Waliomshambulia Mwanafunzi kisa andazi wakamatwa

Milard Ayo
Published: Feb 16, 2023 09:38:50 EAT   |  Educational

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Sekondari Loiler iliyopo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya Peter Emmanuel (29)pamoja na mlinzi wa Shule hiyo Haruna Issa (30) mkazi wa Iwala kwa tuhuma za kumshambulia kwa viboko sehemu mbalimbali za mwili mwanafunzi wa Shule hiyo Laurence Nicholaus (16) na kumsababishia […]

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Sekondari Loiler iliyopo Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya Peter Emmanuel (29)pamoja na mlinzi wa Shule hiyo Haruna Issa (30) mkazi wa Iwala kwa tuhuma za kumshambulia kwa viboko sehemu mbalimbali za mwili mwanafunzi wa Shule hiyo Laurence Nicholaus (16) na kumsababishia majeraha.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP, Benjamin Kuzaga amesema tukio hilo limetokea Februari 12, 2023 katika Shule ya Sekondari Loiler mwalimu huyo kwa kushirikiana na mlinzi wa Shule hiyo walimtuhumu mwanafunzi Nicholous kuiba maandazi matano kwenye duka la shule.

Anasema siku hiyo ya tukio majira ya saa tano usiku walimkimbiza Hospitali Teule ya Ifisi kwa ajili ya matibabu na kwamba Jeshi la Polisi kupitia makachero wake walipata taarifa na kufanya ufuatiliaji na kubaini kutokea kwa tukio hilo na hatimaye kuwakamata watuhumiwa wote wawili.

“Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani aidha tunatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria,” amesema Kuzaga.

Ameongeza kuwa watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.