WADAU mbalimbali wa sekta ya kilimo mkoani Tabora, wakiwemo maafisa kilimo, viongozi wa serikali na vyama vya msingi, wameanza rasmi utekelezaji wa mpango mkakati wa kuendeleza kilimo cha mazao ya biashara huku Lengo kuu likiwa ni kufungua fursa za masoko ya kimataifa na kuwakwamua wakulima kiuchumi, sambamba na kuinua sekta ya kilimo kwa ujumla.

Mazao yanayokusudiwa ni pamoja na dengu, alizeti, choroko na mbaazi.

Wakizungumza katika kikao kazi cha kuhamasisha kilimo cha mazao ya kimkakati kilichofanyika katika Wilaya ya Nzega, maafisa kilimo wilaya ya nzega wameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuondokana na kilimo cha mazoea na kuhamasisha wakulima kuelekea kwenye kilimo chenye tija na chenye mwelekeo wa soko.

Katika kikao hicho, ambacho kimewajumuisha viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi kutoka Wilaya ya Nzega, wadau wa kilimo, na wawakilishi kutoka serikalini, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ambaye ni Afisa Tarafa, amewahakikishia wakulima juu ya uwepo wa masoko ya uhakika, na kueleza kuwa serikali ipo tayari kuwasaidia wakulima kuhakikisha wanafanikiwa.

Mpango huo unatajwa kuwa ni sehemu ya jitihada za serikali na Wizara kuhakikisha kilimo bora cha biashara kwa ajili ya kuinua uchumi wa mkulima pamoja na kuwavutia wawekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya biashara.

Kwa upande wao, baadhi ya wakulima wa mazao ya jadi kama pamba na tumbaku wameeleza matarajio makubwa juu ya mpango huo, huku wakiiomba serikali kuhakikisha kuwa masoko hayo yanakuwa ya uhakika.