Geay apata Sh200 milioni kwa saa mbili

Mwanaspoti
Published: May 31, 2023 13:53:58 EAT   |  Sports

JANA, tuliishia sehemu ambayo Geay anazungumza kuhusu mbio za Boston ambazo zimempa umaarufu mkubwa, leo anaendelea kuzungumza kuhusu mbio hizo, na bei ya kiatu alichovaa siku hiyo. KUHUSU FEDHA ALIZOPATA KWENYE BOSTON “Mara nyingi fedha kwenye mashindano haya zinaonekana, mimi nilipata kiwango cha fedha, siyo kikubwa lakini kwangu siyo kidogo kwani nilipata nafikiri milioni 150, ukichanganya na bonasi na fedha nyingine za mikataba, ilifika milioni 200, kumbuka hii ni kwa saa mbili tu ambazo nilikimbia pale. “Hiki kwangu ndiyo kiwango kikubwa zaidi kuwahi kushika kwa mara moja, nimewahi kushika fedha nyingi zaidi lakini siyo milioni 200 kwa mara moja, zimenisaidia kutimiza baadhi ya malengo yangu muhimu kwenye maisha. “Huko mbeleni kuna mambo nataka kufanya, ili kufanikisha hili ni lazima nianze kupata kidogokidogo kama hivi na malengo yangu mengine nayoana kama vile yapo njiani kutimia. AVAA LAKI NNE MGUU KWAKE Moja ya mambo ambayo yaliteka mitandao mingi ni viatu ambavyo alivyovaa kwenye mbio za Boston ambapo vilikuwa vinatajwa kuwa ni vile ghali zaidi kwenye riadha, wakati anataka kujibu kuna jambo linatokea “Wewe hairuhusiwi kupita na pikipiki hapa, hapa ukipita hutakiwi kuendesha unatakiwa kukokota hivyo shuka Sukuma hadi umalize sehemu ya uwanja hii ni hatari sana kama utawakuta watu wanafanya mazoezi,” alisema mmoja wa makocha ambao walikuwa hapo uwanjani baada ya jamaa mmoja kuja na bodaboda yake kwa spidi kali. Tunaendelea: “Viatu vya riadha mara nyingi vinakuwa ghali kutokana na jinsi ambavyo vimekuwa maarufu kutokana na wale ambao wamevaa wamepata mafanikio gani, mfano kiatu kama alivyoo Usain Bolt lazima kitauzwa ghali kwa kuwa ana mafanikio makubwa kwenye mchezo huu. “Mimi nakumbuka nilivaa kiatu cha Kampuni ya Adidas (tutazungumza mbele kuhusu kampuni hii na Geay), ambacho niliagiza kutoka nje na kilikuwa shilingi laki nne, sijui wengine walivaa cha shilingi ngapi lakini kwangu naona kilikuwa bora na kilichangia pia kwenye mafanikio ya mbio hizi. “Huwa sivai tu viatu naangalia navaa cha namna gani na kipo vipi, lakini nazingatia zaidi kampuni iliyotengeneza kiatu hicho kwa sababu maalumu. ISHU YAKE NA BONGO ZOZO IKOJE? Bongo Zozo anitafuta baada ya Valencia Marathon, ambayo ilifanyika mwaka jana nilishika nafasi ya pili na kuweka rekodi ya nane duniani, baada ya kumaliza aliyenitangulia alikuwa Mkenya na alikuwa na bendera ya nchi yake akiwa anaipeperusha. “Mimi sikuwa na bendera nilitembea tu mwenyewe na hakupenda lile jambo, alinitafuta na kuniambia kwanini ilikuwa vile, nilimweleza akaumia, akasema kwa kuwa najiandaa na Boston basi atahamasisha watu kule ili waweze kunishangilia shangwe ziwe nyingi. “Baada ya hapo aliamua kufunga safari kutoka alipokuwa hadi kuja Arusha ambapo tulifanya maongezi kidogo na ndiyo mwanzo wa kuanzia kuniposti na kuniunga mkono kwenye mbio zile, aliwahamasisha watu na walikuja wengi kwa kweli. “Alikuwa wa kwanza kusema kuwa anaamini nakwenda kufanya mambo makubwa kwenye mbio zile, wengi hawakuamini kuwa naweza kushinda lakini yeye alikuwa kila wakati anaamini hivyo na kuwaambia watu na mimi mwenyewe. “Nakumbuka ndiyo mtu ambaye aliniposti mara nyingi kuliko wengine, hata wakati nakimbia nilijiona siko peke yangu, nilijua kuna watu wanasubiria pale ninapomalizia sitakiwi kuwavunja moyo kwa kuwa walikuwa na Imani kubwa sana name na nilijua kuwa kuna Watanzania wanafuatilia kupitia wao, nashukuru Mungu nilifanya vizuri na pale mwisho niliwaona nao wakiwa na furaha kupita kiasi. “Bongo Zozo kwangu ni mtu ambaye amefanya hamasa kubwa kwenye mbio zile na watu wengi walifahamu kupitia kwake na naona ni mtu ambaye anaipenda Tanzania, nakumbuka kuna wakati alikuwa anapiga kelele kubwa hadi wazungu wakawa wanashangaa kufikiri labda ana tatizo kichwani. “Hizi ndiyo mbio za nje ya nchi ambazo niliona bendera nyingi zaidi za Tanzania, siku hiyo kweli nilijiona nina watu kama ambavyo wamekuwa wakifanyiwa wanariadha wengine, kila siku amekuwa akinifuatilia kufahamu baada ya zile nakwenda wapi tena nafikiri anataka kuendeleza moto uleule. “Kama tukimtumia vizuri naona kuwa ni mtu ambaye yupo tayari kusapoti kila wanamichezo wa Tanzania, hivyo namshukuru kwa jinsi anavyojitoa. MWAKA HUU NAKIMBIA MARATHONI MOJA TU Geay anasema kwa sasa anafanya maandalizi kwa kuwa siku chache mbele atakuwa na mashindano ambayo anaamini kuwa anatamani kuyashiriki. “Mwaka huu nina mpango wa kukimbia marathoni moja tu mwaka mzima, kuna mashindano yanakuja yanaitwa World Athletic Championship yanafanyika Hungary haya kama nchi yangu ikiona nafaa kwenda nafikiri nitashiriki hapa tu, lakini kuna mashindano mengine makubwa huko mbele. “Lakini wakati nashiriki haya, nitachanganya na mbio nyingine fupifupi za kilomita 10, mfano mwezi wa sita ninakwenda tena Boston nimealikwa kushiriki mbio za kilomita 10, baada ya hizi nitakwenda Atalanta, hizi zote nitafanikiwa kupata kiasi cha fedha, siyo chini ya milioni 10 kwa kila moja siyo sawa na kukaa nyumbani, lakini pia ni mazoezi bora kwangu. “Hizi mbio zote nina historia nazo, nakumbuka nimewahi kushiriki na kushika nafasi ya kwanza miaka ya nyuma hivyo naamini nitafanya hivyo hivyo mwaka huu.