OSAKA, JAPAN: Lugha ya adhimu ya Kiswahili na utamaduni wa Mtanzania ni miongoni mwa mambo ambayo yamegeuka kuwa vivutio kikubwa kwa wageni mbalimbali wa kimataifa waliotembelea banda la Tanzania katika Wiki ya Utamaduni na Kiswahili ikiwa ni sehemu ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Osaka 2025-World Expo Osaka 2025 (Expo 2025) yanayoendelea huko Japan.
Watu mashuhuri kutoka mataifa mbalimbali, wametembelea banda hilo ikiwemo Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi la Japan, Koichiro Gemba, Mfalme wa Lesotho, Letsie III na Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Prudence Sebahizi.
Viongozi hao wameonesha na wageni wengine waliopata nafasi ya kutembelea banda hilo wameonesha kuvutiwa kwa kiasi kikubwa na lugha ya Kiswahili na Utamaduni wa Mtanzania kupata nafasi katika maonesho hayo.
Wiki ya Kiswahili na Utamaduni wa Mtanzania, Osaka, Japan
Akizungumza wakati alipotembelea banda hilo Sebahizi alieleza kufurahishwa na namna lugha ya Kiswahili ilivyopewa nafasi katika maonesho hayo ya dunia na kudai Kiswahili kinaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuwaunganisha Waafrika katika juhudi zao za kujiletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
SOMA: REA waitika Samia Kilimo Biashara Expo 2024
Akizungumza na maofisa wa taasisi za Tanzania zinazoshiriki katika maonesho hayo, ikiwemo Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Waziri Sebahizi amesema kuwa lugha ya kiswahili inakidhi kwa matumizi miongoni mwa Waafrika
Viongozi hao pia walipata fursa ya kujionea vivutio vya kitamaduni kama vile mavazi ya jadi, sanaa za mikono, bidhaa za kipekee kama kahawa ya Kilimanjaro, madini ya Tanzanite, viungo vya asili vya Zanzibar na machapisho mbalimbali ya Kiswahili huku Kamusi Kuu ya Kiswahili kutoka BAKITA ikiwavutia wengi.
Ushiriki huu wa Tanzania katika maonesho hayo ambayo kwa upande wa Tanzania yanaratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara za Tanzania (TanTrade), ni sehemu ya juhudi endelevu za kuitangaza lugha ya Kiswahili kama urithi wa Afrika na dunia, sambamba na utamaduni wake tajiri, ili kuimarisha uhusiano ya kimataifa na kuvutia wawekezaji, watalii na washirika wa maendeleo kupitia nguvu ya lugha na utambulisho wa kitaifa.
Kilele cha wiki hii ya Utamaduni na Kiswahili katika maonesho hayo kitafanyika kesho (Julai 7, 2025) ambapo kwa kawaida huwa ni Maadhimisho ya Siku Kiswahili Duniani (MASIKIDU), ambapo kutakuwa na utoaji wa vyeti na tuzo mbalimbali kwa wadau walioshiriki kwa hali na mali kukikuza, kukieneza, na kukiendeleza Kiswahili nchini Japani.




