MAURICIO Pochettino jana alianza rasmi majukumu yake kama kocha mpya wa Manchester United baada ya kuwasili katika uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo wa Carrington.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 54 alisema ni heshima na fursa kubwa kuiongoza timu hiyo maarufu ya Uingereza.
Pochettino aliondoka kambini mwa timu ya taifa ya Amerika Jumanne usiku baada ya kuiongoza kulaza Haiti 2-0 mchana huo, katika mechi ya marudiano ya robo-fainali ya Ligi ya Mataifa ya Amerika Kaskazini na Kati na Caribbean (CONCACAF Nations League).
Alisafiri moja kwa moja hadi Manchester kuanza maandalizi ya kuinoa United, ambayo imempa mkataba wa miaka miwili na nusu baada ya kumruhusu kukamilisha majukumu yake ya kimataifa.
“Nina hamu kubwa kuanza kazi hapa. Ni heshima na fursa ya kipekee kuwa katika klabu hii kubwa. Natarajia kuanza kazi vizuri,” alisema Pochettino baada ya kuwasili uga wa mazoezi wa Carrington, Jumatano.
Kibarua chake cha kwanza ni mechi ngumu dhidi ya Liverpool katika Ligi Kuu Uingereza (EPL) hapo Jumapili.
Baada ya hapo watasafiri kuelekea nchini Ureno wiki ijayo kucheza dhidi ya Sporting Lisbon katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Hana muda mwingi wa kuzoea mazingira yake mapya ya kazi kwani wachezaji waliokuwa wakiwajibikia timu zao za taifa walirejea kambini jana.
Pochettino aliagana na Amerika kwa ujumbe wa kuatua moyo, akisema anajivunia mafanikio ambayo walipata kipindi akiwa usukani.
“Nilipowasili nilitaka timu iamini kuwa inaweza kushindana na yoyote. Natumai imani hiyo sasa imeimarika, si kwa wachezaji pekee bali pia kila mmoja anayeiunga mkono timu hii [ya Amerika],” akasema.
Aliongeza kuwa kuondoka kwake katika kikosi cha Amerika haikuwa rahisi, lakini fursa ya kujiunga na Man United ilifanya kuwa vigumu kukataa ofa hiyo.
Uzoefu wake katika ukocha unajumuisha vipindi aliponoa klabu za Southampton, Tottenham na Chelsea nchini Uingereza, na PSG nchini Ufaransa.
Akiwa kocha wa Amerika alishinda mechi 23, kutoka sare mbili na kupoteza 12 kati ya 37 alizosimamia.
Pia aliongoza Amerika kufika hatua ya 16-bora ya Kombe la Dunia 2026 na fainali ya Kombe la CONCACAF Gold Cup 2025.




