Top headlines and developing stories from Tanzania, Kenya, Uganda and the wider region, gathered from the leading local and international newsrooms and updated throughout the day.
"KAZI MMEIONA HAMJAIONA?" - RAIS SAMIA ATUA KILIMANJARO - APIGA TENA SELFIE KWA KUTUMIA SIMU YAKE... Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na kuzungumza…
KIGOMA: JESHI la Magereza wilayani Kibondo mkoani Kigoma limeanza kutumia mkaa mbadala unaotokana na mchanganyiko wa maranda ya miti na udongo unaozalishwa ndani ya gereza hilo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Serikali la matumizi ya nishati safi ya kupikia. Hayo yamebainika wakati wataalamu kutoka Wizara ya Nishati walipotembelea gereza hilo kwa lengo … The post Gereza la Kibondo labuni mkaa mbadala nishati safi first appeared on HabariLeo.
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imegeukia matumizi zaidi ya data ya kisayansi katika Taasisi ya Kitaifa ya Usajili (NRB) na Idara ya Huduma za Uhamiaji (DIS) kuweka malengo yake ya kusajili wapigakura huku ikisaka usahihi kwenye sajili yake. Awali, IEBC iliegemea mfumo wa zamani wa sensa kuweka malengo yake ya kusajili wapigakura, ambao, inasema sasa “umethibitisha kukosa usahihi, ustawishaji na siyo halisi.” Hata hivyo, huku tume hiyo ya uchaguzi ikitangaza mageuzi hayo katika ripoti iliyowasilishwa na Kamati ya Uangalizi kuhusu Utekelezaji wa Katiba (CIOC) ya Bunge la Kitaifa, ingali na matumaini ya kufanikisha wapigakura wapya milioni 6.3 kabla ya uchaguzi mkuu 2027. Shabaha ya wapigakura wapya milioni 6.3iliwekwa kwa kutumia mfumo wa data ya sensa uliotegemea watu Waliohitimu Umri wa Kupiga kura (VAP), ambao tume sasa inautema na kuegemea “data iliyo sahihi zaidi ya NRB na DIS” inayojikita kwenye Watu Wanaohitimu kuwa Wapigakura (VEP). “Tume iliashiria inahamisha mchakato wa kupanga malengo yake kutoka VAP hadi VEP, inayozingatia zaidi idadi halisi ya wananchi wanaomiliki stakabadhi zinazohitajika za usajili,” inaeleza ripoti ya CIOC, ambayo mwenyekiti wake ni Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi. Katiba kwenye Kifungu 83 inaeleza masharti yanayohitaji kutimizwa ili kusajiliwa kama mpigakura, ambapo matakwa ya kisheria yanajumuisha kumiliki kitambulisho cha kitaifa au pasipoti halisi ya Kenya. Endapo tume itafanikisha kusajili wapigakura wapya 6.3 milioni, wapiga kura waliosajiliwa katika uchaguzi mkuu wa 2027 watafikia 28.4 milioni ikilinganishwa na wapigakura 22.1 milioni walioidhinishwa kushiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022. “Tume ilibaini kuwa mfumo wa VEP unatumia data kutoka NRB na DIS, hivyo basi kupunguza malengo yanayopangwa kutokana na vitambulisho na pasipoti zilizotolewa,” ilisema CIOC. Ripoti hiyo inaeleza kuwa “mwelekeo huu wa malengo yanayoendeswa na data inayotokana na idadi halisi ya vitambulisho vya kitaifa na pasipoti unahakikisha rasilimali zinagawanywa ipasavyo na vigezo vya utendakazi ni vya kihalisia na vinavyoweza kutimizwa”. Tume imekuwa ikitumia data ya sensa kuainisha raia waliohitimu na kukadiria malengo ya usajili wa wapigakura kwa kuhesabu idadi ya watu watakaokuwa wamehitimu umri wa miaka 18 kufikia uchaguzi mkuu. Hata hivyo, tume inasema muundo wa ripoti ya sensa unajumuisha watu ambao hawajahitimu kusajiliwa kama wapigakura. Hii inajumuisha watu wasio raia, ambao hawajaandikishwa na wakimbizi, “na kusababisha ongezeko la shabaha isiyooana na data kwa misingi ya sheria.” Kuhusu usajili wa wapigakura, tume ya uchaguzi ilisema ili kufanikisha malengo ya kusajili wapiga kura na kuhakikisha “hakuna Mkenya anayenyimwa haki ya kupiga kura,” inanuia kutumia “mikakati kadhaa” ikiwemo shughuli endelevu ya kusajili wapigakura katika kila moja ya afisi 290 za IEBC kwenye maeneobunge.
KAULI ya Mbunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika (EALA) Winnie Odinga kuwa ODM itakuwa na mwaniaji wa urais 2027 imeibua taharuki kuhusu ushirikiano baina ya chama hicho na UDA katika uchaguzi mkuu ujao. Aidha, tangazo lake hilo linatarajiwa kuchemsha siasa za ukanda wa Luo Nyanza ikiwa imesalia miezi 18 kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027. Bi Winnie, mwanawe Waziri Mkuu wa zamani marehemu Raila Odinga wikendi alisema chama hicho kitakuwa na wawaniaji katika ngazi zote za uongozi mnamo 2027 ikiwemo urais. “Madhumuni ya chama chochote kile cha kisiasa ni kuchukua mamlaka yote na ninaamini kuwa lazima ODM iwe na wawaniaji kila mahali. Hiyo ndiyo sababu ya kuwa na chama cha kisiasa na hiyo ndiyo demokrasia, si lazima watu wote wafikirie kwa njia inayofanana,” akasema Bi Winnie, akizungumza katika Shule ya Wasichana ya Pioneer ambayo inamilikiwa na bwanyenye Peter Munga. "Watu sharti washindane na lazima ODM iwe tayari kushindana na pia nasi tuwe tayari," akaongeza. Kauli ya ODM kuwania urais inajiri baada ya Bi Winnie kusema kuwa kulikuwa na baadhi ya wanasiasa ambao walikuwa wakipanga kuuza ODM. Alisema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya uwepo wa ODM mwezi uliopita. Bi Winnie ameonekana kumakinikia siasa za ODM kuwasilisha mpeperushaji wa urais baada ya kutaka pia chama kiwe na mwakilishi wa kushauriana na Rais Ruto ndani ya Serikali Jumuishi kutokana na kutokuwepo kwa Raila. "Ushirikiano ndani ya Serikali Jumuishi kwa sasa ni mgumu. Je wanaousimamia wanaweza? Kuna Baba Raila Odinga mmoja tu ambaye angeuweza," akasema wakati wa maadhimisho ya ODM. Alitoa wito wa kuandaliwa kwa Kongamano la Kitaifa la Chama (NDC) ili wanachama waamue kuhusu mwelekeo wa ushirikiano wa ODM na UDA. Baada ya kuonekana kutofautiana kimaoni na amu yake, Dkt Oburu Oginga, ambaye ni kiongozi wa ODM, Bi Winnie wikendi alikanusha kuwa kuna uhasama wowote wa kisiasa ndani ya familia ya Bw Odinga. “Ni ami yangu na ndiye baba pekee niliyebaki naye. Tunaweza kutofautiana kimaoni lakini ukweli ni kwamba sote tuko pamoja katika kuimarisha chama cha ODM,” akasema akiwa Kaunti ya Murang’a. Dkt Oginga mwenyewe aliashiria kuwa ODM iko tayari kushirikiana na Rais Ruto 2027 na akasema wadhifa wa chini zaidi ambao wanaweza kuukubali ni ule wa mgombeaji mwenza. Kauli ya Winnie vilevile inatarajiwa kuchemsha siasa za Luo Nyanza ambako baadhi ya wanasiasa wakuu tayari wamesema watamuunga mkono Rais William Ruto mnamo 2027. Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi na mwenzake wa Fedha John Mbadi wamekuwa mstari wa mbele kumpigia debe Rais Ruto kurejea ikulu 2027. Wawili hao wamekuwa wakishikilia kwamba hakuna mwanasiasa ambaye anatosha kuvalia viatu vya Raila na anayetosha kuwania urais 2027. “Mtu pekee alisimama na Raila na hata kusulubishwa kwa kufanya hivyo ni William Ruto. Ukisema ODM inaweza kutoa mwaniaji wa urais, hakuna mtu amekuzuia, endelea,” akasema Bw Wandayi wiki jana akiwa eneobunge la Gem. “Ukitaka kuwania urais kupitia ODM tafadhali endelea na tuone utapata kura ngapi? Sisi kama jamii ya Waluo tumeamua kumuunga mkono Rais Ruto, ukitaka kuwania urais, endelea mbele lakini nakuhakikishia hutafanikiwa,” akaongeza. Waziri huyo alisisitiza kuwa ataongoza kampeni za Rais William Ruto, Kaunti ya Siaya, akisisitiza kwa sasa hakuna mwanasiasa mwenye uwezo na rasilimali za kufanya kampeni za urais alivyofanya Raila. “Ruto ndiye rais wa kwanza kuhakikisha maendeleo yanafika hapa Nyanza. Njia pekee kwa watu wetu kuendelea kunufaika ni kumuunga mkono Rais Ruto 2027,” akasema. Bw Mbadi naye alisema analenga kuwania urais 2032 baada ya Rais Ruto kumaliza hatamu yake. “Tuwaambie watu wetu ukweli kwa sababu hii ndiyo serikali ambayo imetufikiria. Sisi tutamuunga mkono Rais 2027 kisha 2032 tujiandae kuchukua urais. Kwa sasa hakuna mwanasiasa hapa Nyanza ambaye anaweza kuwania urais,” akasema Bw Wandayi.
DODOMA; WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania watunze akiba ya chakula walichonacho na waepuke matumizi yasiyofaa kutokana na hali ya kuchelewa kwa msimu wa mvua. Dk Nchemba alitoa wito huo jana wakati akizungumza na baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma. Aliwaeleza viongozi hao kutoka mikoa ya … The post Serikali yaagiza wananchi kuweka akiba ya chakula first appeared on HabariLeo.
UMOJA wa Mataifa (UN) umesema Tanzania imeendelea kuwa mfano wa amani na mshikamano ndani ya Afrika na duniani kwa ujumla. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres pia alisema Tanzania imezidi kuwa imara licha ya amani yake kujaribiwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa … The post UN yaisifu Tanzania kuwa mfano wa amani first appeared on HabariLeo.
WASHINGTON DC, AMERIKA RAIS Donald Trump ameelezea wasiwasi kuhusu iwapo chama tawala cha Republican kitadumisha udhibiti wa bunge kwenye chaguzi za muhula wa kati mwaka ujao kwa sababu baadhi ya sera zake kiuchumi bado hazijatekelezwa kikamilifu, shirika la Wall Street Journal liliripoti Jumamosi. Trump, kwenye mahojiano Ijumaa, alieleza shirika hilo, “siwezi nikawaeleza. Sijui ni lini hela zote hizi zitaanza kuwa na matokeo halisi,” alipoulizwa kuhusu iwapo Republican itapoteza bunge Novemba. Ikulu haikujibu mara moja ombi la Reuters la kuzungumzia suala hilo. Rais amehoji kuwa sera zake za kiuchumi, ikiwemo hatua yake ya kuanzisha msururu wa ada za ushuru kwa bidhaa zinazoingizwa nchini, zinaunda kazi, kupiga jeki soko la hisa na kuvutia uwekezaji Amerika. Baada ya kufanya kampeni mwaka jana kwa ahadi za kudhibiti mfumuko wa bei, Trump katika majuma machache yaliyopita amebadilisha kauli na kupuuzilia mbali matatizo yanayohusu bei ya bidhaa kuwa uongo, akimlaumu aliyekuwa rais Joe Biden kuyahusu na kuahidi sera zake kiuchumi zitanufaisha raia wa Amerika mwaka ujao. “Nafikiri kufikia wakati tutalazimika kuzungumza kuhusu uchaguzi, katika muda wa miezi michache ijayo, nafikiri bei zetu zitakuwa katika hali shwari,” alisema Trump kwenye mahojiano. Mwezi uliopita, rais alipunguza ada za ushuru kwa bidhaa zaidi ya 200 za chakula kufuatia kutoridhika kunakozidi kuongezeka miongoni mwa wateja Waamerika kuhusu bei ghali ya bidhaa za chakula. Rais hakusema iwapo atapunguza ushuru kwa bidhaa za ziada, ilisema WSJ. Kiwango cha kumkubali Trump kwa jumla kilipanda hadi asilimia 41 katika kura mpya ya maoni iliyoendeshwa na Reuters/Ipsos lakini kiwango cha kukubali utendakazi wake kuhusu gharama ya maisha kilikuwa asilimia 31 pekee. Wanasiasa wa Democrat wamenyakua misururu ya ushindi kwenye chaguzi za majimbo na majiji nchini ikiwemo Virginia, New Jersey na New York City, ambapo wasiwasi wa wapiga kura kuhusu uwezo wa ununuzi pamoja na bei ghali za bidhaa za chakula, zilikuwa masuala makuu. Maafisa wamesema Trump atajitosa barabarani mwaka ujao kuwafanyia kampeni wagombea wa Republican na kusisitiza ufanisi wa sera zake kiuchumi. Trump amesema hatua yake ya kupunguza ada na ushuru unaotozwa bidhaa za kigeni utaongeza pesa kwenye mifuko ya familia za Amerika.
