Benki ya CRDB na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima waendesha mafunzo hayo DSM

Milard Ayo
Published: Mar 16, 2023 22:19:46 EAT   |  Business

Benki yetu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) leo tumeendesha mafunzo ya uendeshaji wa Akaunti ya Dhamana ya Bima (Trust Account) kwa kampuni na wadau wa sekta ya bima nchini. Mafunzo hayo ambayo yamefanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB yalifunguliwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru […]

Benki yetu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) leo tumeendesha mafunzo ya uendeshaji wa Akaunti ya Dhamana ya Bima (Trust Account) kwa kampuni na wadau wa sekta ya bima nchini.

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB yalifunguliwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru ambaye alisisitiza umuhimu wa kampuni za bima kutumia akaunti hiyo kuweka amana za bima kama ambavyo imeelekezwa katika Kanuni ya Bima ya mwaka 2009.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa benki ya kwanza kusaidia utekelezaji wa uanzishwaji wa akaunti hiyo, pamoja kutoa elimu kwa kampuni, na wadau wa sekta hiyo.

Akielezea umuhimu wa uanzishwaji wa akaunti hiyo, Kamishna wa TIRA, Dkt. Baghayo Saqware alisema itasaidia kuboresha usimamizi kwa kuhakikisha kampuni zinakuwa na ukwasi wa kutosha, na wateja wanapata stahiki zao kwa wakati pindi wapatapo majanga.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ameishukuru TIRA kwa kuipa fursa ya kushiriki katika uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Bima.

Nsekela alipongeza uamuzi wa uanzishwaji wa akaunti hiyo na kusisitiza kuwa inachukua jukumu muhimu katika kukuza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya bima.

Nsekela alimuhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa Benki ya CRDB itaendelea kushirikiana na TIRA na wadau wa sekta ya bima kusaidia kuboresha sekta hiyo.

.

.