Dakika 180 za mtego mastaa Prisons

Mwanaspoti
Published: May 30, 2023 16:06:40 EAT   |  Sports

WAKATI Ligi Kuu Bara ikitarajia kuendelea Juni 6, kocha mkuu wa Tanzania Prisons, Abdalah Mohamed ‘Baresi’ amekataa mapumziko na kutumia kipindi hiki kuwasoma nyota wake ili muda wa usajili ajue pakuanzia. Prisons haijavunja kambi ikiendelea kujifua kwa ajili ya mechi zake mbili zilizobaki dhidi ya KMC, Juni 6 na Yanga Juni 9 kumaliza msimu huu huku ikiwa na uhakika wa kubaki ligi kuu. Baresi alikabidhiwa kikosi hicho katikati ya msimu akichukua mikoba ya Patrick Odhiambo aliyefungashiwa virago kutokana na matokeo yasiyoridhisha kwa mabaosi wake. Kocha huyo aliliambia Mwanaspoti kuwa ameamua kuendelea na mazoezi ili kuangalia penye upungufu ili itakapofika kipindi cha usajili asipate tatizo wapi aongeze nguvu au kupunguza. Alisema kwa sasa ligi imefikia ukingoni na timu nyingi zinaanza kufanya tathmini ya kujua waboreshe maeneo gani, hivyo hata Prisons lazima iendane na wakati ili msimu ujao iwe bora zaidi. “Kwa sasa hatuzungumzi tena mambo ya msimu huu, ligi ni kama imeisha, hivyo lazima tutumie kipindi hiki kuangalia upungufu kutusaidia kipindi cha dirisha kubwa tuone pakuanzia,” “Timu nyingi zinafanya tathimini hivyo hata sisi wenye malengo ya mafanikio lazima tufanye mchujo kwa kupima kila uwezo na ubora wa mchezaji mmoja mmoja kujua msimu ujao itakuaje,” alisema Baresi. Hata hivyo aliongeza kuwa wakati wakisubiri ratiba ya mechi zilizobaki, timu hiyo itakuwa na mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Njombe kombaini watakaoupiga huko Makambako.