
HOTUBA YA RAIS SAMIA KATIKA UFUNGUFI WA MKUTANO WA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI...
🔴#LIVE: HOTUBA YA RAIS SAMIA KATIKA UFUNGUFI WA MKUTANO WA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI... ⚫️ JE, UNA HABARI?
Category
Top headlines and developing stories from Tanzania, Kenya, Uganda and the wider region, gathered from the leading local and international newsrooms and updated throughout the day.

🔴#LIVE: HOTUBA YA RAIS SAMIA KATIKA UFUNGUFI WA MKUTANO WA MAAFISA WAANDAMIZI WA JESHI LA POLISI... ⚫️ JE, UNA HABARI?

WAFANYABIASHARA katika Soko la Keumbu, Kaunti ya Kisii, wanakabiliwa na wakati mgumu baada ya biashara yao kudorora kufuatia vurugu zilizotokea wakati wa mkutano wa kisiasa wa viongozi wa Linda Mwananchi Ijumaa iliyopita. Hali imezidi kuwa mbaya kutokana na kampeni kwenye mitandao ya kijamii inayowahimiza wananchi kususia bidhaa kutoka sokoni humo, kwa madai kwamba baadhi ya wafanyabiashara walihusika katika vurugu hizo. Ingawa hali ya usalama imeanza kutulia, wafanyabiashara wanasema idadi ya wateja imepungua kwa kiasi kikubwa na wengi wao sasa wanapata hasara. Bi Josephine Mang'ere alisema biashara ilikuwa ikiendelea vizuri kabla ya mkutano huo kuvurugika. “Tulikuwa tumewasubiri viongozi wa Linda Mwananchi, lakini baada ya muda mawe yakaanza kurushwa. Tangu siku hiyo biashara imekuwa ngumu. Tunapoenda kuuza bidhaa zetu watu hawazinunui. Tunaomba tusamehewe,” alisema. Kwa upande wake, Bi Sophia Moraa alisema biashara yake ya parachichi imeathirika vibaya kwani wateja wengi wamekataa kununua mazao yake, hali iliyosababisha baadhi yake kuoza. “Sisi ni wafanyabiashara wasio na hatia. Tunapowafuata wateja barabarani wanatuambia tuuze bidhaa zetu kwa viongozi wanaotuhumiwa kusababisha vurugu. Tunataka siasa za amani,” alisema. Bi Mary Moraa alisema wafanyabiashara sasa wanahimiza amani na kuheshimiana kisiasa. “Sisi ni wazazi. Kijana aliyefariki ni mtoto wetu pia, na kifo chake kinatuumiza. Wanasiasa wote waruhusiwe kuhutubia wananchi bila ubaguzi,” alisema. Wakati huo huo, Meshack Yoge, mmoja wa manusura wa shambulizi dhidi ya msafara wa Linda Mwananchi, alisema anaamini alinusurika kifo kwa bahati. Bw Yoge, ambaye alijeruhiwa jicho baada ya kupigwa na jiwe, alisema tukio hilo lilikuwa la kutisha na bado hajapona kikamilifu. Alisema walikuwa wakielekea Keroka baada ya mkutano wa Kisii mjini na walipofika Keumbu, walivamiwa na kundi la watu waliokuwa wakirusha mawe na kubeba rungu, mishale na pinde. “Tuliona watu wakikimbia kuelekea kwetu wakipiga kelele wakisema, 'Waueni!' Dirisha la gari lilivunjwa, jiwe likanigonga usoni na kujeruhi jicho. Nilinusurika kupoteza jicho na meno,” alisema. Aliongeza kuwa walilazimika kukimbia kwa kasi kuokoa maisha yao na baadaye akapelekwa hospitalini Keroka ambako alipatiwa matibabu. Mgombeaji wa udiwani wa Kisii Central, Bw Andrew Moindi Mochache, aliyekuwa ndani ya gari hilo, alisema waliona kifo wazi. "Niliona kifo kwa macho yangu. Watu waliotushambulia walikuwa wamekusudia kutuua," alisema. Kiongozi wa People's Liberation Party (PLP) Martha Karua na Mbunge wa North Mugirango Joash Nyamoko walilaani vurugu hizo, wakisisitiza kuwa siasa zinapaswa kuendeshwa kwa amani. Bi Karua alisema hakuna anayepaswa kuzuiwa kutoa maoni yake au kushiriki shughuli za kisiasa kwa amani, huku Bw Nyamoko akiwataka vijana kuepuka kutumiwa na wanasiasa kuchochea ghasia.

KAMPUNI ya stima Kenya (KPLC) imekanusha madai kuwa iliondoa transfoma 15 kutoka maeneo mbalimbali katika eneo bunge la Mbeere North, Kaunti ya Embu, kwa sababu za kisiasa, ikisema vifaa hivyo vilichukuliwa kwa ukarabati wa kawaida. Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Meneja wa KPLC Kaunti ya Embu, Bw Vincent Okello, alisema transfoma zinapopata hitilafu kama kuingia maji au kasoro nyingine ambazo haziwezi kurekebishwa zikiwa eneo la matumizi, hupelekwa kwenye karakana maalumu kwa ukarabati, majaribio na kukaushwa kwa teknolojia maalumu ili kurejesha ubora wake. Alisema kati ya Mei na Juni mwaka huu, transfoma 15 ziliondolewa Mbeere North kutengenezwa. Kati ya hizo, 14 tayari zimerejeshwa na kufungwa upya, huku moja iliyoharibiwa na wahuni wiki iliyopita ikibadilishwa Ijumaa. "Kazi hizi ni za kiufundi pekee na zinalenga kuhakikisha wananchi wanapata umeme salama, wa kutegemewa na ulio thabiti," alisema Bw Okello. Hata hivyo, wakazi walipinga madai kwamba walihusishwa kabla ya transfoma hizo kuondolewa. Walisema walishtushwa na hatua hiyo na kudai baadhi ya transfoma zilirejeshwa usiku baada ya vyombo vya habari kuripoti kuhusu kero hiyo.

KIONGOZI wa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), Bw Rigathi Gachagua, ameshambulia vikali Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), akiishutumu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba. Bw Gachagua alidai kuwa tume hiyo inafumbia macho madai ya kuhonga wapigakura, vitisho vya kisiasa na maafisa wa serikali kuingilia uchaguzi mdogo wa eneobunge la Ol Kalou utakaofanyika Julai 16. Akizungumza jana, siku moja kabla ya makamishna wa IEBC kutimiza mwaka mmoja afisini, Bw Gachagua alisema jinsi tume hiyo itakavyosimamia uchaguzi wa Ol Kalou, itakuwa kipimo cha iwapo inaweza kuaminiwa kusimamia Uchaguzi Mkuu wa 2027. Alitoa kauli hiyo chini ya saa 24 baada ya Mwenyekiti wa IEBC, Bw Erastus Edung Ethekon, kuonya kuwa tume inaweza kuahirisha au hata kufuta uchaguzi huo iwapo vitendo vya utoaji hongo, vurugu na makosa mengine ya uchaguzi vitaathiri uadilifu wa mchakato huo. Hata hivyo, Bw Gachagua alisema badala ya kuonya kuhusu uwezekano wa kuahirisha uchaguzi, IEBC inapaswa kuwachukulia hatua wanaodaiwa kuhusika na vitendo hivyo. "Mwenyekiti wa IEBC anawezaje kutishia kufuta uchaguzi kwa sababu ya hongo ilhali Katiba na sheria zinampa mamlaka ya kukomesha vitendo hivyo?" alihoji. Alidai kuwa vyombo vya habari vimeripoti visa vya utoaji hongo kila siku, huku mawaziri, makatibu na maafisa wengine wa serikali wakihusika waziwazi katika kampeni na kuwahonga wapigakura. "Badala ya kuwachukulia hatua wanaohusika, IEBC inataka kuwaadhibu wananchi wa Ol Kalou kwa kufuta uchaguzi wao," alisema. Bw Gachagua alinukuu Kifungu cha 81 cha Katiba kinachotaka uchaguzi uwe huru, wa haki na usio na vurugu, vitisho, ufisadi au ushawishi usiofaa. Pia, alirejelea Kifungu cha 38 kinachowapa Wakenya haki ya kushiriki katika uchaguzi wa mara kwa mara ulio huru na wa kuaminika. Alisema tume hiyo imeshindwa kutekeleza masharti hayo ya kikatiba na hivyo kupoteza imani ya wananchi. "Tumekuwa tukieleza kutoridhishwa kwetu na jinsi tume hii inavyofanya kazi. Katiba na imani ya wananchi ndiyo misingi ya uchaguzi wowote, na imani hiyo imeporomoka," alisema. Pia, aliishutumu IEBC kwa kutumia viwango tofauti katika chaguzi dogo tofauti. Alidai tume hiyo haikuchukua hatua katika chaguzi za Mbeere North, Malava, Narok Township na Kasipul, ambako kuliripotiwa vurugu na madai ya hongo, lakini sasa imekuwa ikitoa matamshi makali kuhusu Ol Kalou. "Kulikuwa na vurugu, vitisho na hata mauaji katika chaguzi zilizopita, lakini IEBC haikuwahi kuzungumzia kuahirisha uchaguzi. Kwa nini Ol Kalou iwe tofauti?" alihoji. Bw Gachagua alidai eneo la Ol Kalou limekuwa tulivu isipokuwa visa vichache alivyodai vilihusisha maafisa wa serikali. Alirejelea tukio la Julai 1 katika Hoteli ya Royal Garden ambapo viongozi wa DCP walidai kushambuliwa na polisi pamoja na wafuasi wa chama cha UDA. Aidha, aliwataka maafisa wa polisi waliovalia sare pekee kusimamia usalama siku ya uchaguzi, akidai maafisa waliovalia mavazi ya kiraia wamekuwa wakitumika kutisha wapigakura katika chaguzi zilizopita. Alikosoa serikali kwa kile alichodai ni kupeleka idadi kubwa isiyo ya kawaida ya mawaziri, makatibu na wakuu wa mashirika ya umma kufanyia kampeni mgombeaji wa UDA. Alitaja Waziri wa Ardhi Alice Wahome, Waziri wa ICT William Kabogo, Waziri wa Barabara Davis Chirchir, Waziri wa Utalii Rebecca Miano, Katibu wa Ulinzi Patrick Mariru, Katibu wa Nishati Alex Wachira na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Kenya Philip Mainga. Kwa mujibu wake, viongozi hao wamekuwa wakizindua miradi ya maendeleo huku wakigawa fedha taslimu, godoro, mitungi ya gesi, matangi ya maji na bidhaa nyingine ili kuwashawishi wapigakura. "Ni kama miujiza kwamba miradi yote ya maendeleo ya serikali imehamia katika eneo moja wakati wa kampeni," alisema. Alionya kuwa kuahirishwa kwa uchaguzi wa Ol Kalou kutadhoofisha zaidi uaminifu wa IEBC na kuzua maswali kuhusu uwezo wake wa kusimamia Uchaguzi Mkuu wa Agosti 2027. "Iwapo IEBC haiwezi kusimamia uchaguzi mmoja mdogo wa ubunge kwa sababu ya madai ya hongo na vurugu, itawezaje kuaminika kusimamia Uchaguzi Mkuu?" alihoji.

Critics say the Bill is a ruse for Mnangagwa to stay in power for longer, but its backers say...

WAZIRI wa Fedha, John Mbadi, aliwasilisha jana bajeti ya Sh4.82 trilioni ya mwaka wa kifedha wa 2026/27 huku serikali ikijivunia kuweka mikakati ya kuendeleza uchumi, kuboresha huduma za umma na kuimarisha ustawi wa wananchi. Hata hivyo, kuna uhalisia mchungu kwamba bajeti hiyo huenda ikawa mzigo mwingine kwa mwananchi wa kawaida ambaye tayari anahangaishwa na gharama kubwa ya maisha. Jambo la kwanza linalotia wasiwasi ni kiwango kikubwa cha nakisi ya bajeti ambacho kitalazimisha serikali kukopa takribani Sh1.1 trilioni ili kuziba pengo la matumizi. Kati ya fedha hizo, karibu Sh1 trilioni zinatarajiwa kukopwa katika soko la ndani huku Sh100 bilioni zikitoka masoko ya mikopo ya nje. Hili si jambo la kupuuzwa kwa sababu linaonyesha kuwa serikali bado haijaweza kuwianisha matumizi yake na mapato inayokusanya. Athari za ukopaji huu wa ndani ni kubwa. Serikali inapokopa kwa kiwango kikubwa kutoka kwa benki za kibiashara, taasisi hizo huona ni salama zaidi kuikopesha serikali kuliko wafanyabiashara na wawekezaji binafsi. Matokeo yake ni kwamba sekta ya kibinafsi, ambayo ndiyo mwajiri mkuu nchini, hukosa mtaji wa kupanua biashara zake, kuanzisha miradi mipya na kuajiri wafanyakazi zaidi. Hivyo basi, wakati serikali ikijisifu kuwa imeandaa bajeti ya kukuza maendeleo, ukweli ni kwamba inaweza kuwa inanyima uchumi nguvu zinazotokana na uwekezaji wa kibinafsi. Katika mazingira ambapo maelfu ya vijana huingia kwenye soko la ajira kila mwaka, jambo la msingi lingekuwa kuweka mazingira yanayochochea biashara kustawi. Hata hivyo, bajeti hii haionekani kutoa mwelekeo wa kutosha wa kuhamasisha ukuaji wa sekta binafsi. Badala yake, inategemea zaidi matumizi ya serikali na ukopaji, mkakati ambao umeendelea kutumiwa kwa miaka mingi bila kuleta matokeo mazuri. Aidha, wataalamu wa uchumi wamekuwa wakisisitiza kuwa njia bora ya kuchochea ukuaji ni kupunguza mzigo wa ushuru kwa wananchi na wafanyabiashara. Kupunguza ushuru kungewaachia watu fedha zaidi za kuwekeza, kupanua biashara na kuongeza matumizi katika uchumi. Kadiri shughuli za kiuchumi zinavyoongezeka, ndivyo serikali inavyoweza kukusanya mapato mengi zaidi kutokana na kuongezeka kwa idadi ya walipa ushuru na ukuaji wa biashara. Ni wakati mwadaka kwa serikali kutambua kwamba maendeleo ya kweli hayatokana na ukopaji usioisha. Bajeti endelevu ni ile inayoweka mkazo katika kukuza uzalishaji, uwekezaji na ubunafu wa sekta binafsi. Bila kufanya hivyo, mzigo wa deni utaendelea kuongezeka na mwananchi wa kawaida ndiye atakayebeba gharama kuu. Bajeti ya mwaka huu, kwa hivyo, inastahili kuchunguzwa upya kwa jicho la tahadhari.

