Na Ramadhan Hassan, Dodoma
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imetaja vipaumbele vyake kwa mwaka 2025, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya shule, nyumba za walimu, mabwalo, majiko, matundu ya vyoo, maktaba, maabara za sayansi, na ofisi za walimu.
Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Dk. Erasmus Kipesha, amesema hayo leo Februari 25, 2025, wakati wa kueleza mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa waandishi wa habari jijini Dodoma.
Amesema TEA itaendelea kuwezesha sekta ya elimu kwa kuboresha mazingira ya kujifunza, ikiwemo upatikanaji wa vitabu vya kiada na ziada, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, vifaa vya TEHAMA, pamoja na vifaa maalum kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Aidha, Kipesha amesema kuna mpango maalum wa kuwawezesha wanafunzi wa kike kujiunga na michepuo ya sayansi katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu, ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika nyanja za teknolojia na uhandisi.
Vipaumbele vingine vya TEA ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa majengo ya vyuo vya elimu ya juu, upanuzi wa kumbi za mihadhara, na miradi ya kuongeza fursa za elimu nchini.



