ZANZIBAR; Rais wa Zanziubar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi amesisitiza umuhimu wa sheria na kusema lazima iwe nyenzo ya maendeleo.
Dk Mwinyi alisema hayo jana wakati akifunga Mkutano wa 31 wa Mwaka wa Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki (EALS) uliofanyika Zanzibar.
Mkutano huo ulilenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda, utawala wa sheria, na matumizi ya teknolojia katika sekta ya sheria.
Akizungumza kwenye mkutano huo Dk Mwinyi alisisitiza umuhimu wa sheria katika maendeleo na kusema lazima sheria iwe nyenzo ya maendeleo.
“Sheria lazima iwe nyenzo ya maendeleo, si kikwazo. Ni wajibu wa wanasheria kulinda maslahi ya umma huku wakijenga mazingira rafiki ya uwekezaji,” alisema Dk Mwinyi.
Miongoni mwa mambo muhimu yaliyojitokeza kwenye mkutano huo ni makubaliano ya kuoanisha viwango vya mafunzo ya sheria Afrika Mashariki, uzinduzi wa mfumo wa kidijitali wa kurahisisha kesi za mipakani.
Mengine ni ahadi ya kuendeleza amani na utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi na pia kulitolewa tuzo ya heshima kwa Kampuni ya Showtime inayojishughulisha na uratibu wa matukio mbalimbali.
Tuzo hiyo iliyotolewa na EALS ilikuwa mahususi kutambua mchango wa Showtime kwa kuandaa mkutano huo mkubwa kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tuzo hii ni ushahidi wa uwezo wa kampuni za ndani za Zanzibar katika kuandaa matukio ya kimataifa ya hadhi ya juu.
“Mafanikio ya Showtime yanathibitisha kuwa Zanzibar ni kituo bora cha mikutano ya kimataifa, huku ikiiweka kampuni yetuy kama kinara katika sekta ya usimamizi wa matukio nchini Tanzania,” alisema Meneja Utawala wa Showtime, Neema Azaza baada ya kupokea tuzo hiyo.