RAIS William Ruto Jumapili alionekana kumlenga Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, akimrejelea kama kiongozi ambaye si mpenda maendeleo licha ya kwamba amekuwa kwa siasa kwa zaidi ya miaka 50. Akiongea katika Kaunti ya Kiambu, Rais bila kumtaja Bw Musyoka moja kwa moja, alisema inashangaza kuwa amekuwa akipinga Hazina ya Miundomsingi ilhali barabara za kuelekea kwake ziko katika hali mbaya. Kati ya viongozi wa upinzani, Bw Musyoka, 71 ndiye amekuwa katika siasa kwa kipindi kirefu zaidi. Pia, barabara ya kuelekea kwake Tseikuru, Kaunti ya Kitui kwa wakati mmoja iligonga vichwa vya habari kuwa hali mbaya alipotembelewa na vinara wenzake wa upinzani Bw Musyoka alihudumu kama waziri kwenye wizara mbalimbali wakati wa utawala wa Rais Daniel Moi na pia alikuwa makamu wa rais katika utawala wa Rais Mwai Kibaki kati ya 2008-2013. Bw Musyoka amekuwa akipinga kuanzishwa kwa Hazina ya Miundomsingi akisema kuwa inaenda kinyume cha katiba na Sheria ya Fedha za Umma. Makamu huyo wa rais wa zamani alisema kuwa Bunge halitafuatilia na kukagua matumizi ya pesa hizo, hilo likitilia shaka uwazi katika matumizi ya pesa za umma. Rais alishangaa ni vipi Wakenya wanamtarajia kiongozi kama huyo kumakinikia miradi ya maendeleo ilhali hawakufanya hivyo akiwa na mamlaka. “Yeye mwenyewe, huyo mnamngojea, amekuwa kwa uongozi miaka 50. Barabara ya kwenda kwake ni ya vumbi na matope. Atatoa wapi akili, kama amekosa akili ya kupanga barabara ya kwenda kwake?” Rais Ruto akauliza. Aliongeza kuwa kufeli kwa viongozi ndiko kumewasukuma kusema mpango huo haufanyi kazi. “Ndio maana mnaona wanasema ati haiwezekani. Because they have never planned anything (Kwa sababu hawajawahi kupanga chochote),” akaongeza. Rais Ruto alisema utawala wake unalenga kujenga kilomita 28,000 za barabara kufikia mnamo 2022, akiongeza barabara za kilomita 10,000 ambazo zilijengwa wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta. Alisisitiza kuwa mpango huo ni muhimu katika kuhakikisha Kenya inapiga hatua kiuchumi.
WAZIRI wa zamani Fred Gumo na aliyekuwa Seneta wa Vihiga George Khaniri wametaka uchunguzi ufanywe kuhusiana na kifo cha Mbunge wa zamani Cyrus Jirongo. Wawili hao walishangaa jinsi ambavyo mbunge huyo wa zamani wa Lugari alivyosafiri kutoka Karen hadi Naivasha ilhali alikuwa akienda nyumbani kwake Gigiri Ijumaa usiku. Bw Khaniri alisema Naivasha ni mbali na wanataka kujua jinsi ambavyo Bw Jirongo alivyofika huko kisha akapata ajali akitokea Naivasha kuja Nairobi. Wakati wa mauti hayo ya kuamkia Jumamosi, Bw Jirongo alikuwa pekee kwenye gari lake ambalo liligongana na basi la Climax akitoka kituo cha mafuta Naivasha. Basi la Climax lilikuwa limetoka Nairobi. Bw Gumo ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya mazishi ya mwendazake alisema kuna kamera maeneo mbalimbali jijini na polisi wanastahili kuziangalia katika juhudi za kufahamu ukweli. “Hakuwa anaenda nyumbani kwake Kakamega, alikuwa asafiri kutoka Karen hadi kwake Gigiri. Inakuaje sasa alikuwa akisafiri tena kutoka Naivasha hadi Nairobi? Kuna kamera kote kote na wakiangalia watafahamu ukweli,” akasema Bw Gumo. Kamati andalizi ya mazishi imesema kuwa Bw Jirongo atazikwa Lugari mnamo Desemba 30, 2025. Mwili wake utapelekwa nyumbani kwake Gigiri mnamo Desemba 27 kisha usafirishe Kitale kwa mke wake wa pili Desemba 28. Siku inayofuata ya Desemba 29 utapelekwa nyumbani kwake Lumakanda, Lugari kisha mazishi yafanyike Desemba 30.
MKUU wa Gereza la Bukoba, Aloyce Kalihamwe amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yameleta mageuzi makubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Magereza nchini yakichangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa kazi, kulinda afya na mazingira pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji wa taasisi hiyo. Akizungumza wakati wa ziara ya wataalam kutoka Wizara ya Nishati … The post Nishati safi yaongeza ufanisi magereza first appeared on HabariLeo.
KRISMASI ya mapema kwa wanawake kutoka mtaa wa mabanda wa Langas iliyotolewa na mfanyabiashara mmoja wa eneo hilo nusra iwe karaha pale walengwa walipoanza kung’ang’ania chakula hicho. Ilibidi maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Langas kuingilia kati ili kurejesha utulivu na kutoa nafasi kwa mhisani kugawa chakula hicho katika mazingira tulivu. Chakula hicho kilitolewa na mfanyabiashara Florence Akinyi. Bi Akinyi alifanikiwa kulisha watu wapatao 2,000 huku akitoa wito kwa wahisani wengine kujitokeza na kuwafaa wakazi hao. “Idadi kubwa ya watu ambao wamejitokeza hapa ni ishara ya umaskini katika mtaa huu, kuna haja ya wadau zaidi kujitoekeza angalau kuwasaidia siyo tu wakati wa Krismasi bali mara kwa mara,” alisema Bi Akinyi maarufu Mama Dota. Hata hivyo, Akinyi aliwataka wenyeji kujisajili katika mipango ya serikali ya kuwafaa wananchi wa matabaka ya chini kama vile miradi inayolenga akina mama mboga, walemavu miongoni mwa miradi mingine. “Kama mwenyeji ambaye naelewa hali ya maisha katika kijiji hiki niliamua kuwapa Krismasi ya mapema, nililenga watu 2,000 lakini kuna watu wengi ambao wanahitaji msaada kama huu mtaani humu,” alisema Bi Akinyi. Baadhi ya akina mama walionufaika walisifia Bi Akinyi kwa msaada huo wakisema kuna haja ya serikali kuwezesha wenyeji ili wawe wakijimudu maishani. “Huyu mama amefanya jambo nzuri zaidi, maisha katika mtaa huu ni magumu sana, nataraji huu ndio mwanzo wa misaada zaidi,” alisema Susan Mmbone ambaye ni mmoja wa watu walionufaika. Msaada huo ulikuwa ni unga wa ngano, chumvi, sukari, mchele miongoni mwa vyakula vingine.
WIMBI la huzuni Jumapili, Desemba 14, 2025 liligubika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyamira wakati ambapo familia waliopoteza jamaa zao kwenye ajali walifika kutazama miili yao. Ajali hiyo iliyotokea kwenye barabara ya Bwárani-Tombe katika barabara ya Kericho-Nyamira ilisababisha mauti ya watu wanane. Kati ya miili hiyo minane, wawili walikuwa watoto ambao wapo chini ya umri wa miaka miwili. Uchungu zaidi ni kwamba miili yao ililala kwenye vifua vya mama yao. Jones Kebaso alisema jamaa zake wanne walihusika kwenye ajali hiyo ya saa mbili usiku wa kuamkia Jumapili. Alifiwa na mpwa wake pamoja na dada mkwe. Jamaa zake wengine wawili wamelazwa Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyamira wakiwa katika hali mbaya kiafya. Baadhi wana majeraha mabaya ya kichwa na wapo katika chumba cha wagonjwa mahututi. “Tunaendelea kufanya maandalizi wahamishwe hadi Eldoret. Walikuwa wakitoka Nairobi wakija nyumbani Kenyenya, Nyamira Kusini kwa mazishi ya mjomba wetu,” akasema Bw Kebaso. “Mjomba wetu amekuwa akiugua kwa miaka tisa lakini akaaga na tulikuwa tunajiandaa kwa mazishi yake. Sasa tuna jamaa zetu wawili zaidi wameaga na wengine wawili wakiwa mahututi,” akaongeza. Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu Nyamira Jared Oeba alithibitisha kuwa watu wanane waliaga dunia kwenye ajali hiyo. Wengine saba walinusurika na wakakimbizwa hospitalini huku wanne wakipambana kusalia hai katika chumba cha wagonjwa mahututi. Polisi wanasema ajali hiyo ilihusisha trela KBE 701E ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyetoweka baada ya ajali hiyo. Trela hilo liligongana na gari aina ya Nissan KCF O68V ambalo ni la Quarser Sacco. Dereva wa Nissan aliaga dunia papo hapo “Trela lilikuwa likiendeshwa kuelekea Kericho na lilipofika eneo la ajali, dereva alishindwa kulidhibiti ndiposa likagongana na matatu iliyokuwa ikielekea Nyamira,” ikasema ripoti ya polisi. Katika eneo la tukio, umati ulijawa na uhayawani na ukaanza kufyonza mafuta kutoka trela kisha kuwapora wafu na walionusurika kwenye ajali. Umati huo ulionyesha ukatili zaidi baada ya kuwarushia polisi waliowafurusha mawe. “Mmoja wa afisa wetu alifyatua risasi mara tano hewani kufukuza umati huo,” ikasema taarifa ya polisi. Magari hayo mawili yalikokotwa hadi kituo cha polisi cha Nyamira kufanyiwa ukaguzi. Beatrice Arani ambaye alishuhudia ajali hiyo ikitokea, alisema eneo la Bwárani limekuwa hatari zaidi kutokana na visa vya mara kwa mara vya ajali. “Tunaomba serikali ione mbinu itakayotumia kuepuka ajali zaidi katika barabara hii,” akasema Bi Arani. Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo ambaye aliwatembelea manusura hospitali, alisema kaunti inaendeleza mipango kuhakikisha kwamba wagonjwa wawili mahututi wanahamishwa kwa matibabu spesheli. “Wanahitaji upasuaji kwa sababu wana majeraha mabaya kichwani,” akasema Bw Nyaribo. Gavana huyo alienda katika chumba cha kuhifadhia maiti ambapo aliwafariji jamaa na marafiki. “Tumeanzisha kamati kufahamu jinsi tutakavyosaidia familia zilizoathirika,” akasema Bw Nyaribo.
