KANIKI: Simba haijafeli kuna mapungufu madogo madogo

Mwanaspoti
Published: Jun 02, 2023 15:44:56 EAT   |  Sports

MATATIZO ya mikataba kwa wachezaji na waajiri wao haikuanza miaka ya hivi karibuni bali hata miaka zaidi ya 10 nyuma ilikuwepo. Na hii ni kutokana na wachezaji kukosa uelewa wa mikataba inavyoeleza ama wanaowasimamiza kutozingatia baadhi ya vipengele kwenye mikataba hiyo na kikubwa wanachoangalia ni pesa iliyoandikwa kwenye makaratasi hayo ya kisheria. Hivi sasa sakata la kimkata linaloendelea ni kati ya kiungo wa Yanga, Feisal Salum 'Fei Toto' na mwajiri wake huyo. Fei anapigania kuvunja mkataba kwa madai ya maslahi na pia hana furaha ndani ya klabu hiyo lakini njia aliyotumia viongozi wake hawajaikubali. Mabosi wake wanamtaka aende mezani apeleke ofa ya timu inayomuhitaji ili auzwe jambo ambalo kwake limekuwa gumu na sasa anataka kwenda CAS kufungua kesi ya kuvunja mkataba wake huku Yanga nao wakimshitaki kwenye Kamati yao ya Nidhamu kwa utovu wa nidhamu kwani hayupo kazini na aliwahi kuitwa mara kadhaa arudi kwenye kituo chake cha kazi. Huko nyuma, mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, Joseph Kaniki 'Golota' naye aliwahi kugoma kusaini mkataba mpya Simba aliodai kuwa haukuwa na maslahi mazuri kwake. Lakini Kaniki alifanya hivyo baada ya mkataba wake wa awali kumalizika kitu ambacho ni tofauti na Fei ambaye mkataba haujamalizika na anataka kuuvunja akiwa ndani ya mkataba baada ya kuona hauna maslahi mazuri kwake. Kaniki alivyogoma kusaini aliamua kutimkia Mtibwa Sugar huku akiwa amechukuwa kiasi fulani cha pesa kwa Simba, yaani pesa ambayo walimpa kwa makubaliano kuwa nyingine atamaliziwa akisaini. "Unajua kama unajiamini na kipaji chako huwezi kusaini mkataba mrefu, maana utakubana pale ambapo utahitaji kuondoka ama kutamani maslahi yaongezwe, mimi nilikuwa sitaki mikataba mirefu kwani wakati mwingine ina usumbufu. "Mkataba ulipomalizika Simba walinipa ofa nyingine ambayo sikuikubali, niliwagomea kusaini mkataba mpya, walinipa pesa kiasi kwamba nyingine nitapewa baadaye lakini sikuona sababu ya kuendelea kuwepo hapo nikaenda Mtibwa Sugar." anasema Kaniki na kuongeza; Kaniki amezungumza hayo pamoja na mambo mengine ya kisoka alipokuwa anacheza ndani na nje ya nchi katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. "Nafurahi kukutana nanyi, ila naweza kusema nimekuheshimu sana pamoja na gazeti hili, huwa sipendi kufanya mahojiano kwasababu muda wangu wa ustaa uliishapita, sasa wapo wengine, tunataka kuwasikia hawa wapya." ilikuwa ni kauli ya staa huyo wa zamani kwenye mahojiano kuanza SIMBA HAWAJAFELI Kabla ya yote Kaniki anazungumza timu yake ya zamani ya Simba ambayo imekuwa ikifanya vizuri kwenye michuano ya Kimataifa ingawa kwa misimu miwili haijafanya vizuri ligi ya ndani. "Kama timu ina uwezo wa kufika hatua kubwa ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanasemaje kuwa wamefeli, kuna mapungufu tu madogo madogo ambayo hayawezi kuifanya Simba ionekane imefeli. Kufika