Tanzania, Uturuki wajivunia diplomasia
WAKATI Jamhuri ya Uturuki ikiadhimisha miaka 101 ya taifa hilo, Tanzania inajivunia uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina yao katika maeneo ya biashara, miundombinu, utalii na elimu. Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk Pindi Chana amesema kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, mauzo ya Tanzania kwenda Uturuki yalikuwa wastani wa Dola milioni 15.9, wakati uagizaji kutoka …
The post Tanzania, Uturuki wajivunia diplomasia first appeared on HabariLeo.
WAKATI Jamhuri ya Uturuki ikiadhimisha miaka 101 ya taifa hilo, Tanzania inajivunia uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina yao katika maeneo ya biashara, miundombinu, utalii na elimu.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk Pindi Chana amesema kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, mauzo ya Tanzania kwenda Uturuki yalikuwa wastani wa Dola milioni 15.9, wakati uagizaji kutoka Uturuki ulikuwa wastani wa Dola milioni 242.1.
Akizungumza Oktoba 29, katika maadhimisho ya miaka 101 tangu kutangazwa kwa Jamhuri ya Uturuki yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Dk Chana amesema uwepo wa wawekezaji kutoka Uturuki nchini Tanzania, uanzishwaji wa miradi 106 iliyosajiliwa Tanzania Bara yenye thamani ya Dola milioni 414.23 na miradi 12 Zanzibar yenye thamani ya Dola milioni 96.4, kwa pamoja imezalisha ajira 6,800 vyote vinaonyesha uimara wa mashirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Katika hatua nyingine, Dk Chana amesema Tanzania inathamini ushirikiano uliopo kati yake na Uturuki katika sekta ya utalii, ulioimarishwa na kuanzishwa kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili ambapo imekuwa chachu katika kuchangia ongezeko kubwa la idadi ya watalii wa Kituruki wanaotembelea Tanzania, kutoka wageni 5,177 mwaka 2020 hadi 11,203 mwaka 2023.
Balozi wa Jamhuri ya Uturuki nchini Tanzania, Dk Mehmet Güllüoğlu, amesema kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan mazingira ya biashara na uwekezaji yameboreshwa hivyo kupelekea kuanzishwa kwa kampuni za Kituruki zaidi ya 200 nchini Tanzania.
SOMA: Dk Chana ahamasisha uwekezaji mazao ya misitu
Amesema maadhimisho hayo ni mwanzo mzuri wa kuyaboresha mahusiano kati ya Tanzania na Uturuki katika nyanja mbalimbali ikiwemo afya, elimu, miundombinu, utalii na biashara.
Uhusiano wa Kidiplomasia katika Tanzania na Uturuki ulianza Julai 5, 1963 na umekuwa na manufaa kwa pande zote.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe waheshimiwa mabalozi na makamishna wakuu, wakuu wa mashirika ya kimataifa, viongozi wa serikali na maofisa wa serikali.
The post Tanzania, Uturuki wajivunia diplomasia first appeared on HabariLeo.