Bacca afunguka dakika 90 Yanga

Mwanaspoti
Published: Mar 23, 2023 13:02:06 EAT   |  Sports

BEKI wa kati wa Yanga, Ibrahim Abdallah ‘Bacca’ amesema dakika 90 alizocheza dhidi ya US Momastir zimemwongezea kujiamini na kumpa mwanya wa kuona nafasi yake kikosi cha kwanza cha timu hiyo. Bacca juzi alianza kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika na kuwa miongoni mwa mastaa waliotoa jasho lao na kuisaidia timu hiyo kutinga hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza kupitia makundi baada ya ushindi wa mabao 2-0. Akizungumza na Mwanaspoti, Bacca alisema ametimiza ndoto ya kwanza kucheza mashindano ya kimataifa kwa dakika nyingi na kuwa miongoni mwa mastaa ambao wameandika historia mpya. “Haikuwa rahisi siku mbili kabla ya mchezo kuambiwa mimi ni miongoni mwa wachezaji watakaoanza kwenye mchezo dhidi ya US Monastir, nilijiandaa kisaikolojia na kujiweka timamu kimwili ili kuweza kumwonyesha Kocha Nasriddine Nabi hajakosea kunipa nafasi; “Nilikuwa kwenye hali nzuri zaidi kwa sababu niliambiwa umuhimu wa mchezo wenyewe lakini nilikuwa imara kwa sababu nilicheza na kiongozi wangu uwanjani Bakari Mwamnyeto ambaye muda mwingi alikuwa ananipa maelekezo.” Bacca alisema mbali na nahodha wake, Mwamnyeto pia upande wao wa walinzi walikuwa wanacheza kwa kuelekezana na kukumbushana majukumu yao na hiyo ndiyo siri kubwa ya ubora wao kwenye mchezo huo. Alisema kitendo cha kuaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza kwenye mashindano makubwa kumempa imani ipo siku atakuwa mchezaji tegemeo kikosi cha kwanza cha Yanga kitu ambacho amekuwa akikipambania tangu amejiunga na timu hiyo.