Chama aweka rekodi CAF, haijawahi kutokea Bongo

Mwanaspoti
Published: Mar 23, 2023 09:20:59 EAT   |  Sports

MABAO matatu aliyofunga dhidi ya Horoya, Jumamosi iliyopita katika ushindi wa mabao 7-0 wa Simba yamemfanya Clatous Chama kuandika historia mpya ambayo haikuwahi kuwekwa hapo kabla na mchezaji yeyote aliyewahi kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara. Rekodi hiyo iliyowekwa na Chama ni ile ya kuingia katika 10 bora ya wafungaji bora wa muda wote wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu yalipoanzishwa hadi sasa. Nyota huyo kutoka Zambia, kwa kufunga mabao matatu dhidi ya Horoya juzi amefikisha mabao 19 kuanzia ameanza kushiriki michuano hiyo ambayo yamemfanya ashike nafasi ya tisa katika orodha ya wachezaji waliofunga idadi kubwa ya mabao katika Ligi ya Mabingwa Afrika tangu mwaka 1964 ilipoanzishwa akiwa sawa na nyota wa zamani wa Sudan na Klabu za Al Hilal na Al Merrikh, Bakri Almadin na Emmanuel Osei Kuffour. Kati ya mabao hayo 19 aliyofunga, mabao 15 ameyafunga akiwa na Simba katika nyakati tofauti ambazo ameitumikia timu hiyo huku mengine manne akipachika wakati alipokuwa akichezea Zesco United ya Zambia. Katika msimu huu, amepachika mabao matano ambayo matatu ni dhidi ya Horoya, moja dhidi ya Vipers na lingine alifunga katika mchezo wa raundi ya pili dhidi ya Primiero Agosto. Msimu wa 2021, alifunga mabao matano ambayo ni katika mechi dhidi ya Plateau United, AS Vita, FC Platinum na Kaizer Chiefs na katika msimu wa 2018/2019, alifunga mabao matano ambayo ni katika mechi dhidi ya timu za Mbabane Swallows, Nkana na AS Vita. Orodha hiyo ya wachezaji 10 waliopachika idadi kubwa ya mabao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Chama anashika nafasi ya tisa, inaongozwa na staa wa zamani wa TP Mazembe Tresor Mputu mwenye mabao 39 akifuatiwa na Mohamed Aboutrika mwenye mabao 31 na anayeshika nafasi ya tatu ni Mahmoud El Khatib aliyefunga mabao 28. Flavio Amado anashika nafasi ya nne akiwa na mabao 27, anayefuata ni Emad Moteab aliyefunga mabao 24, Ali Zitouni yuko nafasi ya sita akiwa na mabao 23 sawa na Edward Sadomba. Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anashika nafasi ya saba akiwa na mabao 21 akifuatiwa na Dioko Kaluyituka na Mouhcine Iajour ambao kila mmoja amefumania nyavu mara 20. Nafasi ya 10 inashikiliwa kwa pamoja na wachezaji Gamal Abdel-Hamid, Kelechi Osunwa na Mudather El Tahir ambao kila mmoja amepachika mabao 18.