EWE ndugu yangu ‘Chautundu’, weka kando matusi, dharau na utundu unijibu swali hili: Hivi umewahi kumwangalia mwanasiasa fulani akiropokwa na maneno ukajiambia kimoyomoyo ‘huyu anafaa kuwa mwakilishi wa wanawake bungeni?’ Wala sirejelei matusi yako ya kawaida ya kusema mwanasiasa fulani au fulani usiyempenda ana ‘umama’, la hasha! Narejelea mtu yeyote ambaye anapenda vyeo sana hivi kwamba akipewa cha kuwawakilisha wanawake, yaani awe ‘mama kaunti’, yuko radhi kuvaa rinda. Katika siasa zetu hizi zilizojaa ushindani, labda kuna mwanamume fulani ambaye anakesha usiku kucha ilhali yu macho akiwaza na kuwazua bila mafanikio, akijiuliza inawezekanaje kutwaa mojawapo ya vyeo hivyo maalum vya wanawake. Najua kuna wanaume wengi ambao wanatamani kuwania vyeo vya wawakilishi wa kike bungeni, lakini hawana namna! Wakivaa marinda na sketi ili kupata vyeo watavua lini, tena watarejeaje kwa wananchi, hasa watakapostaafu siasa? Kama nzi anayekuta kinyesi kikavu cha mwaka jana na kujiuliza ‘hiki kilikauka nikiwa wapi?’, baadhi ya wanaume wanajiuliza wadhifa wa ‘mama kaunti’ uliingiaje kwenye sheria zetu bila kupingwa na wanaume. Nimewasikia wengi wakinong’onezana kuwa Kenya haifai kuwa na viti maalum ambavyo ni watu wa jinsia moja tu wanaoruhusiwa kuviwania. Wanadai huo ni uonevu na ubaguzi wa kijinsia eti, hali Katiba ya nchi inakataza ubaguzi wa aina yoyote ile. Wapo wanaohakiki michango ya ‘mama kaunti’ wote waliowahi kuchaguliwa tangu mwaka 2013 na kujiambia wanaweza kufanya kazi bora zaidi kuliko wote. Hiyo inaitwa tamaa ya fisi! Anatazama angani na kuona mawingu meupe, akili yake inamwambia hiyo ama ni pamba, au nyama iliyojaa mafuta. Ghafla anajiambia watu hawawezi kuhifadhi pamba juu hivyo kwa kuwa hakuna mnyama anayetaka kuila, lakini wanaweza kuangika nyama umbali huo ili fisi wasiifikie. Anaketi hapo siku nzima, ila anaishia kunyeshewa tu, au kiza kinampata hapo akisubiri nyama ianguke, mwishowe anajiambia binadamu wamefunga duka la nyama. Naambiwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inapendekeza ipitishwe sheria itakayoipa mamlaka ya kukataa orodha za wabunge maalum wanaoteuliwa na vyama ikiwa hazitazingatia sheria inayosema jinsia moja isishikilie zaidi ya thuluthi mbili za nyadhifa za umma. IEBC imelazimika kufanya hivyo eti kwa kuwa wanaume wasiposhurutishwa hawatawahi kutekeleza sheria hiyo, wataendelea kuvuta ngoma kwao. Napendekeza wanaume wakatazwe kumchagua ‘mama kaunti’, wawaachie wanawake kazi hiyo. Mwanamume kamili unafanya nini katika uchaguzi ambapo wanawake wanamchagua mwakilishi wao?
CHAMA cha UDA mwezi huu kimepata pigo eneo la Pwani baada ya mmoja wa viongozi ambao walitumika kukipigia debe katika uchaguzi mkuu uliopita; Bi Aisha Jumwa kuhama na kujiunga na chama cha Pamoja African Alliance (PAA). Kujiunga na PAA; chama ambacho kinahusishwa na Spika wa Seneti Amason Kingi na kutangaza kuwania kiti cha ugavana, kumevuruga siasa za kaunti hiyo na kutetemesha gavana wa sasa Bw Gideon Mung’aro. Kutokana na hatua hiyo, vita vya ugavana Kilifi kwa sasa vitaonekana kuwa kati ya Bw Kingi ambaye ashampendekeza Bi Jumwa kuwania kupitia chama chake na Bw Mung’aro ambaye atatumia umaarufu wa chama cha ODM kuhifadhi kiti hicho. Huku wanasiasa wakijipanga wakilenga uchaguzi mkuu wa 2027, chama cha PAA kinaonekana kuvuna vilivyo baada ya Spika Kingi kudinda kushurutishwa kuvunjilia mbali chama chake kama viongozi wengine waliojiunga na serikali walivyofanya. “Tayari tumepata viongozi wengi ambao wanataka kujiunga na chama cha PAA si tu Bi Jumwa. Tutawajulisha hivi karibuni. Kwa sasa tunanuia kupata viti katika nyadhifa mbalimbali kuanzia kwa gavana hadi madiwani, ila kwa kiti cha uraisi, tutaunga mkono Rais Ruto,” alisema Bw Sammy Nyundo, kiongozi wa vijana wa PAA. Mchakato wa Wapwani kuwa na chama chao sasa unaonekana kuchukua mkondo mpya kwani viongozi wameanza kuasi vyama vinavyoonekana kuwa si vya eneo hilo. Bi Jumwa ambaye alikuwa na wakati mgumu kupigia debe chama cha UDA eneo la Pwani kuvunja ngome ya ODM, alisema hatua yake ilisababishwa na kimya cha Rais William Ruto kuhusu chama hicho alipozuru Pwani majuzi. Wakati wa ziara yake, Rais Ruto alionekena kupigia debe muungano wa UDA na ODM wala si chama chake. “Nilibaki na maswali kuhusu kwa nini Rais Ruto hakuongelea cha UDA alipokuwa huku. Nilionelea kujiunga na PAA ambacho ni kimoja cha vyama tanzu serikalini,” alisema Bi Jumwa. "Wanasiasa kuhama chama ni jambo la kawaida. Hata Rais Ruto amefanya hivyo mara kadhaa. Hata hivyo, chama cha PAA kiko katika serikali na hakuna kosa lolote nimefanya," alisema Bi Jumwa. Waziri huyo wa zamani anatarajiwa kuteuliwa naibu wa chama na kugombea kiti cha ugavana mwaka wa 2027 baada ya kupoteza nafasi hiyo mwaka wa 2022 ambapo alipata kura 65,893 dhidi ya Bw Mung’a ro ambaye aliibuka mshindi kwa kura 143,773. Bi Jumwa ambaye alikuwa Waziri wa masuala ya jinsia kabla ya kufutwa kazi katika serikali ya Rais Ruto alisema aliona heri kuhamia chama kinachohusishwa na wenyeji anapolenga azma yake ya kumng’oa gavana wa sasa Bw Mung’aro. Kujiunga kwake na PAA na iwapo atapata uungwaji mkono kutoka kwa aliyegombea kiti cha ugavana msimu uliopita kwa tiketi ya chama hicho Bw George Kithi na kupata kura 64,326 kutakuwa tishio kubwa kwa Bw Mung’aro ambaye chama hicho kinaonekana kuyumba baada ya kuaga dunia kwa kinara wake Raila Odinga. Katibu mkuu wa UDA Hassan Sarai alisema tofauti na uchaguzi mdogo ambapo vyana tanzu vya serikali viliunga mkono ODM eneobunge la Magarini, mwaka wa 2027 kila chama kitawasilisha mgombeaji wake. "Baada ya kuondoka kwa Bi Jumwa, tumemteua Bw Kahindi kuongoza chama hicho Kilifi na baadaye kumuunga mkono kuwania kiti cha ugavana," alisema Bw Omar. Bw Kahindi alihama ODM mwaka wa 2022 baada ya chama hicho kuteua Bw Mung'aro kuwa mgombeaji wake wa ugavana. Katika uchaguzi wa Novemba 27, PAA na UDA kiliunga mkono mgombea wa ODM Bw Harry Kombe ambaye aliibuka mshindi dhidi ya Stanely Kenga wa DCP.
WATU kadhaa wameelezea dakika za mwisho za aliyekuwa Mbunge wa Lugari, Cyrus Jirongo, kabla ya kufariki katika ajali mbaya ya barabarani iliyotokea alfajiri ya Jumamosi katika eneo la Karai, Kaunti ya Naivasha, kwenye Barabara Kuu ya Nairobi–Nakuru. Dakika kumi na tano baada ya saa nane usiku, Bw Jirongo, aliyekuwa akiendesha gari lake mwenyewe aina ya Mercedes-Benz rangi nyeupe akiwa peke yake ndani, aliingia katika Kituo cha Mafuta cha Eagol kilichoko Karai. Alikuwa akielekea Nairobi, na kituo hicho kiko upande wa pili wa barabara. Walioshuhudia walisema alipofika katika kituo hicho, alionekana kama alitaka kuelekea kwenye pampu ya kujaza mafuta. Hata hivyo, alipita pampu zote, akageuza gari na kurejea barabarani. Alipokuwa akijiunga tena na barabara kuu ndipo kosa hatari lilipotokea. Kwa mujibu wa maelezo ya mhudumu wa kituo cha mafuta aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina, Bw Jirongo aliingia barabarani lakini akaendelea kuendesha gari katika laini inayotumiwa na magari yanayotoka Nairobi kuelekea Nakuru, yaani njia ya magari yanayotoka upande aliokuwa akielekea. “Nilisikia kishindo kikubwa sana,” alisema mhudumu huyo. Mercedes-Benz aliyokuwa akiendesha Bw Jirongo iligongana na basi la kampuni ya Climax lililokuwa likisafiri kutoka Nairobi kuelekea Nakuru. Baada ya mgongano huo mkali, gari la Bw Jirongo liliburutwa umbali wa mita chache kutoka eneo la ajali kabla ya basi hilo kusimama kabisa. Mhudumu huyo alisema alikimbia eneo la ajali na kujaribu kufungua mlango wa gari, lakini ulikuwa umefungwa. “Niliangalia ndani nikamwona mtu ameinamia usukani, uso ukiwa umeelekea chini, na kulikuwa na damu kichwani,” alisema. Alisema alipiga simu ya dharura saa nane na dakika 37 usiku kuwaarifu polisi kabla ya kujaribu kusimamisha lori kuomba usaidizi. Hata hivyo, dereva wa kwanza hakusimama. Dakika chache baadaye, dereva mwingine alisimama na wakaanza juhudi za kumsaidia dereva wa Mercedes-Benz, lakini waligundua kuwa tayari alikuwa amefariki. Dereva wa basi la Climax, Bw Tirus Kamau, alithibitisha simulizi hilo lakini akaongeza kuwa kulikuwa na msongamano mdogo wa magari katika laini yake kabla ya ajali. Alisema Bw Jirongo alijaribu kupita gari jingine na akaingia kwenye laini yake, hali iliyosababisha mgongano huo. Bw Kamau, ambaye ana uzoefu wa zaidi ya miaka minane barabarani, alisema alikuwa amebeba abiria 65, huku Bw Jirongo akiwa peke yake. “Nilikuwa nikielekea Busia kutoka Nairobi. Gari la Mercedes-Benz lilikuwa linakuja kutoka upande wa pili. Alijaribu kupita, ndipo tukagongana,” alisema. Ripoti ya polisi ilieleza kuwa Bw Jirongo, mwenye umri wa miaka 64, alikuwa akiendesha gari lenye nambari ya usajili KCZ 305C kutoka Nakuru kuelekea Nairobi aliposhindwa kudumisha njia yake na kugongana na basi lenye nambari KCU 576A. Alipata majeraha makubwa ya kichwa na kufariki papo hapo. Kamanda wa Trafiki wa Kanda ya Bonde la Ufa, Bi Sara Chumo, alithibitisha maelezo ya ajali hiyo. Mwili wa marehemu ulipelekwa katika mochari ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha kabla ya kuhamishiwa katika mochari ya Lee, jijini Nairobi. Magari yaliyohusika yalikokotwa hadi Kituo cha Polisi cha Naivasha, yanakozuiliwa kwa uchunguzi zaidi. Polisi walisema wanashuku huenda marehemu alikuwa na silaha wakati wa ajali, ingawa haikupatikana. Bw Jirongo alikuwa maarufu kwa kuongoza vuguvugu tata la Youth for Kanu ’92 (YK92) lililounga mkono kampeni ya kuchaguliwa tena kwa Rais Daniel arap Moi mnamo 1992. Alihudumu kama Mbunge wa Lugari kwa mihula miwili na baadaye alihusishwa na vyama kadhaa vya kisiasa. Pia, aliwahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Maeneo ya Mashambani na aliwania urais katika uchaguzi mkuu wa 2017.
DODOMA; WAUMINI nchini wamekumbushwa kuishi maisha ya imani ili kuandika historia nzuri wakiwa duniani na hata wakitangulia mbele ya haki kama alivyofanya Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama aliyefariki dunia Desemba 11, mwaka huu. Hayo yalisemwa jana na Paroko wa Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, Padri Emmanuel Mtambo … The post Waumini wakumbushwa kuishi kwa imani first appeared on HabariLeo.
RAIS Samia Suluhu Hassan amemmwagia sifa Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama aliyefariki dunia kuwa alikuwa kiongozi mwenye moyo wa kujali maslahi ya taifa na kuwataka wabunge na mawaziri wapya kufuata nyayo zake wakati wa kutekeleza majukumu yao. Akizungumza katika mazishi ya kitaifa ya Jenista jana jijini Dodoma, Rais Samia aliwataka wabunge na mawaziri hususani wale … The post Samia awapa neno mawaziri wapya first appeared on HabariLeo.