ALIPOPATA ujauzito wake wa kwanza, Phidilia Kibirisho Mwendwa na mumewe walikuwa na furaha tele. Walifanya maandalizi yote ya kumpokea kifungua mimba. Walimnunulia malaika huyu nguo, wakapanga tarehe ambayo angebatizwa kanisani na hata kutangaza taarifa kuwa walikuwa wanamtarajia mwanao kwa marafiki na jamaa waliokuwa mbali nao. Hata hivyo, furaha hiyo iligeuka kuwa huzuni mwingi baada ya kuupoteza ujauzito wake katika wiki ya 29. “Nilianza kuhisi maumivu makali sana kisha mume wangu akanipeleka hospitalini lakini kwa bahati mbaya, mtoto wangu alipatikana akiwa ameshaaga tumboni na hivyo madaktari walimtoa akiwa maiti,” Phidiliah anasimulia kwa huzuni. Miezi iliyofuata, Phidilia na mumewe walimuomboleza mwanao. Ilikuwa vigumu pia kwao kuyajibu maswali ya marafiki na jamaa waliokuwa wakiwauliza jinsi mtoto alivyokuwa akiendelea bila kujua alikuwa ameaga. “Mume wangu alikuwa akinifariji mara nyingi sana. Wakati mwingine angenipata nikiwa chumbani nimeshikilia zile nguo tulizokuwa tumemnunulia mtoto wetu kabla ya kuzaliwa lakini angenielewa. Majonzi ya kumpoteza mtoto wetu yaliponizidi, nilimuomba tuhamie nyumba nyingine ya kukodisha na kugawa zile nguo tulikuwa tumemnunulia mtoto wetu aliyeaga dunia na aliniunga mkono.” Miezi iliyofuata, walibahatika tena kupata ujauzito mwingine, lakini kwa bahati mbaya tena walimpototeza alipofikisha wiki ya nane ya ujauzito. “Damu ilianza kutoka kwa uchungu sana na tulipofika hospitalini, daktari aliniambia kuwa nilikuwa nampoteza mtoto wangu na hakuna kitu hospitali ingefanya kumuokoa. Nilijiuliza maswali mengi sana, lakini sikupata majibu.” Phidilia anasema kuwa safari yake ya kuitwa mama ilizidi kuchelewa kwani kadri alivyopata ujauzito, ndivyo alivyozidi kupoteza wanawe. Baada ya kuupoteza ujauzito wa wiki 30, anasema kuwa alimuuliza daktari wake kwa sauti ya unyonge ikiwa kuna siku ataitwa mama. “Niligundua kuwa nilikuwa na ujauzito wangu wa nane katika wiki ya sita. Baada ya kupigwa picha, daktari wangu aliniambia kuwa huo ujauzito haukuwa salama kwani ulikuwa unatingika. Niliwekwa kwenye matibabu na kuruhusiwa kurudi nyumbani lakini siku mbili baadaye, nilikuwa navuja damu. Mume wangu alinirudisha hospitalini na kwa bahati mbaya, niliupoteza ujauzito huo tena,” anasema Phidilia. Siku moja rafiki wake alimshauri kubadilisha daktari wa uzazi wa kina mama. Ushauri ambao aliuzingatia. Siku zilizofuata, alihusishwa kwenye ushauri na mmoja wa madaktari hao. Miongoni mwa mawaidha aliyopewa yalikuwa ni mumewe kumpeleka kwenye likizo sehemu anakopenda ili apumzike, mbali na mazingira ambayo alikuwa ameyazoea. Pia aliambiwa kuwa atoe kwenye fikra wazo la kutaka kumpata mtoto. “Ama kweli ushauri huo ulizaa matunda kwani niligundua nilikuwa mjamzito mara ya tisa. Lakini badala ya kuwa na furaha, nilihofia kuwa nitaupoteza tena ujauzito ule. Siku hiyo daktari wangu aliniambia kuwa nitambeba mwanangu mkononi na kumnyonyesha.” Ujumbe huo ulimpa matumaini pamoja na mumewe japo wanasema kuwa safari ya ujauzito huo ilikuwa ghali mno. “Niliwekwa kwenye muda wa mapumziko na matibabu naye daktari wangu wa uzazi alikuwa akiniangalia kila Jumamosi. Wakati wa usafiri, mume wangu pekee yake ndiye alikuwa dereva ilikuhakikisha kuwa sitingiki kwenye barabara,” anaeleza. Uangalifu huo wa hali hiyo ya juu na madaktari wawili wa uzazi walioshauriana jinsi ya kuhakikisha kuwa Phidilliah hapotezi tena ujauzito huo ulizaa matunda. “Nilipofika wiki ya 29 na siku 3 ya ujauzito, nilijifungua mtoto wangu wa kwanza. Alikuwa na kilo 2.7 na kuwekwa kwenye mashini ya watoto ambao wamezaliwa kabla ya siku zao kutimia. Siku 14 baadaye, nilipopewa mtoto wangu mkononi ndipo niliamini kuwa nimekuwa mama mzazi,” anaeleza kwa tabasamu. Ujio wa malaika huyo ulirahisisha ujio wa watoto wengine wawili miaka iliyofuata na sasa, Phidilia ni mama wa watoto watatu walio na umri wa miaka 12, 8 na 3. “Jambo la kufurahisha ni kuwa ujauzito wangu wa mtoto wangu wa pili ambaye ni wa kiume haukuwa na changamoto yoyote. Alizaliwa akiwa na kilo 3.8 bila upasuaji na sasa ni mtoto ambaye ni mchangamfu,” anasimulia. Hali sawia ilimpata Mactilda Makana. Alipoingia kwenye ndoa mwaka wa 2008. Anasema kuwa alijua kuwa kuitwa mama si jambo la kusubiria. Hata hivyo, hali ilibadilika baada ya kupoteza ujauzito mara tano zilizofuatana. “Mimba ya nne nilibeba hadi miezi saba kisha nikampoteza mtoto huyo. Kisha ya tano nilibeba ujauzito hadi siku ya kujifungua lakini nilimpoteza muda mfupi baadaye,” anasimulia kwa uchungu. Mactilda anasema kuwa baada ya visa hivyo vilivyofuatana vya kuwapoteza watoto vilichangia ndoa yake kuvunjika. “Mume wangu na wazazi wake waliniambia kuwa hawangeendelea kuishi na mwanamke ambaye hawezi kubeba ujauzito na kuzaa watoto walio hai. Nilitoka kwenye ndoa hiyo ya miaka minne nikiwa na msongo mwingi sana wa mawazo,” anakumbuka Mactilda. Anasema kuwa alitumia muda huo mgumu kuomba Mungu kila mara. Kwa wakati mmoja, aliandika barua akiomba dua ya kuitwa mama na kuipeleka kanisani ili aombewe. Na ombi hilo lilijibiwa kwanza alipofunga ndoa tena na kisha kupata ujauzito. “Katika mimba za awali sikuwa napata ushauri wa daktari wa uzazi. Lakini wakati tu niliingia kwenye ndoa ya pili, nilipata ushauri wa daktari wa uzazi hata kabla ya kupata ujauzito. Hatua hiyo ilinisaidia hadi wakati ambapo nilijifungua pacha wangu ambao kwa sasa wana miaka sita,” anaeleza kwa tabasamu. Kulingana na mkuu wa huduma za matibabu spesheli ya uzazi, Dkt Ong’ech Odero, kuna visa vingi nchini vya wanawake kupoteza ujauzito. Anasema kuwa changamoto za kiafya kama vile ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, changamoto na sehemu ya uzazi wa mama au hata baadhi ya virusi na bakteria zinazosababishwa kingono vinaweka mwanamke mjamzito katika hatari ya kumpoteza mwanawe kabla ya kujifungua. “Visa vya wanawake kupoteza ujauzito pia viko juu miongoni mwa wanawake ambao wametimu umri wa miaka 35 na zaidi. Pia hali ya maisha na mazingira kama vile uvutaji sigara, baadhi ya kemikali hatari na utapia mlo pia zinachangia hatari ya mwanamke kuupoteza ujauzito,” anasema Dkt Odero. Dkt Odero pia anaeleza kuwa shughuli za kawaida kama mazoezi, tendo la ndoa, uchovu wa akili unaotokana na kazi za kila siku na visa vidogo vya kuanguka havimweki mjamzito katika hatari za kumpoteza mtoto. “Tafuta ushauri wa kiafya kwa muuguzi endapo unatoa damu, ukiwa na maumivu makali chini ya tumbo, au unapozimia wakati ukiwa mjamzito,” akaongeza Dkt Odero. Naye mwanasaikolojia, Ann Arithi Munyao, anasema kuwa kupoteza ujauzito huwa jambo zito na huathiri mwanamke anayeomboleza. “Huu huwa wakati mgumu sana na mara nyingi unapata wanawake wanajilaumu kuwa wangefanya mambo tofauti huenda halingetendeka. Kuzungumzia ujauzito uliopotea ni ngumu sana kwa sababu si jambo ambalo linazungumziwa hadharani na wakati mwingine jamii huhukumu wanawake waliopoteza ujauzito,” anaongeza Ann.

WASHINGTON, Amerika: AMERIKA na Iran jana ziliendeleza mashambulizi ya angani huku Rais Donald Trump akitishia kuwa Iran itavamiwa zaidi iwapo haitakubali kuingia kwenye muafaka wa amani ya kudumu. Duru zinaarifu kuwa Amerika na Iran zilikuwa zikipanga kuafikiana tena kusitisha vita lakini bado kulikuwa na masuala tata ambayo pande zote hazikuwa zimekubaliana kuzihusu. “Amerika haitawahi kutimiza maslahi yake kwa kuvamia Iran. Vita hivi havitasaidia japo kuna hatua ambazo zimepigwa kwenye mazungumzo,” zikaarifu duru kutoka Iran. Trump mara si moja amekuwa akisema Amerika na Iran zinakaribia kuelewana lakini hakuna ishara zozote za kuonyesha kuwa kauli yake huwa ni ya kweli. Uhasama huo umeendelea wiki hii huku Amerika na Iran zikirushiana makombora. Ndege ya kivita ya Amerika iliangushwa na Iran karibu na Strait of Hormuz mnamo Jumatatu. Pia Iran imekuwa ikishambulia kambi za jeshi za Amerika Mashariki ya Kati hasa Kuwait na Bahrain. Amerika nayo imekuwa ikiendeleza mashambulizi kama mbinu ya kushinikiza Iran ifungue mkondo wa mafuta wa Strait of Hormuz. Trump alisema kuwa Amerika inatathmini kusitisha mashambulizi iwapo tu viongozi wa Iran watakubali kuingia kwenye muafaka wa amani bila masharti makali. Alitishia kuwa mara hii atalipua Iran iwapo nchi hiyo itaendelea kuvuta mchakato wa kusitisha vita. Amerika na Iran zimekosa kukubaliana kuhusu Iran kustawisha viwanda vyake vya nyuklia ambavyo Amerika inasema ni hatari na si kwa ajili ya manufaa ya kawi pekee. Iran pia inasisitiza kuwa kabla ya vita kusitishwa, Israel pia lazima ikomeshe uvamizi dhidi ya Hezbollah kule Lebanon. Vita kati ya Amerika-Israel na Iran vilianza mnamo Februari 28 baada ya mataifa hayo mawili kuvamia Iran kwa makombora ya angani. Maelfu ya watu wameuawa tangu wakati huo hasa Iran na Lebanon.

JUHUDI za kuunda muungano thabiti unaoweza kupambana na Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027 zinaonekana kuingia hatua mpya, kufuatia taarifa za mazungumzo kati ya kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka na kiongozi wa vuguvugu la Linda Mwananchi Edwin Sifuna. Mahojiano kadhaa na viongozi kutoka Muungano wa Upinzani na vuguvugu la Linda Mwananchi yamefichua msukumo wa kusajili muungano utakaofahamika kama Ukombozi-Linda Mwananchi Alliance, huku Bw Musyoka na Bw Sifuna wakitarajiwa kuwa vinara wake. Hata hivyo, huku mazungumzo yakijikita katika uwezekano wa tiketi ya Kalonzo-Sifuna, kuna jambo lingine gumu kupuuzwa: mchango wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta. Vyanzo vya ndani kwenye mrengo wa upinzani vinaashiria kuwepo kwa shinikizo kutoka kwa baadhi ya makundi yakipendelea ushirikiano wa Kalonzo na Fred Matiang’i, ambapo mmoja atakuwa mgombea urais na mwingine mgombea mwenza. Pendekezo hilo linaonekana kuvutia kutokana na uwezo wake wa kupata uungwaji mkono mpana na kunufaika na mitandao inayohusishwa na rais huyo mstaafu. Wachambuzi wa siasa wanakiri kuwa ufadhili wa kampeni utakuwa mchango mkubwa katika kubaini muungano utakaowakilisha upinzani. Kadiri mazungumzo ya muungano yanavyoendelea, viongozi wanapima si tu umaarufu na ushawishi wa kikanda, bali pia uhalisia wa kuendesha kampeni kitaifa. Katika mazungumzo kati ya Bw Musyoka na Bw Sifuna kuna madai kwamba yanaweza kuzaa chama kipya cha kisiasa kinachoitwa kwa muda Ukombozi-Linda Mwananchi Alliance, kilicholenga kuwaleta pamoja viongozi muhimu wa Muungano wa Upinzani na wale wa Linda Mwananchi chini ya muungano mkubwa dhidi ya Rais Ruto. Ingawa hakuna kiongozi aliyethibitisha hadharani kuwepo kwa muungano huo, taarifa hizo zimechochea mjadala kuhusu umoja wa upinzani na juhudi za kuunda muungano thabiti wa uchaguzi wa 2027. Taarifa hizi zinajiri huku viongozi wa upinzani wakizidisha juhudi za kuunganisha nguvu zao wakikabiliana na tamaa za kugombea urais na hesabu tata za kisiasa. Akizungumza kabla ya ziara ya siku tatu ya upinzani eneo la Magharibi mwa Kenya inayoanza leo, kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa alikiri kuwa mazungumzo na viongozi wa Linda Mwananchi yanaendelea, ingawa hakuthibitisha makubaliano rasmi ya muungano. Alisema lengo la sasa ni kuzungumza na wafuasi wao kitaifa na kujenga mwafaka kabla ya kuteua mgombea urais. Kauli yake imechochea tetesi kuwa juhudi za kuunda muungano mkubwa dhidi ya Ruto zinaendelea kwa kasi.Hata hivyo, baadhi ya viongozi walitoa maoni tofauti. Seneta wa Kitui Enoch Wambua alisema hakuna sababu ya kupatia uzito mada hiyo, akisisitiza kuwa Linda Mwananchi tayari inajumuisha wanachama kutoka vyama vilivyo katika Muungano wa Upinzani. Kwa upande mwingine, msemaji wa upinzani Mukhisa Kituyi alikanusha vikali taarifa hizo, huku Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino akisema hana ufahamu wowote kuhusu mazungumzo hayo. Naibu mwenyekiti wa Wiper, Mutula Kilonzo Jnr naye alikanusha kuwepo kwa makubaliano rasmi, ingawa alikubali kuwa mazungumzo yanaendelea. Huku mjadala wa muungano ukiendelea, upinzani sasa umeelekeza nguvu zake Magharibi mwa Kenya, eneo linaloonekana kuwa muhimu katika uchaguzi wa 2027. Wamalwa alisema baada ya mvutano kati ya Rais Ruto na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, muungano wa Kenya Kwanza ulipoteza mshirika mkuu katika eneo la Mlima Kenya. Viongozi wa upinzani wanatarajiwa kuzuru kaunti za Vihiga, Kakamega, Busia, Bungoma na Trans Nzoia katika juhudi za kuimarisha ushawishi wao. Wanalenga pia kujiandaa kwa mkutano mkubwa utakaojadili muundo wa muungano, uteuzi wa mgombeaji na ugavi wa madaraka. Wataalamu wanasema muungano mkubwa ni muhimu ili kushinda rais aliye mamlakani. Wengine wanaotajwa kuwania urais ni pamoja na Kalonzo Musyoka, Fred Matiang’i, Rigathi Gachagua, Martha Karua, Justin Muturi na Eugene Wamalwa. Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa wagombea wengi wanaweza kugawanya kura za upinzani. Bw Sifuna ameibuka kama sura muhimu, akiungwa mkono na vijana na wanamageuzi. Mtaalamu wa siasa Profesa Gitile Naituli anaamini kuwa Sifuna anaweza kuwa mhimili mkubwa katika siasa za 2027, akisema tiketi ya Kalonzo-Sifuna inaweza kuwa tishio kwa Rais Ruto. Kauli hiyo inaonyesha kuwa Sifuna anaweza kuwa daraja kati ya wapigakura wa jadi wa upinzani na vijana wanaotaka uongozi mpya. Hata viongozi wanaokataa uwepo wa muungano wanakiri ushawishi wake unakua. Gavana wa Siaya James Orengo amewahi kusema hata Sifuna “anafaa kuwa Rais wa Kenya,” kauli iliyoongeza joto katika mjadala wa kisiasa na kuzua swali iwapo Linda Mwananchi itatoa mgombea wake wa urais.

