KIONGOZI wa Linda Mwananchi Movement (LMM) Edwin Sifuna ameanzisha harakati za kutafuta ufadhili wa kampeni zake za urais za 2027 nchini Amerika, huku akiwahimiza Wakenya wanaoishi ughaibuni kuchangia azma yake ya kuingia Ikulu.


Barua zilizowasilishwa katika Idara ya Haki, Amerika zinaonyesha kuwa Mkenya anayeishi New Jersey, Dkt Gilbert Shanga, aliomba Oktoba 28 kuratibu ziara ya Seneta huyo wa Nairobi.


Dkt Shanga alipewa jukumu la kufanikisha mikutano ya Bw Sifuna na Wakenya wanaoishi Amerika Kaskazini pamoja na kuratibu shughuli za kuchangisha fedha.


Bw Sifuna na ujumbe wa wanasiasa wanaounga mkono azma yake waliwasili Amerika mnamo Novemba 20 kwa ziara itakayokamilika Disemba 7 kwa chakula cha jioni Silicon Valley.


Katika mkutano na Bw Sifuna, Mkenya anayeishi North Carolina, George Njue, aliahidi kuhamasisha wananchi wanaoishi ughaibuni kuchangisha Sh100 milioni kwa kampeni zake.


Bw Njue, ambaye alisema aliendesha gari kwa saa tisa kuhudhuria mkutano huo, alihimiza Wakenya Amerika kujiunga na juhudi za kifedha za LMM.


“Hamna Wakenya wengi ughaibuni kama ya Amerika. Tuna pesa zote zinazohitajika na Linda Mwananchi kumfanya Sifuna kuwa rais,” alisema.


Alisema Wakenya ughaibuni wanatarajia watanufaika kiuchumi kupitia miradi ya maendeleo iwapo Bw Sifuna atashinda urais.


Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga, ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Sifuna, alisema Bw Njue ameahidi kutoa fedha hizo kabla ujumbe huo haujaondoka Amerika.


Alifichua kuwa Bw Njue pia amelipia makao makuu ya LMM nchini Amerika kwa mkataba wa mwaka mmoja katika mji wa Hackettstown.


Ziara hiyo inajiri huku viongozi wanaounga mkono serikali wakitilia shaka uwezo wa Bw Sifuna kugharamia kampeni za urais na kujenga mtandao wa kisiasa nchini kote.


Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi aliwahi kuhoji uwezo wa mwanasiasa huyo kushindana na vyama vilivyojijenga kitaifa.


Hata hivyo, Bw Sifuna ameendelea kutumia ziara hiyo kueleza sera zake, akiahidi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini, kupambana na ufisadi na kupunguza deni la taifa.


“Ufisadi unarudisha nyuma maendeleo ya nchi yetu. Hakuna uwazi, uwajibikaji wala maendeleo,” akasema katika mkutano na umma Pennsylvania.


Pia alikosoa serikali kwa kukataa kuweka wazi mikataba ya miradi mikubwa, akisema hali hiyo inazua mashaka kuhusu matumizi ya fedha za umma.


“Unapoona Rais Ruto hataki kufichua mikataba ya miradi muhimu, unajua kuna jambo lisilo sawa,” akasema.


Bw Sifuna pia aliwashambulia viongozi wa ODM waliomsukuma nje ya chama hicho, akishangaa kwa nini sasa wanajadiliana na Rais William Ruto kuhusu kugawana mamlaka kwa asilimia 50 kwa 50.


Alisisitiza kuwa msimamo wake wa kisiasa hautabadilika.


“Dhamira yangu tangu mwanzo kuhusu harakati hizi itabaki vilevile. Siwezi kushawishiwa wala kununuliwa,” akasema.


Katika ziara hiyo, Bw Sifuna ameandamana Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, Seneta wa Kisii Richard Onyonka, Bw Kalasinga na aliyekuwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza miongoni mwa viongozi wengine.


Bw Sifuna anatarajiwa pia kukutana na vijana wa Kenya nchini Amerika hasa kizazi cha Gen Z, ambacho anakichukulia kuwa nguzo muhimu ya uungwaji mkono wake.