Firat: Wakenya tulizeni boli

Mwanaspoti
Published: Mar 22, 2023 15:26:22 EAT   |  Sports

KOCHA wa Harambee Stars, Engin Firat, amewataka Wakenya kuwa wavumilivu na kwamba mafanikio hayatakuja haraka kama baadhi yao wanavyodhani ila itamchukua muda kujenga timu ya taifa iliyo imara. Firat alipotua nchini kwa mara ya kwanza, alikaidhiwa mkataba wa muda mfupi lakini safari hii kocha huyo raia wa Uturuki anapewa mkataba wa miaka mitatu ambayo imempa fursa kuisoma historia ya soka la Kenya na kuja na mikakati ya kuipaisha. “Sitaki kuuza matumaini ya uongo,” alisema Firat kuhusu Stars kusajili matokeo chanya hivi karibuni. “Nahitaji muda wa kujaribu wachezaji, na kutafuta mbinu bora zaidi. Hili ndilo lengo letu pekee sasa, na tuko tayari kufanya hivyo lakini tafadhali tupatieni muda na tuwe wamoja.” Firat alisema inashangaza kwamba Wakenya kila mara wanatarajia timu kusajili matokeo mazuri, lakini hakuna juhudi za muda mrefu zilizowekwa ili kuwepo na kikosi cha kutisha. Alisema kukosekana kwa mechi bora kwa timu ya taifa na ubovu wa miundombinu ya michezo nchini pia kunasababisha Harambee Stars kuendelea kufanya vibaya. “Niliangalia historia ya Kenya na nikagundua haijawahi kucheza dhidi ya timu yoyote ya juu kutoka Ulaya. Huu ndio ukweli wa kusikitisha,” alisema Firat na kuongeza atahakikisha Stars inakabiliana na angalau timu moja bora kutoka Ulaya mwakani. Katika kufikia malengo yake ya kuiongoza Stars kupata matokeo chanya kwenye michuano mikubwa, kocha huyo mwenye umri wa miaka 52 alisema ana nia ya kuanzisha timu zenye nguvu za chini ya miaka 20 na 23, ambazo zitalisha timu ya wakubwa na wachezaji bora. Harambee Stars ipo kambini kujiandaa na mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Iran iliyocheza Kombe la Dunia mwaka jana nchini Qatar ikipangwa Kundi B pamoja na England, Wales na Marekani. Mchezo huu wa kirafiki unatarajiwa kupigwa Machi 28 mwaka huu jijini Tehran na hii ni baada ya gemu dhidi ya Burundi kuota mbawa.