UAMUZI wa Mahakama Kuu uliotolewa Jumatatu iliyopita wa kuthibitisha kuondolewa mamlakani kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua Oktoba 2024, umeibua changamoto mpya ya kisiasa kwa Naibu Rais Kithure Kindiki, hasa katika vita vya ushawishi kuhusu mwelekeo wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Huku wandani wa serikali wakitarajia uamuzi huo ungepunguza ushawishi wa Bw Gachagua katika eneo hilo na kusababisha mabadiliko ya uungwaji mkono kuelekea kwa Profesa Kindiki, wengine wanasema hali imeonekana kuwa tofauti. Rais William Ruto bado ana azma ya kurejesha ngome ya kura ya Mlima Kenya iliyomuunga mkono pakubwa katika uchaguzi wa 2022. Hata hivyo, wachambuzi wanasema moja ya changamoto zake kubwa ni jinsi ya kupunguza ushawishi wa Bw Gachagua unaoonekana kuendelea kushamiri katika eneo hilo. “Bila shaka Rais Ruto angependa kurejesha Mlima Kenya ambao kwa kiasi kikubwa ulimwezesha kuwa rais mwaka 2022. Changamoto yake ni jinsi ya kukabiliana na ushawishi wa Bw Gachagua. Baada ya kujaribu mbinu kadhaa za kisiasa katika kipindi cha miezi 20 iliyopita bila mafanikio makubwa, uamuzi wa kumwondoa ungekuwa na manufaa kwake iwapo wafuasi wa Gachagua wangeukubali kama kushindwa. Lakini hilo halijafanyika,” alisema Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya. Bw Natembeya aliongeza kuwa uamuzi huo umeonekana kuibua huruma kwa Bw Gachagua hata nje ya nyanja za siasa, ikiwa ni pamoja na katika sekta ya sheria. “Kilichojitokeza ni mjadala wa kitaifa, hata miongoni mwa wanasheria, wengi wao wakionyesha wasiwasi kuhusu hukumu iliyotambua ukiukaji wa haki za Gachagua lakini bado ikaidhinisha kuondolewa kwake,” alisema. Seneta wa Murang’a, Joe Nyutu, alisema kulikuwa na matarajio kuwa Profesa Kindiki angepata nguvu zaidi kisiasa endapo wapigakura wa Mlima Kenya wangekubali uamuzi huo na kuendelea mbele bila Bw Gachagua. “Hali sivyo ilivyo. Tunachoshuhudia ni maoni ya umma yanayoonekana kutoridhishwa na uamuzi huo, jambo linaloongeza upinzani dhidi ya serikali na kudhoofisha nafasi yake 2027,” alisema Bw Nyutu. Kwa mujibu wa seneta huyo, Profesa Kindiki anahusishwa na matukio yaliyopelekea kuondolewa kwa Bw Gachagua madarakani. “Katika fikra za wengi, Profesa Kindiki anaonekana kama aliyenufaika na mchakato wanaohisi haukuwa wa haki. Taswira hiyo imekuwa vigumu kuondoa,” alisema. Hata hivyo, Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri alimtetea Naibu Rais, akisema ameingizwa bila haki katika mvutano wa kisiasa uliokuwepo kabla ya uteuzi wake. “Profesa Kindiki alihudumu kama Waziri wa Usalama wa Ndani katika serikali ile ile ambayo Gachagua alikuwa Naibu Rais. Gachagua alitofautiana na viongozi wengi wa Mlima Kenya wakaungana dhidi yake. Rais Ruto akamteua Kindiki. Si sahihi kisiasa kudhani angekataa,” alisema Bw Kiunjuri. Mbunge wa Manyatta Gitonga Mukunji, alisema Profesa Kindiki anajikuta upande usiopendelewa na hisia za kisiasa katika eneo hilo. “Haiwezi kuepukika kuwa anahudumu katika serikali inayokabiliwa na upinzani mkali katika Mlima Kenya. Kwa haki au bila, anabeba lawama za serikali,” alisema. Kwa upande wake, Mbunge wa Mbeere Kaskazini Leo Wamuthende, alisema upinzani unalenga kudhoofisha viongozi wa serikali kisiasa. Naye Mbunge wa Gatundu Kaskazini Elijah Kururia, alisema uamuzi wa mahakama umeimarisha nafasi ya Profesa Kindiki kikatiba, akihimiza wakazi wa Mlima Kenya kumchukulia kama uwekezaji wa kisiasa wa siku zijazo. Hata hivyo, Mwakilishi wa Kike wa Kirinyaga Njeri Maina, alisema serikali ya Rais Ruto bado inakabiliwa na upinzani mkali katika eneo hilo, jambo linalomtwika Prof Kindiki mzigo mkubwa wa kisiasa. Utafiti wa hivi majuzi wa TIFA ulionyesha kuwa serikali ya Rais Ruto inaungwa mkono na asilimia 11 pekee katika Mlima Kenya, huku asilimia 89 wakionyesha kutoridhika nayo. Utafiti huo huo ulipata Bw Gachagua ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa zaidi katika eneo hilo kwa asilimia 70. Wachambuzi wanasema takwimu hizo zinaonyesha ukubwa wa changamoto inayomkabili Profesa Kindiki katika kujijenga kama kiongozi mkuu wa serikali katika eneo hilo kuelekea 2027.

SERIKALI haitaanzisha ushuru mpya wala kuongeza viwango vya kodi katika bajeti ya mwaka wa kifedha utakaoanza Julai 2026. Waziri wa Fedha John Mbadi alisema badala yake serikali itazingatia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kupanua wigo wa walipa kodi bila kuwalemea wananchi. Mbadi alisema ameamua kuepuka kuongeza mzigo kwa Wakenya wanaofanya kazi kwa bidii, huku akisisitiza umuhimu wa mageuzi katika mfumo wa ushuru ili kuhakikisha usawa na uwazi. “Kwa makusudi, sijapendekeza ushuru mpya wala kuongeza viwango vya ushuru vitakavyowaongezea mzigo Wakenya. Badala yake, tunalenga kuboresha ukusanyaji mapato, kuleta usawa katika mfumo wa ushuru na kuongeza idadi ya walipa ushuru bila kumlemea mwananchi,” alisema. Alieleza kuwa kwa sasa ni Wakenya milioni 3.1 pekee wanaochangia ushuru kupitia mfumo wa Pay As You Earn (PAYE), ilhali mamilioni ya wengine wanaopata kipato hawachangii. “Wengi wamekuwa wakijaza fomu za ushuru wakionyesha hawapati mapato kila mwaka. Hali hii lazima ibadilike,” aliongeza.

SERIKALI inapanga kukopa zaidi ya Sh1 trilioni kufadhili bajeti ya mwaka wa kifedha ujao ya Sh4.8 trilioni, huku pengo la bajeti likikadiriwa kufikia takriban Sh1.1 trilioni, Waziri wa Fedha John Mbadi amekiri. Akitoa hotuba yake ya bajeti, Mbadi alieleza kuwa makadirio hayo yatafadhiliwa kupitia mikopo ya ndani na nje ya nchi, ambapo Sh116.2 bilioni zitakopwa kutoka kwa wahisani na taasisi za kimataifa, huku Sh1 trilioni zikitarajiwa kupatikana kupitia mikopo ya ndani. Hatua hii inaonyesha hatua ya serikali ya kutegemea pakubwa kukopa ili kuendesha shughuli na mipango yake, licha ya changamoto zinazohusiana na deni la taifa linaloendelea kuongezeka. Katika sekta ya elimu, serikali imependekeza kutoa Sh7 bilioni kwa mpango wa elimu ya msingi bila malipo, Sh54.6 bilioni kwa elimu ya sekondari ya kutwa bila malipo, na Sh30.7 bilioni kwa ufadhili wa sekondari msingi (JSS). Aidha, Sh4.9 bilioni zimetengwa ili kuajiri walimu 20,000 vibarua kuwa wa kudumu na pensheni kuanzia Januari 2027. Kwa mara ya kwanza, serikali imependekeza pia kutenga Sh3.9 bilioni kulipa posho wazee wa vijiji, hatua inayolenga kuimarisha utawala wa mashinani na kutambua mchango wao katika kuhakikisha usalama na utatuzi wa migogoro ya kijamii. Katika sekta ya afya, Mbadi alipendekeza kutenga Sh20.9 bilioni kwa Mamlaka ya Usambazaji wa Dawa (KEMSA), Sh3.1 bilioni kwa Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu (KEMRI), na Sh9.3 bilioni kwa wahitimu wa mafunzo ya udaktari. Vilevile, Sh10.9 bilioni zimetengwa kwa Chuo cha Mafunzo ya Afya (KMTC), huku wahudumu wa afya wa jamii wakipangiwa Sh3.2 bilioni za posho na Sh396 milioni kwa bima ya afya. Serikali pia imeweka kipaumbele sekta ya kilimo kwa kutenga Sh64 bilioni ili kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na kuimarisha uthabiti wake dhidi ya changamoto kama mabadiliko ya tabianchi. Katika juhudi za kukuza uchumi wa baharini, Sh8.2 bilioni zimetengwa kusaidia uvuvi na shughuli nyingine za baharini. Aidha, sekta ya ubunifu imenufaika na mgao wa Sh8.6 bilioni kukuza filamu, muziki, mitindo, sanaa na teknolojia ya kidijitali, huku sehemu ya fedha hizo zikienda kuimarisha miundombinu ya mtandao wa kitaifa. Katika masuala ya ardhi, serikali imepanga kutenga Sh9.4 bilioni kusaidia kuwapa makazi wananchi wasio na ardhi, hatua inayolenga kupunguza migogoro ya ardhi na kuboresha usawa katika umiliki. Mbadi alisema kwamba uchumi wa taifa unatarajiwa kukua kwa asilimia tano mwaka 2026, kiwango kilichopungua kutoka makadirio ya awali ya asilimia 5.3 kutokana na athari za mizozo ya kimataifa, hususan Mashariki ya Kati. Hata hivyo, aliongeza kuwa uchumi unatarajiwa kuimarika tena mwaka 2027 na kukua kwa asilimia 5.2. Serikali pia inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kama vile masoko ya kisasa, ambapo masoko 476 yanapangwa kote nchini huku 354 tayari yakitekelezwa. Miradi hii inalenga kuwapa wafanyabiashara mazingira bora ya kufanyia kazi na kukuza ujasiriamali. Bajeti hii inaonyesha juhudi za serikali kusawazisha kati ya maendeleo ya kiuchumi, utoaji wa huduma za kijamii na changamoto za kifedha, huku ikiendelea kutegemea mikopo.

There has been a wave of anti-immigrant protests, which have sometimes turned violent.

The speaker position could give the former premier a platform to challenge Faye.

This follows months of growing tensions between the two allies-turned-rivals.

The designation bars him from entering the US over the assault of activists Boniface Mwangi...

WANAHABARI wa Nation Media Group (NMG) ambao walikuwa wakifuatilia maandamano ya bei za juu ya mafuta katika barabara ya Thika, jana walivamiwa na kuibiwa na wahuni. Gari ambalo lilikuwa na wanahabari hao lilizingirwa na wahuni hao kisha wakaporwa. Wavamizi hao waliziba barabara kwa mawe na kuitisha hela kabla gari halijapita. Waliovamiwa walikuwa wanabari wa runinga ya NTV na Daily Nation ambao walikuwa wakirejea Nation Center baada ya kufuatilia maandamano na mgomo wa wahudumu wa matatu miji ya Ruiru na Juja. Walivamiwa katika eneo la Ruiru Bypass. Genge hilo liliingia barabarani, likazunguka gari lao na kuwarushia mawe. Walichukua fulani mbili za kuwatambua kama wanahabari, helmeti kisha kuwapora kamera na mkoba wa kubeba kamera hiyo. Waliokuwa kwenye gari hilo ni ripoti wa runinga ya NTV Labaan Shabaan, mnasa video wa NTV Luis Ngari, ripota wa Daily Nation Kevin Cheruiyot, mpiga picha Evans Habil na dereva wao Bernard Magara. Walipiga ripoti kuhusu uporaji huo katika kituo cha polisi cha Gatongora na bado hali ilikuwa tete eneo hilo waandamanaji wakiziba barabara.