IWAPO tafsiri ya sheria ya baadhi ya viongozi itaruhusiwa, basi kuna wanasiasa haramu Kenya; bila hata kutambua haki ya kila raia ya kujiunga na chama cha kisiasa wanachochagua. Haya yamejitokeza kutokana na kauli za Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, ambaye amekemea vikali Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kwa kuidhinisha chama kipya cha aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, cha National Economic Development Party (NEDP). Mbali na Sonko, Bw Cherargei alitaja viongozi anaohisi kuwa hawafai kuunda na kuongoza vyama vya kisiasa humu nchini. Katika taarifa aliyochapisha wiki hii katika mitandao yake ya kijamii, Bw Cherargei alisema kuwa Sonko, aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, wote waliowahi kuondolewa mamlakani kupitia mchakato wa kuwatimua, sasa wana vyama vya siasa, jambo ambalo alisema ni kinyume cha sheria. Ni muhimu kutambua kwamba aliotaja wote wanahusishwa na upinzani.Kwa mujibu wa Cherargei, viongozi waliochunguzwa na kuondolewa mamlakani hawana haki ya kisheria kuunda au kuongoza vyama vya siasa licha ya Katiba kuruhusu uhuru wa kisiasa. Ni muhimu kukumbuka kuwa Bw Cherargei ni wakili anayejua wazi kwamba Katiba inaruhusu kila raia wa Kenya kujiunga na chama cha kisiasa anachopenda.Alitaja hatua ya ORPP kuwa ya kushangaza, isiyo halali, kinyume cha Katiba na ishara ya “ufisadi wa kiwango cha juu.” Kulingana na Seneta huyo, Msajili wa Vyama vya Kisiasa amevunja sura ya katiba kuhusu uongozi na maadili, na anapaswa kuwajibishwa kisheria. Akizungumza baada ya kuzindua chama hicho Jumanne, Desemba 9, 2025, Sonko alisema NEDP inalenga kutoa uongozi mbadala kwa nchi, akidai kuwa Kenya imekwama kwa vyama ambavyo havijawahi kuwapa Wakenya suluhu ya maana.
MIKUTANO miwili ya makundi tofauti ya vinara wa upinzani Alhamisi wiki hii imetoa taswira kwamba muungano wanaosuka kumkabili Rais William Ruto 2027 huenda ukawa hewa, huku dalili za mpasuko zikiwa wazi licha ya kauli zao zinazosisitiza umoja. Kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka aliongoza mkutano wa vinara wa chama cha DCP Rigathi Gachagua, Eugene Wamalwa wa DAP- Kenya na Justin Muturi wa DP uliofanyika katika Chui House, Nairobi, huku naibu kiongozi wa Jubillee Dkt Fred Matiang’i na Martha Karua wa PLP wakiongoza kikao kingine cha faragha walichosema ni kupanga mikakati na kutia nguvu upinzani. Kikao hicho cha Matiangi pia kilihudhuriwa na Peter Munya, Ukur Yatani, Lenny Kivuti, James Magara na msemaji wa muungano wa upinzani Mukhisa Kituyi. Ingawa vinara hao wa upinzani wamekuwa wakikanusha madai ya mgawanyiko, mfululizo wa matukio na matamshi yao wenyewe katika siku za hivi majuzi hasa baada ya chaguzi ndogo za Novemba 26 yamefanya wafuasi wao kutilia shaka umoja wao. Kikao cha kundi la Bw Musyoka katika makao ya DAP-K, Chui House, kilitarajiwa kuonyesha umoja wa vinara wa upinzani katika kukosoa serikali. Kundi hilo lilionya kwamba utawala wa sasa unahatarisha uhuru na taasisi za taifa na kushambulia kwa ukali mwenendo wa Tume Huru ya Uchaguzi, wakisema chaguzi ndogo za Novemba 26 “zilikuwa za aibu.” Ingawa walipuuza tetesi kwamba kukosekana kwa Dkt Matiangi na wenzake kuliashiria mgawanyiko katika muungano wao, Dkt Kituyi ambaye ni msemaji wao alinukuliwa akisema kwamba baadhi ya vinara “waliamua kukwepa mkutano bila hata kuomba radhi.” Kauli hii inatofautiana na ya Bw Wamalwa, aliyesoma taarifa rasmi katika Chui House akisema baadhi ya wenzao waliokosa kuhudhuria waliomba radhi na kutuma wawakilishi. “Chukulia hayo kama uvumi. Tumeungama na tuko na lengo moja. Mtakumbuka tulipoanza Januari 27, baadhi hawakuwa—lakini walituma wawakilishi. Leo pia wametuma wawakilishi. Tuko imara,” alisema. alisema. Dkt Matiang’i alisema mkutano wa faragha wa kundi lake ulikuwa wa kuimarisha umoja, muundo na mkakati wa upinzani. Kupitia ujumbe wake katika X, alisema Dkt Matiangi alisema majadiliano yao yalilenga kuimarisha upinzani kwa kuzingatia azma yao thabiti ya kurejesha uongozi bora nchini. Bi Karua aliongeza maneno ambayo yalizua maswali zaidi akionekana kuunga kauli za Dkt Kituyi. “Huu ulikuwa mkutano uliopangwa kwa pamoja na kukubalika na wote, tafadhali tambua hilo,” alisema kupitia X. Wachanganuzi wa siasa wanaona dalili zote za muungano huo kuporomoka hata kabla ya safari ya 2027 kuanza. Mchambuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki anasema licha ya kauli za viongozi hao wa upinzani kuonyesha wangali wameungana, ishara wanazowasilisha kwa umma ni kuwa kuna mvutano kati yao. “Hauwezi kujenga muungano kwa taarifa mbili zinazotoka siku moja kutoka sehemu tofauti. Huo ni mgawanyiko,” alisema. Naye Bi Dolly Ndirangu, mchambuzi wa utawala na miungano ya siasa, anasema tatizo ni ubabe katika kusaka mgombea mkuu anayeungwa mkono na wote. “Hakuna kinara anayeonekana kuwa ‘nyota’ au chaguo la wote. Hiki ndicho chanzo cha misuguano midogo midogo inayojitokeza. Bila mwelekeo mmoja, upinzani unaweza kuyeyuka kabla ya 2027,” Ndirangu anaeleza. Anasema kuwa kundi la Kalonzo linaonekana kuwa sura ya muungano; wakati Karua na Matiang’i wanaonekana kuunda mrengo mbadala unaotaka kuamua mwelekeo wa upinzani. Hii, anasema, itawakosesha nguvu za kukabiliana na Rais Willam Ruto ambaye amejipanga kushinda atawale kwa muhula wa pili 2027. “Watakuwa wametupa nyota ya kumshinda Rais Ruto ambaye akiwa mamlakani ana nguvu na mikakati bora. Tofauti za nani atapeperusha bendera au ni nani atakuwa nini hazifai kwa sasa. Ni wakati wa kuamua kuunga mmoja na kuweka nguvu na rasilmali za pamoja iwapo wanataka kuondoa utawala wa sasa debeni 2027,” alisema Ndirangu. Dkt Gichuki anasema mvutano huu unaweza kuwa umezidishwa na kauli zao baadhi ya vinara baada ya chaguzi ndogo zilizoashiria wana misimamo kuhusu mgombea urais na kukubaliana kutengea vyama maeneo fulani katika uchaguzi mkuu wa 2027.
WAZEE wa jamii ya Waluhya wanaonekana kuingilia suala la umoja wa jamii hiyo huku maswali yakiibuka kuhusu kujitolea kwao kutokana na kile kinachotajwa kama kuegemea mrengo mmoja. Mnamo Alhamisi, Desemba 11, 2025, Wazee hao walifanya kikao cha mashauriano na viongozi wakuu wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kutoka eneo la Magharibi ili kujadili mustakabali wa jamii hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. “Si mara ya kwanza kwa watu mashuhuri kusaka umoja wa jamii ya Mulembe na kila wakati huwa wanagonga mwamba kwa kutokuwa na mikakati inayoleta pamoja viongozi wote. Mara nyingi azma hiyo huwa ya maslahi ya mrengo mmoja wa kisiasa au ya kibinafsi,” asema mchanganuzi wa siasa Musili Koli. Wazee hao walikutana na Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna na Naibu Kiongozi wa chama hicho, Godfrey Osotsi, wakitaka kufahamu nafasi ya jamii ya Waluhya ndani ya ODM baada ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, marehemu Raila Odinga. “Tuliwaita viongozi hawa wawili wakuu wa ODM watupe taarifa kuhusu yanayoendelea ndani ya chama. Sehemu kubwa ya jamii yetu iko ODM. Kwa hivyo, kinachoendelea humo kinatuhusu,” alisema Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wazee wa Luhya, Fred Omindo na kuongeza kuwa mkutano huo ni sehemu ya juhudi za jamii kuungana upya kabla ya uchaguzi wa 2027 kutokana na kugawanyika kwao kisiasa mara kwa mara, hali inayowanyima nguvu katika majadiliano kitaifa. Hata hivyo maswali yameibuka kuhusu wanavyoshughulikia suala hilo, nia yao na kwa nini hawahusishi viongozi wote kutoka ukanda huo bila kujali mirengo yao ya kisiasa. Japo wanasema wanataka ushirikishaji wa jamii na uwajibikaji katika shughuli zinazogusa eneo hilo ukiwemo uchimbaji dhahabu na kukodishwa kwa viwanda vya sukari, wachambuzi wanahisi wangepanua wigo na kuhusisha viongozi kutoka mirengo tofauti ya kisiasa. Miongoni mwa wazee hao ni Patrick Wangamati, Noah Wekesa, Fred Omido, na Peter Ludava. Maswali yameibuka kuhusu kwa nini hawakuitisha kikao cha pamoja cha viongozi kutoka vyama vingine ambao wamekuwa wakilalamikia jinsi serikali inavyoshughulikia masuala na rasilmali za eneo la Magharibi. Seneta wa Kakamega, Boni Khalwale, ameshikilia msimamo wake kuhusu mvutano wa dhahabu Ikolomani, akisisitiza kuwa rasilmali za eneo hilo ni mali ya wananchi na hakuna kampuni, iwe ya ndani au ya kigeni inayopaswa kuchimba bila uwajibikaji na uwazi. Khalwale aliongeza kuwa ajira kwa vijana, utunzaji wa mazingira, na uwajibikaji wa wawekezaji lazima viwe kipaumbele katika shughuli za uchimbaji.Sifuna aliweka wazi kuwa “rasilmali za Kakamega ni mali ya wananchi, na hatutaki mtu yeyote afaidike kwa siri huku vijana wetu wakiwa hawana ajira na vijiji vyetu vikisalia bila maendeleo.” Wachambuzi wa siasa wasema kuwa kutengwa kwa baadhi ya viongozi hasa wa upinzani katika kikao hiki kunazua maswali. 'Kuandaa kikao cha viongozi wakuu wa chama kimoja kunaonyesha wazee wana lengo ambalo linaegemea upande mmoja. ODM iko ndani ya Serikali Jumuishi na ndicho chama kikubwa Magharibi mwa Kenya. Kualika viongozi wake wakuu kutoka eneo hilo pekee kunazua maswali kuhusu hasa mpango wa wazee hao,” anasema mchambuzi wa siasa Dkt Jeff Omondi. Anashangaa walikokuwa wazee hao wakati kampuni za sukari zilikuwa zikibinafsishwa ndipo wajitokeze sasa hivi wakati joto la kisiasa linaanza kupanda kufuatia mzozo wa dhahabu na uchaguzi mkuu unapokaribia. Anasema mkutano huu unaashiria kuna mpango kati ya wazee hao na baadhi ya wanasiasa. Anaongeza kuwa iwapo ni kwa maslahi ya eneo na kulinda rasilmali, mkutano unafaa kuhusisha viongozi wote kwa nia njema na si kutumiwa kuendeleza maslahi ya wachache kwa kujifanya kutetea jamii. “Muhimu ni umoja wa jamii ya Magharibi ambao umekuwa ukiyeyuka hata kabla ya kuiva,” asema. Wazee hao walisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na ushirikishaji wa umma katika shughuli za uchimbaji wa dhahabu katika maeneo ya Ikolomani na Vihiga ambapo kampuni ya Shanta Gold inakusudia kufanya shughuli hiyo. Pia, waligusia sekta ya sukari, wakikosoa jinsi viwanda vya Mumias na Nzoia vinavyoendeshwa jambo ambalo linaweza kuwa na madhara kwa ustawi wa vizazi vijavyo vya jamii ya Waluhya. Wazee waliongeza kuwa wanakusudia kushirikiana na Baraza la Jamii ya Waluo katika kutatua tatizo la ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi.
