Arafat: Yanga hii tukutane nusu fainali CAF

Mwanaspoti
Published: Mar 23, 2023 08:12:41 EAT   |  Sports

“NI miezi tisa ambayo ina mafanikio mengi tangu tumeingia ndani ya Yanga kwa ajili ya kuiongoza na kuipeleka kwenye lile eneo ambalo tumekuwa tukitamani kuiona Yanga ikifika. Maeneo makuu ambayo tunaelekea nayo ni kuendelea na mabadiliko, lakini pia kwenye eneo la miondombinu na kutengeneza timu imara,” anaeleza Arafat Haji, makamu wa rais wa Klabu ya Yanga wakati akianza kuelezea mwanzo wa utawala wao ndani ya timu hiyo wakati akifanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti, huku akiendelea kusema: “Kutengeneza timu imara lazima uwe na uchumi imara ambao utakuwezesha kufanya mipango yako kuendesha timu. Sasa kwa miezi tisa tangu uongozi huu uingie madarakani maeneo ambayo ndiyo msingi wa safari yetu hii, timu imara, uchumi imara, ni maeneo ambayo tunayapa mkazo kwa kuanzia ili tuweze kuwa na nafasi ya kufanya mengine wakati timu iko imara na uchumi wa kuendesha timu uko imara. “Kwa maana hiyo utaona ndani ya kipindi hiki cha miezi tisa thamani ya klabu imeongezeka, lakini pia wadhamini wameongezeka. Mdhamini mkuu ambaye tulikuwa naye kabla ya uchaguzi SportPesa tumeona mara baada ya kuingia madarakani tumesaini naye mkataba wenye thamani zaidi ya mara tatu ya ule uliokuwepo mwanzoni. “Lakini tumeweza kuongeza wadhamini wengine kama Afya, tumeweza kufanya kazi na taasisi kubwa kama UN lakini tumeona benki kama CRDB nao wamekuja kutaka kufanya kazi na Yanga bila kumsahau mdhamini na mfadhili mwenza GSM ambaye kupitia kampuni zake tofauti amekuwa sehemu ya udhamini wa Yanga. Tumeona karibuni kupitia kwa mshirika wa GSM kampuni ya vifaa vya umeme Haier nao wamekuja kutaka kufanya partnership na Yanga na mkataba mnono mahsusi kwa ajili ya mashindano ya kimataifa. “Nilikuwa naangalia tathmini za haraka mechi yetu ya kwanza na TP Mazembe tulipata watazamaji 42,000 wenzetu walipata 45,000 lakini mechi yetu ya pili tulipata watanzamaji 28,000 wenzetu walipata 22,000. Kwa hiyo unaona kwa kiwango gani Wananchi wameamua sasa kuiunga mkono, kuisapoti timu yao kwa kuwa wao wanajitoa na sisi tumekuwa tukiwahakikishia wanapata furaha, lakini na wao vilevile wanapendeza kupitia kwa mkandarasi ambaye tumempa mkataba wa kuwavalisha. Tumeona kila msimu Yanga inatoa jezi ambazo zimeshinda jezi ya msimu uliopita. Lakini sio tu jezi mavazi ya aina tofauti ambayo Wananchi na wao wanavaa wanapendeza - yote ni kuonyesha thamani ya ukubwa ya Yanga.” SUALA LA MABADILIKO Arafat akizungumzia suala la mabadiliko ambalo ni miongoni mwa mambo wanayoyapigania kuyafanya katika utawala wao, anasema wanaendelea nayo. “Mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji ni sehemu kubwa ya chachu ya kuwavutia watu kuiamini taasisi kufanya nayo kazi. Niligusia nikasema tumefanya na taasisi kubwa ya kimataifa kama UN. Unajua unapofanya kazi na taasisi kubwa ya kimataifa, hata wao kabla ya kuingia mkataba wanafanya uhakiki mkubwa kuhakikisha wanakwenda kufanya kazi na taasisi sahihi yenye utaratibu,” anasema. “Tanzania ni Yanga pekee imepata bahati hiyo ya kukubalika na taasisi kama UN kufanya nayo kazi. Huko nyuma tuliona UN walifanya kazi na Barcelona ya Hispania na kwa Tanzania wameona katika timu ambazo zipo, kwa ukubwa wao na miondombinu ambayo ipo na aina ya uendeshaji kwa mwelekeo mzuri ambayo timu za Tanzania zimeanza kuonekana ni Yanga ambayo imeanza kuonyesha sura ya mabadiliko ya kweli. “Tulisema twende na mfumo ambao wawekezaji watakuwa zaidi ya mmoja ili kuondoa mtu mmoja kujimilikisha timu. Kwa