Utu wa polisi umejitokeza kwa namna ya kipekee katikati ya maandamano yaliyotikisa mji wa Machakos, ambapo maafisa wa usalama walionekana wakimsaidia mwanaume mlemavu aliyekuwa amenaswa katika vurugu akielekea hospitalini. Tukio hilo lilishuhudiwa katikati ya taharuki iliyosababisha kufungwa kwa biashara, shule na kusimama kwa shughuli mbalimbali katika mji wa Machakos huku barabara ya Machakos–Kitui ikifungwa na waandamanaji. Polisi walimwagwa maeneo mbalimbali kujaribu kurejesha utulivu na kuwashawishi vijana kufungua njia. Hali ilianza kuwa tete asubuhi baada ya baadhi ya waendesha bodaboda na madereva wa magari binafsi kusitisha shughuli zao wakitaja mgomo uliotarajiwa kuanza saa nne asubuhi. Hata hivyo, baadhi yao waliendelea kutoa huduma kwa wagonjwa na dharura, wakibeba majeruhi na waliohitaji matibabu. Katika hali ya kushangaza, afisa mmoja wa polisi alionekana akimwendea mwanaume mlemavu aliyekuwa amekwama katikati ya vurugu hizo na kumsaidia kufika kwenye bodaboda. Afisa huyo alimsaidia kupandishwa kwenye pikipiki hiyo na baadaye kulipia nauli yake ili aharakishe kufikishwa hospitalini. Wakazi waliokuwa eneo hilo walieleza kuwa tukio hilo lilitoa taswira tofauti ya maafisa wa polisi, ikionyesha huruma na ubinadamu katikati ya mazingira magumu ya usalama. Hata hivyo, hali katikati ya mji wa Machakos iliendelea kuwa ya wasiwasi baadaye mchana baada ya mapambano makali kati ya polisi na waandamanaji, ambapo gesi ya kutoa machozi na risasi za mpira zilirushwa kuwatawanya vijana waliokuwa wakiziba barabara. Katika tukio jingine la kusikitisha, afisa wa polisi alikimbizwa hospitalini baada ya mkebe wa gesi ya kutoa machozi kulipuka mkononi mwake alipokuwa akijiandaa kuurusha kuelekea kwa waandamanaji. Licha ya ghasia hizo, tukio la kumsaidia mlemavu limebaki kuwa alama ya utu katikati ya mvutano mkali uliotawala Machakos.

NAIBU Rais Kithure Kindiki amesema amefanya mkutano mtandaoni na Rais William Ruto ambapo wamejadili suala la mgomo wa wahudumu wa uchukuzi ambao umesababisha shughuli za usafiri kukwama kote nchini. Prof Kindiki amesema haya wakati wa mkutano na viongozi wa Tharaka uliofanyika nyumbani kwake, Irunduni, Kaunti ya Tharaka Nithi. Rais Ruto naye yumo ziarani nchini Azerbaijan. Mgomo wa wahudumu wa uchukuzi ulioanza kutekelezwa saa sita usiku wa kuamkia Jumatatu umelemaza huduma na biashara katika miji mingi huku Nairobi, Kitengela, Meru, Murang’a, Machakos, Kitale ikiwa miongoni mwa iliyoathirika zaidi. Kufikia saa kumi jioni, usafiri bado ulikuwa nadra katika maeneo mengi huku magari machache yaliyoonekana barabarani yakipigwa mawe na vijana au kushurutishwa kuondoka. Katika miji ya Ruiru, Kasarani na Juja, Nairobi, polisi walikuwa na wakati mgumu kukabiliana na makundi ya wakazi walioanza kuimba nyimbo za kukashifu serikali. Polisi walilazimika kurusha vitoa machozi kutawanya waandamanaji huku hali ikiendelea kuwa ya taharuki.

BARABARA kuu Kenya – inayounganisha jiji la Nairobi na mji wa Thika, Jumatatu asubuhi Mei 18, 2026 ilisalia kufungwa kufuatia mgomo wa matatu dhidi ya bei ya mafuta ya petroli uliotekelezwa maeneo tofauti ya nchi. Wamiliki wa matatu, wahudumu, magari ya kibinafsi, teksi na wana bodaboda walisitisha shughuli za uchukuzi wa umma na usafiri, wakitaka bei ya mafuta ya petroli ishushwe. Aidha, wanapinga bei ya juu ambapo Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) mnamo Alhamisi, Mei 14, 2026 ilitathmini bei itakayotumika kati ya Mei hadi Juni 14. EPRA iliongeza bei ya dizeli kwa Sh46.29 kwa lita, huku bei ya petroli ikiongezeka kwa Sh16.65 kwa lita. Hivyo basi, petroli sasa inauzwa Sh214.25 kwa lita na dizeli kwa Sh242.92, huku bei ya mafuta ya taa ikisalia Sh152.78. [caption id="attachment_188192" align="aligncenter" width="300"] Gari Thika Super Highway likitumia leni isiyofaa kwa hofu ya kuvamiwa na waandamanaji. Picha|Sammy Waweru[/caption] Huku sehemu nyingi za taifa haswa mijini uchukuzi wa umma ukisimamishwa, Thika Super Highway, kati ya asubuhi hadi adhuhuri, mnamo Jumatatu, barabara hiyo kuu ilisalia mahame. Ikiwa ni njia yenye shughuli tele za uchukuzi wa umma na usafiri, barabara hiyo kuu Kenya iliyoundwa na Rais mstaafu marehemu Mwai Kibaki, ni magari machache mno yaliyoonekana yakipita. Majira ya saa tatu na nusu hivi asubuhi (9:30am), makarandinga ya polisi yalionekana yakipita kwa kasi kuelekea Githurai 45 na Ruiru, ambapo ilikuwa imefungwa na waandamanaji. Cha kushangaza, baadhi ya magari yalionekana kufanya abautani – yakitumia leni isiyofaa kwa hofu ya kushambuliwa. Kulingana na wahudumu wa matatu, bei ya EPRA inalemaza biashara – hatua ambayo imewalazimisha kuongeza nauli mara dufu. [caption id="attachment_188193" align="aligncenter" width="300"] Karandinga ya polisi Thika Road ikielekea Githurai 45 na Ruiru kufungua barabara iliyofungwa. Picha|Sammy Waweru[/caption] Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Wamiliki wa Matatu, Albert Karakacha, alidokeza kuwa mgomo huo wa Jumatatu ulifanikiwa kwa asilimia 99, na kwamba Wakenya wanapaswa kutarajia hali hiyo hiyo kuendelea hadi Jumanne. “Hilo litaendelea hadi wakati serikali itakapokubali kuketi nasi mezani kwa mazungumzo na wadau husika mafuta ya petroli yashuke.” Maafisa wa polisi wa kawaida na wale wa kukabiliana na ghasia, mchana kutwa walikabiliana vikali na waandamanaji waliofunga barabara Jijini Nairobi, Nakuru, Kisii, Machakos, Makueni, na miji mingine. Magurudumu yaliwashwa moto na waandamanaji, wakionyesha ghadhabu zao dhidi ya bei ya juu ya mafuta ya petroli. Serikali, hata hivyo, imeendelea kutetea bei ya EPRA ikisema mfumko huo unasababishwa na vita vinavyoendelea kati ya Iran na Israili.

Chadema vice-chairman for Mainland Tanzania, Mr John Heche, said Tanzanians can attain a higher standard of living if they elect leaders through a transparent system that protects citizens’ interests.

MGOMO wa kitaifa wa wahudumu wa matatu dhidi ya bei ghali ya mafuta ya petroli ukiendelea mnamo Jumatatu, May 18, 2026, dada wawili katika Kaunti ya Nairobi walijitokeza kuwapa motisha waandamanaji kwa njia ya kipekee. Salome Muchungu na Ann Muchungu, ambao ni wakazi wa mtaa wa Kasarani walitua kwenye barabara kuu ya Thika – Nairobi, maarufu kama Thika Superhighway, kuuza bendera ya Kenya katika kile walichohoji ni ushirikiano na Wakenya kutaka bei ya mafuta ishushwe. “Maisha yamekuwa magumu, tunataka bei ya mafuta ya petroli ipunguzwe tuweze kulea familia zetu bila mahangaiko,” waliambia Taifa Dijitali. Walisema walichagua kuuza bendera kwa sababu ndio nembo ya taifa, na ilionyesha ushirikiano na umoja kwa ajili ya gharama ya juu ya maisha ‘kwa kiasi kikubwa kuchochewa na mfumko wa bei ya mafuta ya petroli’. [caption id="attachment_188177" align="aligncenter" width="300"] Dada wawili, Ann Muchungu na Salome Muchungu wakichuuza bendera mnamo Jumatatu, Mei 18, 2026 Thika Road wakati wa maandamano ya wahudumu wa matatu dhidi ya kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli. Wanasema hatua ya kuuza bender ani ishara ya kuwapa motisha wahudumu wa matatu na ushirikiano. Picha|Sammy Waweru[/caption] Tunaonyesha ushirikiano na umoja kwa Wakenya wenzetu – wahudumu wa matatu, bei ya mafuta ya petroli yapunguzwe, walisisitiza. Walipoulizwa wangetaka ishushwe hadi kiwango kipi, walitumia mfano wa nauli ambayo wamekuwa wakilipa kutoka Kasarani hadi Nairobi kuelekea kazini. “Waume zetu, kila mmoja akitupa Sh200 kuenda kazini kisha nauli iwe Sh100 kwenda jijini Nairobi pekee hatutasalia na pesa zozote za kununulia watoto chakula,” wakasema. Ann, ni mama wa mtoto mmoja huku dada yake, Salome amejaaliwa na watoto wawili. Uchukuzi na usafiri wa umma ulitatizika mnamo Jumatatu kufuatia mgomo wa kitaifa nchini, uliotishwa na miungano ya wamiliki na wahudumu wa matatu, magari ya kibinafsi, teksi na bodaboda. Wanapinga kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli, ambapo Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) mnamo Alhamisi, Mei 14, 2026 ilitathmini bei itakayotumika kati ya Mei hadi Juni 14. [caption id="attachment_188188" align="aligncenter" width="300"] Ann Muchungu akichuuza bendera mnamo Jumatatu, Mei 18, 2026 Thika Road wakati wa maandamano ya wahudumu wa matatu dhidi ya kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli. Picha|Sammy Waweru[/caption] EPRA iliongeza bei ya dizeli kwa Sh46.29 kwa lita, huku bei ya petroli ikiongezeka kwa Sh16.65 kwa lita. Hivyo basi, petroli sasa inauzwa Sh214.25 kwa lita na dizeli kwa Sh242.92, huku bei ya mafuta ya taa ikisalia Sh152.78. Ni nyongeza ambayo tayari athari zake zimeanza kushuhudiwa haswa kwa nauli, chakula na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi. Maafisa wa polisi na wale wa kukabiliana na ghasia, katika maeneo tofauti nchini walikabiliwa na kibarua kigumu kufungua barabara. Thika Super Highway, kwa mfano, Jumatatu asubuhi ilisalia kufungwa Wakenya wengi wanaofanya kazi jijini Nairobi na mitaa mingine wakitatizika kuripoti gangeni.

MBUNGE wa Makadara George Aladwa sasa anataka UDA iachie ODM kiti cha ugavana wa Nairobi akitaka suala hilo lijumuishwe kwenye muafaka kati ya vyama hivyo viwili kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Bw Aladwa pia ametaka ODM iruhusiwe iwasimamishe viongozi wake katika viti inavyovishikilia kwa sasa maeneo mbalimbali jijini. “Ikiwa Makadara ni ngome ya ODM, basi UDA haifai kuwa na mgombeaji hapo. Vivyo hivyo, ODM haitakuwa na wagombeaji ambako UDA ina uungwaji mkono jijini,” akasema Bw Aladwa. Alikuwa akiongea kwenye ibada ya kanisa Jumapili ambapo alisisitiza kuwa chama hicho hakifai kusalia na makombo ilhali kinaunga mkono azma ya Rais Ruto. “Tunataka kiongozi wa chama chetu Oburu Oginga afuatilie hili kwa sababu tumempa ruhusa ya kujadiliana na UDA. Hata hivyo, ODM lazima idumishe umaarufu wake jijini Nairobi,” akasema Bw Aladwa. Bw Aladwa mwenyewe ametangaza kuwa yuko tayari kuwania kiti cha ugavana wa Nairobi kinachoshikiliwa na Gavana Johnson Sakaja wa UDA. Bw Sakaja pia analenga kukitetea kiti chake mnamo 2027. Kwa mujibu wa Bw Aladwa, kauli ya Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar kwamba chama hicho kitasimamisha wagombea kote nchini inaweza kusababisha mgongano na ODM. "Katibu Mkuu wa UDA si mwenyekiti wa chama. Rais Ruto ndiye mtu pekee anayeweza kutoa mwelekeo wa chama, na ndiye atakayefanya mazungumzo hayo na kiongozi wa ODM,” akaongeza Bw Aladwa. Mbunge huyo pia aliingilia mzozo kati ya Waziri wa Fedha John Mbadi na Mbunge wa EALA Winnie Odinga akisema viongozi hao wanastahili kumakinikia umaarufu wa chama badala ya malumbano yasiyokuwa na maana. "Wote wawili ni viongozi wetu na tunawaheshimu. Masuala yao yanaweza kutatuliwa kwa maelewano. Tumeona walichosema na hakuna kosa lolote katika hilo. Changamoto chache zinatarajiwa kujitokeza baba wa familia anapoondoka, na hilo ndilo tumekuwa tukipitia kama chama lakini polepole tunasonga mbele. Tuna imani na uongozi wa Dkt Oginga."

KIONGOZI wa familia ya marehemu Raila Odinga, Raila Junior, jana aliwataka baadhi ya wanasiasa wa ODM kuheshimu familia hiyo. Kumekuwa na vuta nikuvute kati ya Waziri wa Fedha John Mbadi na familia ya Raila kutokana na matamshi ambayo waziri alitoa Mei 4 katika warsha ya ODM jijini Mombasa. Matamshi ya Mbadi yalifasiriwa na baadhi ya watu kama ya kumdhalilisha marehemu Raila, na yameshuhudia majibizano makali kati yake na mjane Ida Odinga, Mbunge wa EALA Winnie Odinga na Mbunge Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Kisumu Ruth Odinga. Akiongea katika uwanja wa Jacaranda, Nairobi, jana alipokutana na wakazi wa eneo hilo, Junior alifichua kuwa alifanya kikao na kinara wa sasa wa ODM, Dkt Oburu Oginga, ambapo alihimiza kuchukuliwe hatua kali dhidi ya viongozi wanaomkosea heshima marehemu babake. “Kuna matamshi mengi hasi yanatolewa dhidi ya familia. Tunachoomba viongozi ni wawe wavumilivu, na kuonyesha heshima wanapotaja familia yetu na namna wanavyoizungumzia,” akasema Junior. Alieleza kwamba alikuwa amekimya na kujiepusha na siasa tangu mauti ya babake, ila sasa itabidi ajitokeze kupambana na wanaoshambulia familia hiyo na kuidhalilisha. Kuhusu uongozi ndani ya ODM, Junior alisema wanamheshimu Dkt Oginga kama kinara wa chama hicho lakini pia wanataka kama familia washirikishwe katika masuala yanayohusu chama hicho. “Kama familia ya Raila tunataka kuwa na usemi kuhusu yanayoendelea ndani ya ODM. Kama mwanawe Raila nahisi vibaya jinsi watu wanazungumza hapa nje na mkondo ambao mambo yanachukua. “Tafadhali koma kuzungumzia familia ya baba, uwe waziri au katibu. Hii tabia lazima ikome,” akahoji. Junior alidokeza kuwa ana maelezo kuhusu jinsi marehemu babake alitaka familia hiyo iongozwe kwa sababu alikuwa akiandamana naye kwenye mikutano mingi kabla ya mauti yake. Alikataa kuzungumza iwapo wanaegemea mrengo wa Linda Mwananchi au Linda Ground, akisema yeye si mwanasiasa na wanafuata mwelekeo wa dada yake, Winnie. Hata hivyo, alisema babake hafai kushambuliwa mautini ilhali baadhi ya viongozi ambao wanafanya hivyo ndiyo walikuwa wakinufaka kutokana na uongozi wake na hata aliwakuza na kuwalea kisiasa. Mnamo Jumamosi, Mbadi alimkabili Winnie vikali akimtaka awanie kiti cha kisiasa kisha achaguliwe ndipo amzungumzie kuhusu masuala ya kiuchumi katika wizara ya fedha.

