KIGOMA; Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amewataka wahitimu wa kozi za Uhasibu, Biashara na Usimamizi wa Biashara wanaomaliza katika Chuo cha Elimu ya Biashara (TIA), Kampasi ya Kigoma, kutumia ukuaji na maendeleo ya teknolojia nchini kuchochea shughuli za uchumi na biashara kwa jamii na kukuza ajira.
Balozi Sirro alisema hayo katika Mahafali ya 24 ya TIA, huku Kampasi ya Kigoma ikifanya mahafali yake ya nne, na kubainisha kuwa Mkoa wa Kigoma umeteuliwa kuwa mkoa wa kimkakati wa shughuli za uchumi na biashara, hivyo utaalamu katika teknolojia unahitajika sana katika kusaidia biashara za kuvuka mpaka kuelekea nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.
Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dk Rashidi Chuachua, alikipongeza chuo cha TIA Kampasi ya Kigoma kwa ubunifu katika uendeshaji na utoaji wa mafunzo, ambao unawapa nafasi wanachuo wanaomaliza kutumia ujuzi na ubunifu huo katika kuwasaidia vijana wenzao mtaani, ikiwemo matumizi ya teknolojia kwenye shughuli za uchumi na biashara.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa wa Kigoma ametoa wito kwa uongozi wa TIA kupanua udahili wa wanafunzi wanaojiunga na kozi mbalimbali za chuo hicho kutoka nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Burundi, ambao kuna muingiliano wa shughuli za kiuchumi na biashara kwa kiasi kikubwa.
Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Pallangyo, alisema mikopo yenye thamani ya Shilingi milioni 187 imetolewa kwa wahitimu 224 wa chuo hicho kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), ikiwa ni ongezeko la asilimia 50.3 ukilinganisha na wanachuo 149 waliopata mikopo hiyo mwaka uliopita.
Alisema ongezeko hilo la mikopo limechangia pia ongezeko la udahili kwa wanafunzi wa chuo hicho Kampasi ya Kigoma, kutoka wanafunzi 978 mwaka 2025 na kufikia wanafunzi 1,066 kwa mwaka huu, na hivyo kuongeza fursa kwa Watanzania wengi kupata nafasi za masomo ya elimu ya juu.
Profesa Pallangyo alisema kwa mwaka huu, wahitimu 587 wamemaliza masomo kwenye chuo hicho Kampasi ya Kigoma, ikiwa ni asilimia nne ya wanafunzi 14,613 wa chuo hicho katika kampasi nane nchini.



