MBEYA: Serikali kupitia Mradi wa Kuinua Elimu ya Sekondari (SEQUIP) imeendelea kutoa fursa kwa wasichana waliokatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali za maisha kurejea shuleni na kuendeleza ndoto zao za elimu.
Miongoni mwa wanufaika wa fursa hiyo ni Neema Andrea Usia, ambaye safari yake ya elimu ilikatizwa akiwa kidato cha pili, lakini kupitia fursa ya kurejea shuleni ameweza kuendelea na masomo hadi kujiunga na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Neema anasema alihitimu elimu ya msingi mwaka 2013 kwa kupata daraja B na kuchaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Luiwa, iliyopo Wilaya ya Mbarali. Hata hivyo, hakufanikiwa kuendelea na masomo baada ya kukutana na changamoto mbalimbali za kifamilia, ikiwemo hali ngumu ya kiuchumi, kufiwa na mama yake pamoja na kupata ujauzito akiwa kidato cha pili.
Changamoto hizo zilimlazimu kuondoka shuleni na kurejea nyumbani, ambako alikabiliwa na jukumu la kumlea mtoto bila msaada wa baba wa mtoto.
Licha ya hali hiyo, Neema hakukata tamaa ya kutimiza ndoto yake ya kupata elimu. Alijitahidi kujitegemea kwa kuanzisha biashara ndogo ya genge iliyomsaidia kupata kipato cha kukidhi mahitaji yake na mtoto.
Mwaka 2022, akiwa anaendelea na shughuli zake, alipata taarifa kutoka kwa mwalimu wake wa zamani kuhusu fursa ya Serikali kupitia SEQUIP ya kuwawezesha wasichana waliokatisha masomo kurejea katika mfumo wa elimu.
Taarifa hiyo ilimpa matumaini mapya na kumfanya aamue kutumia nafasi hiyo kuanza upya safari yake ya elimu.
Kupitia fursa hiyo, alijiunga na kituo cha masomo katika Shule ya Sekondari Iyai, Wilaya ya Mbarali, kabla ya kuhamishiwa Shule ya Sekondari Kiwira, Wilaya ya Rungwe, baada ya kituo cha awali kufungwa.
Akiwa Kiwira, Neema alisoma hatua ya kwanza na kufanya mtihani wa QT, alioufanya vizuri na kupata nafasi ya kuendelea na masomo ya kidato cha tatu na cha nne.
Baadaye alifanya mtihani wa kidato cha nne katika Kituo cha Rubala na kupata Division II, matokeo yaliyomwezesha kuendelea na masomo ya kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Mwakaleli.
Awali, alichaguliwa tahasusi ya HGL, lakini kutokana na shauku yake ya kusoma masomo ya sayansi, aliamua kubadilisha na kujiunga na tahasusi ya CBG.
Neema anasema alipata ushirikiano kutoka kwa walimu na uongozi wa shule hiyo, jambo lililomsaidia kuendelea na masomo licha ya changamoto alizokuwa amepitia.
Juhudi zake zilizaa matunda baada ya kufanya mtihani wa kidato cha sita na kupata Division I ya pointi nane, matokeo yaliyomfungulia mlango wa kuendelea na elimu ya juu.
Hatimaye, alichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), ambako anasomea Shahada ya Sayansi katika Sayansi na Teknolojia ya Chakula (Bachelor of Science in Food Science and Technology).
Kwa sasa, Neema ameanza masomo yake chuoni hapo, hatua inayotimiza sehemu muhimu ya ndoto yake ya kupata elimu ya juu, ambayo kwa muda mrefu ilionekana kuwa ngumu kuifikia.
Akizungumzia fursa hiyo, Neema ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka utaratibu unaowawezesha wasichana waliokatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali kurejea shuleni na kuendeleza elimu yao.
Amesema fursa hiyo imeleta mabadiliko makubwa katika maisha yake na kutoa nafasi kwa wasichana wengine wenye ndoto za elimu lakini walilazimika kuacha shule kutokana na mazingira mbalimbali.
Anaamini kuwa wasichana wengi wanaopitia changamoto zinazofanana na alizokutana nazo wanahitaji kupewa nafasi nyingine ya kuendelea na masomo ili waweze kutimiza malengo yao.
Safari ya Neema, kutoka kukatisha masomo akiwa kidato cha pili hadi kujiunga na chuo kikuu, inaonesha umuhimu wa kuwapa wasichana nafasi ya pili katika elimu na namna fursa zinazotolewa kupitia Mradi wa SEQUIP zinavyoweza kuwasaidia kurejea katika mfumo wa elimu na kuendeleza ndoto zao.