hatua hiyo CAF si jambo dogo na wala si rahisi. "Ikumbukwe kwamba ubora wanaoupata Yanga sasa umechangiwa pia na ubora uliokuwa nao Simba miaka kadhaa nyuma, Yanga walikuwa wanawasoma Simba wanafanya nini hadi wanafanikiwa, Yanga wamedumu na kocha wao Nabi kwa kipindi kirefu amesoma timu yake inahitaji nini. "Lakini Simba wakaja wakasajili wachezaji wengine ambao hawatumiki, waliwasajili wa kazi gani, wanapaswa kusajili mchezaji ambaye anatumika moja kwa moja, aliondoka Larry Bwalya hadi leo sioni nani mbadala wake, walete wachezaji wa kuwasaidia kwani hawako vibaya sana, sasa hivi wawe makini kwenye usajili," anasema Kaniki Mkongwe huyo pia anasengumzia kati ya timu ambazo amecheza hapa nchini kuwa; "Mimi nimecheza timu nyingi, hapa nchini nimecheza timu nne, Lipuli, Kariakoo Lindi, Simba na Mtibwa Sugar, nikaenda Rwanda (Rayon Sports), Uarabuni na Sweeden. Lakini kwa hapa Simba na Mtibwa tofauti ni mashabiki tu. "Simba ina mashabiki wengi kutokana na ukubwa wake lakini miaka hiyo nacheza kiuwezo Simba na Mtibwa zilikuwa sawa, maana Mtibwa nayo ilikuwa na kikosi bora kabisa." anasema Kaniki anayejulikana pia kwa jina la utani la Golota. Golota alipewa na Marehemu Syllersaid Mziray akimfananisha na bondia mmoja wa Afrika Kusini MAYELE, JOB WAPEWE MAUA YAO Fiston Mayele ndiye kinara wa mabao wa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao 17 na ana mechi mbili mkononi lakini pia ni kinara wa mabao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika akifunga saba na mechi moja mkononi. Kaniki anawazungumzia Mayele na Dickson Job. "Kuna wachezaji wengi wazuri, wapo wengi sana lakini kati yao naweza kusema Job na Mayele ni bora zaidi. Job ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi na anaweza akapangwa kama beki ya kati na kulia na akacheza kwenye ubora ule ule, hapungui ubora. "Mayele alichokifanya msimu uliopita na anachokifanya sasa huwezi kuacha kukubali kuwa ni mchezaji bora. Mayele anacheza kwa kujitoa, anajitoa kwa ajili ya timu unamuona kabisa kuwa amekuja kutafuta mafanikio. Na hata leo hii ukisema nichague mchazaji bora basi Mayele na Job siwezi kuwaacha kuwachagua, wanastahili, pia Clatous Chama pia anastahili ila ameingia doa ana kadi hivyo hamalizi ligi." MECHI YAVUNJIKA Anakumbuka 2001 mechi yao na Ismailia iliyochezwa Uwanja wa Uhuru (Shamba la Bibi) kuwa; "Aisee nilikuwa nafanya mazoezi sana ya kocha na yale ya programu zangu, nakumbuka na sitasahau bao nililowafunga Ismailia maana nilipiga shuti kuanzia katikati ya uwanja hadi golini. "Kwenye mechi hiyo ambayo ilikuwa ya CAF nilifunga mabao mawili na moja alifunga Shekhan Rashid kwa penalti, hadi tunaenda mapumziko tulikuwa tunaongoza mabao 3-0, baada ya kutoka mapumziko mwamuzi alivunja mechi kwa madai kuwa uwanja umejaa maji. "Mvua ilinyeesha ya kawaida tu, sema kulikuwa na fitina sana kwa Waarabu, uwanja ulikuwa unaweza kuchezeka tu ila mwamuzi alivunja mechi, mechi ilirudiwa siku nyingine tuliwafunga tena bao 1-0, bao