NITAKUTAJIRISHA’ au ‘nitatia pesa mfukoni mwako’ ni lugha ya waganga na matapeli!
Naam, ukiyasikia maneno hayo tu gusa mfuko wako ili uhakikishe uko salama, lau sivyo uishie ‘ningalijua’.
Labda umeibiwa hata nauli. Huenda ukachanganya nyayo hadi nyumbani.
Muepuke kama jini au shetani mwanasiasa yeyote anayekwambia umchague au umpe fursa ya kukuongoza kwa muhula wa pili ili akutajirishe.
Anataka kukuangamiza kiuchumi. Usihadaike kitoto!
Walio na uzoefu wa kuzuru kilingeni husema mganga atakuahidi nguvu za kiume na labda ameachwa na mkewe kwa kupungukiwa kwenye maeneo hayo. Mbona asijitibu kwanza?
Atakuahidi kukutajirisha, lakini dalili ziko wazi kwamba hata yeye anahangaika.
Mbona amewahudumia watu miaka yote hii na hajastaafu mapema kwa sababu pesa zimetosha, angaa akapunge upepo ufukweni na ‘kurudishia mwili shukrani’?
Kwa nini asifanye ‘dili’ moja kali pale kilingeni, atajirike mara moja, aache kukesha akikupigia ramli na mambo mengine machafu na ya kishetani kama hayo?
Mbona amekuwa kama bango linalokuelekeza kwa kwenda, lakini kamwe haliendi huko? Kwani yeye hataki kutajirika?
Mambo haya si mageni mjini! Ahadi za kukutajirisha zimekaririwa na wanasiasa tangu zamani. Je, umetajirika? Umeegesha gari lako la kifahari wapi?
Waulize ‘mama mboga’ na vijana wa bodaboda walioahidiwa paradiso na Kasongo wakati wa kampeni za uch-aguzi uliopita iwapo wamefika huko tayari.
Waliahidiwa utajiri kutoka chini hadi juu, kumbe mpango wa hakika ulikuwa kuinuliwa juu, kuinamishwa, kutikiswa ili kila ndururu iliyo mfukoni ianguke, itwaliwe na waachwe solemba!
Anayekuahidi kukutia pesa mfukoni mwambie aanze saa hii!
Badala ya kutumia pesa nyingi kukuhonga ili umchague, aache kuwania wadhifa huo, akupe pesa zenyewe, utajirike kama yeye, nyote mkae raha mstrarehe.
Anafuata nini kwenye siasa? Kukutajirisha au kujitajirisha? Hiyo ni danganya-toto ya mwaka! Wajinga waliisha Kenya hii. Tunawaonea matapeli maguu 18, hatudanganyiki.
Nimekwambia umwambae kama jini mwanasiasa anayekuahidi kukutajirisha.
Amesoma akili yako akajua unatamani sana kutajirika ghafla, yaani leo ulale hohehahe, kesho urauke bwanyenye.
Haiwezekani!
Utajiri hauna miujiza. Sharti ufanye kazi. Anayekuahidi muujiza angejifanyia muujiza wenyewe ili atajirike kwanza.
Ama unataka kuniambia mjanja huyo anakupenda ziadi ya anavyojipenda?
Angekuwa na uwezo wa kufanya muujiza angejifanyia yeye pekee ili ajiongezee mafedha, wewe nami tuwe watumwa wake, vibarua wa kawaida kwenye mashamba yake ya mpunga, mahindi, kahawa, mananasi, korosho, majani-chai na maparachichi.
Ikiwa mganga hawezi kuwafumba macho polisi na walinzi wa benki akaingia mle na kuchota pesa kwa magunia, au akaziagiza pesa zipeperuke hadi kwake, zijae vyumba vyote na asigunduliwe, hawezi kuniambia kitu.
Mwanasiasa vilevile!
- Douglas Mutua ni mwanahabari Mkenya aliyeishi Amerika kwa miaka mingi ([email protected])




