WANASIASA nchini wameanza kutumia mbinu za kipekee kuwavutia wapigakura, huku baadhi ya zawadi wanazotoa zikizua mjadala kuhusu maadili na kampeni za mapema.
Ikiwa imesalia chini ya miezi tisa kabla ya uchaguzi huo, wanasiasa hao wanatoa fedha taslimu, vyakula, fulana na kofia zenye majina yao hadi zawadi zisizo za kawaida kama chupi, magodoro na sare za shule, katika harakati zao za kujijenga kisiasa.
Ingawa kutoa zawadi kwa wapiga kura si jambo geni nchini, baadhi ya wanasiasa wamevuka mipaka ya kawaida kwa kutoa bidhaa ambazo hazikutarajiwa kuwa sehemu ya kampeni za kisiasa.
Tukio la hivi punde lilitokea Novemba 23, wakati mgombeaji wa ugavana wa Kaunti ya Kisii, Kevin Nyamari, alipogawa chupi zenye chapa yake kwa wanawake, hatua iliyozua gumzo kwenye mitandao ya kijamii.
Bw Nyamari alitetea hatua hiyo akisema, ilikuwa njia ya kuunga mkono utu na heshima ya wanawake.
“Kumpa mtu chupi kunaweza kuonekana kama jambo dogo, lakini hakuna mchango mdogo linapojiri suala la utu. Kujiamini kunakotokana na hilo ni kubwa,” alisema.
Aliongeza kuwa kujitolea kwake kusaidia watu walio katika mazingira magumu, hasa wasichana na wanawake kumechochewa na huruma na wajibu wa kijamii.
Hata hivyo, hatua hiyo ilikosolewa na baadhi ya Wakenya, ambao walitilia shaka ufaafu wa zawadi hizo kwa mwanasiasa anayetarajia kuwania kiti cha ugavana.
Mtaalamu wa utawala bora na mwanasiasa, Dkt Peter Mbae, alisema viongozi wanapaswa kuheshimu mipaka ya maadili na badala yake kutoa msaada wenye manufaa ya kudumu.
“Wanasiasa wanapaswa kuheshimu mipaka ya maadili na kutoa msaada wa vitendo au kuwawezesha wananchi kiuchumi badala ya kutoa bidhaa za nguo za ndani,” alisema.
Profesa Tom Nyamache wa Chuo Kikuu cha Turkana, pia alisema wanawake wanahitaji mipango yenye manufaa ya muda mrefu badala ya chupi.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi walimtetea Bw Nyamari, wakisema kutoa zawadi hizo ni njia bunifu ya kuwafikia wapigakura.
Bi Mary Nyanchera, mkazi wa Kisii, alisema hatua hiyo ililenga kuonyesha upendo na kuleta mabadiliko, hata kama mchango huo ulikuwa mdogo.
Miezi michache iliyopita, Mbunge wa Ndia, George Kariuki, pia alizua mjadala baada ya kuwagawia wanafunzi sare za shule zilizokuwa na jina lake.
Mbunge huyo alisema sare hizo zilinunuliwa kwa pesa zake binafsi baada ya kuguswa na hali ya wanafunzi waliokuwa wamevaa nguo zilizochakaa.
Alitetea uamuzi wa kuweka jina lake kwenye sare hizo, akisema hata mashirika ya kimataifa huweka majina yao kwenye misaada wanayotoa.
Hata hivyo, wakosoaji walisema hatua hiyo ilikuwa na sura ya kampeni za kisiasa.
Mjadala huu unaibua kumbukumbu za uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua, ambapo wanasiasa waligawa mitungi ya gesi iliyopakwa rangi ya zambarau, viatu, magodoro na zawadi nyinginezo zenye chapa zao.
Maafisa wakuu wa serikali pia walimiminika eneo hilo, huku miradi mbalimbali ya maendeleo ikitekelezwa kabla ya uchaguzi huo.
Hata hivyo, mgombeaji wa UDA alishindwa na Sammy Kamau Ngotho wa chama cha DCP.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na wakili, Steve Kabita alisema Wakenya wanapaswa kutarajia mbinu zaidi zisizo za kawaida uchaguzi unapokaribia.
“Wanasiasa wanajua kuwa hakuna umaarufu mbaya. Tarajieni mbinu nyingine za kushangaza kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka ujao. Watatumia kila kitu kinachoweza kuwapa manufaa ya kisiasa,” alisema.
Huku hayo yakijiri, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesema zawadi zenye chapa za wanasiasa si haramu, lakini imewaonya viongozi dhidi ya kuanzisha kampeni kabla ya wakati.
Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, alisema kipindi rasmi cha kampeni kitaanza Mei 29, 2027.
“Shughuli rasmi za kampeni zitaanza Mei 29, 2027. Kushiriki kabla ya kipindi rasmi cha kampeni ni kinyume cha sheria,” alisema.
Katika warsha ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) mjini Mombasa, Profesa Patrick Lumumba pia alikosoa mikutano ya kisiasa inayoendelea nchini, akisema viongozi tayari wameanza kampeni kinyume na sheria.
Mkurugenzi wa EACC anayesimamia maadili na uongozi, Pascal Mweu, naye alionya maafisa wa umma dhidi ya kujihusisha na kampeni za mapema, akisema hatua hiyo inaweza kukiuka Sheria ya Migongano ya Maslahi.
Alisema watakaopatikana na hatia watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kushtakiwa mahakamani.




