JKT Queens yaendeleza rekodi, Simba yashushwa

Mwanaspoti
Published: Mar 22, 2023 16:18:00 EAT   |  Sports

Dodoma. JKT Queens imeendeleza rekodi ya kutopoteza mchezo ya Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) mara baada ya kuifunga Baobab Queens kwa mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika jioni ya leo katika uwanja wa Jamhuri. JKT iliwachukua dakika 29 kupata bao la kuongoza lilofungwa na Jackine Shija kwa shuti la karibu mara baada ya mabeki Neema Charles na Neema John kushindwa kuokoa mpira mrefu uliopigwa na kiungo,Donesia Minja. Bao la pili lilifungwa na winga Zabela Mbwale huku la tatu likifungwa na mshambuliaji hatari Stumai Abdallah mara baada ya kuwazidi mbio mabeki wa Baobab Queens. Kivutio katika mchezo huo alikuwa kiungo wa JKT Queens,Donasia Minja ambaye alionesha uwezo mkubwa na kuwapoteza viungo wa Baobab Queens,Halimab Mwaigomele na Josephine Julius. Katika michezo mingine,Yanga Princess imetoka sare ya kufungana bao 1-1 na Simba Queens,huku Fountain ikifunga Mkwawa Queens kwa mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika katika Chuo cha Mkwawa mkoani Iringa. Ceasiaa Queens wameibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Amani Queens katika mchezo uliofanyika mkoani Lindi. Zifuatazo ni dondoo muhimu za mchezo huu. Kipa wa JKT Queens,Najiath Abasi amefikisha Cleensheet saba msimu huu akimpita Monica Chebet wa Fountain Gate Princess mwenye sita. Bao la winga wa JKT Queens,Jacline Shija ni la tano (5) kwake msimu huu kinara kwa ufungaji katika timu hiyo akiwa ni kiungo Donesia mwenye mabao 9. Beki wa kati wa Baobab Queens,Neema Charles ameendeleza rekodi yake ya kuanza michezo yote 12,tisa ya mzunguko wa kwanza na mitatu mzunguko wa pili. Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza JKT Queens waliibuka na ushindi wa mabao 3-0,mchezo uliofanyika katika uwanja wa Meja General Isamuhyo mkoani Pwani. Kwa matokeo hayo JKT imefikisha pointi 28 ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo huku Fountain ikiongoza kwa kuwa na pointi 29. Huu ni ushindi wa nane (8) kwa timu hiyo,msimu huu huku Fountain ikishinda tisa na Simba Queens nane Baobab Queens imeruhusu mabao 15 katika michezo 12 huku ikifunga mabao 13.