‘Taasisi za elimu zilizopatiwa umeme REA zafikia 18,597’

DODOMA: NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatoa kipaumbele katika…
The post ‘Taasisi za elimu zilizopatiwa umeme REA zafikia 18,597’ appeared first on HabariLeo.
DODOMA: NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatoa kipaumbele katika kufikisha umeme kwenye taasisi zinazotoa huduma kwa jamii zikiwemo Taasisi za Elimu.
Kapinga ameyasema hayo leo Februari 10 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Viti Maalum, Neema Rugangira aliyeuliza iwapo serikali haioni haja kupitia upya Mkataba wa REA kuhakikisha umeme unafikishwa Mashuleni ili shule ziunganishwe na huduma za TEHAMA.
“Hadi kufikia mwezi Januari, 2025 taasisi za elimu zilizopatiwa umeme kupitia REA ni 18,597. Serikali kupitia REA itaendela kupeleka umeme kwenye vituo vya huduma nchini kulingana na upatikanaji wa fedha,” amesema Kapinga.
“Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa COVID ambapo Serikali imepeleka umeme kwenye vituo vya afya 111. Upo mradi mwingine ambao unapeleka umeme kwenye pampu za maji takribani 411 na kwenye maeneo ya kilimo na maeneo ya migodi 605.”
Akijibu swali Mbunge wa Viti Maalum, Kabula Shitobela aliyeuliza ni lini Serikali itatoa ruzuku katika nishati safi ya kupikia ili kuwasaidia akina Mama wasifanyiwe ukatili na kuuwawa kutokana na imani potofu, Kapinga amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034.
Amesema kupitia mkakati huo, Serikali imeanza kutoa ruzuku ya asilimia 20 hadi 50 ya bei ya mitungi ya gesi ya LPG kwa watumiaji wa mwisho.
“Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kusambaza majiko banifu 200,000 pamoja na kusambaza umeme ili kuhamasisha matumizi ya majiko ya umeme,” amesema Kapinga.
SOMA: Wadau wajadili umeme nishati salama
Akijibu swali la Mbunge wa Mbulu Mjini, Issaay Zacharia aliyeuliza kutokana na mahitaji ya wananchi kuhitaji huduma ya umeme ni makubwa, Serikali haioni haja ya kuongeza idadi ya vitongoji, Mhe. Kapinga amesema Serikali inaona umuhimu wa jambo hilo ndio maana Serikali inaanza mradi mwingine wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 8000.
Akijibu swali la Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamomga aliyetaka kufahamu mkakati wa Serikali kutenga bajeti ya kutosha ili kuweza kurekebisha miundombinu ya wazalishaji binafsi ili iendane na standard za TANESCO, Kapinga amesema tayari uhakiki umeshafanyika ili kupata gharama halisi kwa ajili ya kufanya ukarabati kurekebisha miundombinu hiyo.
The post ‘Taasisi za elimu zilizopatiwa umeme REA zafikia 18,597’ appeared first on HabariLeo.