MBIO za kumtafuta mgombeaji atakayepeperusha bendera ya upinzani dhidi ya Rais William Ruto katika uchaguzi wa 2027 zinageuka vita vya kizazi, huku vijana wakitaka kuchukua nafasi ya viongozi waliotawala siasa kwa miongo kadhaa.
Kwa upande mmoja kuna Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu) na Babu Owino (Embakasi East), Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya na Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi.
Kwa upande mwingine kuna vigogo kama Kalonzo Musyoka wa Wiper Patriotic Front, Martha Karua wa People’s Liberation Party, Rigathi Gachagua wa Democracy for the Citizens Party (DCP) na Gavana wa Siaya James Orengo.
Pia kuna kundi la wataalamu na vigogo waliotoka nje ya siasa za kawaida za uchaguzi akiwemo aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, mfanyabiashara Jimi Wanjigi na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga.
Hali hii imefanya kambi ya upinzani kuwa na wagombea wengi hata kabla ya vyama kuanza rasmi mchakato wa kumteua mgombea mmoja wa urais.
Wachambuzi wanasema mjadala huu hauhusu umri pekee bali pia uzoefu wa kisiasa, mtandao wa kitaifa, uungwaji mkono wa maeneo, taaluma na uwezo wa kuvutia kizazi kipya cha wapigakura.
Mjadala huo umeonekana zaidi kupitia Seneta Sifuna ambaye amezindua The Equitable Party (TEP), inayotarajiwa kubadilishwa jina kuwa Linda Mwananchi Movement.
Kundi lake linasukuma tiketi inayowapa vijana nafasi kubwa, jambo linaloweza kuathiri mazungumzo ya kuunda muungano mpana wa upinzani.
Mbunge Babu Owino ameunga mkono azma hiyo akisema wakati umefika kwa vijana kuongoza.
“Vijana wa nchi hii huambiwa kila mara kuwa wao ni viongozi wa kesho. Sasa tunasema sisi ni viongozi wa leo na wakati wetu umefika,” alisema.
Hata hivyo, juhudi za vijana zinakabiliwa na ukweli kwamba vyama mbalimbali vya upinzani vina watu wanaotaka kuwania urais.
Seneta wa Kitui Enoch Wambua, mshirika wa Bw Musyoka, amesema anaendelea kumuunga mkono kiongozi huyo wa Wiper, ingawa hakufunga mlango wa ushirikiano na mrengo wa Sifuna.
“Ukiangalia kwa karibu, Linda Mwananchi ina watu kutoka vyama mbalimbali vya Muungano wa Upinzani. Timu hizi mbili zina lengo moja la kuhakikisha Rais Ruto anahudumu kwa muhula mmoja,” alisema.
Wakati huohuo, DCP ya Bw Gachagua imeibua mvutano na \Bw Nyoro.
Katibu Mkuu wa DCP John Methu alishambulia People’s Progressive Party (PPK), akiitaja kama wilibaro ndogo na kudai inalenga kuwachanganya wapigakura na kupunguza ushawishi wa DCP eneo la Mlima Kenya.
Mchambuzi wa siasa Javas Bigambo alisema Bw Nyoro ana haki ya kuwania urais.
“Mkenya yeyote anaweza kuwania nafasi yoyote,” alisema, akiongeza kuwa hakuna mwanasiasa au chama chenye haki ya siasa za eneo fulani.
Kwa upande wake, Dkt Matiang’i ametoa wito kwa wanasiasa wa upinzani kutotafsiri ushindani wao kama uadui.
“Kenya yetu ni demokrasia ya vyama vingi. Hata sisi Jubilee tunataka kiti hicho cha urais na wengine pia wanakitaka, lakini sisi si maadui,” alisema.
Bw Musyoka anajipanga kama mmoja wa vigogo wanaotaka kuunganisha makundi mbalimbali ya upinzani, huku Bw Gachagua akijikita zaidi katika kuunganisha Mlima Kenya chini ya DCP.
Bi Karua na Bw Orengo pia wameonyesha nia ya kuwania urais.
Wataalamu wanasema changamoto kubwa kwa vijana ni kubadilisha umaarufu na ushawishi wa mitandao ya kijamii kuwa mtandao wa mashinani unaohitajika katika uchaguzi wa urais.
Wakati huo huo, wagombea kama Dk Matiang’i, Bw Wanjigi na Bw Maraga wanajaribu kutumia rekodi zao za kitaaluma, utawala na utumishi wa umma kama njia mbadala ya siasa za kawaida.
Seneta wa Busia Okiya Omtatah naye anajikita katika mageuzi ya Katiba, utawala wa sheria na kupunguza mamlaka makubwa ya urais.
