CHAMA cha Jubilee kilichomuingiza madarakani Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na kilichowahi kutawala siasa za Mlima Kenya, sasa kinakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Democracy for Citizens Party (DCP) cha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.


Katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwake Mei 2025, DCP imevutia viongozi waliokuwa wanachama wa Jubilee, na hivyo kuzidisha vita vya kisiasa kuhusu nani atatawala eneo hilo kuelekea uchaguzi wa 2027.


Baada ya Gachagua kung’olewa mamlakani Oktoba 2024, Jubilee ilianza juhudi za kurejesha ushawishi wake. Uhuru alitangaza kuwa chama hicho kingerejea chini ya uongozi wa Dkt Fred Matiang’i, aliyekuwa akitajwa kuwa mgombeaji wake wa urais.


Lakini Gachagua alipozindua DCP, ushindani wa kisiasa ulizidi. Alisema chama chake ndicho kingekuwa chombo pekee cha kisiasa cha Mlima Kenya, huku vingine vikijivuta.


Miongoni mwa viongozi waliohama kutoka UDA na kujiunga na DCP ni magavana Irungu Kang’ata wa Murang’a na Kiarie Badilisha wa Nyandarua, pamoja na wabunge Wachira Karani, Muchangi Karemba, Rahab Mukami na Martha Wangari.


Aliyekuwa Mbunge wa EALA Kanini Kega, ambaye alikuwa mmoja wa washirika wa karibu wa Uhuru, pia alihamia DCP mwaka 2025. Alisema Jubilee ilikosa uongozi na kwamba wanachama walikuwa wakiondoka kwa wingi.


Huko Nairobi, wabunge wote watatu waliochaguliwa kwa tiketi ya Jubilee—Yusuf Hassan wa Kamukunji, Mark Mwenje wa Embakasi Central na Amos Mwago wa Starehe—wametangaza kuwa watatetea viti vyao kupitia DCP.


Chama hicho pia kimepokea madiwani wa Jubilee jijini Nairobi.


Pigo jingine lilitokea katika uchaguzi mdogo wa Ol Kalou, ambapo DCP ilipata asilimia 86 ya kura, ikilinganishwa na asilimia 13 za UDA. Jubilee ilipata kura 128 pekee.


Mnamo Septemba 22, Uhuru alimkabidhi Matiang’i uongozi wa Jubilee. Hata hivyo, viongozi wa DCP walianza kueneza ujumbe kuwa chama hicho kilikuwa kimeelekezwa zaidi eneo la Gusii, huku DCP ikijikita Mlima Kenya.


Baadaye, Uhuru alipohudhuria mazishi ya babake Martha Karua Kirinyaga Oktoba 3, alitoa wito kwa viongozi wa upinzani kuungana na kumteua mgombeaji mmoja wa urais dhidi ya Rais William Ruto mwaka 2027. Kauli hiyo ilitafsiriwa na baadhi ya wanachama wa Jubilee kama ishara kuwa hakuwa na nia ya kufufua chama hicho.


Aliyekuwa Mbunge wa Mwea Kabinga wa Thayu alisema alihama kwa sababu Jubilee ilikuwa ikijaribu kujifufua huku mwanzilishi wake akionyesha kutopendezwa na siasa za vyama.


Matiang’i, hata hivyo, amepuuzilia mbali madai ya mgawanyiko, akisema taarifa kuhusu mvutano kati ya viongozi wa upinzani zinalenga kuwatenganisha.


Gachagua naye anasema hahusiki moja kwa moja na uhamaji huo, akidai viongozi wanashinikizwa na wafuasi wao kujiunga na DCP. Anasema kazi yake ni kuwapokea na kuratibu mikutano yao katika makao yake Wamunyoro.


Hata hivyo, aliyekuwa Naibu Kiongozi wa Jubilee Jeremiah Kioni alijiuzulu Novemba 25, 2026 akisema anajiandaa kuanzisha jukwaa jingine la kisiasa.


Jubilee, chama cha PPK cha Ndindi Nyoro, PLP cha Karua na PNU cha Peter Munya sasa vinafanya kampeni zao tofauti katika Mlima Kenya.


Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Jubilee Zack Kinuthia amesema chama hicho kitarejea kwa nguvu na kuendelea kutetea demokrasia ya vyama vingi.


Amesema hali ya sasa ni ya muda tu na hakuna eneo la nchi linalopaswa kutawaliwa na chama kimoja pekee.