CYRUS Jirongo aliingia katika siasa za Kenya kama upepo mkali uliokuwa vigumu kupuuzwa, na hatari kuaminiwa kikamilifu. Kwa muda, hakuwa mtu tu bali mfumo mzima: sura changa kisiasa, na kapu la fedha wakati ambapo pesa zilizungumza kwa sauti kuliko alama za vyama. Jirongo alipokuwa kileleni, hakupita tu kwenye siasa za Kenya; alizitia mafuta kwa pesa. Katika msimu wa uchaguzi wa vyama vingi wa 1992, akiwa mwenyekiti wa Youth for KANU ’92 (YK’92), aligeuka kuwa mashine ya fedha ya chama tawala kilichokuwa kikihangaika kuendelea kuwa madarakani. “Kila mwanasiasa ana bei yake,” alinukuliwa akisema—kauli iliyotua kama tishio lililojificha ndani ya busara. Kwa wafuasi wake, ilikuwa uhalisia wa siasa; kwa wakosoaji, ilikuwa kukiri wazi jinsi YK’92 ilivyokusudia kununua mamlaka kama kabeji sokoni. Kuanzia ofisi za YK’92 katika KICC hadi Anniversary Towers, fedha hazikutiririka tu—zilifurika. Zilionekana katika mikutano ya kisiasa, bahasha na mabegi kama “gharama za kurahisisha mambo”. Nchi ilishuhudia utajiri wa ghafla ambao haukuakisi hali ya uchumi nje ya msafara wa kampeni. YK’92 ilitembea kwa jeuri na kelele kiasi kwamba Wakenya waliipa noti mpya ya Sh500 jina la “Jirongo”—heshima ya ajabu na kali kwa mtu aliyekuwa kiini cha sakata hilo. Alipofariki katika ajali ya barabarani usiku wa Ijumaa,Desemba 12 2025, Jirongo alikuwa akipambana na kesi nyingi zilizohusishwa na usimamizi wa fedha alizokusanya kupitia YK’92. Ingawa alipanda ngazi hadi kuwa Waziri katika utawala wa Moi, sura yake ilibaki ya broka wa mamlaka—mtu wa kutaka mambo ya haraka, aliyeandamwa daima na kivuli cha YK’92. Nguvu zake zilikuwa kubwa kiasi cha kuonekana akitembea kwa saa kadhaa na Rais Moi katika viwanja vya Ikulu tofauti nchini. Marafiki wanasema aliwahi hata kuhudhuria kikao cha Baraza la Usalama wa Taifa, ambacho huhudhuriwa na wachache sana. Inadaiwa pia kuwa akiwa YK’92, alikuwa akitembea na mabomu ya mkono ndani ya gari lake. Ikiwa ufisadi wa miaka ya 1990 ungevaa uso wa ujana, basi ungekuwa wa Jirongo—aliyetumia ukuruba wake kushawishi vijana kudhoofisha upinzani kwa wanasiasa kuhama vyama, vitisho na, kwa madai ya wengine, vurugu. Kuandika kuhusu Jirongo ni kurejea kipindi tata cha mpito wa Kenya kuelekea demokrasia ya vyama vingi, wakati ambapo maadili yalikuwa tu katika hotuba, lakini upendeleo ulitawala. Swali linalosalia hadi leo ni moja: fedha za YK’92 zilitoka wapi? Hakuna anayejali kwamba YK’92 ilitumia fedha nyingi kupita kiasi. Haikufadhili kampeni pekee, bali iligeuza siasa kuwa tamasha. Wapiga kura walisafirishwa kwa malori na mabasi, wakaburudishwa na mara nyingine kulipwa pesa taslimu. Mabango, fulana na kofia zilifurika masokoni. Katika kilele cha shamrashamra hizo, Goldenberg International—kampuni ya Kamlesh Pattni na James Kanyotu—iliendelea kufaidika kutoka Benki Kuu ya Kenya kwa madai ya “fidia” ya dhahabu feki. Hazina ya NSSF iligeuzwa kuwa chanzo cha fedha za kisiasa, ikinunua ardhi iliyoporwa kwa bei ya juu kupita kiasi. Mashirika ya umma yaligeuzwa mashine za kampeni. Jirongo, kupitia kampuni yake ya Sololo Outlets, alitajwa kupata zabuni ya kujenga nyumba za NSSF. Kamlesh Pattni aliambia tume iliyochunguza Goldenberg kuwa alifadhili YK’92, lakini kwamba serikali yenyewe ilifungua milango ya fedha bado inaendelea kuandama historia. Bunge ilielezwa kuwa NSSF ilinunua mali mbili za Sololo kwa Sh1.2 bilioni, zaidi ya thamani yake halisi. Zaidi ya Sh2.5 bilioni zilidaiwa kupitishwa kupitia Post Bank Credit, benki iliyokuwa tayari taabani, hatua iliyochangia kuporomoka kwake. Takwimu hizi zilionyesha ukweli mmoja: fedha za YK’92 hazikutokana na utajiri wa kawaida. Katikati ya yote alikuwa Cyrus Jirongo—kama mnufaika mkuu, mpangaji na mhandisi mkuu wa mpango huo. Baada ya uchaguzi wa 1992, YK’92 ilianza kuwatisha wale waliokuwa wamenufaika nayo. Ilionekana kama kituo cha mamlaka kisichodhibitika. Hatimaye, Rais Moi alisitisha shughuli zake mwaka 1993 baada ya Jirongo kumshambulia hadharani Makamu wa Rais George Saitoti. Kisha mfumo ukaonyesha upande wake mwingine wa kuadhibu. Kampuni zake ziliwekwa chini ya usimamizi maalum, zikapokonywa zabuni, na madai ya ushuru yakafuata. Hata hivyo, ni wachache waliokabiliwa na mashtaka ya jinai. Licha ya yote, Jirongo hakutoweka. Alihudumu kama Mbunge wa Lugari mara mbili na akaendelea kuwa katika ulingo wa siasa. Lakini jina lake lilibaki kuibua kumbukumbu za pesa nyingi, kesi nyingi na maswali yasiyojibiwa. Kwa msingi huu, Cyrus Jirongo anabaki kuwa alama zaidi ya mtu: broka wa mali aliyegeuka wa kuamua wafalme, kijana aliyegeuka radi ya kisiasa. Kukwea kwake ngazi ya ushawishi kunaonyesha nguvu ya upendeleo; kuporomoka kwake kunaonyesha ukatili wa mfumo huo huo. Na ikiwa Kenya itataka kufunga ukurasa wa “Jirongo” kama jina la noti ya pesa, haitakuwa kwa kumsahau mtu huyo—bali kwa kurekebisha mfumo uliomruhusu kuwepo.
MUUNGANO wa Upinzani unakumbwa na jaribio lake kubwa zaidi hadi sasa, vita kati ya wafuasi wa kiongozi wa Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka na wale wa Naibu Kiongozi wa Jubilee Fred Matiang’i na kuanika mgogoro kati ya vinara hao. Kilichoonekana kama ushirikiano dhidi ya utawala wa Rais William Ruto, sasa kimegeuka kuwa mzozo mkali wa ndani kwa ndani, huku upinzani ukigawanyika kati ya kundi linalompigia debe Kalonzo linalotiwa moyo na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua na jingine la Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, linalomuunga mkono Dkt Matiang’i. Kauli ya hivi majuzi ya Bw Gachagua kwamba Musyoka ni 'chaguo bora” la upinzani limechochea mvutano mpya katika muungano huo.Muungano wa Upinzani ambao unajumuisha Wiper ya Musyoka, DCP ya Gachagua, PLP ya Martha Karua, DP ya Justin Muturi, Jubilee ya Kenyatta, DAP-K ya Eugene Wamalwa na PNU chake Peter Munya, ulianzishwa kwa msingi wa malalamishi ya pamoja dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza na haja ya kumtangaza mgombea mmoja wa urais. Hata hivyo, kauli ya Gachagua ya kumuunga mkono Musyoka inaonekana kuuvunja na kusababisha mikutano miwili tofauti Alhamisi iliyopita kabla ya sherehe za Siku ya Jamhuri.Katika mahojiano na Taifa Jumapili, Martha Karua alisema hakuwa na habari yoyote kuhusu mpango wowote wa kumtangaza Musyoka kuwa mgombea wao wa urais, huku akisisitiza kuwa mashindano ni muhimu. “Binafsi, sihusiki na mpango huo,” alisema kuhusu kauli ya Gachagua kuidhinisha Musyoka. “Lakini mwanachama au wanachama wa muungano wa upinzani wana haki ya kupendekeza mtu. Msimamo wa pamoja utatangazwa kadri uchaguzi unavyokaribia. Kwa sasa mimi na wengine tunajenga majina yetu kama inavyotokea katika mashindano ya kidemokrasia.” Katika kambi ya Musyoka, kuna hali ya kujiamini – lakini pia kuna shaka kuhusu uingiliaji unaoonekana.Mwandani wa Kalonzo, Seneta wa Kitui Enoch Wambua, mmoja wa watetezi wakuu wa Musyoka, anachukulia mvutano unaoendelea kama njama ya makusudi kutoka kwa wapinzani wao. Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni anajitenga na “maamuzi ya siri” kuhusu mgombea wa urais. “Katika Jubilee wito wetu mkuu ni, wacha watu waamue,” alisema. “Kama Katibu Mkuu wa Jubilee sijawaona nyaraka zozote kuhusu mgombeaji. Bado ni mapema sana. Maamuzi haya ni bora kufanywa siku chache kabla ya uchaguzi.” Aliongeza “Uamuzi kuhusu nani atakuwa mgombeaji wa urais lazima ufanywe na watu wengi. Hauwezi kuwa matokeo ya mkutano au vyama viwili tu. Raila alifariki akipigania demokrasia ya vyama vingi. ” Kauli zake hazikupokelewa vizuri na viongozi kutoka Wiper na DCP, ambao wanashutumu Jubilee kwa kuwa na ndimi mbili. “Tabia ya Jubilee ni kwamba ina mguu mmoja katika upinzani na mguu mmoja serikalini,” anasema Seneta wa Makueni Dan Maanzo. “Wanapaswa kujadili badala ya kulazimisha mambo yao. Hata walipoteza wabunge wao wote kwa Ruto.”
RAIS Samia Suluhu Hassan ameongoza familia, viongozi, wabunge na waombolezaji wengine, katika ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Joakim Mhagama, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Mwenyeheri Maria-Theresa Ledochowska, Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, leo Desemba13, 2025. Akizungumza katika ibada hiyo kuhusu Jenista Rais Samia amesema: … The post Samia: Umetimiza wajibu wako kwa uaminifu mkubwa first appeared on HabariLeo.
KUZINDULIWA kwa chama kipya cha kisiasa cha aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko, National Economic Development Party (NEDP), kumesababisha taharuki ya kisiasa Ukambani huku Wiper Patriotic Front (WPF), kilicho maarufu eneo hilo, kikijaribu kupunguza hofu kwamba kurudi katika siasa kwa Sonko kunaweza kuathiri hesabu za Kalonzo Musyoka katika uchaguzi mkuu wa 2027. Bw Musyoka ambaye ni Kiongozi wa WPF, anakabiliwa na mabadiliko mapya ya kisiasa katika ngome yake, jambo lililosababisha chama hicho kuweka mkakati wa kujilinda, huku baadhi ya washirika wake wakihofia nia, na athari zinazoweza kutokea kutokana na kurudi kwa Sonko katika siasa. Licha ya kukabiliwa na mashtaka ya kisheria na changamoto za kisiasa, Sonko bado ana nguvu kisiasa zinazoweza kuvuruga uthabiti wa kisiasa. Hii ndiyo sababu, licha ya Wiper kuepuka kuonyesha hofu hadharani, kinafikiria kimya kimya jinsi ya kumkabili. “Chama hiki cha Sonko ni tishio kubwa kwa chama chetu hasa Ukambani na hapa Nairobi. Uongozi wa juu wa Wiper unahitaji kuwa makini. Ima tushughulikie chama hiki kipya kwa nguvu zote au tuketi pamoja na Sonko. Tubadilishe mkakati ili Wiper ibaki maarufu hasa katika ngome zake,” asema Fred Musau, aliyekuwa mgombeaji wa kiti cha Bunge la Afrika Mashariki (EALA) 2022. Hata hivyo, Bw Sonko anasisitiza kuwa anachofanya ni kutumia haki yake ya kikatiba. Kulingana naye, kuanzisha chama cha kisiasa si mapinduzi wala hujuma, bali ni hatua anayofuata katika safari yake ndefu ya kisiasa. “Ni haki yangu ya kikatiba na kidemokrasia kuanzisha na kuwa na chama,” Sonko alisema. “Ninaheshimu sana kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, na hili halihusiani na chama chake au ushawishi wake. Hata alinipigia simu kunipongeza.” Anakanusha madai yanayoongezeka hasa kutoka ndani ya Wiper, kwamba chama chake ni mradi wa Serikali ulioanzishwa na Rais William Ruto kuharibu muungano wa upinzani unaoongozwa na Rigathi Gachagua na Kalonzo. “Chama changu si mwanachama wa Muungano wa Upinzani, wala si mradi wa Ruto,” anasisitiza. “Kama ningekuwa mradi, kwa nini Serikali ilifunga akaunti zangu na kunizuia kutumia fedha zangu? Nia yangu ni kuwa Rais siku moja.” Lakini licha ya ujasiri wake hadharani, kuna chuki dhidi ya kile anachokiita kesi za kisheria zinazotumika kisiasa. “Sheria imetumika kwa ubaguzi dhidi yangu. Mahakama zimetumika kujaribu kudhoofisha kazi yangu ya kisiasa. Tutapigana hadi haki itendeke. Ni kosa kutangaza kifo changu kisiasa,” alisema. Mnamo Jumanne, Sonko alipokea cheti cha usajili wa chama na akatangaza nia yake ya kurejea katika siasa za jiji na nchi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027. “Tunakaribisha kila mtu kutoka kizazi cha Gen Z hadi wazee, kutoka asili zote za kisiasa na yeyote anayelenga kubadilisha nchi yetu. Tushirikiane na tufanye kazi pamoja. Tutajikita katika kuwahudumia Wakenya,” alisema Sonko.
