ZANZIBAR imeendelea kujitokeza kama moja ya vivutio muhimu vya utalii nchini, safari hii ikipokea ugeni wa Miss World 2026, Joheirry Molla aliyewasili visiwani humo Novemba 19, 2026, akiwa ameambatana na warembo kutoka mabara sita.
Ujio huo si ziara ya kawaida ya urembo bali ni sehemu ya juhudi za kuitangaza Tanzania kupitia fursa zinazotokana na mashindano ya kimataifa ya Miss World. Mapokezi ya Molla na ujumbe wake yanaipa Zanzibar nafasi ya kuonesha utajiri wake wa utamaduni, historia na mandhari ya kuvutia, ambavyo vimekuwa sehemu ya vivutio vinavyowavutia watalii kutoka mataifa mbalimbali.
Katika ziara hiyo, Molla anatarajiwa kutembelea hoteli na maeneo mbalimbali ya utalii yatakayohusishwa na historia ya mashindano ya Miss World 2027, yanayotarajiwa kufanyika nchini Tanzania. “Nimevutiwa sana na Tanzania hasa utamaduni wa Tanzania pamoja na mapokezi mazuri ninahamu ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Zanzibar ili kujionea uzuri wa visiwa hivyo”alisema Molla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Emmanuel Ishengoma, amesema Serikali inalenga kutumia fursa ya kuandaa mashindano ya Miss World kujinufaisha kiuchumi, kukuza sekta za utalii na utamaduni pamoja na kuitangaza Tanzania kimataifa. SOMA: Namna ya kujali ngozi kwa urembo wa asili
Kwa mantiki hiyo, maandalizi ya mashindano hayo yanatoa fursa ya kuitangaza Tanzania kwa hadhira ya kimataifa na kuonesha uwezo wake wa kutumia matukio makubwa kukuza sekta mbalimbali. Hata hivyo, manufaa ya fursa hiyo yanategemea namna nchi itakavyotumia ziara na mashindano hayo kuendeleza utalii, kuongeza thamani ya utamaduni na kuchochea shughuli za kiuchumi.




