MVUTANO kati ya Rais William Ruto na Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya kuhusu kutenga vibanda katika Soko la Masinde Muliro, Kitale, ulichacha jana huku polisi wakitumwa kulinda usalama na wafanyabiashara wakilalamikia kupoteza mapato.
Maafisa wenye silaha kutoka Kikosi cha Kukabili Fujo (GSU) na Polisi wa Utawala (AP) walitumwa katikati ya mji wa Kitale, huku baadhi ya barabara zikifungwa na wafanyabiashara kufunga maduka yao kutokana na hofu ya ghasia.
Hali ya wasiwasi pia ilizuka katika makao makuu ya kaunti ya Trans Nzoia baada ya polisi kuvuruga mkutano wa maombi uliokuwa ukiendelea.
Gavana Natembeya amesema ataomba Seneti na mahakama kuingilia kati kutatua mzozo huo, akisisitiza kuwa suala hilo linahusu ugatuzi na mamlaka ya serikali ya kaunti.
“Nataka Seneti iingilie kati na kusaidia kutatua mzozo huu. Seneti iliundwa kuwa mtetezi wa ugatuzi, na sasa ni wakati wa Bunge hilo kuingilia kati,” alisema Natembeya wakati wa ibada ya kanisa Jumapili.
Soko hilo lenye thamani ya zaidi ya Sh800 milioni lilijengwa na serikali ya kaunti kwa usaidizi wa Benki ya Dunia. Hata hivyo, mchakato wa kugawa vibanda umesababisha mzozo kati ya viongozi wa kitaifa na wale wa kaunti.
Rais Ruto amepinga mchakato wa ugavi uliofanywa na serikali ya kaunti na kusema vibanda vilivyosalia vitagawiwa kwa njia ya bahati nasibu.
Bw Natembeya, kwa upande wake, amedai kuwa wafanyabiashara kutoka Uganda walipewa vibanda vingi ingawa madai yake hayajathibitishwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wafanyabiashara Kenya (KNCCI) katika kaunti hiyo, Titus Kilong’i, alizua maswali kuhusu mamlaka ya kamishina wa kaunti kuhusika katika ugavi wa vibanda.
“Je, kamishina wa kaunti ndiye aliyejenga soko hili kiasi cha kuingilia kati na kugawa vibanda? Baada ya kuvigawa, ndiye atakayekusanya mapato? Je, sheria inamruhusu kufanya hivyo?” aliuliza.
Bw Kilong’i alisema orodha za mgao ina utata, akidai kuwa jina la mtu mmoja lilionekana hadi mara nane katika orodha tofauti za masoko.
“Tunatakiwa kulipa ushuru, lakini kuna mkanganyiko na tunatishwa. Tutawezaje kuendelea kuishi?” akauliza.
Mkurugenzi mtendaji wa KNCCI, Antony Masika, alisema wafanyabiashara wameathirika tangu Alhamisi, huku baadhi yao wakikadiria hasara kutokana na biashara kuvurugwa.
Mfanyabiashara Belinda Nakhumicha alisema kufungwa kwa maduka na hali ya wasiwasi imewaathiri wafanyabiashara wanaotegemea mapato ya kila siku.
Hata hivyo, washirika wa Rais wameunga mkono miradi yake ya maendeleo katika eneo hilo.
Aliyekuwa Waziri wa Afya Susan Nakhumicha alisema wakazi wanafurahia hatua za serikali ya kitaifa kuhusu miradi ya maendeleo na kuingilia kati katika kutenga vibanda sokoni humo.
“Tunafurahia yale ambayo Rais ametufanyia, ikiwemo ziara yake katika kaunti wiki iliyopita. Sisi kama wakazi wa Trans Nzoia tunamshukuru sana,” akasema
Natembeya, Ruto wakabana koo shughuli zikikwama Kitale

This story was originally published by Taifa Leo.
