MOROGORO: MFUMO wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma kwa njia ya kielektroniki (NeST) umeokoa zaidi ya Sh bilioni 13.3 kutokana na kupunguza matumizi ya karatasi, gharama za uendeshaji na kurahisisha michakato ya ununuzi wa umma nchini tangu ulipoanza kutumika.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ,Dk Mussa Ali Mussa amesema hayo kwenye hotuba yake ya ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na mfumo wa NeST kwa wajumbe wa Bodi za Zabuni kutoka taasisi nunuzi ambayo yaluandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Hotuba hiyo imesomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu wa Mkoa huo, Sebastian Masanja.
Amesema mfumo huo umewezesha makundi maalumu yakiwamo wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu kupata zabuni zenye thamani ya takribani Sh bilioni 90 tangu ulipoanzishwa Julai 2023 hadi Novemba 2026 hapa nchini.
Amesema matumizi ya mfumo huo yameleta mageuzi makubwa katika sekta ya ununuzi wa umma kwa kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi, na kutoa fursa za kiushindani kwa wazabuni wenye sifa na vigezo vinavyotakiwa.
Dk Mussa amesema pia umesaidia kupunguza muda na gharama za michakato ya zabuni, kurahisisha maandalizi ya vikao vya Bodi za Zabuni, uwasilishaji wa nyaraka na upatikanaji wa taarifa zinazohitajika katika kufanya maamuzi.
Amesema NeST pia umeimarisha uwajibikaji kwa kuwa kila mtumiaji huacha alama za kielektroniki zinazowezesha kufuatilia hatua mbalimbali za michakato ya ununuzi na hivyo kupunguza mianya ya ubadhirifu na kutupiana lawama.
Akizungumzia umuhimu wa sekta ya ununuzi wa umma, alisema zaidi ya asilimia 70 ya bajeti ya Serikali hutumika katika ununuzi wa umma, huku asilimia 100 ya fedha za maendeleo zikipitia katika sekta hiyo.
Dk Mussa amesema kuwa matumizi ya teknolojia pekee hayawezi kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana bila watendaji kuzingatia uadilifu, uzalendo na weledi katika kutekeleza majukumu yao.
“Uadilifu ni kutenda kwa usahihi hata pale ambapo hakuna mtu anayefuatilia, huku uzalendo ukiwa ni kupenda nchi na watu wake kwa vitendo” amesema Dk Mussa katika hotuba hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Utafiti, Maendeleo na Ubunifu wa PPRA, Mhandisi Masunya Nashon, amesema mamlaka hiyo inalenga kuhakikisha washiriki wa mafunzo wanafahamu matakwa ya Serikali katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Naye Meneja wa Kuendeleza Uwezo na Huduma za Ushauri wa PPRA, Gilbert Kamnde, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuhakikisha watumiaji wa mfumo wa NeST na wote wanaojihusisha na masuala ya ununuzi na ugavi wanapata elimu sahihi ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Benedict Bugambi na Lenatha Miruko, kwa nyakati tofauti wamesema mafunzo hayo yatawaongezea ujuzi na kuwasaidia kwenda na kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika utekelezaji wa shughuli za ununuzi wa umma.




