kichwani umefyatuka. Miongoni mwa rekodi ambazo sidhani zitavunjwa ni za mchezo wa mpira wa magongo katika uwanja wa barafu kwa wanawake. Katika mashindano ya Bara la Asia na Oceania yaliyofanyika Latvia 1998, wachezaji wanawake wa chini ya miaka 18 wa Korea Kusini waliwachapa wenzao wa Thailand 92-0. Wachezaji na viongozi wa Thailand waliporudi nyumbani kila mmoja alipewa zawadi ya nyanya 92 zilizowekwa vizuri katika paketi iliyoandikwa 'Ahsante’. Shirikikisho la Kimataifa la Mchezo wa Magongo katika Barafu lilisema hii ni rekodi ya dunia ya mabao mengi katika mchezo huu kwa kinamama. Rekodi nyingine ni ya wanawake wa Slovakia kuwafunga wenzao wa Bulgaria 82-0 (narudia 82-0) katika pambano la kutafuta tiketi ya kucheza fainali za michezo ya Olimpiki. Slovakia walisukuma mikwaju 130 golini na kufanikiwa kupata idadi hiyo ya mabao ambayo ni ya wastani wa bao moja baada ya kila sekunde 44. Bulgaria walihemewa kama vile walifungwa pingu za miguu na kutoweza kuwazuia wapinzani wao ambao waliwatawala kwa mbio, mbinu na ustadi. Bulgaria iliongoza 7-0 dakika tano baada ya mchezo kuanza, 19-0 baada ya dakika 10 na 31-0 kilipomalizika kipindi cha kwanza. Kikosi cha Bulgaria pia kilifungwa 30-1 na Croatia na pia 41-0 na Italia katika michezo mingine ya kundi hilo. Vioja vya aina hii ni maarufu katika soka. Kwa mfano Abroath iliifunga Bon Accord 36-0 baada ya kuongoza 15-0 wakati wa mapumziko katika ligi ya Scotland 1885. Kule Madagascar yalifanyika mambo sio ya kawaida Oktoba 31, 2002 na tangu wakati huo siku hiyo hukumbukwa kwa tamasha linalohimiza mchezo safi na usio na uhuni. Hii ilitokana na burudani usiyoweza kuilinganisha na nyingine ya mchezo huu duniani ya klabu zenye utani wa jadi na uhasama katika nchi hiyo. Klabu hizo ni AS Adema na SO Emyrne zote za jijini Antananarivo ambazo zilipokutana kwa mchezo wa mwisho uliokuwa uamue ipi ni bingwa ya nchi hiyo. Mchezo huo uliokuwa na vioja ulimalizika kwa Adema kushinda 149-0 na hii ndio idadi kubwa ya mabao kufungwa katika mchezo wa kandanda duniani. Timu hizo miaka michache iliyopita zilikubaliana kukutana kwa mchezo wa kirafiki kuikumbuka siku ile iliyozusha kichekesho na hasira miongoni mwa viongozi na mashabiki wa kandanda. Katika tamasha hilo hutolewa fulana na beji zilizoandikwa 149 -0. Wageni wanaoalikwa katika mchezo huo ni pamoja na wale waliofanya ule mkasa wa mwaka 2002. Kilichotokea ni timu hizo mbili mara baada ya kuingia uwanjani viongozi na wachezaji wa Emyrne walimkataa mwamuzi Benjamina Razafintsalama. Ombi lao lilikataliwa na shirikisho la kandanda la nchi hiyo na baada ya uamuzi huo Emyrne walikubali kucheza, lakini walifanya mambo sio ya kawaida. Watazamaji wengi walikasirika, lakini watoto walifurahia mvua ya mabao na wakati watoto walipofurahia mashabiki walivunja viti, milango na vifaa vya uwanja wakidai kurejeshewa fedha. Hii ni kwa sababu walitarajia mchuano mkali ambao ulikuwa uamue timu ipi iwe bingwa na ipi ishike nafasi ya pili. Lakini tangu ilipopulizwa filimbi ya kuanza mchezo wachezaji wa Emyrne walisimama kama nguzo hawakuhangaika na waliwaachia wapinzani wafunge mabao kwa raha zao. Wapinzani walipokawia kufunga bao wachezaji wa Emryne waliukimbilia mpira na kwenda kujifunga wenyewe. Wachezaji wawili walibaki kwenye goli wakati wote kuhakikisha wapinzani wao hawapuliziwi filimbi ya kuotea walipokwenda kufunga bao. Kila walipofungwa bao waliruka na kupiga makofi kushangilia kama vile wao ndio walifunga na kujihakikishia kuwa mabingwa. Mpira ulipowafikia miguuni waliwapa pasi haraka wapinzani na kuwahimiza waende kufunga bao. Kipa sio tu hakujaribu hata mara moja kuuzuia mpira usingie golini, bali alisaidia kuusindikiza wavuni na haraka kuupeleka kati ili wafungwe mabao zaidi. Shirikisho la Kandanda la Madagascar lilimfungia kocha Zaka Be kwa miaka mitatu na alipohojiwa aliomba adhabu yake iongezewe sifuri mbele ili isomeke 30. Tangu siku ile ikitokea timu ya Madagasacar kumkataa mwamuzi shirikisho la kandanda lilimbadilisha haraka kwa kuhofia kutokea mkasa uliofanywa na Emyrne. Michezo mingine iliyokuwa na vituko ni ya ligi ya daraja la kati ya Nigeria iliyochezwa Julai 7, 2013 kati ya Plateau United Founders na Akurba FC na Police Machine FC dhidi ya Bubayaro FC. Plateau ilishinda mabao 79-0 na Police kushinda 67-0 na kuiwezesha Plateau United kupanda daraja kwa idadi kubwa ya mabao ya kufunga. Katika michezo yote miwili zaidi ya nusu ya mabao yalifungwa na wenyewe wachezaji. Aprili 11, 2001 Australia na American Samoa zilipambana katika mchezo wa kutafuta tiketi ya fainali za Kombe la Dunia 2002. Kwa ujumla mchezo wa kandanda huwa na vituo ambavyo huvitegemewi. Suala linalouulizwa ni kituko gani kipya kitaonekana siku za mbele.