TUNDUMA: Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameuagiza Wakala wa Barabara (TANROADS), kufanya tathmini ya kutanua barabara katika mpaka wa Tunduma unaopitisha magari yaendayo nchi jirani za Zambia na DR Congo ili kupunguza msongamano wa magari katika eneo hilo. Ulega ametoa agizo hilo akiwa Tunduma mkoani Songwe na kueleza kuwa Serikali inatambua changamoto wanayopitia wasafirishaji na … The post Serikali yatoa maagizo kuondoa foleni Tunduma first appeared on HabariLeo.
CHAMA cha Makanisa na Wahubiri Nchini (CCAK) kimepinga vikali kile kinachotaja kuwa mpango wenye upendeleo wa serikali kuharakisha kupitishwa kwa Sera ya Mashirika ya Kidini 2024 na Mswada wa Mashirika ya Kidini 2024. Kupitia kwa mwenyekiti wake wa kitaifa, Askofu Hudson Deda, chama hicho kilieleza kusikitishwa na hatua ya serikali kutojumuisha maoni ya viongozi wa makanisa ambayo yaliwasilishwa kuingizwa katika rasimu ya mwisho kabla ya kupelekwa kwa ushirikishaji wa umma. Katika taarifa ya Desemba 12, chama hicho kilisema kilishtushwa na notisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, iliyoitisha ushirikishaji wa umma kuhusu mswada huo unaolenga kuongoza shughuli za taasisi za kidini nchini. “Tunatambua kuwa ushirikishaji wa umma umejengwa ndani ya Katiba, na kwamba Ofisi ya Mkuu wa Mawaziri inajaribu kutekeleza wajibu huo. Hata hivyo, makanisa na wahubiri nchini wana wasiwasi kuhusu muda na kasi kinachotumika kuendesha mchakato huu,” alisema Askofu Deda. Aidha, chama hicho kilisema kuwa ingawa kikao cha mwisho cha kamati ya pamoja, kilichohudhuriwa na Bw Mudavadi, kilikubaliana kufanyika kwa mkutano mwingine na Mwanasheria Mkuu, kikao hicho hakijafanyika jambo linaloibua maswali kuhusu nia ya serikali. Pia chama hicho kilisema kuwa juhudi zake za kumfikia Katibu wa Wizara ya Uratibu wa Kitaifa, Ahmed Abdisalan Ibrahim, hazijafaulu. “Kwa mshangao wetu, tuliona tena ule mwaliko wa awali wa ushirikishaji wa umma ambao tulipinga. Tuliwasiliana na Mheshimiwa Ahmed, akatuahidi kuwa baada ya kupokea maoni, tutafanya mkutano mwingine pamoja. Kwa bahati mbaya, tumeachwa nje, na sasa tunashuhudia mwito mwingine wa ushirikishaji wa umma kuhusu hati ambayo sisi hatuijui,” alisema Askofu Deda. Kwa mujibu wa notisi ya serikali, wananchi wametakiwa kuwasilisha maoni yao kuhusu mswada huo kati ya Desemba 10 na 15, 2025. Mswada huo uliandaliwa na jopo kazi lililoongozwa na Padre Mutava Musyimi, lililoanzishwa kufuatia vifo vya waumini wa dhehebu la Shakahola ambapo kufikia sasa zaidi ya miili 400 imefukuliwa, mojawapo ya maafa mabaya zaidi ya imani potofu nchini. Ingawa lengo la mswada ni kudhibiti shughuli za taasisi za kidini na kuzuia maafa kama ya Shakahola, makanisa, yaliyotajwa kuwa wadau wakuu, yanataka uwazi na muda wa kutosha kushughulikia mapungufu yanayodaiwa kupatikana. “Tunasoma hila katika muda uliotolewa, kwani Disemba ni mwezi ambao wahubiri wengi wana majukumu mengi. Muda uliotolewa hautoshi kutupatia nafasi ya kushughulikia sera na mswada huu ipasavyo, tunavyoona, serikali imelenga kuhakikisha mswada unapitishwa haraka. Hii ni kinyume cha Katiba,” chama hicho kilisema. Aidha, Askofu Deda alisema kuwa mara tu nyaraka hizo zitakapopitia hatua ya ushirikishaji wa umma, haitakuwa rahisi kwa maoni ya viongozi wa dini kuingizwa mwishoni mwa mchakato wa utungaji sheria. “Kanisa na wahubiri nchini wanapinga hatua hii ya ushirikishaji wa umma. Mchakato huu hauna baraka zetu,” alisema Askofu Deda.
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA). Hayo yamejiri katika mkutano wa saba wa Baraza hilo uliofanyika katika Makao Makuu ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), jijini Nairobi, Kenya. Uchaguzi … The post Mhandisi Masauni Makamu wa Rais UNEA first appeared on HabariLeo.
Aliyekuwa Waziri na Mbunge wa Lugari, Cyrus Jirongo, ameaga dunia kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyotokea mapema Jumamosi usiku katika barabara kuu ya Nakuru–Naivasha. Kwa mujibu wa ripoti ya polisi kutoka Kituo cha Naivasha, ajali hiyo ilitokea leo, Desemba 13, 2025, saa tisa usiku katika eneo la Karai. Jirongo, mwenye umri wa miaka 64, alikuwa akiendesha gari aina ya Mercedes Benz lenye nambari ya usajili KCZ 305C kutoka upande wa Nakuru akielekea Nairobi. Ripoti hiyo inaeleza kuwa alipofika eneo la ajali, alishindwa kudhibiti gari lake na likatoka laini yake sahihi, hali iliyosababisha kugongana ana kwa ana na basi lenye nambari ya usajili KCU 576A, linalomilikiwa na kampuni ya Climax. Basi hilo lilikuwa likiendeshwa na Tiras Kamau Githinji, mwenye umri wa miaka 52, ambaye alikuwa akitokea upande wa Nairobi akielekea Nakuru. Kutokana na ajali hiyo, Jirongo alipata majeraha makubwa ya kichwa na alifariki papo hapo. Polisi walifika eneo la tukio na kuchukua hatua zinazohitajika. Mwili wake ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Naivasha ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa maiti. Magari yote mawili yalivutwa hadi kituo cha polisi na kuzuiliwa kwa uchunguzi zaidi wa kiufundi. Polisi wamesema chanzo cha ajali bado kinachunguzwa, Jirongo aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Maendeleo ya Maeneo ya Mashambani katika utawala wa hayati Rais Daniel Moi mwaka 2002, na pia alikuwa Mbunge wa Lugari katika mihula miwili tofauti. Kifo chake kimezua huzuni miongoni mwa viongozi na wananchi, wengi wakimtaja kama mwanasiasa na mfanyabiashara aliyetoa mchango mkubwa katika siasa za Kenya.
WAZEE wa jamii ya Luhya Desemba 11, 2025 walifanya kikao cha mashauriano na viongozi wakuu wa ODM kutoka eneo la Magharibi ili kujadili mustakabali wa jamii hiyo kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Wazee hao walihoji Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, na Naibu Kiongozi wa chama hicho, Godfrey Osotsi, wakitaka kufahamu nafasi ya jamii ya Waluhya ndani ya ODM baada ya enzi za aliyekuwa Waziri Mkuu, marehemu Raila Odinga. Taarifa ambazo Taifa Leo imepata zinaonyesha kuwa wazee walitaka ufafanuzi kuhusu hali ndani ya chama na madai ya kutengwa kwa jamii hiyo katika serikali Jumuishi. Wakiongozwa na Mzee Patrick Wangamati na aliyekuwa rais Noah Wekesa, wazee walilalamika kuwa hawajawahi kupewa taarifa zozote kuhusu makubaliano ya kuunda serikali jumuishi, licha ya jamii hiyo kuwa miongoni mwa wafuasi sugu wa ODM. Aidha, mkutano huo uliibua maswali kuhusu kile walikitaja kuwa njama za kisiasa dhidi ya Bw Sifuna kutokana na msimamo wake mkali wa kupinga makubaliano kati ya Bw Odinga na Rais William Ruto, msimamo ambao umemfanya akinzane na baadhi ya viongozi wa chama wanaounga mkono mpango huo. “Tuliwaita viongozi hawa wawili wakuu wa ODM watupe taarifa kuhusu yanayoendelea ndani ya chama. Sehemu kubwa ya jamii yetu iko ODM, kwa hivyo kinachoendelea humo kinatuhusu. Hakuna mtu aliyetuambia chochote kuhusu mpango wa serikali jumuishi,” alisema Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wazee wa Luhya, Fred Omondi. Baadhi ya maafisa wa juu wa ODM walioingia serikalini kupitia mpango huo ni John Mbadi (Waziri wa Fedha ), Ali Hassan Joho (Madini na Uchumi wa Bahari), Opiyo Wandayi (Kawi na Petroli), Wycliffe Oparanya (Ushirika) na Beatrice Askul (Maeneo Kame). Mbali na Bw Oparanya, ukanda wa Magharibi pia una Musalia Mudavadi ( Mkuu wa Mawaziri) na Deborah Barasa (Waziri wa Mazingira). Kadhalika, Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula, anatoka katika eneo hilo. Bw Wekesa alisema mkutano huo ni sehemu ya juhudi za jamii kuungana upya kabla ya uchaguzi wa 2027 kutokana na kugawanyika kwao kisiasa mara kwa mara, hali inayowanyima nguvu katika majadiliano kitaifa. “Sisi ni jamii ya pili kwa idadi nchini, lakini hatuchukuliwi kwa uzito. Tutahakikisha tunaenda katika uchaguzi tukiwa kitu kimoja. Huu ni mwanzo tu wa mikutano zaidi ijayo,” alisema Bw Wekesa. Katika taarifa ya pamoja baada ya mkutano wazee walisema wameamua kuhimiza umoja ili jamii “isitengwe pembeni”. “Ni kwa maslahi binafsi ya baadhi ya wanasiasa kugawanya jamii ya Waluhya ili tusinufaike na nguvu ya idadi ambayo tumekirimiwa na Mungu,” ilisema taarifa hiyo. Wazee walisema wameunda kikundi cha viongozi, wazee, wataalamu na wafanyabiashara ili kuanzisha mazungumzo ya kina ndani ya jamii na pia na jamii nyingine za Kenya. “Hii ndio njia ya haki ya kupata mwafaka ili tusigeuke kuwa waathiriwa wa mabroka wa kisiasa wanaotumia nguvu ya idadi ya Waluhya kwa maslahi yao binafsi,” waliandika. Akizungumza kando ya mkutano huo, Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka alitoa wito kwa viongozi wa jamii ya Mulembe kuweka tofauti zao kando na kuungana katika ajenda moja ya pamoja ya eneo la Magharibi.