hiyo mchakato huu unaendelea ndani kwa kuendelea kuunda idara mbalimbali, ndio maana mnaona sisi wengine sio waajiriwa wa kila siku, lakini wapo watu ambao wanaendesha klabu kwa kufanya kazi za kila siku tofauti na huko nyuma na mambo yanaenda, klabu inaendelea kupiga hatua.” MJUMBE HADI MAKAMU Kwa mashabiki na wanachama wa Yanga wanajua Arafat ameitumikia katika maeneo tofauti ikiwamo ujumbe wa Kamati ya Utendaji, lakini wakamwamini na kumchagua kusaidiana na rais Hersi Said na hapa anasema: “Unapokuwa mjumbe wa Kamati ya utendaji eneo lako kubwa ni jinsi unaweza kushauri au kusaidia kutoa mawazo kama jambo au kuhusu shughuli gani unaona zifanyike. “Mara nyingi sio vitu ambavyo unaweza kuvifanya kila siku, lakini unapokuwa kwenye nafasi hizi za juu kama rais au makamu wa rais ni sehemu ambayo kwanza hata aina ya maisha yako yanahitajika kubadilika kwa sababu hata kauli utakayoitoa popote pale wengine wataona kama ni kauli ya mamlaka. “Changamoto moja ni kwamba unalazimika kuwa makini sana katika kile ambacho utakisema, utakiandika au hata kufanya. Kiutendaji unakuwa sehemu ya maelekezo kwamba taasisi ielekee wapi. Bahati nzuri juu yangu yupo rais ambaye tunajuana kwa muda sasa ni mweledi na anayejua maadili ya kiuongozi, ana maono ya mbali lakini niseme anaipenda sana klabu hii. Mnaiona jinsi anavyoamua kujiweka katika presha kubwa ili tu kuhakikisha jambo la Yanga linafanikiwa. Hii sio sifa ambayo viongozi wengi wanayo, ni wachache sana. “Kama wapinzani wetu huko nje wangekuwa wanaotushuhudia tunavyoishi humu ndani wangekuwa wanazimia wakisikia Hersi anakwenda kufanya au kusimamia jambo fulani. Huyu ni mtu ambaye unaweza kumuamsha usiku mkubwa akaambiwa kuna hili la Yanga nenda kalipiganie basi atakwambia niachieni mimi na hapo tunakuwa na imani kubwa kwamba Yanga heshima yake ipo mikono salama na tunafanikiwa kama Wananchi. Kwa hiyo hii ni sehemu ya wepesi wa majukumu yangu kwa kuwa juu yangu yupo rais mchapakazi. “Ugumu wangu binafsi ni kutokana na majukumu yangu mengine. Mimi ni mtumishi wa serikali ya Zanzibar kwa hiyo kuna wakati lazima nitatakiwa kugawanya muda wangu kwa usahihi ili kote kusiyumbe, lakini kwa kuwa sio mtendaji wa kazi za kila siku hapa Yanga inanipa nafasi ya kufanya majukumu ya kiserikali vizuri. YANGA TIMU IPO Arafat anaeleza jinsi uongozi wao unavyoendelea kuhakikisha Yanga inakuwa bora uwanjani licha ya utawala wao kudharauliwa kwa kuonekana wengi ni vijana wapya. “Unajua wakati tunaingia madarakani kwa uongozi, watu wengi walituona kama vile ni wachanga sana kwenye soka la hapa nchini na Afrika kwa ujumla. Watu walitubeza kwamba itakuwa ngumu kufanikiwa, lakini baada ya kuingia madarakani na kupata ushirikiano, umoja kutoka kwa wanachama na mashabiki bila kuwasahau wadau sasa watu wanaona mafanikio ya mapema sana katika utawala wetu,” anasema. “Ukiangalia katika mashindano ya kimataifa tulivyoshiriki mpaka sasa, mapema tu tulijua hayatakuwa rahisi. Yana mahitaji makubwa. Tulihitajika kujipanga vizuri kuna safari za kwenda ugenini. Hizi ni safari zenye gharama kubwa, lakini pia ushindani ni mkubwa sio tu ugenini hata nyumbani kila timu imejipanga. “Wapo ambao walitubeza tulipotolewa Ligi ya Mabaingwa Afrika na Al Hilal ya Sudan, lakini tunaishuhudia Al Hilal ndio inashindana kwa kukaa juu ya msimamo wa kundi lake, wakishindana na klabu kubwa kama Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini na hapo tukumbuke kigogo Al Ahly yuko chini. Nadhani watu wajue kwamba Yanga tulikuwa na timu ipi. Uwanja ambao tulifungwa kule tena kwa tabu amebaki Mamelodi