nililifunga mwenye lakini tukawa tumetolewa maana mechi ya kwanza walitufunga kwao mabao 2-0. "Fitina zilikuwa nyingi kwasababu mpira ulikuwa hauonyeshwi kwenye televisheni na timu zetu hazikuwa vizuri kiuchumi hivyo haikuwa rahisi kushindana na mwarabu kwenye fitina maana wao wana pesa. "Siku hizi fitina sio nyingi, mpira unaonyeshwa kwenye televisheni pia Ligi yetu imekuwa kubwa kwani wadhamini wapo hivyo kiuchumi hatuko vibaya, timu zikisafiri kwenda nje zina uwezo wa kusafiri na vyakula vyao na maji, zikajiandalia mazingira mazuri ya ugenini wenyewe. "Kanuni za CAF ni kwamba mwenyewe anatakiwa kukuandalia kila kitu hapo ndipo fitina zilikuwa zikifanywa sana, tofauti na sasa kanuni hiyo ipo lakini uwezo wa timu kujiandalia mazingira yao wanafanya wenyewe, haikatazwi," anasema Kaniki WANYIMWA ZAWADI YA UBINGWA "Kutokana na ukata uliokuwepo enzi zetu kwa maana ya kwamba wadhamini hawakuwa wengi, tuliwahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu 2001 lakini hatukupewa zawadi ya ubingwa hadi leo. "Ni kwasababu mdhamini wa wakati huo aliishia njiani kwani ilielezwa kuwa makubaliano na malengo ya mkataba ilikuwa ni Sita Bora watoe Sh 30 milioni kwa bingwa ila haikuwa hivyo wakajitoa. "Kwenye ligi nzima nilikuwa mfungaji bora nilifunga mabao 15 nilipata Sh 1 Milioni, ila hatua ya Sita Bora tulikuwa wachezaji watatu wote kutoka Simba, mimi, Emmanuel Gabriel 'Batgol' na Nteze John ila hatukupa kitu maana mdhamini alikuwa amejitoa tayari." NI KOCHA "Kwa sasa ni kocha, nina leseni Diploma D na C sasa nasubiri kusoma Diploma B maana hii unatakiwa ukae mwaka mmoja ndipo uisomee, tatizo lililopo ni kupata sehemu ya kufundisha kwa maana ya timu, ndiyo maana utaona Tanzania ina makocha wengi lakini wana vyeti vyao nyumbani. "Nadhani hapa hatuaminiani hata timu za madaraja ya chini, ili tukatoe ujuzi wetu huko, ukiona mchezaji wa zamani anasomea ukocha ujue ana kitu cha kutoa kwa jamii ya soka, maana anaujua mpira ulivyo kwani anakuwa ameucheza. "Hata nilipokuwa Ulaya nilikuwa nikifundisha kama kocha msaidizi kwenye vituo vyetu maana wenzetu wameendelea tofauti na hapa, hivyo nilikuwa na programu zangu ambazo natamani ningekuwa nazitumia hapa kuwapa ujuzi wachezaji wetu," anasema Kaniki na kuongeza; "Ulaya kuna vituo vingi na hata klabu zina akademi zake, viwanja, mashule inakuwa rahisi kwa makocha kupata ajira, huku unakuta makocha wapo mtaani hata timu za daraja la tatu hawapati nafasi ya kufundisha, ni changamoto sana unaishia kujitolea tu. Makocha wana vitu vingi lakini hakuna pa kuvipeleka." YANGA NAO WALIMTAKA "Mpira wangu wa ushindani nilianzia Lipuli baadaye nilienda Kariakoo Lindi, na nimecheza hata Ligi Daraja la Kwanza (Championship) nimeenda Simba nikiwa na miaka miwili kwenye ligi, hivyo Simba hawakunitoa kisoka kwani tayari nilikuwa nimeishatoka. "Unajua nilipokuwa Lipuli timu zote hizo zilikuwa zikihitaji huduma yangu lakini sikukubali kwasababu haukuwa muda muafaka wa mimi kuzichezea timu hizo, Simba