Mchambuzi Dismas Mokua anasema vita hivyo huenda visitatuliwe na umri wa wagombea bali uwezo wao wa kuunda muungano mpana unaovuka misingi ya kikabila, maeneo na vyama.
Vita vya ubabe kati ya vijana na wazee vyatikisa upinzani

This story was originally published by Taifa Leo.
Read the full story at Taifa LeoRelated stories
NewsIcoT yatakiwa kuongeza wataalamu ujenzi
MOROGORO: Serikali imesema itaendelea kuiimarisha Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), ili kutayarisha wataalamu wengi wenye ujuzi na umahiri watakaoweza kujiajiri na kuajirika kikamilifu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi, Aisha Amour amesema hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa mafundi sanifu na wataalamu wa kada mbalimbali…
NewsKampuni za Amerika zashinda zabuni kuchimba madini Kwale
MUUNGANO wa kampuni nne za Amerika umeshinda zabuni ya kuendeleza uchimbaji na uchakataji wa madini-adimu na niobium katika eneo la Mrima Hill, Kaunti ya Kwale, ambayo thamani yake inakadiriwa kuzidi Sh6 trilioni. Waziri wa Madini Hassan Joho alitangaza Frontier Minerals Consortium kuwa mshindi wa zabuni hiyo ya matrilioni ya fedha baada ya mchakato wa tathmini na ukaguzi wa ununuzi kukamilika. Ushindi huo unaipa Amerika nafasi muhimu katika sekta ya madini ya kimkakati nchini Kenya, huku ikiendelea kushindana na China kudhibiti upatikanaji na uchakataji wa madini hayo duniani. Kampuni zinazounda muungano wa ushirika huo ni Frontier Minerals LLC, Bunker Hill Mining Corp, ReElement Technologies na American Resources Corporation. Kila kampuni ina utaalamu wake katika uchimbaji, upatikanaji wa madini adimu, uchakataji na usafishaji wa madini muhimu kwa viwanda vya kisasa. Madini ya niobium katika Mrima Hill hutumika katika utengenezaji wa vifaa vya anga, huku madini-adimu yakihitajika katika magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki, mitambo ya upepo, silaha za kisasa na teknolojia ya Akili-Unde. Kampuni ya ReElement Technologies tayari imevutia uwekezaji wa serikali ya Amerika wa Dola milioni 25 (takriban Sh3.2 bilioni) uliotangazwa mnamo Julai 2026 kusaidia uwekaji wa vifaa katika kiwanda chake cha kusafisha madini adimu katika jimbo la Indiana, Amerika. Uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Amerika kupunguza kutegemea China, ambayo inaongoza duniani katika uchakataji wa madini hayo. Kampuni saba ziliorodheshwa kushindania mradi huo mnamo Julai, zikiwemo kampuni mbili za China, miungano miwili ya kampuni kutoka Amerika, muungano wa Australia na ubia wa Kenya na Uingereza. Kampuni za China baadaye zilijiondoa. Joho alisema kushinda zabuni hakumaanishi kampuni hiyo inaweza kuanza uchimbaji mara moja. Inapaswa kwanza kupata leseni zinazohitajika, kutekeleza masharti ya kisheria na kushirikisha jamii ya eneo hilo. Serikali pia imesisitiza kuwa madini hayo hayapaswi kuuzwa yakiwa ghafi, bali yaongezwe thamani nchini kupitia viwanda vya uchakataji. Muungano huo umesema utajenga uwezo wa kuchakata madini nchini, hatua inayoweza kuunda nafasi za ajira na kuongeza mapato. Kwa Kenya, mradi huo unatoa fursa ya kupanua uchumi ambao kwa muda mrefu umetegemea kilimo na utalii. Mapato ya sekta ya madini yalipungua kutoka Sh35 bilioni mwaka 2022 hadi Sh20.3 bilioni mwaka jana, hasa kutokana na kufungwa kwa migodi ya madini ya titanium katika Kaunti ya Kwale. Hata hivyo, mafanikio ya mradi wa Mrima Hill yatategemea uwekezaji, masharti ya leseni na namna jamii zitakavyoshirikishwa na kunufaika.
News2027: ACF warns of emerging political violence, urges restraint
…Forum urges Tinubu, governors to ensure fairness to opposition By Ibrahim Hassan-Wuyo The Arewa Consultative Forum (ACF) has raised concerns over emerging signs of political violence ahead of the 2027 general elections, urging political leaders, security agencies and Nigerians to embrace restraint and protect democratic values. The forum warned that provocative demonstrations, stone-throwing, abusive chants […]
NewsUtatu haki jinai watakiwa kuimarisha ushirikiano
ARUSHA: Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP) na Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za haki jinai, kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu na uzalendo ili kujenga imani ya wananchi kwa Serikali. Johari amesema hayo leo jijini Arusha…