FAMILIA zinazoishi katika maeneo ambayo huathiriwa na mafuriko Kaunti ya Tana River, zimetaka serikali itafute suluhisho la kudumu ili kushughulikia suala la kuhama kila mara mvua nyingi inaponyesha maeneo ya juu nchini. Katika kijiji cha Bularahma kilicho Galili, Tana Delta, maji ya mafuriko yamezamisha mashamba na kuacha makazi yakiwa yamezingirwa na maji kiwango cha maji kwenye Mto Tana kikipanda. Mafuriko hayo pia yanahusishwa na maji kufurika kutoka baadhi ya mabwawa ya Seven Forks yanayotumiwa kuzalisha umeme na kampuni ya KenGen. “Maji yalijaa yakaharibu mashamba yetu. Tulikuwa tumepanda mboga, nyanya na matunda lakini kila kitu kikaharibika,” Bi Nina Ali Kulo, mkazi, alisema akikadiria hasara. Familia zinazoishi katika kijiji hicho zinajiandaa kuhama, na kutatiza tena maisha yao. Bw Said Zajardul anasema jamii zilihamia kijiji hicho baada ya kuhamishwa na mafuriko eneo la Gamba. Makumi ya makazi yameathirika katika eneo hili pekee. “Sasa wanalazimika kuhama tena. Wamekata miti ili waende kujenga kwingine. Wameteseka kwa zaidi ya miaka 12,” akasema Bw Zajardul. Katika kijiji jirani cha Lango la Simba, Bw Joseph Masila anatumia mashua yake ndogo kupitia maji ya mafuriko akitafuta vifaa vya ujenzi. Anasema kuhama mara kwa mara ni mzigo mkubwa wa kiuchumi na unaumiza sana familia ambazo tayari zinapitia ugumu. “Kila mara unapohama unalazimika kuanza upya. Wakati utakaporejea kwako pia utakuta mali ulizoacha zimeharibika, kwa hivyo utaanza tena maisha,” akasema kwa masikitiko. Kwa mujibu wa wakazi, mafuriko yanaleta pia mamba na nyoka, pamoja na magonjwa ya maji na yale yanayoenezwa na mbu. Bw Masila anasema usumbufu huu wa mara kwa mara pia umeathiri elimu katika eneo hilo. Bw Mohamed Golo ni miongoni mwa mamia waliotoka kijiji cha Bandi huko Gamba, lakini akalazimika kuhama tena baada ya mafuriko kuharibu makazi yao ya muda upande mmoja wa barabara Minjila. Karibu watu 400 wamehamia eneo la Minjila kwa usalama wao, na sasa wanalazimika kuishi upande mmoja wa barabara ambao hauathiriwi na mafuriko. Bw Golo anasema serikali ya kaunti iliruhusu wajenge nyumba hapo, lakini wengi ni maskini na hutegemea mahema yaliyotolewa na Shirika la Kenya Red Cross. Bw Bobode Ali, mmoja wa waliokumbwa na mafuriko, alieleza changamoto za kutegemea mahema kama makazi. “Hizi hema tulipewa na Red Cross lakini sasa zimetoboka. Mvua inaponyesha, huwa kwavuja ndani. Pia kuna joto jingi humo ndani, kisha wazazi na watoto wote wanalala kwa hema moja, hakuna usiri,” akaeleza. Katika kambi hizo, wanategemea sana wahisani kwa chakula, maji safi na mahitaji mengine muhimu kama vile vyandarua na dawa. Hali hii kwa familia ambazo zimezoea kujitegemea inawapokonya utu wao. Wakazi wengi wamebaki wakijiuliza kwa nini mabwawa hayawezi kujengwa kuhifadhi maji badala ya kuyaacha yaelekee Bahari ya Hindi. Serikali ya Kaunti ya Tana River ilishauri waathiriwa kuhamia maeneo ya juu huku juhudi zikifanywa kuweka suluhu za kudumu. Gavana Dhadho Godhana alisisitiza kuwa, serikali ya kaunti ina mpango unaoendelea wa kuwahamisha wakazi wanaoishi katika maeneo hatari kwenda katika vijiji salama watakavyojengewa.

BAADHI ya viongozi wa ODM kutoka Kaunti ya Kisumu wameonya chama hicho kwamba hawatakubali demokrasia ya maafikiano katika kinyang’anyiro cha ugavana mnamo 2027, wakisisitiza kuwa wapigakura lazima wapewe nafasi ya kuchagua viongozi wanaowataka. Wakiongozwa na Mbunge wa Muhoroni, James Onyango K’Oyoo, Mbunge wa Kisumu Kati, Joshua Oron, pamoja na zaidi ya wanachama 20 wa Bunge la Kaunti ya Kisumu (MCAs), viongozi hao wameapa kupinga msimamo wa chama na kufuata mkondo wao wa kisiasa iwapo uteuzi wa mgombea wa ugavana hautakuwa wa haki na huru. Bw K’Oyoo, ambaye anaunga mkono azma ya Dkt Oron ya kuwania ugavana, alianza kwa kutangaza kuwa hawatakubali uamuzi wowote wa vikao vya siri ambao utampa mgombea mwengine tiketi ya moja kwa moja. “Tunataka kuambia ODM kwamba wakati huu hakuna mambo ya mtu kuletwa na cheti. Cheti pekee tutakachokubali ni chako wewe (Dkt Oron) kwa sababu ya yale ambayo umefanya na uungwaji mkono ulio nao kwa sasa,” akasema Bw K’Oyoo. Alikuwa akizungumza katika uwanja wa Shule ya Upili ya Withur, wadi ya Kabonyo Kanyagwal eneobunge la Nyando. Hafla hiyo ilitumiwa na ukoo wa Kano kutoka Kaunti ndogo ya Kadibo kutangaza kuwa wanaunga mkono azma ya Dkt Oron wakimtaja kama kiongozi ambaye atatimiza miradi ya maendeleo na kuinua eneo hilo kisiasa. “Kama ilivyo Nyando, Muhoroni pia inaunga mkono Dkt Oron na tunajua kuna watu watakuja na pesa, lakini waelewe kuwa wakati huu hatutabadili msimamo wetu kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa chama,” akaongeza Bw K’Oyoo. Kinyang’anyiro cha ugavana wa Kisumu kimezua ushindani mkali ndani ya ODM, huku suala la usawa wa uwakilishi wa maeneo likitawala mijadala ya kisiasa miongoni mwa wanaotafuta kuungwa mkono. Mbali na Dkt Oron, wengine waliotangaza nia ya kuwania kiti hicho ni Seneta wa Kisumu Tom Ojienda, Naibu Gavana wa Kisumu, Mathews Owili, Mbunge wa Nyakach Aduma Owuor, Gavana wa kwanza wa Kisumu Jack Ranguma, pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Kisumu Kati Ken Obura. Gavana Anyang’ Nyong’o, ambaye anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho, amekuwa kimya na hajatangaza hadharani mwaniaji anayemuunga. “Nina matumaini kwamba nitawashinda wapinzani wangu ndani ya ODM kwa sababu hata kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge, nilikuwa nikifanya kazi kwa ajili ya watu wetu. Miradi niliyoanzisha na kukamilisha hapa Nyando ipo wazi kwa kila mtu kuona, na nitakapokuwa gavana, kazi yangu ya kwanza itakuwa kuboresha miundombinu ambayo ni duni katika eneo hili,” akasema. Bw Oron ambaye anahudumu muhula wake wa kwanza. Mwanasiasa mkongwe wa Nyando Lumumba Ouya ‘Kalausi’ alisema kuna wagombea wengine wa ugavana wanaowachanganya wapigakura na wanapaswa kupuuzwa. Hafla hiyo ilihudhuriwa na zaidi ya madiwani 20 wa Bunge la Kaunti, aliyekuwa mgombea wa ugavana na sasa anayewania ubunge wa Muhoroni Dkt Hezron Mc’Obewa, ambaye alivutia hisia mnamo 2017. baada ya kuongoza kampeni ya ugavana iliyokuwa ya kifahari na iliyopangwa kwa ustadi mkubwa.

TAHARUKI inaendelea kutanda katika Kaunti ya Kilifi kutokana na tishio la usalama baada ya makundi ya uhalifu kuendelea kutishia wakazi, biashara na sekta ya utalii. Viongozi wamejitokeza kukashifu kudorora kwa usalama wakiitaka idara ya usalama kudhibiti hali ambayo inazidi kuzorota. Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, ambaye aliongoza kikao cha kiusalama baada ya kuongezeka kwa visa vya utovu wa nidhamu na hofu ya usalama katika kaunti hiyo, aliwataka viongozi kuimarisha ushirikiano na serikali, vyombo vya usalama, na kuandaa baraza za umma ili kuelimisha wakazi kuhusu jukumu muhimu la polisi kwa jamii katika kudhibiti usalama mitaani. Katika kikao hicho kilichoongozwa na Kamanda wa Polisi wa Ukanda, Bw Ali Nuno, Kamati ya Usalama ya Kaunti ya Kilifi, wabunge wa Kilifi akiwemo Bw Owen Baya (Kilifi Kaskazini) na mwenzake wa Malindi, Bi Amina Mnyazi, waliamua kushirikiana ili kuhakikisha kuna usalama Kilifi. “Tumejadili matukio ya hivi karibuni na kuongezeka kwa hofu ya usalama, na tumekubaliana kwa pamoja kuimarisha operesheni za usalama katika maeneo yote yaliyoathirika yakiwemo Malindi, Gede, Kakuyuni, Mayungu, Mtwapa, Mji wa Kilifi na makazi mengine ya Kaunti,” alisema Gavana Mung’aro. Bw Mung’aro alisema serikali yake imejitolea kushirikiana na maafisa wote wa usalama kuhakikisha utulivu unarejea. Bw Baya, alisema viongozi na vyombo vya usalama wameweka mikakati kabambe ya kukabiliana na hali ya usalama inayozorota katika kaunti hiyo. Alisema mkutano huo ulilenga kupanga na kuimarisha operesheni za usalama ili kudhibiti makundi ya wahalifu. “Tumekutana na vyombo vya usalama kupanga na kuweka mikakati ya kuboresha hali ya usalama inayozorota. Tutakabiliana na magenge ya wahalifu. Mawoza, wabakaji na wahalifu hawatatuendesha, tutawakabili ipasavyo,” alisema Bw Baya akisisitiza kuwa usalama wa wakazi wa Kilifi ni kipaumbele na akahimiza ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na vyombo vya usalama ili kuhakikisha usalama. Aliyekuwa Waziri wa Jinsia, Bi Aisha Jumwa alisema suala la usalama linazidi kuwasumbua wakazi wa Kilifi. “Suala la usalama limekuwa tishio na kero kwa wakazi wa Kilifi. Lakini vyombo vya usalama vinaendelea na operesheni madhubuti ya kurejesha amani na usalama, na havitayumbishwa wala kuzuiwa kutekeleza wajibu wao,” alisema Bi Jumwa. Aliwasihi wananchi kuwapa maafisa wa usalama nafasi ya kufanya kazi yao ili kuwaondoa wahalifu hao. “Hatutakubali jamii yetu kuendelea kuishi kwa hofu kutokana na vitendo vya kihalifu. Sheria itachukua mkondo wake dhidi ya yeyote atakayehusika na uhalifu. Tutapigana na wahuni,” alisema Bi Jumwa.

WAZIRI wa Fedha John Mbadi anaonekana kuimarisha juhudi za kudhibiti siasa za Luo Nyanza na kuamua mwelekeo wa ODM baada ya mauti ya marehemu Raila Odinga. Akiwa kati ya wanasiasa walioshirikiana na marehemu Odinga kwa miaka mingi, Bw Mbadi anaonekana kuchukua mwelekeo ambao utahakikisha ana ushawishi mkubwa eneo hilo 2027 na hata 2032. Waziri huyo, alitangaza kuwa hatawania kiti chochote cha kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao. Kauli ya waziri huyo kwenye video aliyoweka kwenye ukurasa wake wa Facebook kutokana na mkutano wa ODM mnamo Mei 4, jijini Mombasa, umezua mdahalo baadhi wakifasiri alimkosea heshima marehemu Raila. “Huwezi kutuambia kuwa baba alisema hili au baba hakusema lile. Huyo baba yuko wapi atupee ushahidi kuhusu kile alichosema au hakusema,” akasema Bw Mbadi akionekana kuwa na hasira. “Ni miezi sita na baba alitufanyia mengi lakini nasi tulipigania baba. Haingekuwa sisi, basi baba hangekuwa mtu wa hadhi yake alipokufa,” akasema Bw Mbadi. Kauli yake imezua maoni mseto miongoni mwa wafuasi wa ODM kwenye mitandao ya kijamii. Wakati baadhi waliiona kama kutoheshimu Raila, wengine walimtetea Bw Mbadi wakisema chama kinapaswa kukubali ukweli kwamba kiongozi wake wa muda mrefu hayupo tena na kuanza kujipangia mustakabali wake. Matamshi hayo yamemweka Bw Mbadi kwenye mvutano na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kisumu Ruth Odinga, ambaye aliwashutumu baadhi ya viongozi kwa kushindwa kudumisha umoja wa ODM. Bi Odinga alimshutumu waziri huyo kwa kudharau jina la Odinga ambalo alilitumia kujikweza kisiasa. Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Mbadi alisema matamshi yake hayakuwa na chochote kibaya ila kila mtu ana hiari ya kuifasiri jinsi anavyotaka. “Raila alitujenga, lakini kama jamii ya Waluo, tulifanya kazi kubwa sana kumuunga mkono. Wapo wanaounga mkono nilichosema na wapo wanaopinga, na sioni tatizo lolote katika hilo,” akasema. “Sioni jambo lolote la kuomba msamaha kwa sababu mimi ndiye niliyeachia video hiyo hadharani, na sina uwezo wa kudhibiti jinsi mtu anavyoitafsiri,” akaongeza. Ijumaa iliyopita, Bw Mbadi alitawazwa kuwa mlezi wa Baraza la Wazee wa Luo, Tawi la Nairobi, hatua ambayo baadhi ya wachanganuzi wa kisiasa wanaiona kama sehemu ya mikakati ya kuimarisha nafasi yake kisiasa. “Muhimu zaidi, nataka kuwahakikishia wazee na jamii kwa ujumla kuhusu dhamira yangu ya kweli ya kuwatumikia kwa bidii na kwa uaminifu katika nafasi hii ya ulezi waliyonipa,” alisema. Katika miezi ya hivi karibuni, Bw Mbadi ameongeza kwa kiasi kikubwa shughuli zake za kisiasa kote Nyanza. Mara kwa mara amekuwa akitumia helikopta kuhudhuria mazishi, hafla za michango na mikutano ya kisiasa, huku akijaribu kuimarisha uungwaji mkono wa Rais Ruto katika eneo hilo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Bw Mbadi aliwahi kuwa Mbunge wa Gwasi kati ya mwaka 2007 na 2013 kabla ya kuchaguliwa tena mwaka 2013 na 2017 kama Mbunge wa Suba Kusini, baada ya eneo hilo kubadilishwa jina. Mwaka 2022, alikuwa ameonyesha nia ya kuwania ugavana wa Homa Bay, lakini alishawishiwa na marehemu Odinga kumuunga mkono Gladys Wanga. Hata hivyo, wakati wa hafla ya umma iliyohudhuriwa na Rais Ruto na marehemu Odinga huko Homa Bay mnamo Mei 30, 2025, Bw Mbadi alitangaza kuwa hatawania nafasi yoyote ya kisiasa mwaka 2027.

