DAR ES SALAAM: RAIS wa Kamati ya Olimpic Tanzania (TOC), Anthony Mtaka, ametoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania (TAVA), Muharami Mchume, akieleza kuwa alikuwa kiongozi, mshauri na mwalimu wa uongozi aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya michezo nchini.

Mtaka amesema mwaka 2012, alipokuwa akiandaa kugombea nafasi ya Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), alimtafuta Muharami pamoja na Filbert Bayi na Suleiman Nyambui kwa ajili ya kupata ushauri, ambapo kila mmoja alikuwa mshauri wake katika eneo tofauti.

Amesema licha ya Muharami kuwa mbobezi zaidi katika mpira wa wavu, alikuwa mwalimu mahiri wa uongozi na siasa za michezo, na aliendelea kuwa baba na mshauri wake hata baada ya kushinda nafasi ya Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania.

Mtaka amesema hata mwaka 2024, alipokuwa akiandaa kugombea urais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, alimtafuta tena Muharami ambaye alimshauri kuhusu mikakati ya ushindi na maeneo muhimu ya kuzingatia ili kuleta mageuzi katika kamati hiyo.

Amesema Muharami alikuwa mdau mashuhuri wa harakati za Olimpiki na alihudumu kwa muda mrefu kama Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Olimpiki Tanzania.

Aidha, mwaka 2023 aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Pierre de Coubertin (IPCC), yenye makao yake makuu nchini Uswisi, na kutunukiwa tuzo ya heshima ya Pierre de Coubertin.

Mtaka ameongeza kuwa marehemu alitafsiri kitabu cha Olympic Memoir kwa Kiswahili, kazi iliyotambuliwa na kupongezwa na Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) kwa mchango wake katika kueneza elimu na maadili ya Olimpiki. Pia aliwahi kuongoza timu ya Tanzania katika Mashindano ya Jumuiya ya Madola mwaka 2014.

Katika salamu zake, Mtaka ametoa pole kwa familia ya marehemu, wadau wa michezo, Chama cha Mpira wa Wavu Tanzania na Kamati ya Olimpiki Tanzania, akisema wengi walinufaika na busara na uongozi wake.

Amesema maisha ya mwanadamu ni hadithi, hivyo kila aliye hai anapaswa kuiandaa hadithi yake vizuri ili siku moja wengine wapate cha kujifunza.

Amehitimisha kwa kumwombea marehemu apumzike kwa amani na Mungu aifariji familia yake katika kipindi hiki cha majonzi.

Muharami Mchume alifariki dunia jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, ambapo anazikwa leo makaburi ya Mtoni Kijichi, jijini Dar es Salaam.