Read the full story at Taifa LeoRelated stories
NewsIcoT yatakiwa kuongeza wataalamu ujenzi
MOROGORO: Serikali imesema itaendelea kuiimarisha Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT), ili kutayarisha wataalamu wengi wenye ujuzi na umahiri watakaoweza kujiajiri na kuajirika kikamilifu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi, Aisha Amour amesema hatua hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa mafundi sanifu na wataalamu wa kada mbalimbali…
NewsKampuni za Amerika zashinda zabuni kuchimba madini Kwale
MUUNGANO wa kampuni nne za Amerika umeshinda zabuni ya kuendeleza uchimbaji na uchakataji wa madini-adimu na niobium katika eneo la Mrima Hill, Kaunti ya Kwale, ambayo thamani yake inakadiriwa kuzidi Sh6 trilioni. Waziri wa Madini Hassan Joho alitangaza Frontier Minerals Consortium kuwa mshindi wa zabuni hiyo ya matrilioni ya fedha baada ya mchakato wa tathmini na ukaguzi wa ununuzi kukamilika. Ushindi huo unaipa Amerika nafasi muhimu katika sekta ya madini ya kimkakati nchini Kenya, huku ikiendelea kushindana na China kudhibiti upatikanaji na uchakataji wa madini hayo duniani. Kampuni zinazounda muungano wa ushirika huo ni Frontier Minerals LLC, Bunker Hill Mining Corp, ReElement Technologies na American Resources Corporation. Kila kampuni ina utaalamu wake katika uchimbaji, upatikanaji wa madini adimu, uchakataji na usafishaji wa madini muhimu kwa viwanda vya kisasa. Madini ya niobium katika Mrima Hill hutumika katika utengenezaji wa vifaa vya anga, huku madini-adimu yakihitajika katika magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki, mitambo ya upepo, silaha za kisasa na teknolojia ya Akili-Unde. Kampuni ya ReElement Technologies tayari imevutia uwekezaji wa serikali ya Amerika wa Dola milioni 25 (takriban Sh3.2 bilioni) uliotangazwa mnamo Julai 2026 kusaidia uwekaji wa vifaa katika kiwanda chake cha kusafisha madini adimu katika jimbo la Indiana, Amerika. Uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Amerika kupunguza kutegemea China, ambayo inaongoza duniani katika uchakataji wa madini hayo. Kampuni saba ziliorodheshwa kushindania mradi huo mnamo Julai, zikiwemo kampuni mbili za China, miungano miwili ya kampuni kutoka Amerika, muungano wa Australia na ubia wa Kenya na Uingereza. Kampuni za China baadaye zilijiondoa. Joho alisema kushinda zabuni hakumaanishi kampuni hiyo inaweza kuanza uchimbaji mara moja. Inapaswa kwanza kupata leseni zinazohitajika, kutekeleza masharti ya kisheria na kushirikisha jamii ya eneo hilo. Serikali pia imesisitiza kuwa madini hayo hayapaswi kuuzwa yakiwa ghafi, bali yaongezwe thamani nchini kupitia viwanda vya uchakataji. Muungano huo umesema utajenga uwezo wa kuchakata madini nchini, hatua inayoweza kuunda nafasi za ajira na kuongeza mapato. Kwa Kenya, mradi huo unatoa fursa ya kupanua uchumi ambao kwa muda mrefu umetegemea kilimo na utalii. Mapato ya sekta ya madini yalipungua kutoka Sh35 bilioni mwaka 2022 hadi Sh20.3 bilioni mwaka jana, hasa kutokana na kufungwa kwa migodi ya madini ya titanium katika Kaunti ya Kwale. Hata hivyo, mafanikio ya mradi wa Mrima Hill yatategemea uwekezaji, masharti ya leseni na namna jamii zitakavyoshirikishwa na kunufaika.
News2027: ACF warns of emerging political violence, urges restraint
…Forum urges Tinubu, governors to ensure fairness to opposition By Ibrahim Hassan-Wuyo The Arewa Consultative Forum (ACF) has raised concerns over emerging signs of political violence ahead of the 2027 general elections, urging political leaders, security agencies and Nigerians to embrace restraint and protect democratic values. The forum warned that provocative demonstrations, stone-throwing, abusive chants […]
NewsUtatu haki jinai watakiwa kuimarisha ushirikiano
ARUSHA: Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (DPP) na Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za haki jinai, kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uaminifu na uzalendo ili kujenga imani ya wananchi kwa Serikali. Johari amesema hayo leo jijini Arusha…