WAHALIFU wa mtandaoni waliovamia na kudukua tovuti ya eCitizen wameanza kusambaza taarifa za kibinafsi za Wakenya zaidi ya 32 milioni katika mtandao fiche wa Dark Web, hatua inayowaweka mamilioni ya watu katika hatari ya utapeli.
Taarifa zilizopatikana na ‘Taifa Leo’ zinaonyesha kuwa wadukuzi hao waliiba rekodi za Wakenya 32,128,394, zikiwemo nakala za pasipoti, picha za pasipoti, nambari za vitambulisho vya kitaifa na tarehe za kuzaliwa.
Pia waliiba nambari za usajili za Mamlaka ya Ushuru Kenya (KRA), alama za vidole na nambari za kidijitali za afya zinazotumiwa na wanachama wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).Baadhi ya vitambulisho vya kikazi vya maafisa wa serikali pia vimesambazwa, hali inayozua hofu kuwa taarifa hizo zinaweza kutumiwa kuomba mikopo kwa majina yao au kuwatapeli.
Kikundi cha wahalifu wa mtandaoni kinachojulikana kama ByteToBreach kimekiri kuhusika na shambulizi hilo.Kikundi hicho kinadai kuwa kiliingia katika mifumo ya eCitizen na kuiba gigabaiti 600 za stakabadhi za kuthibitisha utambulisho wa wateja, gigabaiti 100 za taarifa za data na gigabaiti 40 za msimbo unaoendesha mifumo hiyo.Taarifa hizo ziligunduliwa Jumatatu na kampuni ya Amerika ya usalama wa mtandao, Vecert, inayofuatilia vitisho na shughuli za wahalifu katika mitandao fiche.
Wachunguzi wa kampuni hiyo walikagua rekodi za wahalifu hao na kubaini kuwa huenda walipata nafasi ya kuingia katika mitambo ya eCitizen Novemba 15 kwa kutumia udhaifu katika data inayotumika kuthibitisha utambulisho wa watumiaji.Dark Web ni sehemu fiche ya mtandao ambayo haipatikani kupitia injini za kawaida za kutafuta taarifa kama Google.
Mara nyingi hutumiwa na wahalifu kuuza taarifa zilizoibwa na huduma za udukuzi.Wataalamu wanaonya kuwa taarifa zilizoibwa zinaweza kutumiwa kutuma jumbe za ulaghai zinazodaiwa kutoka kwa serikali, benki au taasisi za afya ili kuwashawishi wananchi kutoa nywila na taarifa zao za siri.
Pia wahalifu wanaweza kutumia taarifa hizo kufungua akaunti za kifedha, kuomba mikopo kwa majina ya waathiriwa au kuwatishia kusambaza taarifa zao za faragha wasipolipa pesa.Hatari ni kubwa zaidi kwa sababu baadhi ya taarifa zilizoibwa ni za kibayometriki na afya.
Tofauti na nywila, alama za vidole haziwezi kubadilishwa kirahisi zinapovuja.Mtafiti wa usalama wa mtandao na Mkurugenzi Mkuu wa Cyber Guard Africa, Dkt Bright Gameli, alisema kuvamiwa kwa mfumo mmoja wa utambulisho kunaweza kuhatarisha huduma nyingine zinazotegemea mfumo huo.
“Ukiukaji wa usalama wa mfumo mkuu wa uthibitishaji wa utambulisho unaweza kutoa njia ya kuingia katika huduma nyingine zilizounganishwa nao, kutegemea jinsi mifumo hiyo ilivyoundwa na kiwango cha kupenya alichopata mvamizi,” alisema.
ByteToBreach ilitaja SHA, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Huduma ya Kitaifa ya Polisi miongoni mwa taasisi zinazoweza kuathiriwa kupitia mfumo huo.
Hata hivyo, hakuna ushahidi uliotolewa kuthibitisha kuwa mifumo ya taasisi hizo ilivamiwa.Mnamo Jumanne, Wizara ya Masuala ya Ndani ilikiri kupokea taarifa kuhusu kuingia bila idhini katika data za eCitizen na kusema timu za kiufundi na usalama zilikuwa zikichunguza ukubwa wa tukio hilo.
Wizara hiyo ilisema huduma za eCitizen zinaendelea kupatikana na wananchi wanaweza kuendelea kuzitumia kama kawaida.eCitizen ni jukwaa kuu la serikali linalowawezesha wananchi na wakazi kupata huduma zaidi ya 22,000, ikiwemo maombi ya pasipoti, leseni za udereva, vitambulisho, vyeti vya kuzaliwa na ndoa, vyeti vya tabia njema na usajili wa biashara.
Wizara haijatoa taarifa nyingine kuhusu matokeo ya uchunguzi huo. Mamlaka ya Mawasiliano nchini nayo ilielekeza maswali kuhusu tukio hilo kwa Shirika la Kitaifa la Usalama wa Mtandao, ambalo halikuwa limejibu maswali kufikia wakati wa kuchapishwa kwa habari hii.




