MWANZA:MRADI wa Dhahabu wa Nyanzaga uliopo Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza, unatarajia kumimina dhahabu ya kwanza Januari 2027 baada ya kukamilisha miaka 17 ya utafiti na ujenzi.
Mradi huo unaoendeshwa na Sotta Mining Corporation Limited, ubia kati ya kampuni ya Perseus Mining inayomiliki asilimia 80 na Serikali ya Tanzania yenye asilimia 20, umeshiriki katika Mkutano wa Saba wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026) ukiwa katika hatua za mwisho za maandalizi ya kuanza uzalishaji.
Safari ya mradi huo ilianza kwa utafiti katika ukanda wa dhahabu wa Ziwa Victoria, ikifuatiwa na shughuli za uchorongaji, tafiti, upatikanaji wa vibali na majadiliano na Serikali.
Mwaka 2024, Perseus Mining ilinunua mradi huo na kufanya uamuzi wa mwisho wa uwekezaji Aprili 2025.
Tangu wakati huo, mradi umeunganishwa na gridi ya taifa, umeanza kupata maji kutoka Ziwa Victoria, umekabidhi nyumba kwa familia zilizopisha eneo la mradi na unaendelea kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji dhahabu.
Kati ya Julai 2024 na Machi 2026, Nyanzaga ilichangia thamani ya kiuchumi ya moja kwa moja ya Sh bilioni 457.7 nchini, ikiwamo Sh bilioni 371.6 zilizolipwa kwa wazabuni wa ndani na Sh bilioni 60.7 zilizolipwa Serikalini.
Aidha, zaidi ya watu 3,600 wanafanya kazi katika eneo la mradi huo, wakiwamo wafanyakazi 281 wa moja kwa moja, wengi wao wakiwa Watanzania.
Katika upande wa huduma za kijamii, mradi umetoa fursa 202 za mafunzo, kujenga miundombinu ya maji kwa jamii, shule mbadala ya msingi na zahanati mpya.
Akizungumza katika Kikao cha Saba cha Mjadala kuhusu Uongezaji Thamani Madini jijini Dar es Salaam, Meneja Mkuu wa Nchi wa mradi huo, Isaac Lupokela, alisema ushiriki wao katika TMIC 2026 unaakisi hatua muhimu ya kujiandaa kuingia rasmi katika uzalishaji.
“Nyanzaga imejengwa kwa miaka 17. Tunapoelekea kumimina dhahabu ya kwanza mwezi Januari 2027, tunashiriki TMIC kama mchezaji mpya hai katika sekta. Dhahabu ya kwanza itaonyesha kwamba madini ya Tanzania bado yana tija na faida kwa taifa,” alisema Lupokela.
Nyanzaga unatarajiwa kuwa mgodi wa nne wa Perseus Mining barani Afrika na kuzalisha wastani wa zaidi ya wakia 200,000 za dhahabu kwa mwaka kuanzia mwaka wa fedha 2028 hadi 2035.




