NINGEPENDA tutafakari kwa pamoja uwezekano wa kuwa na siku zijazo zilizo bora zaidi katika uhusiano kati ya Marekani na Tanzania ambapo tutakuwa tumejenga ustawi mkubwa kwa mataifa yetu yote mawili.
Katika siku njema zijazo, safari za ndege za moja kwa moja zitaiunganisha Marekani na Tanzania, zikisafirisha mamia ya maelfu ya watalii wa Kimarekani kila mwaka kuja kufurahia hifadhi za wanyamapori, fukwe na hoteli za Tanzania.
Kampuni kubwa za Kimarekani zitakuwa zinawekeza mabilioni katika sekta za madini, utalii na sekta nyinginezo hapa Tanzania huku zikizalisha nafasi nyingi za ajira na utajiri kwa Wamarekani na Watanzania. Majeshi yetu yanashirikiana kudumisha utulivu wa kikanda na kulinda njia na bandari za kibiashara katika Bahari ya Hindi, kuhakikisha njia salama, pana na anuai za ugavi kwa uchumi wa dunia.
Wanasayansi wetu na wataalamu wa afya duniani wanashirikiana kufanya utafiti ili kulinda mataifa yetu na dunia nzima dhidi ya janga kubwa lijalo la kiafya. Bidhaa, huduma na uwekezaji kutoka Marekani zinaingia Tanzania bila vikwazo visivyo wazi au visivyo vya haki. Mustakabali huu ni wenye matumaini na uliojaa fursa.
Tunaweza kuanza kuujenga mustakabali huu sasa. Marekani imewekeza mabilioni ya Dola katika miongo iliyopita kwenye sekta za afya, elimu na kilimo nchini Tanzania, ikiokoa maisha na kuboresha riziki.
Ni wakati sasa kuthibitisha uimara wa uwekezaji huu na kwa Tanzania kama nchi ya kipato cha kati yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi, kuingia katika hatua mpya ya ukuaji unaoongozwa na sekta binafsi.
Marekani inafurahi kufungua ukurasa huu mpya pamoja na ninyi ili kusonga mbele kwa pamoja katika enzi mpya ya ushirikiano ambapo biashara na uwekezaji ndivyo vinakuwa kipaumbele katika uhusiano rasmi kati ya Marekani na Tanzania unaozinufaisha pande zote mbili.
Marekani inataka ushirikiano uliojikita katika fursa za pamoja za kiuchumi. Kuna makampuni ya Kimarekani yaliyo tayari kuwekeza katika fursa zinazowanufaisha Wamarekani na Watanzania zitakazounda ajira zenye thamani kubwa kwa pande zote mbili.
Kampuni hizo ziko tayari kushirikiana katika uwekezaji utakaoiwezesha Tanzania kunufaika kikamilifu na rasilimali zake za madini na nishati; kupanua upatikanaji wa mtandao wa intaneti nchi nzima; kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo ili kuongeza kuijumuisha kikamilifu Tanzania katika minyororo ya ugavi na usambazaji ya kimataifa na kuongeza tija kwa wakulima.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya uwekezaji huu umekwama kutokana na majadiliano yaliyokwama au yanayochukua muda mrefu kupindukia, masharti magumu ya kodi yanayokinzana na vivutio vya uwekezaji vilivyoahidiwa na vikwazo vingine visivyo vya kibiashara.
Tukiondoa vikwazo hivi na kukamilisha mikataba, tutazalisha simulizi nzuri zitakazovutia wawekezaji wengi zaidi kuja Tanzania. Mafanikio huzaa mafanikio.
Uchaguzi huru na wa haki uliofanyika kwa amani, ambapo Watanzania wana nafasi ya kusikika kwa kuchagua mustakabali wao, ni muhimu kwa mafanikio yetu ya pamoja katika kuharakisha za ukuaji unaoongozwa na sekta binafsi, kupambana na rushwa na kuimarisha mifumo ya ndani, pamoja na kupanua biashara na uwekezaji wa pande mbili unaowanufaisha wananchi wote.
Kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Rubio alivyoeleza mara kadhaa, “Marekani kwanza haimaanishi Marekani peke yake.” Ili Marekani ifanikishe malengo yake, lazima tushirikiane na nchi washirika kama Tanzania kufungua fursa za kiuchumi, kushirikiana kwenye vipaumbele vya kiusalama na kufanikisha ukuaji.
Mustakabali huu wa uhusiano kati ya Marekani na Tanzania uko karibu kuliko tunavyodhani. Kuufikia kunahitaji
dhamira ya kisiasa kutoka kwa nchi zetu zote mbili na kujitolea kwa dhati kujenga ushirikiano wa kweli.
Zama mpya za ushirikiano Tanzania, Marekani

This story was originally published by Habari Leo.
Read the full story at Habari LeoRelated stories
TravelMiss World Kufungua Milango ya Utalii
ZANZIBAR imeendelea kujitokeza kama moja ya vivutio muhimu vya utalii nchini, safari hii ikipokea ugeni wa Miss World 2026, Joheirry Molla aliyewasili visiwani humo Novemba 19, 2026, akiwa ameambatana na warembo kutoka mabara sita.
TravelAskari Tanapa, TFS mbaroni mauaji ya wabeba mkaa
KAGERA; Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera linawashikilia askari 13, wakiwemo wa wanyamapori wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), askari wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na askari mgambo, kwa tuhuma za mauaji ya watu wanne yaliyotokea Kijiji cha Kanyamika, Kata ya Karambi, Tarafa ya Kimwani, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera. Taarifa…
TravelNgorongoro scoops continental gong
ACCRA: THE Ngorongoro Conservation Area Authority (NCAA) has won the Excellence in Sustainable Tourism and Conservation Management Award at the Africa Business Forum & Awards 2026. The award recognises Ngorongoro’s contribution to biodiversity conservation, sustainable tourism development and the protection of its outstanding natural and cultural heritage. The awards ceremony was held in Accra, Ghana,…
TravelDk Kijaji: Mashindano makubwa gofu Afrika kufanyika Serengeti
MARA; Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, amesema Uwanja wa Gofu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti utawezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya gofu ya Afrika na kimataifa, hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya watalii, mapato na kuitangaza nchi kupitia utalii wa michezo. Akizungumza leo Oktoba 18, 2026, wakati wa uzinduzi wa…