ARUSHA; ASKARI wa Jeshi USU la Shirika la Hifadhi ya Taifa (TANAPA), Zuberi Msemo na watoto wake watatu wamekufa kwa kuungua na moto unaosadikiwa ulitokana na kulipuka kwa simu au kompyuta mpakato.
Tukio hilo lilitokea eneo la Matejo juzi usiku wa kuamkia jana nyumbani kwa Msemo na mazishi yanatarajiwa kufanyika leo wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro. Kwa Mujibu wa Diwani wa Kata ya Sakina, Elvicent Lembris vifo vilijulikana jana asubuhi na miili ya Msemo na wanae itasafirishwa kwenda Mwanga kwa mazishi.
Watoto waliokufa ni pamoja na Mariam Msemo mtoto wa kwanza wa askari huyo, Salma Msemo mtoto wa pili na Bisma Msemo mtoto wa tatu kuzaliwa.
Waliojeruhiwa na moto huo ni pamoja na Mussa Msemo mdogo wa askari huyo, Mariam Zarawanga ambaye ni mama mzazi wa askari huyo, mke wa Msemo, Jasmin Msuya, dada wa askari huyo Mwanaidi Mussa, dada wa kazi Esther, Abdulkarim Mrindoko ambaye ni mtoto wa kaka yake na Firdaus Msemo ambaye ni mtoto mchanga wa askari huyo.
Chanzo cha moto kwa mujibu wa Jeshi la Zimamoto Arusha ni kompyuta mpakato au simu iliyokuwa inachajiwa kwenye sofa kupata moto na kuunguza sofa na moto huo kuenea maeneo mengine katika nyumba.
Msemo alifariki dunia jana baada ya kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru, lakini wengine walikufa papo hapo nyumbani kwa kuungua na moto.
Habari kutoka katika Hospital ya Mount Meru zilisema kuwa majeruhi wanaendelea kupata matibabu katika hospitali hiyo ila hali zao sio nzuri kwa kuwa majeruhi wengine wamevuta moshi mwingi wa moto huo uliochanganyika na wa jiko la gesi na wanaendelea kupatiwa huduma ya dharura.
Wote waliopoteza maisha ambao ni wa familia moja pamoja na baba yao wamehifadhiwa katika chumba cha maiti katika Hospitali ya Mount Meru jijini Arusha. Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Justin Massejo hakuweza kupatikana kuelezea tukio hilo kwa kuwa simu yake ya mkononi haikupatikana.
The post Moto waua askari Tanapa, watoto wake 3 first appeared on HabariLeo.




