RAIS William Ruto alianza kusambaza bonasi ya Sh1.2 bilioni kwa wakulima wa miwa katika eneo la Magharibi mwa Kenya jana, huku akiahidi kuongeza maradufu malipo hayo mwakani ili kuimarisha kilimo cha miwa nchini.


Jana, Rais alikabidhi hundi za bonasi za Sh195 milioni kwa wakulima wa miwa wa kiwanda cha sukari cha Nzoia, huku akitangaza kuwa wenzao wanaosambaza mazao yao katika kiwanda cha Mumias watapokea malipo yao wiki ijayo. Wakulima wa Chemelil, Muhoroni, Miwani na Sony pia wanatarajiwa kunufaika na bonasi hizo.


Akizungumza katika uwanja wa kiwanda cha Nzoia Sugar, eneobunge la Kanduyi, Kaunti ya Bungoma, katika siku ya nne ya ziara yake Magharibi, Rais alisema malipo hayo ni ishara ya kutimizwa kwa ahadi yake ya kufufua sekta ya sukari na kilimo cha miwa.


Alisema kukodishwa kwa kiwanda hicho kwa kampuni ya Rai Group kumebadilisha shughuli zake na kukirejesha katika hali ya kupata faida baada ya kukaribia kusambaratika miaka mitatu iliyopita.


“Miaka minne iliyopita tuliposimama katika uwanja huu na kuahidi kufufua kiwanda hiki, kilikuwa miongoni mwa viwanda visivyo na ufanisi zaidi. Leo wakulima wanalipwa ndani ya wiki moja baada ya kuwasilisha miwa, huku wafanyakazi wakipokea mishahara yao kwa wakati kila mwisho wa mwezi. Hii ni siku ya kihistoria kwa Nzoia Sugar,” akasema.


Rais alisisitiza kuwa kiwanda hicho na shamba lake kuu la miwa bado ni mali ya wananchi wa Bungoma, akipuuza madai ya upinzani kwamba serikali imekabidhi umiliki wake kwa mwekezaji.


Aliahidi kuwa bonasi za wakulima zitaongezwa maradufu mwaka ujao iwapo kiwanda hicho kitaendelea kuimarika kifedha na kuongeza uzalishaji.


Mkurugenzi Mkuu wa Nzoia Sugar Tejveer Rai, alisema kampuni hiyo imekarabati mashine na kuboresha ufanisi wa uzalishaji tangu ilipochukua usimamizi wa kiwanda hicho.


Alisema awali tani 17 hadi 21 za miwa zilihitajika kuzalisha tani moja ya sukari, lakini sasa tani 11 pekee zinatosha.


Aliongeza kuwa miwa hupimwa kwa mizani ya kidijitali na wakulima hulipwa ndani ya siku saba baada ya kuwasilisha mazao yao.


Bw Rai alisema kampuni hiyo imewahifadhi wafanyakazi 923, ambao hulipwa mishahara yao kwa wakati. Alifichua kuwa imelipa Sh1.6 bilioni kwa wafanyakazi mwaka huu, Sh150 milioni kwa wakataji wa miwa na Sh688 milioni kwa serikali kupitia ushuru, VAT na ada mbalimbali.


Aidha, imelipa Sh739 milioni kama ada ya upangishaji na makubaliano ya kuendesha kiwanda hicho, huku uwekezaji wa Sh5.7 bilioni ukiendelea kuboresha mashine na miundomsingi.


Sehemu kubwa ya uwekezaji huo itaelekezwa katika kuweka mfumo wa unyunyiziaji maji kwenye ekari 3,600 za shamba kuu la kiwanda, alisema.


Alisema bei ya miwa imedumishwa katika Sh5,500 kwa tani, huku mbolea ya ruzuku ikiuzwa kwa Sh2,000 kwa gunia ikilinganishwa na Sh7,500 awali, hatua inayopunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima.


Mkuu wa Mawasiliano wa Kiwanda cha Sukari cha Rai George Muruli, alisema wakulima 13,949 waliokuwa na mikataba na Nzoia na kuwasilisha miwa kati ya Januari na Septemba wametambuliwa kuwa wanastahili bonasi.


Gavana wa Bungoma, Ken Lusaka alisema kiwanda hicho kilikuwa katika hali mbaya kabla ya kufufuliwa, akiwahimiza wakulima kutumia fursa zilizopo kuimarisha kilimo cha miwa.


Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alisema serikali imetimiza ahadi zake na kwamba viongozi hawataruhusu kiwanda hicho kurejea katika hali ya kushindwa iliyokidhoofisha hapo awali.


Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi aliitaka jamii ya Mulembe kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027, huku Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya akisema kufufuliwa kwa sekta ya miwa na sukari nchini kumepunguza haja ya kuagiza sukari kutoka nje.


Rais Ruto alihitimisha ziara yake ya siku nne Magharibi jana, lakini anatarajiwa kurejea Novemba 28 kwa ziara nyingine ya siku nne.


Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang'ula alisema serikali imetimiza ahadi zake na kwamba viongozi hawataruhusu kiwanda hicho kutumiwa tena kama uwanja wa kushindwa kwa uongozi.


Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi naye aliitaka jamii ya Mulembe kumuunga mkono Rais Ruto katika uchaguzi wa 2027, huku Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya akisema kufufuliwa kwa kilimo cha miwa na sukari nchini kumepunguza mahitaji ya kuagiza sukari kutoka nje.


Rais Ruto alihitimisha ziara yake ya siku nne Magharibi Jumatatu, lakini anatarajiwa kurejea Novemba 28 kwa ziara nyingine ya siku nne.