ARUSHA: Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP) na Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za haki jinai, kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu na uzalendo ili kujenga imani ya wananchi kwa Serikali.
Johari amesema hayo leo jijini Arusha wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Sita wa Umoja wa Taasisi za Haki Jinai, akisisitiza kuwa umoja huo unapaswa kuwa chombo muhimu katika mapambano dhidi ya uhalifu na kuimarisha usalama wa wananchi kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Alisema umoja huo unapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea kwa kasi duniani kwa kuimarisha ushirikiano na kutumia teknolojia ya Akili Unde (AI) katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Alibainisha kuwa usalama na amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya Taifa, hivyo taasisi zinazohusika na usimamizi na utekelezaji wa sheria na haki jinai zinapaswa kushirikiana kwa karibu katika kuzuia na kupambana na uhalifu kwa ufanisi.
Aidha, alisema ni muhimu kwa taasisi hizo kutumia ubunifu, maarifa na teknolojia katika kukabiliana na mabadiliko ya aina za uhalifu pamoja na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Johari alieleza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kushughulikia changamoto zinazoukabili umoja huo ili kuuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.
Alisisitiza pia umuhimu wa kuimarisha mifumo ya kidijitali na ushirikiano baina ya taasisi hizo, akisema hatua hiyo itasaidia kuboresha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya uhalifu nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali (DPP), Sylvester Mwakitalu, alisema ushirikiano baina ya taasisi zinazohusika na usimamizi na utekelezaji wa sheria na haki jinai umeongeza ufanisi katika utendaji kazi na kusaidia kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Mwakitalu alisema taasisi hizo zina majukumu yanayotegemeana, hivyo ni muhimu kufanya kazi kwa pamoja badala ya kila moja kutekeleza majukumu yake bila kushirikiana na nyingine.
Akizungumza katika mkutano huo uliowakutanisha viongozi wa taasisi hizo kutoka ngazi za mikoa na wilaya, Mwakitalu alisema ushirikiano huo ulianzishwa mwaka 2021 ukiwa na taasisi tatu, lakini kwa sasa umepanuka na kujumuisha Idara ya Uhamiaji pamoja na Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA).
“Tusiposhirikiana, haki za watu zinachelewa na wakati mwingine zinapotea. Ndiyo maana kwa dhati kabisa tuliamua kushirikiana kuanzia ngazi ya Taifa mpaka wilayani,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Mashtaka wa Serikali ya Zanzibar, Mgeni Jailani Jecha, alisema mkutano huo ni muhimu kwa mstakabali wa nchi kwa kuwa unatoa fursa ya kujadili mikakati ya kuimarisha usalama, nidhamu na utekelezaji wa majukumu ya kitaifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna wa Polisi Ramadhani Kingai, akizungumza kwa niaba ya wenzake kutoka TAKUKURU na Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, alisema mchango wa taasisi hizo umekuwa muhimu katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na amani na utulivu.
Alisema hali nzuri ya usalama iliyopo nchini imewezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu, hivyo ni muhimu kwa taasisi hizo kuendelea kushirikiana katika kulinda usalama na ustawi wa Taifa.