KUHAMISHWA kwa magunia 26, 220 ya sukari inayoshukiwa kuwa hatari kutoka bohari ya Mombasa kwenda Nairobi kupitia Reli ya Kisasa (SGR) kumeibua hofu bungeni, huku wabunge wakieleza kwamba huenda tayari imeingia sokoni na kutumiwa na wananchi wasio na habari. Shehena hiyo ni sehemu ya zaidi ya tani 27,839 za sukari iliyodaiwa kuingizwa nchini kwa matumizi ya viwandani Januari 15 2026. Hata hivyo, sasa wabunge wanataka Bodi ya Sukari Kenya kutoa majibu ya kina kuhusu mchakato mzima wa usafirishaji, uhifadhi na iwapo sukari hiyo imeingia katika biashara ya kawaida. Katika kikao na Kamati ya Bunge kuhusu Biashara, Viwanda na Ushirika, wabunge walihoji Kaimu Afisa Mkuu wa Kaunti wa Bodi ya Sukari Kenya, Jude Chesire, kuhusu jinsi sukari hiyo ilivyohamishwa kutoka Mombasa hadi Nairobi bila taarifa za wazi za usalama. Bw Chesire alishindwa kueleza kwa kina nambari za mabehewa ya SGR yaliyobeba magunia hayo 26,220 na pia hakuweza kutoa majina ya mabohari ambayo sukari hiyo inadaiwa kuhifadhiwa baada ya kufikishwa Nairobi, jambo lililozua shaka zaidi miongoni mwa wabunge. “Tunahitaji stakabadhi hizi kwa dharura ili kuhakikisha maisha ya Wakenya yanalindwa,” alisema Mwenyekiti wa kamati hiyo, Benard Shinali, akionya kuwa ukosefu wa uwazi unaweza kuhatarisha afya ya umma. Naibu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Marianne Keitany, alihoji kwa nini mzigo huo uliondolewa Mombasa na kupelekwa Nairobi kabla ya kukamilika kwa taratibu za uhakiki na usalama. “Afisa huyu si mkweli; hivi ndivyo sukari hatari ilivyoingia sokoni miaka iliyopita. Kwa nini haikubaki Mombasa hadi mmiliki apate vibali?” alihoji Bi Kitany. Mbunge wa Mathare, Anthony Oluoch, aliunga mkono kauli hiyo akisema kuwa historia ya bidhaa hatari kuingia sokoni mara nyingi huanza kwa kuhamishwa ghafla kati ya mabohari. “Mara nyingi tunaambiwa bidhaa iko salama, kuna timu ya mashirika mbalimbali, lakini baadaye tunakuta bidhaa hiyo sokoni tayari,” alisema. Hata hivyo, Bw Chesire alijaribu kuwahakikishia wabunge kwamba sukari hiyo haijawahi kuingia sokoni na bado iko chini ya ulinzi mkali wa polisi. Alieleza kuwa sukari hiyo iliingizwa ikiwa ghafi kwa matumizi ya viwandani na bado iko katika bohari la forodha ndani ya Mamlaka ya Bandari ya Kenya (KPA), Mombasa, ikisubiri kukamilishwa kwa taratibu za forodha. “Mzigo huu haujawahi kusambazwa nchini. Bado umehifadhiwa salama Mombasa chini ya ulinzi mkali,” alisema. Stakabadhi zilizowasilishwa bungeni zinaonyesha kuwa mzigo huo ulipata kibali cha forodha Aprili 24 2026, na usafirishaji wake ulianza Mei 2, 2026, huku mabehewa 19 ya kwanza yakifika Nairobi Mei 3, 2026 yakiwa na magunia 26,220. Bodi ya Sukari ilisisitiza kuwa sukari hiyo ni ya viwandani, ambayo si salama kwa matumizi ya binadamu na hutumika katika viwanda kama vile mikate, vinywaji na usindikaji wa chakula. Serikali pia ilieleza kuwa iliunda kikosi cha mashirika mbalimbali ikijumuisha Bodi ya Sukari, KRA, KEBS, Wizara ya Viwanda na Polisi ili kusimamia uingizaji na matumizi yake na kuzuia kuingizwa sokoni. Hata hivyo, wabunge walitaka majibu zaidi, wakionya kuwa ukosefu wa uwazi unaweza kuhatarisha afya ya mamilioni ya Wakenya iwapo sukari hiyo itaingia sokoni kwa siri.

DAKTARI mtaalamu wa moyo Daniel Gikonyo jana aliambia Mahakama Kuu kuwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alikuwa mgonjwa kweli na hakujifanya ili kukwepa Seneti wakati wa mchakato wa kumtimua ofisini huku kicheko, kejeli na majibizano makali yakitawala kikao kilichokuwa na mvutano mkubwa wa kikatiba. Dkt Gikonyo pia alieleza kuwa alimuarifu Rais William Ruto kuhusu hali ya afya ya Gachagua baada ya kupata idhini yake. Kikao hicho cha majaji watatu kiligeuka kuwa cha aina ya kipekee, huku mawakili wakipinga stakabadhi za hospitali zinazodai kuwa Gachagua alilazwa Hospitali ya Karen Oktoba 17, 2024 kutokana na maumivu makali ya kifua. Kiini cha kesi hiyo ni iwapo kulazwa hospitalini kulikuwa kwa kweli au mbinu ya kukwepa kikao cha Seneti kilichoishia kumuondoa madarakani usiku huohuo. Dkt Gikonyo, mwanzilishi wa Hospitali ya Karen, alisisitiza kuwa mgonjwa alihitaji matibabu ya haraka na alikuwa chini ya uangalizi wake. “Nilikuwa nikimtibu pamoja na timu yangu. Alikuwa mgonjwa. Tuna data,” alisema. Mvutano uliongezeka baada ya wakili wa Naibu Rais Prof Kithure Kindiki kudai Gachagua alijilaza hospitalini ili kukwepa Seneti. Kauli hiyo ilisababisha kicheko kortini kabla daktari kupinga. Alieleza kuwa vipimo vilifanywa na akapendekeza alazwe kwa saa 48 hadi 72 kwa uangalizi. Majadiliano yalichukua mvutano zaidi kuhusu majina ya mgonjwa, baada ya stakabadhi kuonyesha herufi “R.G” badala ya jina kamili. Daktari alieleza kuwa hilo lilikuwa kulinda faragha ya mgonjwa. Mahakama iliendelea kujawa na vicheko huku mawakili na daktari wakibadilishana maneno makali kuhusu stakabadhi za matibabu. Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa.

HUKU wapigakura wa eneobunge la Emurua Dikirr, Kaunti ya Narok wakielekea katika vituo vya kupigia kura leo kuchagua mbunge mpya, macho yataelekezwa katika pambano kali la kisiasa kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa Naibu wake, Rigathi Gachagua. Uchaguzi huo mdogo umegeuka kuwa kipimo muhimu cha nguvu za kisiasa kati ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na chama kipya cha Democracy for Citizens Party (DCP) kinachoongozwa na Bw Gachagua. Rais Ruto anataka chama chake kihifadhi kiti hicho kilichobaki wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge Johana Ng’eno, huku Bw Gachagua akitarajia kupata ushindi wa kwanza wa chama chake katika Bunge la Kitaifa. Bw Ng’eno alifariki Februari 28, 2026 baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria kuanguka katika eneo la Mosop, kaunti ya Nandi. Katika ajali hiyo, rubani George Were, mpiga picha Nick Kosgei, mwalimu Carlos Kibet Keter, askari wa Huduma ya Misitu Kenya (KFS) Amos Kipngetich Rotich na afisa wa itifaki wa serikali ya Narok Wycliff Kiprotich Rono pia walipoteza maisha. Masuala aliyokuwa akipigania marehemu sasa yamekuwa msingi wa kampeni za uchaguzi huo mdogo. Barabara mbovu, ukosefu wa hospitali bora, uhaba wa maji safi na miundombinu duni ni baadhi ya masuala yanayotawala kampeni huku serikali ikilaumiwa kwa kuwasahau wakazi baada ya uchaguzi mkuu. Wagombeaji watano wameidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kushiriki uchaguzi huo. Wanaopigiwa upatu ni David Kipsang Keter wa UDA na Vincent Rotich wa DCP. Wengine ni Desma Cherono wa PNU, Gideon Koech wa NVP na Keneth Kiprono wa RLP. Uchaguzi huo umeonekana kuwa wa hadhi ya juu kwa kuwa unafanyika miezi 16 kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, huku kila upande ukitaka kuonyesha kuwa una ushawishi mkubwa katika eneo la Bonde la Ufa ambalo lina kura nyingi. Wakili wa Nairobi Kipkirui Kemboi Kap Telwa alisema uchaguzi huo ni mtihani mkubwa kwa UDA. “Uchaguzi wa Emurua Dikirr utaonyesha iwapo Rais Ruto bado ana ushawishi katika Bonde la Ufa. Wakazi wa eneo hilo wamewahi kuasi viongozi walio mamlakani hapo awali,” alisema. Aliongeza kuwa tangu mwanzo, ilikuwa wazi kuwa Rais, Naibu wake Kithure Kindiki na mawaziri hawakukaribishwa kufanya kampeni eneo hilo kwa sababu wangemletea mgombea wa UDA madhara badala ya faida. Bw Gachagua pia alitarajiwa kufanya kampeni eneo hilo lakini akashauriwa asifanye hivyo kwa madai ya sababu za kiusalama. Rais Ruto, licha ya kuwa na makazi katika eneobunge jirani la Kilgoris, hajahudhuria hafla yoyote Emurua Dikirr tangu mazishi ya Bw Ng’eno Machi 6. Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki pia hakufanya kampeni eneo hilo licha ya kuongoza kampeni za UDA katika maeneo mengine hapo awali. Katika hatua isiyo ya kawaida, viongozi wakuu wa UDA waliinua mikono na kuwaachia viongozi wa eneo hilo kuendesha kampeni. Gavana wa Narok Patrick Ntutu pia hakushiriki moja kwa moja kampeni hizo na badala yake alimtuma naibu wake Tamalinye Koech kuongoza shughuli za kampeni. Inasemekana Bw Ntutu hakuelewana kisiasa na Bw Keter na alikuwa amemuunga mkono Bennard Ngeno, aliyekuwa msaidizi wa marehemu Ng’eno, wakati wa kura za mchujo za UDA. Katika kura hizo za mchujo zilizofanyika Machi 27, Bw Keter alipata kura 13,749 dhidi ya kura 13,394 za Bw Ngeno. “Tumefanya kampeni kubwa za nyumba kwa nyumba na tuna imani tutashinda kiti hicho,” alisema Bw Tamalinye. Kwa upande mwingine, DCP ilipata nguvu baada ya ushindi katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Narok Town mwaka jana ambapo mgombeaji wake alimshinda yule wa UDA.

HATUA ya chama cha Jubilee kusimamisha mgombea wake katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Ol Kalou unaotarajiwa Julai imeonekana kutikisa chama cha Democracy for Citizens Party (DCP), kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. Muungano huo wa upinzani,unahofia kuwa vyama hivyo, vinaweza kugawanya kura na kupatia chama cha United Democratic Alliance (UDA) ushindi kirahisi. Chama cha People’s Liberation Party kinachoongozwa na Martha Karua, ambacho pia ni sehemu ya muungano huo, kimemteua Martin Wambugu kuwania kiti hicho. Hali imekuwa ngumu zaidi baada ya wagombeaji wote wa Jubilee na UDA walioshindwa kwenye kura za mchujo kutangaza kumuunga mkono mgombea wa chama chao, huku wagombeaji watatu pekee kati ya wanane wa DCP wakikubali kumuunga mkono mshindi Kamau Ngotho. Bi Beatrice Kamau na Bw Isaac Wanjiru waliokuwa wamejitosa kwenye kura za mchujo za Jubilee, walisema wanaunga mkono uamuzi wa chama hicho kumpa tiketi Mhandisi Wilson Kigwa. Bi Kamau alisema tayari amekubaliana na Bw Kigwa kwamba angempa nafasi wakati huu kwa kuwa alikuwa amejiandaa zaidi kisiasa. “Nilihisi sikuwa tayari kikamilifu kwa uchaguzi huu mdogo ambao ulitangazwa ghafla baada ya kifo cha marehemu David Kiaraho. Nitamuunga mkono mgombea wa Jubilee kwa sababu nina imani na chama hicho,” alisema. Bw Wanjiru naye alisema atamuunga mkono Bw Kigwa huku akijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka ujao. Wachambuzi wa siasa wanasema idadi ya wapiga kura waliojitokeza katika kura za mchujo haiwezi kutumika kutabiri matokeo ya uchaguzi mdogo wa Julai 16. Wanasema kuna uwezekano hata mgombea huru au wa chama kidogo kushinda kutokana na mgawanyiko uliopo. Sababu nyingine inayotajwa ni siasa za ndani za eneo hilo ambazo zinaweza kuathiri uchaguzi huo licha ya umaarufu ambao DCP inadaiwa kuwa nao. Aliyekuwa waziri Maina Kamanda, alisema DCP inataka kuepuka migogoro ya ndani iliyogharimu Jubilee katika uchaguzi mdogo wa Rurii mwaka 2021 na uchaguzi mkuu wa 2022. Katika uchaguzi mdogo wa Rurii, makundi mawili yaliyokuwa yakimuunga mkono mgombea wa Jubilee yalijitokeza, moja likiongozwa na aliyekuwa gavana Francis Kimemia na jingine na aliyekuwa Waziri Sicily Kariuki. Migogoro hiyo ilipelekea mgombea wa UDA Francis Muraya Githaiga kushinda na kuwa kiongozi wa kwanza wa UDA kuchaguliwa Nyandarua. Mvutano huo uliendelea hadi uchaguzi mkuu wa 2022 wakati Bi Kariuki alikataa kufanya kampeni za pamoja na Bw Kimemia. Sasa siasa hizo zimeibuka tena katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou. Bw Kimemia anamuunga mkono mgombea wa Jubilee Wilson Kigwa, huku Bi Kariuki akimuunga mkono mgombea wa DCP Kamau Ngotho. Mwakilishi wa wanawake Faith Gitau, ambaye pia anawania ugavana wa Nyandarua mwaka 2027, anamuunga mkono mgombea wa UDA Muchina Nyaga. Bi Gitau alisema UDA haitakumbwa na migogoro ya ndani kwa sababu yeye ndiye mgombea pekee wa ugavana ndani ya chama hicho. Alisema UDA itashinda uchaguzi huo kwa kishindo licha ya DCP kudai kupata idadi kubwa ya wapiga kura katika kura za mchujo. Naibu kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alitilia shaka uhalali wa kura za mchujo za DCP akisema kila mtu aliruhusiwa kupiga kura bila kuwa mwanachama rasmi wa chama hicho. Kwa upande mwingine, DCP ina wagombeaji watatu wa ugavana wanaotumia uchaguzi huo kujitangaza kisiasa. Bw Kamanda alisema viongozi hao wanapaswa kufanya kazi pamoja ili kuepuka migawanyiko iliyowahi kuangusha Jubilee. Bw Kimemia alikiri kuwa migogoro ya ndani iligharimu Jubilee katika chaguzi zilizopita lakini akasema kwa sasa anajikita katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou.

