SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imeponea mzigo wa kuwarejeshea wakazi na wafanyabiashara kodi na ushuru iliyokusanya kwa kipindi cha mwaka mzima chini ya Sheria ya Fedha ambayo Mahakama Kuu imebaini kuwa ilitungwa kinyume na Katiba.


Katika hukumu iliyotolewa Novemba 20, Mahakama Kuu mjini Mombasa ilikiri kuwa serikali ya kaunti na Bunge la Kaunti zilikiuka wajibu wao wa kikatiba wa kuwashirikisha wananchi katika utungaji wa sheria.


Hata hivyo, mahakama ilisema kubatilisha ukusanyaji wa mapato ya mwaka mzima kungevuruga utoaji wa huduma za umma.


Mahakama ilikataa kubatilisha Sheria ya Fedha ya mwaka 2024 (Na. 6 ya 2024) wala kuamuru kurejeshwa kwa fedha zilizokusanywa, ikisema walalamishi walishindwa kuwataja wasafirishaji au wafanyabiashara waliolipa ushuru uliopingwa na kuwasilisha ushahidi wa malipo hayo.


“Kasoro niliyoibaini inahusu utaratibu uliofuatwa. Sijabaini kuwa ada yoyote mahususi ilitozwa nje ya mamlaka ya kaunti,” mahakama ilisema.


Sheria hiyo ilianza kutekelezwa Januari 1, 2025 na kutumika mwaka mzima.


Mahakama ilibainisha kuwa kaunti ilikuwa tayari imetumia mapato hayo kutoa huduma za umma, huku wafanyabiashara wakipata vibali, leseni na huduma nyingine badala ya malipo yao.


Mahakama pia iliwakosoa walalamishi kwa kusubiri hadi Aprili 2025 kuwasilisha kesi kupinga sheria ambayo tayari ilikuwa imeanza kutekelezwa, ikisema kuwa kufikia wakati huo wafanyabiashara wengi walikuwa tayari wamelipa.


Mashirika mbalimbali ya wafanyabiashara yaliwasilisha kesi hiyo Aprili 2025.


Walalamishi walidai kuwa serikali ya kaunti iliwanyima wakazi fursa ya kutosha kuchunguza na kuwasilisha maoni yao kuhusu Mswada wa Fedha kabla ya kupitishwa kuwa sheria.


Walisema kaunti ilichapisha tangazo la kuwaalika wananchi kuwasilisha maoni yao Septemba 23, 2024, na kuwapa siku mbili pekee, hadi Septemba 25, kuwasilisha mapendekezo yao.


Pia walipinga kikao kimoja cha kusikiliza maoni ya umma kilichofanyika katika Ukumbi wa Jamii wa Tononoka Novemba 14, 2024, wakisema mkutano huo wa saa mbili haukufanyika ipasavyo na haukuweza kuwakilisha kwa njia ya kutosha wakazi wa wadi zote 30 za kaunti.


Licha ya zoezi hilo kutofaulu, walisema Bunge la Kaunti liliidhinisha ripoti ya ushirikishwaji wa umma na kupitisha Mswada huo wakati wa kikao maalumu kilichofanyika Desemba 23, 2024.


Walalamishi pia walipinga madai kuwa Sheria hiyo ilidumisha viwango vya awali vya ushuru, wakitaja ongezeko la gharama za vibali vya biashara.


Walitaja ongezeko la ushuru kwa hadi karibu Sh35,000 kwa baadhi ya biashara.


Katibu wa Kaunti, Jeizan Faruk, alipinga kesi hiyo akisisitiza kuwa serikali ya kaunti ilizingatia matakwa ya kisheria kuhusu ushirikishwaji wa umma.


Hata hivyo, mahakama ilibaini kuwa washtakiwa walishindwa kuthibitisha kuwa wakazi walipewa fursa ya kutosha kushiriki katika mchakato huo.


Mahakama ilikataa hoja kuwa vurugu zilizotokea Tononoka zilihalalisha kusitishwa kwa zoezi hilo, ikisema wakazi ambao hawakuhudhuria mkutano huo hawakupaswa kunyimwa haki yao ya kutoa maoni.


Jaji alionya kuwa michakato ya baadaye ya ushirikishwaji wa umma lazima iwe ya maana na yenye kuzingatia maoni ya wananchi, akiongeza kuwa kikao cha kusikiliza maoni kinapovunjika au kushindwa kufanyika, Bunge la Kaunti lazima liitishe kikao kingine.