DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema inaendelea kuimarisha miundombinu ya reli za Kisasa (SGR), reli ya Mita (MGR) na TAZARA kwa lengo la kuongeza usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda maeneo mbalimbali nchini na nchi jirani.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema uwekezaji unaofanywa katika reli hizo unalenga kuongeza matumizi ya usafiri wa reli katika kusafirisha mizigo, kupunguza changamoto za usafirishaji na kuimarisha ushindani wa kibiashara.

Kihenzile amesema hayo wakati akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam, ambapo amesema umuhimu wa kuboresha miundombinu hiyo unatokana na matarajio ya kuongezeka kwa shehena ya mizigo itakayohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam.

Amesema makadirio yanaonesha kuwa ifikapo mwaka 2030, bandari hiyo inatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia tani milioni 62 za mizigo, hivyo kuhitaji reli zenye uwezo wa kusafirisha shehena hizo kwa ufanisi.

Amesema Serikali inaendelea kufanya mageuzi katika sekta ya uchukuzi, hususan reli, ili kuimarisha huduma za usafirishaji, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ushindani wa biashara.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2025, Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilisafirisha abiria 3,294,934 kupitia reli ya SGR mwaka 2025, ikilinganishwa na 1,422,116 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 131.6.

Aidha, katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, jumla ya abiria milioni 2.51 walisafirishwa kupitia reli hiyo, ikilinganishwa na milioni 2.05 katika kipindi kama hicho mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 22.4.

Kwa upande wa usafirishaji wa mizigo, Kihenzile amesema TRC ilisafirisha tani 102,452 kupitia SGR katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026.

Amesema takwimu hizo zinaonesha mchango wa uwekezaji wa Serikali katika kuboresha huduma za reli, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha miundombinu ya SGR, Meter Gauge na TAZARA ili kukidhi mahitaji ya usafirishaji wa mizigo yanayotarajiwa kuongezeka.

Aidha, amewapongeza watumishi wa sekta ya reli kwa mchango wao katika kupanga, kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za sekta hiyo, akisema wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio yanayopatikana.