pekee hajakwenda, wengine wamekwenda na wamepoteza. Kwa hiyo tuna timu imara.” Safari ya NUSU FAINALI Kiongozi huyo anasema baada ya kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, safari ya kuisaka nusu fainali inaanza kwa kasi. “Baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa tukasema sasa tujipange kufanya vizuri kwenye Shirikisho. Nadhani mwenye macho haambiwi tazama hata wale ambao walikuwa wanatuombea kufanya vibaya wamelazimika kuwa upande wetu. Tunakwenda sasa kupigania kucheza robo fainali. Tumeona Mazembe alikuja hapa akapotea wale Bamako nao ikawa hivyo hivyo. Malengo yetu mapya yatakuwa kutinga nusu fainali.” NABI bo nge la KOCHA Wakati kila shabiki wa soka nchini akiizungumzia Yanga kuwa katika mikono salama uwanjani chini ya kocha Nasreddine Nabi, Arafat anasema jamaa anajua sana. “Haya matokeo yanathibitisha kwamba tuna kikosi bora licha ya changamoto mbalimbali zinazotukabili, lakini pia ufike wakati wa kutambua kwamba Yanga sasa ipo chini ya kocha mwenye ubora mkubwa Nasreddine Nabi. Huyu ni kocha ambaye amethibitisha kwamba ni moja kati ya makocha bora wanaofundisha soka la Afrika. Ukiona ubora ambao Yanga inauonyesha sasa watu watakubaliana nami. Anajua kuwasoma wapinzani, nadhani ubora wake ukichanganya na wasaidizi wake mtaona tuna benchi lililoenea. “Watu waelewe jambo moja vyeti vya ukocha vya Nabi anaweza kufundisha klabu yoyote Ulaya unayoijua wewe. Kwa hiyo ubora huu hauji kirahisi, kuna uwekezaji umefanyika kupata kocha bora wa namna hii. “Lakini tulichofanya pia ni kuboresha benchi lake baada ya kupata kocha bora msaidizi, kocha wa makipa, kocha wa mazoezi ya viungo. Tumemuongeza pia mtaalamu wa kuchambua mikanda ya video kwa wapinzani na hata mechi zetu wenyewe hii inakwenda kuwarahisishia makocha wetu kazi. Afya za wachezaji nazo tumezizingatia. Ili uwe na timu bora lazima uwe na mazingira muafaka ya kuwatibu wachezaji. Tumethibitisha kwamba hakuna mchezaji atakayeumia ndani ya Yanga na kutibiwa kwa kubahatisha,” anasema Arafat. “Tuna mikataba na hospitali mbalimbali kubwa Afrika. Tukiona hapa huwezi kupona tutakupeleka nje. Nadhani tulishuhudia kilichotokea kwa Yacouba (Sogne) na baadaye kipa wetu Mshery (Aboutwalib). Tunapofurahia kazi zao bora tuna jukumu pia kuhakikisha ndoto zao hazikatishwi kwa majeraha.” YANGA NA USAJILI Arafat ambaye pia ni mtendaji mkuu wa Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) anaeleza uongozi wao unavyoachana na usajili wa mazoea na kufanyia kazi mahitaji ya makocha. “Ukiangalia utawala wetu tumesema tuachane (na usajili) na mambo kufanyika kisiasa. Uongozi kazi yetu ni kufanya mambo ya kiutawala hasa kuwawezesha makocha kutimiza yale wanayoyataka,” anasema. “Akili hii ndio ambayo tunakwenda nayo tunapotaka kusajili. Tunachukua mahitaji ya makocha na kwenda nayo sokoni tukipata watu hao tunarudi kwao kujadiliana nao kisha tunafanya uamuzi. “Yanga tayari tuna timu bora lakini ukiangalia mfano dirisha dogo la usajili tukasema tukaboreshe maeneo ambayo tunaona yana changamoto. Tukamleta Metacha (Mnata) ambaye usajili wake ulikuwa maalumu baada ya Mshery kuumia, tukaongeza mshambuliaji Musonda (Kennedy) nadhani tunaona ubora wake. Tukampa nafasi Mudathir ambaye alikuja kututuliza zaidi pale kati na tukamleta Mamadou (Doumbia) ili kuja kuweka idadi sawa ya mabeki wa kati. Wapo wanaona kama hatumpi nafasi, hiyo ni hesabu za makocha kwa kuwa wanaona kwa mabeki tulionao sasa siyo afya kuwatenganisha kwa haraka eti kisa tu kuna beki mpya amekuja.” ITAENDELEA KESHO UNA MAONI YOYOTE? TUMA SMS KWA NAMBA 0658-376417