KAGERA: Utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR) umeendelea kutajwa kuwa suluhisho muhimu katika kuimarisha amani na mshikamano katika familia na jamii, huku wananchi wakihimizwa kutumia njia za mazungumzo na usuluhishi badala ya kufikishana mahakamani kwa migogoro inayoweza kumalizwa kwa njia ya maridhiano. Hayo yamewekwa wazi katika mafunzo ya kuyajengea uwezo mabaraza ya Usuluhishi wa … The post Mabaraza ya usuluhishi yatakiwa kutanguliza maridhiano first appeared on HabariLeo.

DAR ES SALAAM: Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Mhe. Jackson Kiswaga, ameeleza kuwa licha ya Serikali kuwekeza kiasi kikubwa cha takriban Sh trilioni 4 katika miradi ya maji, changamoto ya huduma hiyo bado ni kubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi na ongezeko kubwa la watu. Kiswaga aliyasema hayo wakati … The post Kiswaga atahadharisha mabadiliko tabianchi first appeared on HabariLeo.

UJENZI wa mradi wa bwawa la Mwache wa Sh20 bilioni unakabiliwa na matatizo ya kifedha ambayo yanahatarisha kukwamisha kukamilika kwa mradi huo kwa wakati uliopangwa. Bwawa hilo lenye kina cha mita 84 na ambalo linatarajiwa kuhifadhi zaidi ya mita milioni 127 za maji, linaendelea kwa kasi ya chini zaidi na linaweza kusimama iwapo serikali haitatoa Sh1.9 bilioni kwa ajili ya fidia na kazi nyinginezo. Wanachama wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Maji, Umwagiliaji na Uchumi wa Bahari walieleza hofu kuhusu kucheleweshwa kwa mradi huo, lakini wakaendelea kuwa na matumaini kuwa Hazina ya Taifa itatoa fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo. [caption id="attachment_188004" align="alignnone" width="2000"] Rais William Ruto wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Bwawa la Mwache, Kwale, Aprili 6, 2023. Bwawa hili lilitarajiwa kukamilika ndani ya miezi 36. Picha|Maktaba[/caption] Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Kangogo Bowen, alisema serikali imetenga Sh52.8 bilioni kwa mwaka wa kifedha wa 2026/2027 kusaidia mradi huo. “Tuna matumaini kuwa fedha za mwaka ujao wa kifedha zitatolewa kama ilivyopangwa na kwa wakati ufaao, kwani ucheleweshaji wowote utakwamisha mradi huu kabisa,” alisema Bw Bowen. Bw Bowen alisema fedha hizo zitasaidia kukamilisha ujenzi wa mtambo wa kusafisha maji pamoja na uwekaji wa mabomba ya usambazaji maji. Kamati hiyo wakati wa ziara yake ilithibitisha kuwa kampuni ya Sinohydro Corporation Limited inayotekeleza mradi huo imeripoti kupungua kwa kasi ya kazi kutokana na madeni ambayo hayajalipwa ya kiasi cha Sh1.9 bilioni. Mradi wa bwawa la Mwache ambao kwa sasa umefikia asilimia 83 unatarajiwa kuongeza usambazaji wa maji kwa Mombasa ambayo kwa sasa ina upungufu wa asilimia 75, na pia utatoa maji ya umwagiliaji kwa zaidi ya ekari 6,000 kwa wakulima wa Kwale.

CHAMA cha Orange Democratic Movement kimeanzisha mikakati ya ndani ya kujitathmini kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 huku kukiwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wake bila kiongozi wake wa muda mrefu Raila Odinga, kugombea urais. ODM sasa imewaalika wanachama wanaotaka kuwania nyadhifa mbalimbali kupitia tiketi ya chama hicho kuwasilisha maombi yao katika hatua ambayo viongozi wa ndani wanasema inalenga kupima nguvu na udhaifu wa chama katika maeneo mbalimbali nchini. Kupitia zoezi hilo, ODM inalenga kubaini maeneo ambayo bado ina ushawishi mkubwa kisiasa na yale ambayo huenda yanaanza kuitema baada ya Bw Odinga. Katika tangazo lililochapishwa kwenye magazeti ya humu nchini, ODM imewaalika wanaotaka kuwania urais, ugavana, useneta, wawakilishi wa kike, ubunge na wawakilishi wa wadi kuwasilisha maombi yao kabla ya Juni 30. Tofauti na chama cha United Democratic Alliance cha Rais William Ruto pamoja na chama cha Democracy for the Citizens Party kinachohusishwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambavyo vinatoza hadi Sh50,000 kwa usajili wa wagombeaji, ODM haitaki ada yoyote. “Lengo letu ni kujua maeneo tulio na nguvu kisiasa. Orodha ya wanaotuma maombi itatusaidia kupanga mikakati ya uchaguzi wa 2027,” afisa mmoja wa ODM alisema. Kwa miaka mingi, ODM imekuwa ikitegemea ngome zake za kisiasa katika maeneo ya Nyanza, Magharibi, Pwani, Turkana, sehemu za Kaskazini Mashariki na jamii ya Wamaasai. Hata hivyo, viongozi wa chama wana hofu kuwa hali inaweza kubadilika 2027 kwa kuwa Bw Odinga hayupo kwenye kinyang’anyiro cha urais. Wakati huo huo, ODM inakabiliwa na mgawanyiko wa ndani kuhusu iwapo inafaa kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027. Mgawanyiko huo umezaa makundi mawili yanayoshindana ndani ya chama, moja likiongozwa na kinara wa chama Oburu Oginga chini ya kaulimbiu ya Linda Mwananchi na lingine likihusishwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna. Lengo la mkakati mpya wa ODM ni kurejesha imani ya wanachama katika mchakato wa uteuzi wa wagombeaji ambao kwa miaka kadhaa umekumbwa na lawama za wizi wa kura na utoaji wa tiketi za moja kwa moja. Katika kikao cha chama kilichofanyika Mombasa hivi majuzi, ODM iliagiza Kamati ya Kitaifa ya Kuratibu Uchaguzi (NECC) kuweka mifumo itakayohakikisha haki na uwazi katika kura za mchujo. Chama hicho pia kilikataza utoaji wa tiketi za moja kwa moja. “Tumeagiza kamati ya uchaguzi kubuni mifumo madhubuti ya kuhakikisha kura za mchujo zinafanyika kwa njia ya haki, uwazi na uaminifu,” chama kilisema. Ripoti ya ndani ya ODM ya mwaka 2023 ilibaini kuwa mfumo wa kidijitali uliotumika katika kura za mchujo za 2022 ulikuwa na mianya iliyowezesha udanganyifu. Ripoti hiyo ilionyesha kuwa baadhi ya vifaa vya kupigia kura havikuwa na mfumo wa kuzuia wizi wa kura huku baadhi ya wagombeaji wakidaiwa kushirikiana na maafisa wa uchaguzi kuvuruga mfumo huo. Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM, Gladys Wanga, alikiri kuwa kura za mchujo zimekuwa tatizo kubwa kwa chama hicho. “Timu ya uchaguzi imepewa maagizo madhubuti kuhakikisha kuna mfumo unaoaminika na unaowapa wagombeaji nafasi sawa,” Bi Wanga alisema. Mbunge wa Uriri Mark Nyamita, alisema ufanisi wa ODM mnamo 2027 utategemea uwezo wake wa kuendesha kura za mchujo za haki. “Tumaini pekee la ODM mwaka wa 2027 ni kura za mchujo zilizo huru, za haki na za kuaminika,” alisema Bw Nyamita.

SENETI imetilia shaka ushahidi wa matibabu uliowasilishwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika kesi inayoendelea kuhusu kuondolewa kwake mamlakani. Kupitia Karani wa Seneti Jeremiah Nyegenye, Seneti pamoja na Spika Amason Kingi imehoji uhalali, muda na stakabadhi za hospitali zilizowasilishwa na daktari wa moyo Daniel Gikonyo. Seneti inasema rekodi hizo zina utata, zina mapungufu na hazikuwahi kuwasilishwa mbele ya maseneta wakati wa kusikizwa kwa kesi ya kumbandua Gachagua ofisini. Gachagua na walalamishi wengine 40 wanadai Seneti ilikiuka haki yake ya kusikizwa kwa haki kwa kuendelea na mchakato huo wakati alikuwa mgonjwa na kulazwa hospitalini. Dkt Gikonyo aliambia mahakama kuwa, Gachagua alilazwa Oktoba 17, 2024 akiwa na maumivu makali ya kifua yaliyohitaji matibabu ya dharura na uangalizi wa saa 48 hadi 72. Hata hivyo, Seneti sasa inasema ripoti ya hospitali inaonyesha Gachagua alilazwa Oktoba 17 na kuruhusiwa kuondoka Novemba 20, hali ambayo inaashiria alikaa hospitalini kwa siku 31. Seneti inasema muda huo unakinzana na maelezo ya daktari huyo na unafanya ushahidi huo kutiliwa shaka. Pia Seneti imehoji kwa nini mawakili wa Gachagua hawakuwasilisha stakabadhi hizo wakati wa kusikizwa kwa kesi licha ya kuahidi kufanya hivyo.

IRINGA: Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamezindua kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Isimani kwa kumwaga sifa kwa mgombea wa chama hicho, Emanuela Kaganda Mtatifikolo, wakieleza kuwa anastahili kupewa jimbo hilo kwasababu ya rekodi yake ya utendaji, uwezo wa kusimamia maendeleo na ukaribu wake kwa wananchi. Uzinduzi wa kampeni hizo ulifanyika katika Kata ya … The post Mgombea amwagiwa sifa, CCM ikizindua kampeni Isimani first appeared on HabariLeo.

WAKAZI wa kijiji cha Chesongo, Baringo Kati, wamebaki wakishangaa baada ya daraja jipya la watembea kwa miguu kusombwa na mafuriko saa chache tu baada ya kuzinduliwa rasmi. Daraja hilo lilizinduliwa Jumapili na Afisa Mkuu wa Kilimo wa Kaunti ya Baringo, Milka Toromo, ambaye pia anawania kiti cha ubunge cha Baringo Kati. Hata hivyo, usiku huo huo mafuriko makubwa yalilisomba daraja hilo lililokuwa limejengwa kwa chuma na simiti. Kwa miaka mingi, wakazi walikuwa wakitumia daraja la mbao kuvuka mto huo hasa wakati wa mvua. Watoto wa shule ndio wamekuwa waathiriwa wakuu kwa kulazimika kuhatarisha maisha yao kila mto ulipofurika. Wakazi walichanga Sh500 kwa kila familia kujenga daraja jipya lakini fedha hazikutosha. Bi Toromo na wafadhili wengine walichangia zaidi ya Sh150,000 kukamilisha mradi huo. Mkazi Vincent Kiloo alisema alitumia daraja hilo kupeleka mtu hospitalini Jumapili mchana lakini Jumatatu akaarifiwa lilikuwa limesombwa. “Bado nashangaa jinsi daraja la chuma na simiti linaweza kusombwa ndani ya siku moja ilhali lile la mbao lilidumu zaidi ya miaka mitano,” alisema. Wakazi walipata mabaki ya daraja hilo umbali wa mita 200 chini ya mkondo wa mto. Baadhi ya wakazi sasa wanadai daraja hilo lilijengwa vibaya kwa kutumia vifaa dhaifu. “Hilo daraja lilikuwa janga linalosubiri kutokea,” alisema mkazi mwingine, Edwin Chacha. Alisema wakazi walikuwa wameonya kuwa chuma zilikuwa dhaifu mno kuhimili nguvu za mafuriko. Wakazi sasa wanaomba serikali ya kaunti kuwasaidia kujenga daraja jipya huku watoto wakilazimika kubebwa mgongoni kuvuka mto kwenda shule.