KIONGOZI wa Democracy for the Citizens Party (DCP), Rigathi Gachagua, Desemba 10, 2025 aliwajibu wakosoaji wanaomlaumu kwa kuzungumza kupita kiasi na kufichua siri za kisiasa zinazofaa kubaki kwenye milango ya mazungumzo, hasa kabla ya makubaliano yoyote kutiwa saini. Naibu rais huyo wa zamani alisema hana mpango wa kunyamaza na ataendelea kujieleza bila kizuizi chochote, akisisitiza kuwa anaongozwa na ukweli, uwazi na uadilifu. “Nimesikia watu wakisema nisiweke wazi mikakati ama siri zangu, hakuna siri. Mimi ni kitabu wazi,” aliambia KTN. Aliongeza: “Ninazungumza kwa niaba ya watu wanaoniunga mkono, na wana haki ya kujua ninachowapangia.” Bw Gachagua alisema hatashiriki katika siasa za kuchezeana karata ama kufanya maamuzi ya siri. “Mimi si mtu wa kukubaliana kwa faragha. Nitakuja mbele ya wafuasi wangu kuwaeleza bayana aina ya makubaliano ninayowaingiza,” alisema. Alisema kuwa hulka ya kufanya mambo kwa siri ndiyo inaathiri serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto, “kwa kuwa hatukuwahi kuwaambia wananchi tulichokubaliana naye.” Katika mahojiano hayo, Bw Gachagua alizungumzia pia utata ulioibuka baada ya kudai kwamba ana makubaliano na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, kuhusu kugawana viti Nairobi, kauli iliyozua upinzani mkali ndani ya muungano wa upinzani. “Namaanisha nilichosema, na si kwa DCP pekee. Ni baina ya Wiper na DCP — mimi na Kalonzo,” alisema. Alisisitiza kuwa hotuba yake ya Novemba 30, 2025 katika Kanisa la PCEA Embakasi ilipotoshwa kudai kwamba alitaka viti vya Nairobi vihifadhiwe kwa jamii ya Wakikuyu. “Sikusema hivyo. Nilisema tu kwamba namtambua Bw Musyoka kwa nafasi yake muhimu katika siasa za Nairobi, na amekuwa akisaidia ODM kushinda viti huko,” akasema. Katika hotuba hiyo, alisema:“Tuna makubaliano na Kalonzo Musyoka na chama cha Wiper kwamba DCP itachukua ugavana, useneta, mwakilishi wa wanawake, na kwa pamoja tuchukue maeneo bunge 16 kati ya 17, na wadi 75 kati ya 85.” Katika mahojiano alisisitiza “Si uwongo, maana hata Bw Musyoka ameeleza wazi kwamba tumekubaliana kushirikiana ili kuimarisha ushindi.” Bw Gachagua alisema ana kila haki ya kutafuta nafasi muhimu za kisiasa kwa chama chake ndani ya muungano wa upinzani na kwamba kama kushirikiana na Wiper kunahitajika, basi atafanya hivyo. “Watu wanadhani mimi ni nani? Nisishughulikie maslahi ya chama changu? Nisiwe na mikakati ya kushinda Nairobi? Ningekuwa mjinga. Nimeongea na Kalonzo, na nitaendelea kufanya hivyo,” alisema. Kwa upande wake, Bw Musyoka amekuwa akibadilisha misimamo, akikanusha kwanza kuwepo kwa mkataba wowote, kisha baadaye akamsifu Gachagua kwa “ukweli na ujasiri.” Hata hivyo, alisisitiza kuwa Nairobi haiwezi kugawanywa kwa misingi ya vyama. “Nairobi haiwezi kuwekewa mipaka ya vyama. Hili ni jiji la kimataifa, linahitaji demokrasia ya wazi,” alisema. Bw Gachagua alidai kuwa Rais Ruto na washauri wake “wana wasiwasi” kuhusu umaarufu wake unaoongezeka na kukua kwa ushawishi wa DCP kuelekea 2027. “Ndio maana wanapiga kelele kwamba mimi ni mkabila na kwamba DCP ni chama cha kujitenga. Hawatafanikiwa,” alisema. Alisema yeye na Bw Musyoka wamekubaliana kuepuka “kuumizana kisiasa” Nairobi katika Uchaguzi Mkuu wa 2027 “ili kumnyima Rais Ruto mianya ya kushinda viti.” Alirudia madai kwamba baadhi ya vyama vya upinzani vinasaidia UDA kwa siri, akirejelea alama ya UDA ya wilibaro Alitaja mfano wa uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini ambapo mgombeaji wa upinzani Newton Kariuki alishindwa na Leonard Wa Muthende wa UDA. Alisema chama cha Moses Kuria, Chama Cha Kazi (CCK), kiligawanya kura za upinzani.
RAIS William Ruto jana aliendelea kutoa ahadi kuhusu hatua muhimu za kugeuza Kenya kuwa taifa lenye uchumi wa kisasa na uhuru wa kiuchumi kwa wananchi wote. Rais Ruto alisema kuwa marekebisho ya sera za kiuchumi yamesaidia kuimarisha uchumi, kurejesha imani ya wawekezaji, na kuongeza thamani ya sifa ya mkopo wa taifa. Hii ni sehemu ya mpango wa Sh 5 trilioni unaolenga kufanikisha nchi kuwa ya uchumi wa kiwango cha kwanza. Rais Ruto alitaja hatua tatu kuu zinazounda msingi wa mpango wake wa taifa. Serikali imepanga mradi wa miaka 10 wa barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na mabomba ya mafuta, ikiwa ni pamoja na upanuzi wa barabara kuu za miji mikuu na kuunganisha mashamba, viwanda, na masoko. Hivi karibuni, serikali ilizindua ujenzi wa barabara ya Nairobi–Nakuru–Mau Summit na Nairobi–Maai Mahiu–Naivasha, mradi wenye thamani ya KSh 180 bilioni. “Wiki iliyopita, wananchi wenzangu, tulichukua hatua kutoka kwa ahadi hadi utekelezaji kwa kuanzisha ujenzi wa barabara ya Nairobi–Nakuru–Mau Summit na Nairobi–Maai Mahiu–Naivasha, uwekezaji wa zaidi ya Sh180 bilioni katika barabara ya kisasa,” alisema. Aidha, serikali imepanga kujenga barabara kuu za kilomita 2,500 ili kuunganisha kaunti zote 47, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na wananchi, na kuimarisha uchumi wa viwanda na kilimo. Upanuzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Naivasha hadi Malaba, pamoja na upanuzi wa bomba la mafuta kutoka Eldoret hadi Uganda, pia umekusudiwa kufungua njia mpya za usafirishaji ndani ya nchi na kieneo. 'Mnamo Februari 2026, tutaanza kupanua Reli ya Kisasa kutoka Naivasha hadi Malaba, na mwishoni mwa mwaka, kupanua bomba la mafuta kutoka Eldoret kwenda Uganda, kufungua mlango mpya wa usafirishaji na majirani zetu na bara lote,' alisema. Katika hotuba yake Rais Ruto alianika mikakati na ahadi za serikali yake zinazolenga kuimarisha uchumi wa Kenya na kufanikisha uhuru wa kiuchumi. Rais aliahidi barabara ya Expressway kutoka Thika hadi Museum Hill kuanzia mwaka ujao, akisema hatua hiyo itapunguza msongamano wa magari mjini Nairobi. 'Kuna mambo mengi tuliyokubaliana na Serikali ya Kaunti ya Nairobi kuendeleza mjini. Tutajenga barabara zote ambazo zilikuwa zimekwama hapa Nairobi, na tayari tumeafikiana kurudisha wakandarasi wote,' alisema Ruto. Rais pia alibainisha kuwa kilomita 60 za barabara tayari zinaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali jijini. “Kuanzia Desemba hii, wakati mtakuwa mnasafiri kwa Krismasi, tutajenga upya barabara kutoka JKIA hadi ABC na kupamba jiji ili Nairobi ionekane kama mji wa kisasa,' alisema. Ruto pia aliahidi upanuzi wa eneo la Nairobi Metropolitan, akilenga sehemu ambazo wakazi wanakabiliwa na msongamano mkubwa kila siku. 'Tunajua Wakenya wengi wanaishi ndani ya eneo la Nairobi na kufanya kazi mjini—watu wanaoishi Kiserian, Rongai, Ngong—wanaopitia msongamano mkubwa asubuhi na jioni. Kuanzia mwaka ujao, barabara kutoka Bomas of Kenya hadi Rongai na Kiserian, na kutoka Karen kupitia Ngong hadi Kiserian, itapanuliwa,' alisema. Akitaja barabara ya Thika, Rais alisema: 'Ninaelewa kuwa watu wengi wanaoishi Thika na kutumia Thika Road wanakabiliwa na msongamano mkubwa. Kuanzia mwaka ujao, kama ilivyo Expressway kutoka JKIA, pia tutajenga Expressway kutoka Thika hadi Museum Hill ili kupunguza msongamano.' Rais Ruto pia alitaja mipango ya kuboresha bandari za Mombasa na Lamu na viwanja vya ndege vya kitaifa, ikiwemo JKIA, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa bidhaa, watu na huduma, na kufanya Kenya iwe kitovu cha biashara kanda nzima. Alisisitiza kwamba miradi hii yote itapunguza gharama za usafirishaji, na kuunda fursa mpya za biashara na uwekezaji. Kuhusu kilimo na utoshelevu wa chakula, Rais Ruto aliahidi mabwawa makubwa 50, madogo 200, na madogo zaidi 1,000 katika kaunti zote, hasa katika maeneo kame na nusu kame. Miradi hii inalenga kuongeza ardhi inayopandwa chakula, kuongeza uzalishaji wa chakula, na kuwezesha Kenya kuzalisha bidhaa za kilimo na viwandani. “Hii si tu utoshelevu wa chakula na maji, bali ni uwekezaji unaoathiri taifa mzima,” alisema. Katika sekta ya kawi, Rais Ruto alitaja mipango ya kuongeza uzalishaji wa kawi hadi Megawati 10,000 katika miaka saba ijayo. Kenya ina rasilmali kubwa za kawi endelevu.
ZANZIBAR: Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, leo amepokea tuzo ya kuwa Kivutio Bora cha Mikutano ya Kimkakati Barani Afrika (African’s Best Corporate Retreat Destination 2025). Tuzo hiyo imetolewa baada ya Zanzibar kushinda katika Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards 2025) zilizofanyika nchini Bahrain. Rais Mwinyi amekabidhiwa … The post Dk Mwinyi apokea tuzo kivutio bora Afrika first appeared on HabariLeo.
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) William Lukuvi ametoa wito kwa vijana kuendelea kujijengea uwezo ili kuwa na uelewa kuhusu mazingira. Ametoa wito huo alipokutana na vijana wa kitanzania wanaojihusisha na masuala ya mazingira jijini Nairobi, Kenya unakofanyika Mkutano wa Saba wa Baraza la Mazingira la Umoja wa … The post Lukuvi asihi vijana kuwa uelewa wa mazingira first appeared on HabariLeo.
TANZANIA inaendelea kung’ara kimataifa kupitia sekta ya madini, huku Twiga Minerals Corporation yenye ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Barrick ikichukua nafasi ya kipekee katika kukuza uchumi wa taifa. The post Twiga Minerals Yaipa Tanzania Nuru Mpya ya Maendeleo first appeared on HabariLeo.
SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati imesema imekuwa na mazungumzo na Wizara ya Fedha kupunguza gharama na kodi katika vifaa vinavyotumika kubadilisha mfumo wa vyombo vya usafiri wa moto kutoka kutumia mafuta hadi gesi. Naibu Waziri wa Nishati wa Nishati Salome Makamba amesema hayo wakati alipotembelea kituo mama cha kujaza gesi kilichopo eneo la Mlimani City … The post Mazungumzo mabadiliko matumizi ya mafuta kwenda gesi first appeared on HabariLeo.
KAMPUNI ya Mgodi wa Bucreef imetumia sh bilioni 1.8 kutekeleza miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) wilayani Geita ndani ya miaka minne kati ya mwaka 2020/21-2024/25. Aidha Mgodi wa Bucreef umefanikiwa kuongeza kiwango cha CSR kutoka wastani wa sh milioni 450 kila mwaka hadi kufikia wastani wa sh milioni 600 kwa mwaka wa … The post Bil 1.8/- zatumika miradi ya CSR Geita first appeared on HabariLeo.
ARUSHA; CHAMA cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Osunyai jijini Arusha, kimesema katika kujiimarisha kiuchumi, kipo katika mpango wa ujenzi wa ukumbi wa kisasa kwa shughuli mbalimbali za kijamii. Akizungumza na DailyNerws Digital, Katibu Kata ya Osunyai, Zubeda Abdallah amesema chama hicho kina mpango wa kufanya harambee ili kujenga jengo hilo . Amesema likikamilika jengo hilo … The post CCM Kata Osunyai waja kivingine first appeared on HabariLeo.