ilikuwa inafukuza sana wachezaji wakati Yanga ilikuwa vizuri sana hata kiuchumi. Nilijipa muda zaidi. "Nilienda Kariakoo Lindi, huku nilishiriki ligi pia na niliwafunga Yanga nje ndani kwenye mashindano maana tulipangwa kundi moja, hapo sasa Simba wakarudi tena huku Yanga nao kupitia Francis Kifukwe wakaibuka tena maana nao tangu nikiwa Lipuli walinihitaji, aisee nilienda sana ofisini kwa Kifukwe lakini bado sikuona namna ya mimi kucheza Yanga maana nafasi yangu pale ingekuwa ngumu kutoboa. "Nilipo nilipokubali kusaini Simba ambako haikuwa ya moto sana na sikuanza kikosi cha kwanza moja kwa moja, nilikuwa naanzia benchi wakati huo kocha alikuwa ni Marehemu Mziray, ili muda niliokuwa napewa kucheza nilifanya jambo kubwa, na tuliwafunga Yanga kwa penalti, hapo ni kujituma tu. "Nilijiunga Simba wakati wanashiriki Kombe la Nyerere, sikuruhusiwa kucheza ligi kwasababu tayari nilikuwa nimecheza nikiwa na Kariakoo Lindi sheria hazikuruhusu, Simba niliwakuta pia mastaa kama akina George Masatu, Madaraka Seleman na wengine kibao tulitwaa ubingwa na kushiriki Kombe la Washindi na CAF." anasema Kaniki SIANG'A BABA LAO "Kama nilivyosema kuwa ubora wangu haukuanzia Simba tu, nilitoka nao Lipuli lakini baada ya kuja kocha Marehemu James Siang'a huyo sasa alinifanya niimarike zaidi, mbele ya Siang'a kama unafanya vibaya hawezi kukuacha nje, alimwamini kila mchezaji anayefanya vizuri, hivyo tangu uwepo wake nilicheza kikosi cha kwanza. "Kila kocha ana mifumo na salsafa zake huku akisimamia kile anachokiamini, hivyo hata kwa Marehemu Mziray kutonianzisha kikosi cha kwanza ulikuwa ni mfumo wake tu alioutumia ndio maana alinianzishia benchi, pia sitaacha kumshukuru kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio' alifanya kazi kubwa sana kwangu ya kisoka ikiwemo ushauri." MABEKI/PACHA "Kutokana na ubora wa Simba kwa wakati huo sikuwahi kupata tabu yoyote kutoka kwa mabeki wa timu pinzani, tulicheza kwa umoja zaidi na timu ilikuwa imara, kila mchezaji alijitoa kuipambania timu. "Nilifurahia kucheza na mchezaji yoyote lakini nikicheza na Shekhan nilifurahia zaidi kwasababu pasi zake zilikuwa zinafika kwa usahihi, alirahisisha kazi ya kufunga pamoja na Nteze." anasema KINACHOWAKWAMISHA NJE "Wengi wanaamini kucheza nje ni lazima utoke Simba au Yanga, kitu ambacho sio sahihi, mimi kwenda nje sikutokea Simba, nilitokea Mtibwa na hata hao Simba nilipokataa kusaini mkataba walijua nitashindwa kwenda kucheza soka la kulipwa. "Lakini kinachowashinda wengi kufanya vizuri nje na kurudi ni mazingira magumu, hali ya hewa, wengine hawako fiti kwa maana mazoezi wanayopewa hapa tofauti na kule ukilinganisha pia na vyakula wanavyokula miili yao haiwi fiti kucheza kwa kiwango bora. Ukishindwa kumudu mazoezi lazima ushindwe. "Wanatoka mazingira ya joto wanakwenda kwenye baridi, hawawezi kuvumilia hilo, wenzetu wanafanya mazoezi kweli kweli ndio maana miili yao iko imara wakati wote. Mimi niliweza kwasababu tayari nilikuwa profeshono kwani nilicheza