Kanoute arudi Mali, aitega Simba

Mwanaspoti
Published: Jun 01, 2023 12:55:23 EAT   |  Sports

SIMBA ina kazi kubwa mbele yake, wakati inapambana kusajili mastaa wapya wa kuongeza nguvu kikosini, ina mtihani wa kumbakiza kiungo wao mkabaji Sadio Kanoute aliyetoa sharti gumu la kuendelea kuchezea klabu hiyo. Taarifa ya uhakika inasema Kanoute kamaliza mkataba na Simba na yupo nchini kwao Mali, wakati viongozi wanamtaka wakae mezani ili kumpa kandarasi mpya, akawatajia mamilioni ya pesa ikawabidi warudi nyuma kwanza kuvuta pumzi. Chanzo cha taarifa hiyo kinasema "Kanoute ametaja pesa ambayo haikutarajiwa, sasa ilibidi apewe kazi Mels Daalder ambaye ni skauti mkuu ili azipitie kazi za mchezaji huyo kama atafaa kuisaidia klabu ndipo waanze kufanya makubaliano naye. "Wanasubiri Daalder afanye tathimini ya kazi yake aliyoifanya kwa msimu, kisha wajue kipi kitafuata kwa mchezaji huyo, lengo kubwa ni kuhakikisha timu inakuwa na wachezaji wa viwango vya juu watakaofanikisha malengo makubwa. Katika mahojiano ya kocha wa timu hiyo, Roberto Oliveira 'Robertinho' na mitandao ya klabu hiyo, alisema "Kila nafasi anahitaji wachezaji wawili wanaolingana uwezo, mfano wa Mzamiru Yasin akikosekana, Kanoute anafanya jukumu kikamilifu, hivyo nahitaji kila anayesajiliwa awe kwenye kiwango kikubwa." Kwa upande wa Kanoute alisema "Hadi sasa mkataba umemalizika nipo kwetu kwa ajili ya mapumziko, bado hatujafanya mazungumzo yoyote na waajiri wangu." Kwa kauli ya kocha itawalazimu viongozi wa Simba kufanya jitihada za kuhakikisha Kanoute anasalia kikosini, kwani anaona eneo hilo wanalitendea haki akiwa na na Mzamiru.