GAVANA wa Nairobi, Johnson Sakaja ametoa wito kwa serikali ya Rais William Ruto kubadilisha jina la uwanja wa Talanta kwa heshima ya aliyekuwa Waziri Mkuu marehemu Raila Odinga. Gavana huyo alitoa wito huo wakati wa sherehe za 62 za Jamhuri katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi. Gavana Sakaja alitumia hotuba yake kumrai rais kuzingatia maombi ya wakazi wa Nairobi wanaotaka uwanja huo upewe jina Raila. Matamshi yake yalipokelewa kwa shangwe kwani hii ndio Jamhuri Dei ya kwanza kusherehekewa bila Raila kuwepo. Sakaja aliambia umati kuwa kuanzia mwaka ujao, hafla kuu za kitaifa zitaandaliwa katika uwanja wa Talanta, akiongeza kuwa wakazi wa Nairobi waliona inafaa kukipa kituo hicho jina la Raila Amolo Odinga Stadium, ombi lililoibua shangwe kutoka kwa waliohudhuria sherehe hizo. "Tunajua kuwa kuanzia mwaka ujao, zoezi hili litafanyika katika uwanja wa Talanta hapa Nairobi. Kwa niaba ya wakazi wa Nairobi, tunakuomba ukubali kubadilisha jina la uwanja huo kuwa Uwanja wa Kimataifa wa Raila Amolo Odinga, kama njia ya kutoa heshima kwa Bw Odinga," Sakaja alisema.
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua za haraka, shirikishi na zenye matokeo katika kukabiliana na changamoto za mazingira zinazoendelea kuikabili dunia. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye Ulemavu) William Lukuvi ametoa wito huo katika hotuba aliyoitoa kwa niaba ya, … The post Tanzania yasihi dunia kukabili changamoto za mazingira first appeared on HabariLeo.
MWANZA: Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amemuelekeza Mkandarasi Jassie and Company (JASCO) anayetekeleza ujenzi wa Daraja la Mkuyuni kukabidhi daraja hilo ifikapo Januari 15, 2026 ili wananchi waondokane na changamoto wanayopata katika eneo hilo hasa kipindi cha mvua. Ulega ametoa maelekezo hayo Desemba 11, 2025 mkoani Mwanza akiwa katika ziara maalumu ya kukagua maendeleo ya … The post Ulega ambana mkandarasi daraja la Mkuyuni Mwanza first appeared on HabariLeo.
HOSPITALI ya Mama na Watoto ya Margaret Kenyatta jijini Nakuru ambayo ni ya pili kwa ukubwa ya aina hiyo nchini baada ya Pumwani jijini Nairobi, inakabiliwa na msongamano mkubwa ambapo hadi akina mama wanne pamoja na watoto wao wanalazimika kutumia kitanda kimoja. Hospitali hiyo yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 250, iliyoko ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Nakuru Level Five, imefurika kupita kiasi. Uchunguzi wa kina uliofanywa na Taifa Leo umebaini kuwa vitanda vilivyo katika wadi havitoshi kuhudumia idadi kubwa ya wanawake wanaotafuta huduma za kujifungua. Ingawa jengo hilo la kisasa linaonekana maridadi kwa nje, hali ya ndani ni ya kusikitisha na imeendelea kudorora, na kuwaacha wagonjwa katika hali ya kukata tamaa. Akina mama wajawazito na waliojifungua hulazimika kulala kwa zamu, huku wengine wakilala sakafuni kutokana na ukosefu wa vitanda. Kutokana na msongamano mkubwa, akina mama watatu na watoto wao wachanga hutengewa kitanda kimoja, na mara nyingine hadi wanne. “Hali hairidhishi kabisa,” walisema akina mama waliolalamika walipoongea na Taifa Leo. Ziara za hivi karibuni katika wadi ya uzazi zilionyesha kuwa tatizo hilo limekuwepo kwa muda mrefu, bila ishara yoyote ya hatua ya dharura kuchukuliwa. Mama mmoja, Velyn (si jina lake halisi), anayemlea mtoto mchanga katika kituo hicho, aliambia Taifa Leo kuwa yeye na akina mama wengine watatu wamelazimika kutumia kitanda kimoja wakati wote alikuwa hapo. “Tunalala kwa zamu. Wakati mwingine tunalala kitanda kimoja watu wanne, na wengine hulala sakafuni. Unatumia nguo na leso zako kujifariji kwa sababu hakuna mashuka wala magodoro ya kutosha,” alisema. “Wakati mwingine tunakesha usiku kucha ili tu watoto wetu wapate kulala,” akaongeza. Kitengo hicho ambacho kinapaswa kuwa mahali salama kwa wajawazito sasa kinawaweka katika hatari ya kuambukizwa maradhi kutokana na msongamano mkubwa. Muuguzi mmoja katika kituo hicho, ambaye hakutaka kutajwa, alifichua kuwa kutokana na wingi wa wajawazito wanaowasili, mara nyingi hulazimika kutandaza vitanda vya dharura sakafuni au kuwaweka akina mama kwa pamoja kitandani. “Idadi ya wajawazito imekuwa ikiongezeka sana miezi ya karibuni na wakati mwingine hatuna chaguo ila kuwaweka akina mama pamoja. Hatuwezi kuwakataa waliofika tayari kujifungua,” alisema muuguzi huyo. Wakazi na wanaharakati wa mashirika ya kiraia sasa wanaitaka serikali ya Kaunti ya Nakuru kuchukua hatua za haraka kuboresha hali katika wadi hiyo ili kuepuka hatari ya maambukizi. Maafisa wa afya wamethibitisha uzito wa tatizo hilo, wakisema linatokana na wagonjwa kuwa wengi. Mnamo Jumatatu jioni, maafisa wa Afya wa Kaunti ya Nakuru walikiri kuwepo kwa msongamano, wakidai unatokana na idadi kubwa ya watu wanaotegemea hospitali hiyo. “Idara ya afya inataka kutoa ufafanuzi kuhusu wasiwasi ulioibuliwa kuhusu msongamano katika Kitengo cha Mama na Mtoto cha Margaret Kenyatta ndani ya Hospitali ya Nakuru Level Five. Kama hospitali ya rufaa inayohudumia Nakuru na zaidi ya kaunti sita jirani, wakati mwingine shinikizo la mahitaji na matarajio ya huduma huongezeka,” alisema Waziri wa Afya wa Kaunti ya Nakuru, Bi Roselyn Mungai.
TUME ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani uliotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imeanza rasmi kazi zake. Tume hiyo chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Novemba 19, mwaka huu ikiwa na wajumbe wengine saba ambao ni Watanzania wabobezi katika masuala mbalimbali. The post Tujitokeze kuipa taarifa Tume ya vurugu Oktoba 29, tulisaidie taifa first appeared on HabariLeo.
DODOMA: PRESIDENT Samia Suluhu Hassan yesterday appointed the new Director General of the Public Service Social Security Fund (PSSSF) and Chairperson of the Board of Directors of the Tanzania Electric Supply Company (TANESCO). According to a statement issued by the Chief Secretary, Ambassador Dr Moses Kusiluka, the Head of State has appointed Mr Fortunatus Magambo … The post Samia picks new PSSSF boss, Tanesco’s Board chair first appeared on Daily News.
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa wito kwa vijana walinde amani ya Tanzania. Ulega alisema amani ni nguzo ya maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi. The post Ulega: Vijana lindeni amani first appeared on HabariLeo.
NGOMA ya kitamaduni ya jadi ya Taita Taveta inayojulikana kama 'Mwazindika' imetambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN) na itakuwa ikilindwa kimataifa kupitia kwa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco). Tangazo hilo lilifanywa katika mkutano wa shirika hilo uliofanyika Desemba 9 nchini India, ambapo UN ilitangaza kushirikiana na Kaunti hiyo na taasisi zingine ili kulinda ngoma hiyo. Ngoma hiyo, ambayo imekuwa ikipingwa na viongozi wa dini hasa makanisa, huchezwa na wanaume na wanawake, hasa wakati wa sherehe kama vile harusi, mazishi, na tamasha zinginezo. Aidha, huonyesha utamaduni wa jamii hiyo, pamoja na historia yao, maadili, na kanuni za kijamii. Wakati wa kucheza ngoma hiyo, wanaoshiriki husisimuka kiasi kwamba wakati mwingine huonekana kupagawa, hasa wakati ngoma inapopigwa. Wakati wa kucheza nyimbo za Mwazindika, wanaoshiriki hutumia ngoma kubwa zilizotengenezwa kwa shina za miti zilizochimbwa, zikipambwa kwa ngozi ya ng’ombe na shanga na vilevile kupiga firimbi na vigelegele. Wachezaji huvaa kofia za aina ya kipekee vichwani, mikufu, bangili, na vikuku vya miguu. Bw Mwaliko wa Maghenda, mmoja wa wazee wa Taita, alisema ngoma hiyo imekuwa ikididimia kutokana na vijana kuhamia mijini pamoja na kutozingatia mila na desturi. “Kukumbatia dini na vijana wengi kuhamia mijini ni mmoja ya sababu ambazo tunaona ngoma hiyo inazidi kudidimia, wazee wanakufa ilhali vijana hawataki kufunzwa jinsi ya kuicheza. Vilevile, wakazi wengi wamezingatia dini na kushirikisha ngoma hiyo na uchawi na utamaduni,” alisema Bw Maghenda. Wakati wa kuorodheshwa, naibu gavana wa Taita-Taveta Christine Kilalo, alisema ni fahari kubwa kwani Unesco itasaidia kupitisha ujuzi huo kutoka kizazi kimoja hadi kingine. “Kwa kurekodi ngoma hiyo, Mwazindika itaweza kutangazwa kote nchini na kuvutia watalii wengi katika Kaunti yetu hivyo kuwanufaisha watu wetu kiuchumi,” alisema Bi Kilalo. Mchakato wa kuorodhesha ngoma hiyo ulianza Februari 20, 2024 ambapo wataalamu wa Unesco, wakiongozwa na mshauri wa utamaduni wa ukanda wa Afrika Mashariki Masanori Nagaoka na Mkurugenzi wa Utamaduni wa Tume ya Kitaifa Julius Mwahunga, walizuru kaunti hiyo ili kushirikiana na wadau mbalimbali kuhusu mchakato wa kuandikisha ngoma hiyo. Wajumbe hao walikutana na maafisa wa serikali na wale wa taasisi mbalimbali, wachezaji wa Mwazindika kutoka makundi tofauti, na baraza la wazee kutoka sehemu mbalimbali za kaunti. Siku ya Jumatatu, katika kikao maalumu cha 20 cha mwaka mwenyekiti wa ujumbe maalumu wa unesco Vishal V. Sharma, alitangaza kuidhinishwa kwa hoja hiyo baada ya kujadiliwa na ujumbe katika makao makuu ya umoja wa Mataifa Paris Oktoba 23, 2025. Kwa kuidhinishwa, ngoma hiyo italindwa na kukuzwa na Unesco kwa kuihifadhi na kurekodi ngoma hiyo, ili kupitishwa kutoka kizazi hadi kizazi kingine,” alisema Bw Sharma.
RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ametaja vipaumbele sita, vikiwa ni mwongozo wa utekelezaji na usimamizi wa majukumu kwa viongozi wakuu wa serikali katika taasisi wanazoziongoza. Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Raqey Mohamed ameeleza Dk Mwinyi alitaja vipaumbele hivyo alipofungua mafunzo ya awali kwa viongozi wakuu wa serikali katika Chuo cha IIT Madras, Bweleo, Mkoa wa Mjini Magharibi. The post Rais Mwinyi ataja vipaumbele 6 vya usimamizi first appeared on HabariLeo.
SERIKALI imeiagiza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma itimize wajibu wake ili kumaliza tuhuma dhidi ya viongozi wa serikali. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Ridhiwani Kikwete ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba na watendaji wa sekretarieti hiyo Dodoma. The post Serikali yaibana Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi first appeared on HabariLeo.
MWANASIASA mkongwe aliyewahi kuwa waziri na mbunge kwa miaka 25, Jenista Joakim Mhagama (58) amefariki dunia. Kwa mujibu wa Spika wa Bunge, Mussa Zungu, Jenista ambaye hadi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu alikuwa Waziri wa Afya, amefariki dunia jana Dodoma. The post Buriani Jenista Mhagama 1967 – 2025 first appeared on HabariLeo.
MUUNGANO wa Upinzani umeendelea kukosoa utawala wa Rais William Ruto, ukidai Kenya haiko salama chini ya uongozi wake, huku Wakenya wakiadhimisha miaka 62 tangu nchi ilipopata uhuru. Katika taarifa ya pamoja Alhamisi, viongozi hao walikosoa jinsi serikali inavyoshughulikia masuala ya kitaifa na kudai Rais hana heshima kwa utawala wa sheria. Kiongozi wa Democratic Action Party–Kenya […]