WASHINGTON, Amerika: MATUMAINI ya kupatikana kwa muafaka kati ya Amerika na Iran yalididimia Jumanne baada ya Rais Donald Trump kusema mazungumzo yalikuwa yanaelekea kusambaratika. Hii ni baada ya Iran kukataa pendekezo la Amerika la kumaliza vita hivyo na kushikilia orodha ya matakwa yake ambayo lazima yatimizwe. Trump alikuwa amerejelea orodha hiyo kama ‘takataka’. Iran ilikuwa imependekeza mwisho wa vita hivyo ushirikishe hadi Lebanon ambako Israel, mshirika wa Amerika, inapambana na Kundi la Hezbollah. Aidha, Iran ilisisitiza kuwa mkondo wa mafuta wa Strait of Hormuz ni himaya yake wala haufai kuingiliwa na pia ikataka fidia kutokana na uharibifu wa mali na maafa yaliyotekelezwa na Amerika. Isitoshe, ilitaka Amerika iondoe meli zake ambazo zimezuia uchukuzi Pwani mwa Iran kati ya masharti mengine. Trump Jumanne alisema Iran haina nia ya kumalizwa kwa vita hivyo na mazungumzo hayo yaliyoanza Aprili 7 baada ya kusitishwa kwa vita, yananingínia padogo. Maafisa wa Iran nao wametoa kauli zinazoashiria kuendelea kuwa imara licha ya shinikizo za Amerika katika vita hivyo. Ripoti ya shirika la habari la Fars ilimnukuu Mohammad Akbarzadeh, naibu mkurugenzi wa masuala ya kisiasa wa Jeshi la Wanamaji la IRGC, akisema kuwa Iran imeongeza udhibiti wake wa Strait of Hormuzz na kuugeuza kuwa makao makuu ya oparesheni zake za kijeshi. Mnamo Jumatatu, Amerika iliweka vikwazo vipya dhidi ya watu binafsi na kampuni ilizodai zinasaidia Iran kusafirisha mafuta hadi China, kama sehemu ya juhudi za kuzuia ufadhili wa kijeshi na nyuklia kwa Iran. Haya yanajiri huku Trump akitarajiwa kuwasili Beijing leo, ambapo suala la Iran linatarajiwa kuwa miongoni mwa mada zitakazojadiliwa na Rais wa China Xi Jinping. Mzunguko wa meli kupitia Strait of Hormuz umepungua sana ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya vita. Takwimu za usafirishaji kutoka kampuni za Kpler na LSEG zilionyesha kuwa meli tatu za mafuta ghafi zilivuka njia hiyo wiki iliyopita zikiwa zimezima vifaa vyao vya ufuatiliaji ili kuepuka kushambuliwa na Iran. Nchini Amerika, tafiti zinaonyesha kuwa vita hivyo havina uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa raia, ambao sasa wanakabiliwa na ongezeko la bei ya mafuta chini ya miezi sita kabla ya uchaguzi wa kitaifa. Uchaguzi huo utakaamua iwapo chama cha Republican cha Trump kitaendelea kudhibiti Bunge la Congress.

Kenyan President also pushed for a shift from historical bilateral tensions toward a...

RAIS William Ruto amefanya mabadiliko makubwa katika mkakati na kikosi chake cha wanasiasa washirika katika eneo la Mlima Kenya, hatua inayolenga kuimarisha uungwaji mkono kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Hatua hiyo inajiri huku aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua, akiendelea kushambulia vikali serikali ya Kenya Kwanza katika eneo hilo lenye kura nyingi. Katika mkakati huo mpya, Rais anategemea kikosi cha wanasiasa, wataalamu wa serikali na viongozi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) ili kuimarisha ushawishi wake. Kinara wa mkakati huo ni Naibu Rais Kithure Kindiki, ambaye ameibuka kama mhimili mkuu wa juhudi za kuimarisha uungwaji mkono wa serikali katika eneo hilo. Profesa Kindiki sasa anaongoza kile kinachotajwa kama “kikosi cha kampeni” ya Rais Mlima Kenya, akichanganya uhamasishaji wa kisiasa, ujumbe wa maendeleo ya serikali na mipango ya mawasiliano ili kurejesha imani ya wananchi. Katika mikutano ya hadhara ya hivi karibuni, Rais Ruto amekuwa akimsifu wazi wazi Naibu wake, akionyesha imani naye na hata kuwataka wananchi kuthibitisha uungwaji mkono wao. Kauli hiyo imechochea tetesi kuwa Profesa Kindiki huenda akawa mgombea mwenza wa Rais katika uchaguzi wa 2027. Miongoni mwa viongozi walioko katika kikosi hicho ni Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah na Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri, ambaye pia ni kiongozi wa chama cha TSP. Wengine ni pamoja na Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma Amos Gathecha, mwenyekiti wa bodi ya uchaguzi ya UDA Anthony Mwaura, Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, Waziri wa Ardhi Alice Wahome, Katibu wa Nishati Alex Wachira na Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni. Aliyekuwa Waziri wa Biashara Moses Kuria na baadaye mshauri mkuu wa uchumi, anaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika mikakati ya kisiasa ya Rais, hasa katika uhamasishaji wa mashinani. Katika ngazi ya chama, Gavana wa Embu Cecily Mbarire ambaye pia ni mwenyekiti wa kitaifa wa UDA, anasimamia shughuli za chama na kuimarisha miundo ya mashinani. Viongozi wengine wanaosaidia juhudi hizo ni Mbunge wa Mathira Eric Wamumbi, Mbunge wa kuteuliwa Sabina Chege, Mbunge wa Maragua Mary Wamaua, Mwakilishi wa Wanawake wa Murang’a Betty Maina, Seneta wa Nyeri Wahome Wamatinga, Gavana wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki na Gavana wa Meru Mutuma M’Ethingia. Kwa mujibu wa wachambuzi, mkakati huo unalenga kuunganisha maendeleo ya serikali na ujumbe wa kisiasa ili kuwavutia wapigakura, huku ukijibu madai ya upinzani kuwa eneo hilo limetengwa. Katika mikutano yake, Profesa Kindiki amekuwa akisisitiza kuwa kuunga mkono muhula wa pili wa Rais Ruto mwaka 2027 kutafungua njia kwa Mlima Kenya kupata urais mwaka 2032. “Ni rahisi kungoja miaka mitano kuliko kumi. Huo ndio mkakati wa kisiasa,” amesema katika mikutano ya hivi karibuni. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Multimedia Profesa Gitile Naituli anasema mbinu ya Naibu Rais kupunguza mashambulizi dhidi ya Gachagua ni ya kimkakati, ingawa huenda isitoshe kubadili hisia za wapigakura. Hata hivyo, kivuli cha Rigathi Gachagua kinaendelea kutanda katika eneo hilo, akiwa amejitangaza kama mtetezi wa maslahi ya Mlima Kenya na kukosoa serikali kwa madai ya kupuuza eneo hilo. Wakati huo huo, juhudi za Rais Ruto zinajiri huku kukiwa na mazungumzo ya kisiasa na Orange Democratic Movement (ODM), hatua inayoweza kubadilisha mwelekeo wa siasa za kitaifa. Kwa sasa, mkakati wa Rais unaonekana kulenga kudumisha uungwaji mkono wa Mlima Kenya huku akipanua ushawishi wake kitaifa—mizani ambayo wachambuzi wanasema itakuwa muhimu katika safari yake ya kutetea kiti chake mwaka 2027.

SENETA wa Nairobi, Edwin Sifuna, amesema bado hajaamua atagombea wadhifa gani katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, licha ya umaarufu anaopata kupitia mrengo wake wa Linda Mwananchi ndani ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM). Akizungumza jana, Bw Sifuna alisisitiza kuwa juhudi zake hazilengi maslahi yake binafsi bali ustawi wa wananchi, akiongeza kuwa anataka kujikita katika mjadala wa pamoja unaoweka wananchi mbele. “Tulicho nacho ni wazo la maslahi ya wote, linaloungwa mkono na wananchi. Tunapaswa kuwaambia kuwa hatutawaangusha. Tunapotaka mabadiliko ya uongozi, lazima pia tutoe sababu ya kuaminika kwamba tuko tayari kuchukua nafasi hiyo,” alisema. Alisema mwelekeo huo ndio unaomsukuma kushiriki katika juhudi za kumshinda Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027, akidai maoni kutoka kwa wafuasi wake yanaonyesha hamu ya “kuikomboa nchi” kutoka kwa utawala wa sasa. Akizungumza katika kituo cha redio cha Spice FM, Bw Sifuna, aliyejitaja kama kinara wa jamii ya Abaluhya, alisema mpango wake wa kwanza ni kuzuru maeneo mbalimbali nchini pamoja na washirika wake ili kukusanya maoni ya wananchi na kuunda mkakati madhubuti wa kisiasa. “Sifuna kuwa rais? Si kuhusu Sifuna. Kwanza tunajenga vuguvugu lenye nguvu. Tunahitaji idadi ya kutosha kushinda serikali. Masuala ya azma binafsi tutayashughulikia baadaye. Hii lazima iwe kampeni ya wananchi,” alisema. Aliongeza kuwa mtazamo wake umechochewa na marehemu Raila Odinga, ambaye alisema alimhimiza kusimama upande wa wananchi bila woga. “Raila alinifunza kuwa ukiwa upande wa wananchi, huna cha kuogopa. Hilo ndilo linafanya shughuli za Linda Mwananchi kufanikiwa,” alisema. Bw Sifuna pia alidai kuwa marehemu Odinga hakuwahi kuunga mkono azma ya Rais Ruto ya kuchaguliwa tena mwaka 2027, akisema aliamini kuwa Rais huyo amedhoofika kisiasa. Kwa mujibu wake, upinzani wake dhidi ya serikali hauchochewi na chuki bali ni kutokana na kile alichokitaja kuwa kuvunjwa kwa matarajio ya wananchi waliopiga kura mwaka 2022. “Vijana hasa wamesema wazi wanataka serikali hii iondoke. Wanataka uhuru na utawala unaozingatia Katiba,” alisema. Alishutumu serikali kwa kutoa ahadi zisizotekelezeka na kutumia miradi ya maendeleo vibaya. “Maendeleo ni mazuri, lakini lazima yawe na nia njema. Hauwezi kujenga barabara ili kurahisisha utekaji wa vijana. Jenga viwanja vya michezo, lakini kwa uwazi katika zabuni. Hauwezi kuwapa vijana fedha bila kusema ni mkopo wa Benki ya Dunia,” alisema. Aidha, alimkosoa Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw Kipchumba Murkomen, kwa madai ya kusambaza taarifa zisizo na msingi kuhusu ufadhili wa vuguvugu lake. Bw Sifuna alikanusha madai kwamba wanapokea fedha kutoka kwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, akisema shughuli zao zinafadhiliwa na michango ya wanachama na wafadhili binafsi. “Wanaodai hivyo hawajatoa ushahidi. Tunaweza kuonyesha jinsi tunavyojifadhili. Hata mkutano wa Kisumu ulifadhiliwa na wanachama na wafadhili wengine,” alisema. Alisema wafuasi wa ODM wameungana kupinga kuchaguliwa tena kwa Rais Ruto. “Wafuasi wote wa ODM hawataki Rais Ruto arejee madarakani. Hakukuwa na uamuzi wowote wa chama kumuunga mkono. Maoni tuliyopokea yanaonyesha wazi hawamtaki,” alisema. Alisisitiza kuwa upinzani lazima ujibu kilio cha wananchi kwa kurejesha utawala unaozingatia uwazi, haki na uadilifu. “Hatuwezi kuendelea na mfumo ambao unaathiri ajira na huduma za umma. Tunataka kurejesha misingi ya haki na uwajibikaji nchini,” alisema.

AFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) bado haijamkabidhi msanii wa Bongo Flava kutoka Tanzania, Sefu Shabani Ramadhan almaarufu Matonya, stakabadhi muhimu za ushahidi zinazohusiana na kesi ya ubakaji inayomkabili. Mahakama iliambiwa jana kuwa upande wa mashtaka haujajitayarisha kikamilifu na kwa sasa hauna vielelezo vinavyomhusisha msanii huyo na tuhuma zinazomkabili. Aidha, mahakama ilifahamishwa hakimu aliyekuwa akisimamia kesi hiyo awali amepandishwa cheo kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Upande wa mashtaka uliiomba mahakama kutoa mwelekeo zaidi kuhusu hatua zinazofuata kabla hawajapata stakabadhi muhimu. Stakabadhi hizo zinajumuisha maelezo ya mashahidi, ripoti za matibabu zinazothibitisha madai ya ubakaji pamoja na ushahidi wa kisayansi unaoweza kumhusisha Matonya na tukio hilo. Matonya alitiwa kizimbani kwa madai ya kutekeleza kitendo hicho cha unyama kwenye mjengo mmoja mtaani Nyali. Ni mashtaka aliyokana msanii huy wa Bongo na akapewa dhamana ambayo amekuwa akisakasaka kuipata ili aweze kufanya kesi hiyo akiwa nje. Alinyimwa chaguo la kutoa pesa taslimu baada ya upande wa mashtaka kuambia Mahakama kuwa si Mkenya, hivyo basi si salama kumwachilia kwa pesa taslimu. Kama sehemu ya masharti hayo, alitakiwa kuwasilisha pasipoti yake mahakamani. Hata hivyo, Matonya kwa sasa yuko huru baada ya kuwasilisha stakabadhi zilizohitajika na mahakama ili kuondoka gerezani alikokuwa amezuia. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Juni 17.

KIGOMA; SERIKALI ya Tanzani imeifunga rasmi kambi ya wakimbizi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma, iliyokuwa ikihifadhi wakimbizi wa Burundi. Hatua ya kufunga kambi hiyo imekuja baada ya wakimbizi zaidi ya 166,000 waliokuwa wakihifadhiwa kwenye kambi hiyo kurudishwa nchini mwao, huku Waziri wa mambo ya Ndani, Patrobas Katambi akihimiza umuhimu wa kutunza amani ya … The post Serikali yafunga kambi ya Nduta, yahimiza amani first appeared on HabariLeo.

DAR ES SALAAM; Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), kupitia Mpango wa Ubunifu wa FUNGUO, limehitimisha kwa mafanikio hafla ya utoaji wa Tuzo za YouthIgnite Awamu ya Tatu sambamba na kuzindua dirisha la tano la ufadhili wa kichocheo. Hatua hiyo inalenga kuimarisha ujasiriamali unaoongozwa na vijana pamoja na mifumo ya ubunifu … The post UNDP yanogesha ujasiriamali kwa vijana Dar first appeared on HabariLeo.

GEITA; TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Geita imewafikisha mahakamani watumishi sita wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita kwa tuhuma za ubadhirifu wa Sh milioni 261.4 za mirathi. Watumishi hao wa mahakama na watumishi wanne wa idara zingine za serikali pamoja na wafanyabiashara wanne walifikishwa katika mahakama hiyo na kufunguliwa … The post Vigogo 6 wa mahakama kortini fedha za mirathi first appeared on HabariLeo.

DODOMA: MBUNGE wa Jimbo la Malinyi, Dk. Mecktridis Mdaku, ameiomba Serikali kuchukua hatua za makusudi za kuboresha Sekta ya kilimo wilayani humo, akisisitiza kuwa maboresho ya miundombinu na upatikanaji wa ardhi ndiyo suluhu ya kuinua uchumi wa wakulima wadogo na wa kati. Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa … The post Dk Mecktridis ahamasisha kilimo cha kisasa first appeared on HabariLeo.

DAR ES SALAAM: BENKI ya Ushirika (Coop Bank) imeendelea kuimarisha mkakati wake wa kukuza uchumi jumuishi kwa kuongeza kiwango cha utoaji mikopo kwa sekta ya kilimo, hatua inayolenga kuongeza tija kwa wakulima na kuchochea uzalishaji nchini. Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Godfrey Ng’urah, amesema benki imejipanga kuwa mshirika muhimu wa … The post Benki ya ushirika yaimarisha mkakati uchumi jumuishi first appeared on HabariLeo.

DODOMA: Serikali imesisitiza kuwa, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatoa kipaumbele cha pekee kwa ushiriki wa vijana katika maendeleo, kwa lengo la kuinua vipaji, uwezo, na ari yao katika kufanikisha ukuaji wa uchumi jumuishi. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, … The post Serikali yasisitiza ushiriki wa vijana Dira 2050 first appeared on HabariLeo.