WAGONJWA wa saratani nchini wameibua wasiwasi kuhusu kucheleweshwa kwa matibabu, kukataliwa kwa maombi ya dawa na kupunguzwa kwa kiwango cha fedha wanacholipiwa na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).
Wanasema mfumo mpya wa kuidhinisha matibabu umewalazimu kulipa fedha za ziada ili kupata huduma ambazo awali ziligharamiwa kikamilifu na bima ya afya.
Katika Hospitali ya Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH), kati ya maombi 30 ya matibabu yaliyowasilishwa kwa SHA Jumatatu, ni 12 pekee yaliidhinishwa.
Daktari mmoja mtaalamu wa saratani alisema hata wagonjwa walioidhinishwa walitakiwa kuongeza fedha kutoka mifukoni mwao.
Alitaja mgonjwa wa saratani ya utumbo aliyelazimika kulipa Sh20,000 kwa vipimo, licha ya kuwa awali gharama hizo zililipwa na SHA.
Daktari alisema hali hiyo imacha wagonjwa wasiojiweza kifedha wakisimamisha matibabu kwa kukosa pesa za kuongeza.
Mgonjwa mmoja wa saratani ya matiti alisema kiwango chake cha fedha za kununua dawa ya Letrozole kimepunguzwa hadi Sh5,400, ilhali anahitaji zaidi ya Sh20,000 kwa dawa hiyo inayosaidia kudhibiti ukuaji wa saratani inayochochewa na homoni.
“Ninahitaji zaidi ya Sh20,000 kununua dawa zangu. Kiasi hicho kinapopunguzwa nalazimika kuongeza fedha za ziada. Bila dawa hizo huenda nishindwe kudhibiti homoni,” akaeleza.
Mfumo huo mpya pia umeongeza muda wa kusubiri dawa hospitalini. Maombi ya matibabu sasa yanahitaji kupitishwa na muuguzi, daktari mtaalamu na mfamasia kabla ya kuidhinishwa.
Muuguzi katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta alisema foleni katika kliniki za saratani zinaongezeka huku wagonjwa wakingoja vibali.
Mgonjwa Mary Adhiambo pia alisema kituo cha saratani cha Texas kimeacha kuuza dawa kwa wagonjwa wanaopokea matibabu katika hospitali zingine, na badala yake kuwataka wahamie huko.
Mabadiliko hayo yameathiri wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na Hospitali ya Mafunzo, Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH), ambao awali walinunua baadhi ya dawa katika vituo vingine.
Mkurugenzi wa muungano wa mashirika ya kansa Kenya Network for Cancer Organisations, Phoebe Ongadi, alitaka SHA kueleza sababu za mabadiliko hayo na jinsi wagonjwa watakavyolindwa.
“Kwa nini mfumo unabadilishwa na kuathiri matibabu? Saratani haisubiri. Hatupaswi kuchezea matibabu ya wagonjwa,” alisema Ongadi.
Hata hivyo, SHA ilisema mabadiliko hayo yanalenga kuboresha huduma kwa kuoanisha matibabu na mwongozo wa kitaifa wa saratani pamoja na kuweka viwango sawa vya bei za dawa na huduma.Iliongeza kuwa kiwango cha fedha kinategemea mwongozo wa matibabu, bei zilizoidhinishwa na masharti ya ufadhili.
Vile vile, ilisisitiza kuwa wagonjwa hawapaswi kutozwa tena kwa huduma ambazo tayari zimelipiwa na mamlaka hiyo, na gharama zozote za ziada zinapaswa kuelezwa wazi na kuthibitishwa.
Mamlaka hiyo ilisema kila mgonjwa anastahili kupata kifurushi cha Sh800,000 cha matibabu ya saratani, kinachojumuisha Sh400,000 kupitia SHIF (Bima ya Afya ya Jamii) na Sh400,000 kutoka kwa hazina ya magonjwa ya dharura, sugu na hatari.