Rwanda na Uarabuni, hivyo mazingira kwangu hayakuwa magumu na nilivumilia changamoto zingine." KIBALI CHA KUISHI ULAYA Anasema muda wowote ana uwezo wa kwenda Ulaya kwani tayari ni mwanafamilia wa nchi hiyo; "Ulaya kwangu ni kama nyumbani kwani nina kibali cha kuishi huko naishi kama raia wa huko, huwa narenew kila baada ya miaka sita, hivyo muda wowote naruhusiwa kwenda bila pingamizi." anaeleza KUSTAAFU Majeraha ndiyo yaliyopelekea kustaafu soka, yeye anaelezea zaidi; "Nilipokuwa Mtibwa Sugar niliumia msuli wa nyuma ya mguu wa kulia, nadhani sikupata matibabu mazuri hivyo nilipoenda Ulaya ambako nilikuwa naichezea timu ya Konyaspor walinifanyia uchunguzi na kubaini kwamba nahitajika kufanyiwa upasuaji, nilifanyiwa na kuambiwa natakiwa kukaa nje kwa miezi 48 (miaka minne) na huo ndio ukawa mwisho wangu wa kucheza soka la ushindani. "Lakini utaratibu wa wenzetu huko kuna bima ya maisha, hivyo ilikuwa ni rahisi kwangu na walinilipa kwa kipindi chote nilichokuwa nje ya uwanja, hii pia ilisaidia kwa vile kibali changu kinaniruhusu kuishi nchini humo kama raia wao." KIKOSI CHAKE Anataja kikosi chake cha wakati wote kuwa ni Mohamed Mwameja, Said Sued, Boniface Pawasa, Seleman Matola, Huresh Ufunguo, Shekhan, Emmanuel Gabriel, Abdi Said, Nteze na Madaraka Seleman. "Kwa ufupi ile timu ambayo ilitwaa ubingwa 2001 na 2002. CAF tulicheza sana lakini hatukufikia hatua hii ambayo Simba ya sasa inafika, sababu ni zile zile uchumi wetu ulikuwa mdogo ingawa timu zilikuwa nzuri, hivyo tulihujumiwa sana. Mashindano makubwa kwetu yalikuwa Kombe la Kagame. "Lakini ukija upande wa Stars, ile Stars yote ya Mercio Maximo ilikuwa bora sana, imeacha historia kubwa kwangu binafsi ilitupa pesa na tulisafiri nchi nyingi ambazo sikuwahi kufikiria kama ningeenda, kuna ile Stars ambayo tulicheza michuano ya Kombe la Castle 2001." WACHEZAJI WA KIGENI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliruhusu klabu za Ligi Kuu Bara kusajili wachezaji 12 wa kigeni na wote wanaruhusiwa kucheza katika mechi moja na haijalishi hata kama kikosi kizima kocha anapanga wageni. Kaniki anazungumzia juu ya uwepo wa wachezaji wa kigeni; "Wageni wanachangamsha ligi, wanafanya vizuri hivyo lazima wazawa wapate changamoto pia klabu zina kila sababu ya kusajili wageni ambao watakaocheza kwa kiwango kikubwa, pia wazawa waamke, wajitume naamini nao ni bora kwani kuna wazawa wanafanya vizuri sana kama Mzamiru Yassin wa Simba, kuna Job (Yanga) na wengine baadhi wanaojitambua wanafanya nini, wawe na wivu wa maendeleo. "Ndio maana unaona ni wachezaji wachache sana wa zamani wenye mafanikio makubwa ukilinganisha na sasa hivi, ila unajiuliza kwanini hawadumu muda mrefu kwenye soka, lazima wajitambua mpira sasa una pesa." Kaniki anaeleza pia mabadiliko ya soka nchini kuwa; "Soka la sasa hivi limebadilika kutokana na udhamini uliopo huwezi kulinganisha na wakati tulipokuwa tunacheza, ilikuwa ni kwa ridhaa zaidi, sasa hivi soka linaelekea kuwa la kulipwa hapa kwetu."