MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino sasa amejipata katika hali ngumu ya kutimiza azma yake ya kuwa gavana kutokana na cheche kali kati yake na Kiongozi wa Linda Mwananchi Edwin Sifuna.
Bw Owino ana kibarua kigumu katika siasa za jijini huku mikakati ikiendelea kusukwa pia na mrengo wa DCP ambao Kinara wake Rigathi Gachagua alitangaza kuwa gavana mpya wa jiji atatoka chama hicho.
Wiki hii, Bw Sifuna alimkabili vikali Bw Owino kuhusu uongozi wa chama cha Linda Mwananchi (LMM) akikanusha kuwa hakumsaliti mbunge huyo katika mpangilio wa uongozi ambao wawili hao walikuwa nao.
“Katika vyama vyote vilivyoko nchini, nitajie chama kimoja ambacho mgombeaji urais si kiongozi wake,” akauliza Bw Sifuna.
“Mlipokuwa mkibishana kuhusu nani awe kiongozi wa chama, niliwauliza, mnawezaje kuniamini niwe rais wa nchi lakini msiniamini kuwa kiongozi wa chama? Sasa msaliti ni nani?”
Alikuwa akikanusha matamshi ya Bw Owino kuwa walikubaliana kuwa Bw Sifuna angekuwa mgombeaji wa urais huku naye mbunge huyo akiongoza chama ambacho wangekiunda.
Kwa sasa Bw Owino yuko katika chama cha Mwananchi (TMP) ambacho alikichukua kutoka kwa aliyekuwa Gavana wa Makueni Profesa Kivutha Kibwana.
Kando na kutangaza kuwa atawania ugavana kupitia chama hicho, Bw Owino pia anapanga kuwasilisha wagombeaji wa udiwani kupitia chama hicho si Nairobi pekee bali kote nchini.
Ingawa hivyo, tangu 2013 walioshinda ugavana wamekuwa wakitoka kwenye vyama vikubwa.
Mnamo 2013, Evans Kidero alishinda kupitia ODM, Mike Sonko kupitia Jubilee mnamo 2017 kisha mnamo 2022 Gavana wa sasa Johnson Sakaja akawahi kupitia chama cha UDA.
Je, Bw Owino ataweza kupitia TMP ambacho si kati ya vyama vikubwa nchini?
Upinzani ukiafikiana kuwasilisha mgombeaji mmoja wa urais 2027, kiti cha ugavana wa Nairobi kinaweza kujumuishwa katika makubaliano hayo.
Iwapo Bw Sifuna atapeperusha bendera ya upinzani, itakuwa vigumu sana kwa ugavana kusalia katika mrengo wake wa Linda Mwananchi.
Licha ya kuwa wako vyama tofauti sasa, Bw Owino amekuwa akitangaza kuwa atamuunga mkono Bw Sifuna kuwa rais wa sita wa Kenya.
Aidha baadhi ya wafuasi wa Bw Sifuna ambao ni wapigakura jijini na wanatoka ngome yake ya Magharibi, wamekuwa wakidai kuwa heri wamchague mgombeaji mwengine kuliko Bw Owino kama gavana iwapo ataendelea kumponda seneta huyo wa Nairobi.
Katika mrengo wa DCP, Bw Gachagua anaonekana kumakinikia kuwahi ugavana na kugawana viti na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka kuliko azma ya Bw Owino.
“Gavana ambaye atabadilisha Nairobi atatoka DCP,” alisema Bw Gachagua wiki hii.
Alipuuza azma ya Bw Sakaja kutetea wadhifa wake na nia ya mbunge wa Kasarani Ronald Karauri.
Mnamo, Disemba mwaka jana, Bw Gachagua alisema kuwa walikubaliana na Bw Musyoka kuwa DCP itawasilisha wagombeaji wa viti vya ugavana, useneta na mwakilishi wa kike.
Aliongeza kuwa watagawana viti 17 vya ubunge na wadi 85 za udiwani kwa kutegemea nguvu za Wiper na DCP.
Aidha upinzani ukikubali kuwa na mwaniaji mmoja wa ugavana, basi itabidi Bw Owino awanie ugavana kivyake na hilo linaweza kulemaza uhakika wake wa kushinda.
Hesabu za Bw Owino zinakuwa ngumu zaidi kwa sababu naye pia hawezi kupata uungwaji mkono wa ODM baada ya kuhepa chama hicho.
Bw Owino tayari amewakasirisha baadhi ya viongozi wa ODM kwa kudai atafanya kampeni kali Nyanza na Nairobi kuhakikisha hawachaguliwi tena.
Viongozi hao ni Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Mbunge wa Homa Bay mjini Opondo Kaluma na mwenzake wa Ruaraka TJ Kajwang’.
Wiki jana, Bw Kajwang’ alimshutumu Bw Owino akidai kuwa aligeuka jamii yake, kuwakosea heshima viongozi wakuu akidai alifanya hivyo ili kuwahi uungwaji mkono wa wapigakura kutoka eneo la Mlima Kenya.
“Tulifikiria tungempa ugavana na uungwaji mkono lakini hali si hivyo. Akitaka kupata kura za jamii yetu, lazima awe na heshima kwa viongozi wakuu na wazee,” akasema Bw Kajwang’.
Wiki jana, Bw Owino alililia jamii yake ya Waluo kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, akisema ndiyo inampinga katika azma yake badala ya kumuunga mkono.
“Kila mtu katika upinzani ananiunga mkono ila jamii yangu ya Waluo inanipinga. Mbona mnanipiga vita ilhali mimi ni mtoto wenu? Nimekosea nini? Msinipinge,” akasema Bw Owino.
“Bado mimi ni yule yule Babu ambaye ni mtoto wenu. Msinipinge kuwafurahisha watu wengine,” akasema.
Jinsi hali ilivyo kwa sasa ambapo ODM inaonekana kulenga unaibu gavana Nairobi huku nafasi ya kuwa na mgombeaji mwenza upande wa Rais Ruto ukiendelea kuwa ngumu, itakuwa vigumu sana kwa Bw Owino kupata uungwaji mkono wa chama hicho.




